JIHADHARI NA KUOSHWA MIGUU ISIVYOPASWA.

JIHADHARI NA KUOSHWA MIGUU ISIVYOPASWA.

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe…Ni kwa Neema zake tumeiona tena siku ya leo..hivyo hatuna budi kumshukuru sana kwa Fadhili zake nyingi kwetu, na kuchukua nafasi hii angalau kujifunza Neno lake.

Masomo yaliyotangulia tuliona ni jinsi gani..Maagizo ya kushiriki meza ya Bwana na kuoshana miguu yalivyo ya muhimu sana kwa kila mkristo kuyazingatia. Kuoshana miguu ni tendo jepesi kulifanya lakini Adui kalifanya kuwa gumu na hata kuliharibu au kulifanya lifanyike isivyopaswa.

Ukiona unasema umeokoka lakini kuna ugumu katika kuosha miguu ya mtakatifu mwenzako basi kuna kasoro katika wokovu wako…Bwana Yesu alisema katika;

Mathayo 18:3.. “ Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.

4 Basi, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni.”

Ikiwa na maana kuwa kuna mambo madogo sana ambayo yanaweza kumkosesha mtu mbingu, na moja ya jambo hilo ni kukosa unyenyekevu.

Na kipimo cha kwanza cha unyenyekevu kwa kila mkristo ni kujishusha na kushika miguu ya mwenzake?..Je! unaweza kujishusha chini na kuosha miguu ya dada mwenzako? Na kuifuta kwa kitambaa??…Je! unaweza kujishusha chini na kuosha miguu ya jirani yako yenye mavumbi?…Kama huwezi basi Bwana Yesu anasema ni ngumu kuuingia ufalme wa mbinguni.

Yohana 13:12 “Basi alipokwisha kuwatawadha miguu, na kuyatwaa mavazi yake, na kuketi tena, akawaambia, Je! Mmeelewa na hayo niliyowatendea?

13 Ninyi mwaniita, Mwalimu, na, Bwana; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo.

14 Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi.

15 Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo.

16 Amin, amin, nawaambia ninyi, Mtumwa si mkuu kuliko bwana wake; wala mtume si mkuu kuliko yeye aliyempeleka.

17 Mkiyajua hayo, heri ninyi mkiyatenda”.

Lakini pamoja na hayo yote shetani naye anafanya kazi kwa nguvu kuhakikisha kwamba watu wanakwenda kuzimu kihalali…Anachokifanya ni kumfanya mtu afanye dhambi ya makusudi ili siku ile asiwe na la kujitetea mbele ya kiti cha hukumu. Kwamfano atamzuia mtu asiende kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi, ambapo ni kitendo cha dakika moja tu kuzama mwili wote na kunyanyuka juu na anakifanya mara moja tu katika Maisha yake…atamzuia kufanya hivyo lakini atamshawishi kwa nguvu nyingi kwenda kila siku kuogelea kwenye fukwe za bahari au katika mabwawa ya starehe hata kwa masaa kadhaa bila kuchoka …Hiyo yote ni ili akose la kujitetea katika siku ile ya hukumu.

Kadhalika atamzuia mtu na kumfanya apinge vikali kukaa katika sala au ibada masaa 6 lakini atamweka katika kumbi za starehe au katika televisheni au mitandao kwa masaa hata 10 kwa siku..ili kwamba siku ile atakaposimamishwa mbele ya kiti cha hukumu asiwe na cha kujitetea.

Vivyo hivyo atamzuia leo hii asishiriki kuosha miguu ya watakatifu lakini huyo huyo kijana atakuwa tayari kwenda kuosha wanawake miguu katika vibaraza na masaluni. Na mwanamke hivyo hivyo hatataka kushiriki kufanya ibada ya kuosha au kuoshwa miguu kanisani na wanawake wenzake lakini kila baada ya siku 3 ataketi vibarazani kuoshwa miguu tena na jinsia tofauti na yake. Hiyo ndiyo kazi ya shetani kukoroga mambo…

Ndugu kama unafanya hivyo fahamu kuwa hutakuwa na la kujitetea siku ile ya hukumu.

Mwanamke au binti kama unakwenda kuoshwa miguu na kusuguliwa kucha na wanaume saluni au vibarazani..basi fahamu kuwa bado neema ya Mungu haijakaa juu yako (bado kuna nguvu za giza zimekushika)! Tena zimekushika kweli kweli..Unahitaji kumpokea Yesu Kristo kwasababu Mtu aliyeokoka kwa kudhamiria kabisa kumfuata Yesu Kristo, mambo hayo hawezi kuyafanya wala hata hayamwingii akilini…..

Vitu vya kwanza kabisa Roho Mtakatifu kumshuhudia mtu aviache ni uasherati na vichocheo vyake vyote. Na kichocheo kimojawapo cha uasherati ni kuoshwa miguu na wanaume vibarazani, hakuna namna yoyote kitendo hicho kisiwe kichocheo cha uasherati..hakuna!!..Kila anayefanya hivyo au anayefanyiwa kuna roho ya uasherati ipo ndani yake. (Na waasherati wote hawataurithi ufalme wa mbinguni biblia inasema hivyo katika 1wakorintho 6:9)…Na licha tu ya Roho ya uasherati kuna roho nyingine zinakuwa zinamwingia kila anayefanyiwa hivyo…

Wengi wanaooshwa miguu wakitoka pale shetani anaingiza roho ya muunganiko kati ya hao wawili, unakuta mtu alikuwa ameolewa lakini hampendi tena mume wake wala Watoto wake..anakuwa anapenda jamii ya watu au rika la watu kama wale waliomwosha miguu…na hata ile hamu na kiu ya kumtafuta Mungu inakufa!..Ile Nuru ndogo ambayo pengine ilikuwa imeshaanza kuangaza ndani yake inazima..hata kama alikuwa ametoka kwenye mahubiri na yamemchoma na hivyo ameamua kugeuka..kitendo tu cha kushuka pale na kuosha miguu..shetani anaiiba ile mbegu..Na Maisha ya huyo mtu yanaharibika mara mbili Zaidi. Na kama binti hajaolewa, kitendo cha kwenda kuoshwa miguu tayari ameikusanya hatima yake mikononi mwa shetani..kuolewa kwake inakuwa ni ngumu, au hata akiolewa ataolewa na mtu ambaye si sahihi..

Wanawake wengi imekuwa ni rahisi kushambuliwa na nguvu za giza kwa namna hiyo, kwasababu kila mlango wanaouona mbele yao bila kuhakiki kwanza wanaiga, na mwisho wa siku wanaangukia katika mitego ya shetani bila wao kujijua.

Madhara hayo pia yanawapata wanaume wanaooshwa miguu na wanawake au wanaooshwa vichwa masaluni na kufanyiwa massage. Madhara ni hayo hayo..

Hivyo kama unajiona unaweza kukesha kwenye mitandao usiku kucha huo ni uthibitisho kwamba unauwezo wa kukesha ukisali usiku mzima, kama ulikuwa unauwezo wa kuogelea masaa kadhaa bila kuchoka pwani basi unaweza kwenda kubatizwa kitendo cha dakika moja tu..kama ulikuwa unaweza kuosha au kuoshwa miguu masaluni..unaweza kufanya hayo hayo kwa watakatifu wenzako wa jinsia moja na wewe kanisani au manyumbani na ukapata baraka nyingi zaidi badala ya laana.

Ukiwaosha watakatifu wenzako miguu wa jinsia moja na wewe..utaonyesha ishara ya unyenyekevu na hivyo Bwana atakukweza badala ya kukushusha…Na pia utaongeza uhusiano wako na wakristo wenzako jambo ambalo halitampa nafasi shetani kuwajaribu.Na utafanikiwa katika mambo yote, na Zaidi sana kujiwekea nafasi nzuri ya kuingia mbinguni.

Ubarikiwe sana.

Kama ulikuwa hujaokoka na leo umekusudia kabisa kuokoka na kuacha vitu vyote viovu ulivyokuwa unavifanya ikiwemo kuhudhuria kuoshwa au kuosha miguu kwenye masaluni ya kike…

Basi uamuzi unaoufanya ni wa busara sana ambao hautakaa uujutie maisha yako yote kama ilivyokuwa hata kwetu sisi. Unachopaswa kufanya, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, .

NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, ikiwemo kuhuhudhuria kwenye vibaraza vya kuoshwa miguu na kuacha mambo yote ya kiulimwengu..Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako. Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.

Ubarikiwe sana

Mada Nyinginezo:

MEZA YA BWANA, NA KUTAWADHANA MIGUU.

LOLOTE ATAKALOWAAMBIA FANYENI.

Nini tofauti ya haya maneno. 1) KUOKOKA, 2) WOKOVU, 3) KUONGOKA.?

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

JE! UNAYO NAFASI MBINGUNI?

KUOTA UNAFANYA TENDO LA NDOA.

KUOTA UMEPOTEA.

KUOTA UPO UCHI.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments