NI NINI TUNAJIFUNZA JUU YA MT. DENIS WA UFARANSA?

NI NINI TUNAJIFUNZA JUU YA MT. DENIS WA UFARANSA?

Shalom. Jina la kuu la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe.

Karibu katika mwendelezo wetu unaoangazia matendo ya baadhi ya watu walioishindania imani hadi kufa bila kuiacha..Tulishawaona baadhi nyuma na Leo tutamwangazia mwingine anayeitwa Mtakatifu Denis wa Ufaransa.

Mtu huyu, alitokea karne ya tatu, Ni maarufu sana katika historia ya nchi Ufaransa, na hata katika vitabu vinavyoelezea historia ya mauaji ya wakristo, Huyu alikuwa kama mmishionari aliyezaliwa Italy, na kusafiri yeye pamoja na wenzake wawili nchini Ufaransa kwa lengo la kupeleka habari njema za Yesu Kristo,..Alipofika kule, Mungu alikuwa pamoja naye kwani alikuwa na bidii kubwa sana ya kuwageuza watu kwa Kristo, na hata wale makuhani wa dini za kipagani walipoona wanapotezewa waumini wao wengi, wanageuzwa na kuwa wakristo, wakaamua kuwaaundia visa watu hawa. Kama tu vile wakati mtume Paulo alipofika Efeso na kuwageuza watu wengi, na wale wenyeji wa mji walipoona wanapata hasara ya watu kutonunua bidhaa za miungu yao wakawaletea visa, ili Paulo na wenzake waletewe dhiki. Na ndivyo ilivyotokea kwa hawa.

Na sasa serikali ya Rumi iliposikia habari yao, ikawakamata na kuwafunga, ikumbukwe kuwa Rumi wakati huo ilikuwa katika vita vikali dhidi ya watu wote waliokuwa wanaonekana kueneza imani ya kikristo duniani. Lilikuwa ni taifa la kipagani asilimia 100. Hivyo Waliwafunga wakawaacha magerezani kwa muda mrefu, na mwisho wa siku wakawatoa magerezani na kuwachukua mpaka katika kilele cha mlima mmoja ili kuwaua kwa kuwakata vichwa, waliwakata wote lakini walipofika kwa mtakatifu Denis, na kukiondoa kichwa chake, walishaangaa kuona anakiokota tena kichwa chake, na kuanza kutembea maili kadhaa, akihubiri injili kila alipopita.

Tendo hili liliwaogopesha watu wengi sana waliokuwa wanashuhudia maajabu yale, na mahali alipoacha kuhubiri na kuanguka chini Mahali palepale ndipo ulipogeuzwa mji ule na kuitwa kwa jina lake ambao hadi sasa upo huko ufaransa,. Na juu ya kaburi lake wakatoliki baadaye walijenga kanisa lijulikanalo kama Basilica of Saint-Denis. (lakini kumbuka huyu Mt. Denis mwenyewe hakuwa mkatoliki wala mafundisho yake hayakuwa ya kikatoliki bali ya kanisa la kwanza la mitume wa Yesu Kristo, yaani Neno la Mungu lisiloghoshiwa).

Hadi leo sanamu lake limewekwa huko katika makumbusho za kitaifa huko Paris. Hizi ni historia ambazo zimethibitishwa. Hatuna mengi ya kuzungumza Lakini Tukiwatazama watu kama hawa tunapata ujumbe gani?

Biblia inasema..

Waebrania 12:1 “Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu,

2 tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu”.

Ikiwa tunazungukwa na watu waolikuwa tayari kufungwa, hadi kuuawa kwa kukatwa vichwa kama hawa na bado walikuwa hawana hata mpango wa kumwacha Mungu, hadi Mungu anawapa nafasi ya kuendelea kuhubiri angali vichwa vyao havipo, sisi je tunapaswa tuweje?..Ikiwa hatujafikia hatua ya kumwaga damu kwa ajili ya ushuhuda kwa Kristo, lakini ni rahisi kurudishwa nyuma na mambo madogo, madogo tu yasiyokuwa na maana, tujiulize siku ile tutawezaje kusimama pamoja na watu kama hawa mbele ya Kristo? Tutawezaje kupata thawabu moja na wao watu ambao wamepiga mbio bila kuishiwa pumzi, wameishindania imani ipasavyo, kama biblia inavyotuambia katika sura iliyotangulia waebrania sura ya 11

“36 wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani;

37 walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizunguka-zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya;

38 (watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao), walikuwa wakizunguka-zunguka katika nyika na katika milima na katika mapango na katika mashimo ya nchi.

39 Na watu hao wote wakiisha kushuhudiwa kwa sababu ya imani yao, hawakuipokea ahadi;

40 kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea sisi kitu kilicho bora, ili wao wasikamilishwe pasipo sisi”.

Umeona mstari wa 40 unavyosema, hawakukamilishwa, hawakuipokea ahadi au thawabu yao, kwa ajili yetu sisi, mpaka sisi nasi tutakapomaliza mbio, ili kwa pamoja tupokee tuzo bora..Lakini kama sisi tutaendelea kuwa vuguvugu, na walegevu, tutaendelea kuuchezea wokovu, tutaendelea kuishi kama vile sio watu waliomaanisha kweli kuenda mbinguni, Siku ile biblia inatuambia tutatupwa katika giza la nje,.

Hakuna tukio lingine lolote tunalolisubiria mbele yetu isipokuwa tukio la unyakuo tu, dalili zote zimeshatimia, siku yoyote parapanda inalia na wafu waliolala katika Kristo, watafufuka, kisha wataungana na watakatifu walioko duniani, na kwa pamoja tutakwenda mbinguni kwenye karamu ya mwana kondoo.

Utajisikiaje siku hiyo kujiona umebaki hapa chini, na kibaya zaidi ukikumbuka umehubiriwa injili mara nyingi lakini ulishupaza shingo yako. Utakuwa katika hali gani..Hao ambao unawafurahisha siku ile wote kwa pamoja mtakuwa katika majonzi na majuto ya milele.

Huu ni wakati wa kumaanisha kumfuata Kristo kwa moyo wote, bila kujali, ndugu watakuonaje, marafiki watakuonaje, kazini watakuonaje, shuleni watakuonaje..ni wakati wa kupiga mbio kwa kutua mizigo yote ya dhambi, kisha kumtazama yeye aliyetuita,..Kumbuka toba ya kweli inatoka moyoni na sio kinywani, unaweza ukaongozwa sala ya toba hata mara 100 kama toba yako haikutoka moyoni ni sawa na kazi bure..yule mwanamke kahaba aliyemfauta Yesu akamlilia, akammwagia machozi yake mengi, miguu pake hakuwa anafanya jambo la kuigiza tu, kama linavyofanywa na wengi leo hii, bali alikuwa anaonyesha ni jinsi gani amemaanisha kutubu dhambi zake, na ukahaba wake, hadi akashindwa kuzungumza mbele zake,.na Yesu kuona vile tu bila hata ya kuisikia sauti yake au maneno yake, alisema amesamehewa dhambi zake..Unaona hakuongozwa sala yoyote pale, lakini alipoona moyo wake umetubu na kugeuka, japokuwa dhambi zake zilikuwa nyingi, alisamehewa zote..

Vivyo hivyo na wewe ukidhamiria kuacha dhambi zako kwa moyo wako wote, na kwa nguvu zako zote, ukageuka na kusema kuanzia leo mimi na ulimwengu basi nimeamua kumfuata Yesu bila kugeuka tena nyuma..Ujue kuwa hapo ndipo Mungu atakapokusamehe dhambi zako, kinachobakia kwako ni kuukamalisha wokovu wako kwa kwenda kubatizwa na kumwishia Kristo maisha yako yote yaliyobakia hapa duniani..

Hivyo kwa kumalizia unapokutana na hili Neno WINGU LA MASHAHIDI, kichwani kwako usiusahau ujumbe huo, kuwa lipo wingu kubwa la mashahidi wa Kristo linalotuzunguka, ndilo linalotuhimiza na sisi tupige mbio kama wao, katika mashindano tuliyowekewa mbele yetu kushinda tulivyokuwa tunapiga hapo mwanzo, na mbio hizo tunapiga kwa kutua kila mizigo ya dhambi inayotusonga kwa kadiri tuwezavyo ili tuwe wepesi Zaidi na zaidi..Ili na sisi tukapokee tuzo iliyobora kama wao, hata zaidi ya wao siku ile.

Ubarikiwe sana.

Mada Nyinginezo:

ANTIPA SHAHIDI WANGU, MWAMINIFU WANGU.

WINGU KUBWA LA MASHAHIDI.

JIFANYIE RAFIKI KWA MALI YA UDHALIMU.

KIFO CHA REINHARD BONKEY KINAACHA UJUMBE GANI KWETU?

 

HERI NINYI MLIAO SASA, KWA SABABU MTACHEKA.

TABIA YAKO NI YA MNYAMA GANI?

DANIELI: Mlango wa 9

UFUNUO: Mlango wa 11

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments