NINI KINAFUATA SIKU ILE ILE YA KUOKOKA!

NINI KINAFUATA SIKU ILE ILE YA KUOKOKA!

Ni nini kinafuata siku ile ya kuokoka!? Ni swali linaloulizwa na wengi…

Shalom.Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe…Karibu tujifunze Biblia, Neno la Mungu ambalo ni mwanga wa njia zetu na Taa ya miguu yetu.

Watu wengi wanajiuliza ni nini kitafuata baada kumpokea Yesu, Nimeshatubu ndio! Je ni nini kinafuata baada ya hapo ili niendelee kusonga mbele katika Imani?. In

Baada ya kumruhusu Bwana Yesu Kristo aingie moyoni mwako…siku hiyo hiyo uliyofungua mlango wa yeye kuingia ndani yako..Tayari Roho Mtakatifu aliingia ndani yako…aliingia kama Roho ambayo pengine usingeweza kuhisi chochote nje…pengine ungesikia tu amani Fulani lakini usione chochote…Na Siku zinavyozidi kwenda kama utaendelea kuushikilia wokovu wako na kuukulia ndipo atakavyozidi kujaa zaidi ndani yako…Na utafikia kipindi utapokea Ujazo kamili wa Roho Mtakatifu kwaajili ya kazi yake.

Sasa siku hiyo unapotubu…hatua inayofuata kabla hata ya kwenda kutafuta kanisa la kujiunga, au kabla hata ya kwenda kubatizwa…hatua inayofuata ni kuacha yale yote uliyokuwa unayafanya…Kama ulikuwa ni mlevi unadhamiria kuacha ulevi pamoja na vyanzo vyake vyote..unaacha kwenda Bar, unakwenda kuvunja chupa zote za Bia ulizonazo nyumbani, unaacha kazi ya Bar kama ulikuwa ni muhudumu wa bar, unaiacha kampani yote ya walevi uliyokuwa unakutana nayo..

Kadhalika kama ulikuwa unavuta sigara, unakwenda kutupa pakti zote za sigara ulizokuwa nazo, unafuta namba za watu waliokuwa wanakuletea sigara hizo au bangi hizo…na unaacha moja kwa moja! Huachi kidogo kidogo hapana..unaacha moja kwa moja…usidanganywe na uongo wa shetani kwamba ukiacha ghafla utakufa!..hutakufa! Bwana atakusaidia kuishinda hiyo hali..Lakini ukiogopa na kuhisi kwamba utakufa utakapoacha madawa ya kulevya ghafla nataka nikuambie usipoacha ndio utakufa…hivyo acha!…Bwana hawezi kukuambia uache halafu ashindwe kujua namna ya kukuzuia usipate madhara, yeye si mwanadamu. Anaposema acha kitu Fulani anajua ni namna gani ya kukusaidia kushinda hicho kitu.

Kadhalika kama ni Mwasherati na unayejichua unaacha uasherati wako na kujichua kwako! Na mustarbation zako,..unaacha na vyanzo vyake vyote na malighafi zake zote…Unatoka kwenye huo mtandao wa makahaba uliopo sasa, unajitenga na kuliacha lile kundi ambalo mlikuwa mkikutana na kuzungumzia tu habari za zinaa..kama ulikuwa ni mfiraji na msagaji na shoga unaacha hivyo vitu kwa kumaanisha kabisa…tangu siku hiyo unatupa vile vitu ulivyokuwa unavitumia katika kusagana na unavichoma moto saa ile ile uliyomkaribisha Yesu moyoni mwako. Unafuta pia na picha zote chafu za ngono kwenye simu yako au laptop yako na unavunja vunja cd zote za ngono ulizokuwa nazo, na muvi zote ambazo unajua kabisa hazikujengi kwa lolote,na nyimbo zote za kidunia, unazifuta kwenye simu yako,. Kumbuka mambo haya yote yanapaswa yafanyike siku ile ile uliyookoka! Na sio baada ya wiki au mwezi.

Vivyo hivyo ulikuwa umepaka wanja, unakwenda kuufuta saa hiyo hiyo, na unakusanya kalamu zote za wanja na lipstick unakwenda kuzichoma moto..usimpe mtu baki …wala usitafute ushauri kwa mtu… wewe kuwa kama kichaa usiangalia kushoto wala kulia…vivyo hivyo kusanya nguo zako zote fupi na za kubana na suruali..kwa pamoja kazichome moto..hata kama utabakiwa na nguo moja tu..sema moyoni mwako kwamba “Umebeba msalaba wako umeamua kumfuata Yesu”..

Una suruali model unachoma, ulikuwa umenyoa mtindo ujulikanao kama kiduku, nenda kinyozi siku hiyo hiyo kaondoe…ulikuwa unacheza kamari, na kuhudhuria disko unahitimisha siku hiyo hiyo.. na pia kama ulikuwa unafuatilia matamthilia ya kiulimwengu ambayo dhima yake ni kuchochoea tamaa za vitu visivyofaa unaacha kuziangalia zote. Unapiga Break..Ulikuwa umejiunga na magroup ya whatsapp na facebook ya kidunia unaleft kwenye hayo magroup na kubakia tu na yale ya kikristo..Ulikuwa ni muhudhuriaji kwa waganga wa kienyeji na mshirikina na mchawi..unautupa na kuuchoma ushirikina wako na hirizi zako, na dawa zote ulizopewa na waganga….

Na mambo mengine yote ambayo hayajatajwa hapa maovu unayaacha..siku ile ile unayotubu…usisubiri baada ya siku 2 au tatu…Roho Mtakatifu hataweza kuvumilia ndani yako siku hizo zote ukiwa unaendelea na hivyo vitu…atakuacha! Na utabaki bila badiliko lolote. Na toba yako itakuwa ni bure.

Kitu ambacho watu wengi hawajui na kusababisha kila siku kuongozwa sala ya kutubu na kuwafanya wabakie katika hali ile ile ya kutokuwa na badiliko lolote rohoni..ni kwasababu huwa hawaamui kuacha dhambi pindi wanapomgeukia Kristo. Usipoamua kuacha vyote vya kiulimwengu na kumfuata Kristo hapo bado hujaokoka!..haijalishi umeombewa mara ngapi au umeongozwa sala ya kutubu mara ngapi.

Tunaona jambo hilo hata katika kanisa la kwanza…Watu baada ya kutubu walichoma mambo yao yote yaliyokuwa yanawafanya watende dhambi..

Matendo 19:17 “Habari hii ikajulikana na Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawaingia wote, na jina la Bwana Yesu likatukuzwa.

18 Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao.

19 Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu”.

Unaona hapo!…Biblia inasema wakachoma mbele ya watu wote!..Na wewe choma usimwangalie mtu.

Sasa baada ya kufanya hayo yote, baada ya kuchoma suruali zako, kuchoma hirizi zako, vipodozi vyako, baada ya kujitenga na vikao vya walevi uliokuwa unalewa nao, baada ya kuleft magroup ya kidunia ambayo walikuwa wamekuzoea kuchangia mada, baada ya kufuta namba za wale uliokuwa unafanya nao uasherati, baada ya kuacha uasherati…

Hapo utakuwa umejikana nafsi yako!..Hivyo jambo litakalofuata hapo ni shetani kutaharuki, hapo ndipo atakaponyanyuka kinyume chako wewe, Huna budi kujaribiwa….Umemkataa shetani kwa ghafla namna hiyo! Ni lazima atanyanyuka ili kukupinga kwa nguvu..wale uliokuwa unafanya nao uasherati watakutafuta kwa nguvu na kutamani kukurudisha na kukutishia hivi au vile endapo hutarudiana nao…Huo ni wakati wa kubeba msalaba wako na kuendelea mbele..usirudi nyuma.

Wale wachawi wako ambao mlikuwa mnashuka wote vilindini..watakutafuta na kukurudia na kukutishia hivi au vile..huo ni wakati wa kubeba msalaba. Ndugu zako ambao walikuwa wamezoea kukuona ni mshabiki wa tamthilia Fulani au kitu Fulani cha kidunia watakuja na kukuuliza kulikoni?…

Huo ni wakati wa kusonga mbele usiangalie nyuma..Utapitia matusi, dhihaka, wakati mwingine kutengwa na kudharauliwa kwa kipindi Fulani lakini Kristo atakuwa upande wako…Japokuwa utakuwa unapitia dhiki nje lakini ndani yako kutakuwa na furaha ya ajabu na amani ambayo watu wa nje watakuwa hawawezi kuiona. Furaha hiyo na Amani hiyo Kristo haishushi kwa kila mtu tu, anayedai ameokoka, bali anaishusha kwa watu maalumu waliojitwika msalaba wao na kumfuata yeye.

Sasa ukiona kwamba baada ya kuokoka ndio hayo mambo yameanza…huo ndio uthibitisho kwamba kweli umempokea Kristo..lakini kama huoni chochote..basi jitathmini mara mbili mbili..inawezekana hakuna badiliko lolote katika maisha yako…

Na ukiyashinda hayo ambayo yatapita kwa muda tu, basi ipo neema ya ziada itaachiliwa kwako, na wewe utahesabiwa kama mwana wa Mungu, na mwanafunzi wa Kristo halali kama vile wale mitume wake, hivyo licha tu ya kupata uhakika wa kwenda mbinguni lakini pia jiandae kukutana na Kristo maishani mwako kwa viwango vingine ambavyo hukuwahi kukutana navyo au kumjua Kristo katika hivyo, tofauti na wanadamu wengine wa kawaida.

Hivyo ndugu yangu kama hujaokoka na leo unasema unataka kuanza maisha mapya na Kristo..gharama ni hizo hapo juu…kama upo tayari kuzichukua hizo gharama ni vyema lakini kama hujawa tayari..haulazimishwi…

Hivyo kama upo tayari, basi uamuzi unaoufanya ni wa busara sana ambao hautakaa uujutie maisha yako yote kama ilivyokuwa hata kwetu sisi. Unachopaswa kufanya, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

“EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE. NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE”.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako. Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.

Zingatia hayo na Bwana atakusaidia.

Ubarikiwe sana

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Maran atha!


Mada Nyinginezo:

Unyenyekevu ni nini?

NI NINI TUNAJIFUNZA JUU YA MT. DENIS WA UFARANSA?

KWANINI MUNGU ALIMTUMIA MUSA KWA VIWANGO VILE?

NJIA YA MSALABA

TIMAZI NI NINI

“Si watu wa kutumia mvinyo sana”, je tunaruhusiwa kutumia mvingo kidogo?(1Timotheo 3:8).

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments