KUOTA UPO UCHI.

KUOTA UPO UCHI.

Ufunuo 16:15 “(Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.)”

Kipindi Fulani nyuma kabla sijampa Bwana maisha yangu, niliota ndoto moja ambayo hadi leo sitaisahau, niliota nimejikuta nipo uchi, halafu nakatiza barabarani mjini maeneo ya posta Dar es salaam, sasa nilipojiona nipo vile nikawa ninatafuta namna ya kujificha..

Nikawa ninajibanza banza kwenye vikona vya majengo, nikivizia watu wapungue kisha nikimbilie upande mwingine, hivyo hivyo hadi kigiza kingie nikimbilie nyumbani, na kweli nilifanikiwa kujificha ficha hivyo hivyo nisionekane na watu au marafiki zangu mpaka nilipofanikiwa kufika  nyumbani nikafurahi sana kwasababu nilijiona kama sijaoenekana  na watu wengi, hususani na wanaonijua, lakini muda kidogo nikashangaa marafiki zangu wa chuo, tena wa kike wananijia kwa mshangao, wakiniambia mbona tumeona picha zako na video zako zimezagaa mtandaoni ukiwa uchi unakatiza barabarani, kwa kweli wakati nikiwa huko huko kwenye ndoto niliishiwa nguvu, nilijiona nipo katika aibu na fedheha ya milele isiyoweza kufutika, nikawa nawaza ni heri nisingezaliwa, kwasababu jambo kama  lile halina tofauti na wale wanaoigiza mikanda ya video za zinaa, ambalo litaendelea kuwepo mitandaoni daima..

Sasa wakati nikiwa katika hali mbaya sana huko huko kwenye ndoto neno moja la kiingereza likaja mbele yangu, ambalo sikuwahi hata kulijua wala kulisoma mahali popote na hilo ndilo lililonifanya mpaka leo hii ninaikumbuka ndoto hiyo na neno lenyewe ni hili “NUDE”.. Muda huo huo nikashutuka,  nikafurahi kwa kuwa kwa kuwa ilikuwa ni ndoto lakini nikasema ngoja nilitazame kwenye kamusi ya kiingereza lile neno lina maana gani ndipo nikakuta lina maana ile ile ya UCHI kama nilivyokuwa katika ndoto.

Kwa kweli nilikaa muda mrefu sana bila kuelewa ndoto ile ilikuwa na maana gani. Lakini siku nilipokuja kumpa Kristo maisha yangu, ndipo Bwana aliponifundisha maana ya ile ndoto niliyoita.. Nataka nikuambie ukiota ndoto yoyote upo uchi, halafu upo katikati ya kadamnasi, au mahali popote pale iwe shuleni, au kazini, au stendi ya mabasi, au sokoni, basi fahamu kuwa ndivyo hali yako ya kiroho ilivyo kwa sasa.

Sikuzote UCHI unazaa ni Aibu, na Aibu inakupelekea mtu kwenda kujificha..Adamu na Hawa walipoasi pale Edeni, walijiona kuwa wapo uchi, ndipo aibu ikawaingia na hapo hakuna kingine zaidi ya kwenda kutafuta namna ya kujisitiri..

Mwanzo 3:8 “Kisha wakasikia sauti ya Bwana Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga; Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya bustani, Bwana Mungu asiwaone.

9 Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi?

10 Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha”.

Hivyo unapoota ndoto hii moja kwa moja ujue  kuwa utukufu wa Mungu umeondoka juu yako, au upo mbioni kuondoka  kabisa juu yako kama hutataka kutubu dhambi zako, Na ndio maana Mungu anakuonyesha kwa jinsi hiyo hiyo unavyoweza kuona aibu ndivyo itakavyokuwa siku ile siri zako zote na dhambi zako zote unazofanya kwa siri zitakapowekwa wazi mbele ya malaika wake wote wa mbinguni

Warumi 2:16 katika siku ile Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu, sawasawa na injili yangu, kwa Kristo Yesu.

Danieli 12:2 “Tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele”.

Jiulize siku hiyo utakuwa katika aibu ya namna gani, utakuwa katika hali ya kudharauliwa kwa namna gani…ubaya zaidi aibu hiyo itakuwa ni ya milele..Mimi nilipokuwa katika dhambi Mungu aliniotesha hilo na haikuwa mara moja, ziliendelea kuja hivyo hivyo  mara kwa mara mpaka nilipompokea Bwana Yesu.

Vilevile ndoto hii haimuhusu aliye nje ya Kristo tu peke yake hapana hata Yule ambaye yupo ndani ya Kristo lakini bado ni vuguvugu, Kristo anamtaka na yeye ayatengeneze mambo yake sawa kabla ya siku za aibu ya milele hazijamfikia..

Ufunuo 3:14 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.

15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.

16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.

17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, NA UCHI.

18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, NA MAVAZI MEUPE UPATE KUVAA, AIBU YA UCHI WAKO ISIONEKANE, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.

19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.

20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.

21 Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.

22 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa”.

Unaona? Mungu anakupenda na anahitaji siku ile uweze kuketi pamoja naye katika kiti chake cha enzi, lakini kama tu leo hii utakuwa tayari kununua kwake mavazi meupe ili aibu ya uchi wako isionekane ambayo hiyo inakuja kwa KUTUBU, yaani kuufungua tu mlango wa moyo wako aingie ndani yako..Fungua tu mlango naye ataingia, anakupenda ndio maana anakuonyesha ndoto kama hizo.

Ubarikiwe.

Group la whatsappJiunge na Group letu ya whatsapp, la masomo ya kila siku kwa kubofya hapa > Group-whatsapp


 

 

Mada Nyinginezo:

KUOTA UNAFANYA MTIHANI.

KUOTA NYOKA.

KUOTA UNASAFIRI.

MTETEZI WAKO NI NANI?

FUATILIA NDOTO HII, UTAJIFUZA KITU.

TOFAUTI KATI YA NDOTO NA MAONO NI IPI?


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Christina Martni
Christina Martni
3 years ago

Asante kwa maneno mazuri naamini kwamba Mungu aliyetupenda upeo atatusaidia nasi tukiwa tayari amina

Jasmini Chisinjila
Jasmini Chisinjila
3 years ago

thank you