USIMPE NGUVU SHETANI.

USIMPE NGUVU SHETANI.

Biblia inatuonyesha yapo majaribio matatu ambayo shetani atajaribu kuyafanya ili kuupandikiza ufalme wake.

Jaribio la kwanza ni lile alilolifanya mbinguni, lakini akashindwa, pale alipopigwa na akina Mikaeli pamoja na malaika zake..

Ufunuo 12:7 “Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake;

8 nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni.

9 Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye”

Jaribio la pili, atakuja kulifanya mara baadaya ya unyakuo kupita..Hapo ndipo Ibilisi atayakusanya mataifa yote ulimwenguni yaliyomwasi Mungu ili kupigana na Mungu mwenyezi, Hii ndio ile vita ya Harmagedoni.

Ufunuo 16:13 “Nikaona roho tatu za uchafu zilizofanana na vyura, zikitoka katika kinywa cha yule joka, na katika kinywa cha yule mnyama, na katika kinywa cha yule nabii wa uongo.

14 Hizo ndizo roho za mashetani, zifanyazo ishara, zitokazo na kuwaendea wafalme wa ulimwengu wote kuwakusanya kwa vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi.

15 (Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.)

16 Wakawakusanya hata mahali paitwapo kwa Kiebrania, Har-Magedoni”.

Na jaribio la tatu na la mwisho, litakuja mara baada ya ule utawala wa miaka 1000 kuisha,.Pale atakapofunguliwa kwa muda mchache tu kayadanganya mataifa tena., siku hiyo mataifa yatakusanyika pamoja, na kwenda kuizingira kambi ya watakatifu, hili nalo litashindwa vilevile kwani muda huo huo moto utashuka kutoka mbinguni na kuwaangamiza wote..Na shetani mwisho wake utakuwa umefika..Na majeshi yake yote..Kwani atakamatwa na kutupwa katika lile ziwa la moto na kuteswa huko milele na milele.

Ufunuo 20:7 “Na hiyo miaka elfu itakapokwisha, Shetani atafunguliwa, atoke kifungoni mwake;

8 naye atatoka kuwadanganya mataifa walio katika pembe nne za nchi, Gogu na Magogu, kuwakusanya kwa vita, ambao hesabu yao ni kama mchanga wa bahari.

9 Wakapanda juu ya upana wa nchi, wakaizingira kambi ya watakatifu, na mji huo uliopendwa. Moto ukashuka kutoka mbinguni, ukawala.

10 Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo. Nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele”.

Sasa ukichunguza hapo utaona shetani tayari alishashindwa tangu zamani katika jaribio la kwanza, na hukumu yake ilishapitishwa kabla hata ya wanadamu kuumbwa..Alikuwa ameshatupwa chini akingojea siku yake ifike ateketezwa kabisa, Lakini ghafla alipoona Mungu anaanza kuiumba tena dunia, na kuifanya kuwa sehemu ya kukaliwa na viumbe hai, na kumwona mwanadamu aliyeumbwa na Mungu kwa mfano wake na sura yake amewekwa katika bustani nzuri ya Edeni..

Alijaribu bahati yake, aone kama ataweza kuupata ufalme kwa kupitia hawa wanadamu walioumbwa kwa mfano wake na sura yake, Na alipoona jaribio lake la kwanza limefanikiwa, ndipo alipopata nguvu ya kuiendeleza kazi hiyo kwa kasi, ikawa kazi yake ni moja tu KUDANGANYA. Basi..akawaletea huduma na nyingine nyingi kama vile uchawi, uuaji, uongo, wizi n.k ili atimize tu azimio lake la kuwateka wanadamu wote..

Alipoona watu wengi wanazidi kuwa upande wake, ndipo akazidi kupata nguvu ulimwenguni, nafsi yake ikahuika upya, mawazo yake ya kuwa ameshindwa yakafa, akazidi kuidanganya dunia kwa bidii kubwa hadi karibu watu wote ulimwengu wakatekwa na yeye kipindi cha Nuhu, ndipo akawa mungu wa ulimwengu huu.

Lakini Mungu alipoona hivyo akaiangamiza dunia katika gharika,..Sasa kuanzia huo wakati akawa anawatumia wanadamu kujaribu kuuangusha ufalme wa Mungu, kwasababu yeye mwenyewe tayari alishashindwa zamani..Akaanza kutumia wafalme wengi sana kujaribu kuuangusha ufalme wa mbinguni ndani ya watu wa Mungu Israeli, huo ndio mpango wake hadi siku za mwisho kutumia mataifa kupambana na uzao wa Mungu.

Lakini kama kawaida atashindwa..

Ninachotaka leo tuone ni kuwa.. Shetani kama shetani hawezi kupata nguvu kama sisi, wenyewe hatutamruhusu apate nguvu.

Unapovaa vimini, na nguo fupi na kutembea uchi barabarani unampa shetani ufalme na nguvu, na sababu za yeye kuendelea mbele kuiharibu hii dunia na kuwapeleka maelfu ya watu kuzimu..Unapokunywa pombe, unapofanya uzinzi, unapokwenda disko, unapofanya mambo yote yasiyompendeza Mungu..Basi hapo ni unampa ibilisi nguvu za kuimiliki hii dunia..

Hata mpinga-kristo atakaponyanyuka,hatanyanyuka kwa nguvu zake mwenyewe bali atapewa nguvu na watu waovu wasiomcha Mungu. Shetani yeye mwenyewe alishashindwa, na wala hana nguvu yoyote ya kupigana, ni kiumbe dhaifu tu cha kushindwa siku zote, alikuwa kwenye giza nene bila tumaini lolote, lakini pale tunapomsifia kazi zake, tunapozifurahia kazi zake, basi anahuika na kupata nguvu ya kuwaharibu watu.

Hizi ni nyakati za mwisho. Angalia mataifa yote sasa yanaelekeza macho yao Israeli, idadi ya mataifa yanayolipinga taifa la Israeli yanazidi kuongezeka kwa kasi, na huo ni mpango wa shetani mwenyewe tangu zamani..na hiyo ni mojawapo ya dalili za siku za mwisho,…kwasababu anajua kuwa Masiya (YESU KRISTO) atashukia pale, na pale ndipo patakapokuwa makao makuu yake wakati wa kipindi cha utawala wa miaka 1000. Hivyo anachofanya kwa bidii sasa kuyaleta mataifa haya yote pamoja, ili kutimiza lile azimio la vita vya harmagedoni,..

Leo hii wala usitishwe kuona migogoro ya mataifa mengine, labda Korea, na Marekani, au Irani, au Urusi ukadhani kuwa hayo ndiyo yataleta vita ya Harmagedoni, hapana, iangalie Israeli kwasababu pale ndipo lile bonde la kukata maneno litakapokuwepo,..Pale ndipo patakapokuwa mwisho wa kila kitu..tageti yote ya shetani ipo pale..

Ndugu kama hujaokoka, ni heri ukafanya hivyo sasa, tubu dhambi zako, mkaribishe YESU maishani mwako, ili uache kumpa nguvu shetani kiumbe cha kushindwa, na uanze kuujenga ufalme wa BWANA YESU KRISTO, Mfalme wa wafalme, ambaye ufalme ni wake, na nguvu, na utukufu hata milele..

Shetani wakati wake ni mfupi sana, lakini Bwana wetu YESU KRISTO, ni mfalme wa milele, yeye hashindwi, wala hashindani, atakapokuja kutawala na sisi wakati huo hakika tutaufurahia ufalme wake, atatufuta haya machozi, wala hizi shida hazitakuwepo tena, wala madhaifu, wala magonjwa, wala mateso wala shida…hivyo tukaze mwendo ili tufikie huo.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Ikiwa utapenda tuwe tunakutumia masomo kwa njia ya whatsapp ya kila siku basi, bofya hapa uweze kujiunga >>> WHATSAPP Au tuandikie kwa namba hizi +255789001312

Mada Nyinginezo:

ANGUKO LA UFALME WA SHETANI:

NILIMWONA SHETANI, AKIANGUKA KUTOKA MBINGUNI.

MAONO YA NABII AMOSI.

UFUNUO: Mlango wa 16.

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

Nifanyeje niwe mwombaji mzuri, wa masafa marefu?

Walakini ataokolewa kwa uzazi wake.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments