JE! UNAYO NAFASI MBINGUNI?

JE! UNAYO NAFASI MBINGUNI?

Umewahi kujiuliza kwanini Bwana Yesu alisema, Anakwenda kutuandalia makao? (Yohana 14:2), Na kwanini mbinguni kunafananishwa na karamuni?…Ni dhahiri kuwa utaratibu wa maandalizi ya karamu unafanana sana na utaratibu wa kuingia mbinguni. Kwahiyo tukizijua tabia za karamu ndio tutajua mbinguni kutakuwaje!

Kwanza Karamu ni lazima iandaliwe, siku gani itafanyika na wapi itafanyikia, na ni lazima iandaliwe kwa kupambwa vizuri, ni lazima pia iwe na vyakula na vinywaji, na ni lazima iwe na ndugu waalikwa…sherehe isiyokuwa na watu hiyo sio sherehe….

Na karamu kama Harusi sio ruhusa kila mtu kuingia, isipokuwa walioalikwa tu! Na ni kwanini sio watu wote wanaruhusiwa kuingia karamuni?..Ni kwasababu ya bajeti!…Waliochangia mara nyingi ndio wanaopewa kadi ya mwaliko. Na sherehe nyingi siku chache kabla ya tukio lenyewe, kadi zote zinakuwa zimeshagawiwa kwa wahusika, na hivyo hakuna nafasi tena ya mtu mwingine kuingia, Idadi ya viti imehesabiwa na Idadi ya watu imeshajulikana, mwingine yeyote akitaka kujichomeka kwenye karamu ile, siku ya Harusi atazuiliwa mlangoni…Na sababu ya kuzuiliwa mlangoni sio kwamba ni kwasababu anachukiwa, au kwasababu ni mtu mbaya sana hapana! Sababu pekee ni kwasababu nafasi yake haipo kwenye karamu hiyo, na hiyo inatokana na pengine hakuchangia, na hivyo akakosa kadi, na hata akiingia nafasi ya kiti hatapata humo ndani kwasababu Kila kitu kipo kwenye mahesabu, hivyo ataishia kuvuruga tu karamu badala ya kuipendezesha.

Kwasababu uwepo wa hiyo karamu ni kutokana na michango ya waalikwa..Gharama zote zimetokana na michango ya waalikwa.

Na katika ufalme wa Mbinguni ni hivyo hivyo… Ufalme wa Mbinguni unajengwa na michango ya Watakatifu. Bwana alipokwenda mbinguni yeye ni kama Mwana-kamati Mkuu, na Mkuu wa Sherehe..Gharama zote za maandalizi, zinatokana na Maisha ya watakatifu huku ulimwenguni…Kila atakayechangia gharama hizo, ndivyo anavyojiwekea nafasi nzuri ya kuwepo ndani ya ile karamu Mbinguni. Ndio maana Bwana Yesu mwenyewe alisema…

Mathayo 11: 12 “Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka”. Kwahiyo kama tunasubiri unyakuo wa ghafla, na hakuna chochote tunafanya kwa ajili ya ufalme wa mbinguni, hicho kitu tuondoe kwenye akili..Watakaonyakuliwa ni wale tu watakaoalikwa, na walioalikwa ni wale waliochangia kitu katika ufalme wa Mbinguni.

Sasa tutachangiaje katika Ufalme wa Mbinguni ili tuweze kuuingia?

Biblia inasema katika kitabu cha Luka..

Luka 10:25 “Na tazama, mwana-sheria mmoja alisimama amjaribu; akisema, Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?

26 Akamwambia, Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje?

27 AKAJIBU AKASEMA, MPENDE BWANA MUNGU WAKO KWA MOYO WAKO WOTE, NA KWA ROHO YAKO YOTE, NA KWA NGUVU ZAKO ZOTE, NA KWA AKILI ZAKO ZOTE; NA JIRANI YAKO KAMA NAFSI YAKO.

28 Akamwambia, Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi”

Kwahiyo Mchango mkubwa unaohitajika ili kujitengenezea nafasi katika Ufalme wa Mbinguni NI UPENDO WA MUNGU NA WA NDUGU..HIZO NDIZO TIKETI!.

Kumpenda Mungu kwa Nguvu zetu zote maana yake unatumia nguvu zako za mwilini na rohoni kutimiza mapenzi ya Mungu..Nguvu zako za ujana ambazo ungepeleka kutatufa mambo ya ulimwengu huu, unazitumia kumtafuta Mungu, Nguvu zako zote unazipeleka katika kuhubiria wengine injili, nguvu zako za kuimba, za kucheza, za kusoma..unazitumia kumwimbia Mungu, kumchezea Mungu, kusoma Neno la Mungu….. wakati huu ambao unaweza kutembea, kukimbia..Ndio wakati wa kukimbia kwenda kuihubiri Injili, wakati huu ambao mwili wako una nguvu na afya, ndio wakati wa kufunga, na kuomba katika kumtafuta Mungu.

Na inaposema Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, maana yake unampenda pasipo unafiki, Unapompenda mtu kwa moyo, huwezi kumuumiza, utajitoa kwake kwa kila kitu, huwezi kufanya jambo ukitazamia malipo, na unapofanya jambo kwa moyo siku zote huwezi kufanya kwa kulazimishwa kwasababu unafanya kwa moyo…. kadhalika tunapaswa tumpende Mungu kwa moyo, ikiwa na maana kuwa hatupaswi kumtafuta kwa kulazimishwa lazimishwa, wala hatutakiwi kufanya kazi yake kwa kusukumwasukumwa..walata hatutakiwi tumtafute kwasababu tunataka fedha kutoka kwake, au tunataka utajiri kutoka kwake, tunamtafuta kwasababu tunampenda kutoka moyoni, kwasababu yeye ni Mungu wetu, na tukimpenda kwa Namna hiyo atahakikisha anatutimizia mahitaji yetu pasipo hata sisi kumwomba kwani anajua tunayohitaji kabla hata hatujamwomba..

Tatu, tunapaswa tumpende Mungu kwa Akili zetu zote, Maana ya kumpenda Mungu kwa akili maana yake ni kutumia akili katika kumtafuta na kumtumikia Mungu..Na akili hiyo inatokana na kulinganisha mambo, unajifunza kuweka mambo mawili kwenye mizani na kuchagua moja lililo na uzito..Kwamfano kununua kiatu cha laki moja na huku huna biblia mkononi, huko ni kutotumia akili, kutokusoma Neno kwasababu huna Biblia na huku una smartphone mkononi mwako, huko pia ni kutokumia akili, kwasababu ungeweza kusoma kwa kutumia hata hiyo hiyo simu yako ya mkononi.. Kushindwa kumjua Mungu kwasababu tu hujakutana na mhubiri wa kukuhubiria barabarani, huko pia ni kutokutumia akili, kwasababu ungeweza kutumia simu yako hiyo hiyo kupata mafundisho yoyote yamhusuyo Kristo katika Mtandao. Kwahiyo kwa ulegevu kama huo unaweza kusababisha kukosa nafasi katika karamu ile.

Na tiketi ya nne ni kumpenda Mungu kwa roho yako yote. Kumpenda kwa roho ni Zaidi ya kumpenda kwa moyo, kwa roho maana yake unampenda mtu kwa utu wa ndani kabisa, (Utu wa Ndani unahusisha Ibada), ukimpenda mtu kwa moyo unakuwa humwabudu, lakini ukimpenda kwa roho ni unafikia kiwango cha kumwabudu….unakuwa tayari kufa hata kwaajili yake na kwaajili ya Injili, unakuwa na shauku ya kumwona Mungu, unakuwa na shauku ya kumwabudu na unakuwa pia na shauku ya kumaliza kazi ya Mungu kwa gharama yoyote ile ili ukamwone uso kwa uso. Kila siku unafikiria namna ya kuimaliza kazi ya Mungu kama alivyokuwa Bwana.

Na mwisho kabisa ni kuwapenda majirani zetu kama nafsi zetu..kama vile unavyojipenda wewe, hakuna hata siku moja umefikiria kujilipizia kisasi au kujisengenya mbele ya mwingine, au kujiangamiza mwenyewe vivyo hivyo tunapaswa tuwapende wale wanaotuzunguka kwa upendo wa viwango hivyo hivyo.

Vigezo hivyo vitano ndivyo vinavyotumika kuandaa nafasi za Wateule karamuni, mambo hayo 5 ndio kadi ya mwaliko…Kila mmoja, haijalishi ni Mtume,mchungaji, mwalimu, mwinjilisti, mwimba kwaya,Nabii, mpiga gitaa kanisani, au msafisha choo cha kanisa, au mtunza bustani wa kanisa…ni Lazima afanye mambo hayo ili aurithi uzima wa milele, ili aingie karamuni…Vigezo hivyo vitano ndio vinavyotumika kutengeneza kadi ya mwaliko wa kuingia kwenye mji ule.

Ndio maana Bwana Tangu wakati ule mpaka leo bado anaandaa makao…kila kizazi watu watu wajiingiza kwa nguvu, wanatengeneza tiketi zao na kujitwalia nafasi. Kila kizazi watu wanajiingiza kwa nguvu…Hakuna nafasi za watu wasiojishughulisha na ufalme wa Mbinguni.

Luka 16:16 “Torati na manabii vilikuwapo mpaka Yohana; tangu wakati huo habari njema ya ufalme wa Mungu hutangazwa, na kila mtu hujiingiza kwa nguvu”.

Je! Na wewe umealikwa?..Unayo Kadi yako mkononi? Unayo nafasi katika ufalme wa Mbinguni? Umeingia kwa nguvu? Au unaendelea na matendo mabaya ya giza na huku unasubiria unyakuliwe?.. Biblia inasema pia waovu wana sehemu yao katika lile ziwa la moto, ikiwa na maana kuwa, hata kuzimu nako watu wanajitengenezea nafasi zao kule kuanzia sasa.

Ufunuo 21:8 “ Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili”.

Kama hujampa Kristo masha yako, mlango upo wazi sasa, Lakini upo karibuni kufungwa, karamu inakaribia kuanza, fanya hima upate kadi ya mwaliko, kwa kutubu dhambi zako zote, kubatizwa na kuishi kwa vigezo hivyo vitano hapo juu.

Bwana akubariki sana.

Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group


Mada Nyinginezo:

TAZAMA, NASIMAMA MLANGONI.

RUDIA, TENA NA TENA KUMWOMBA MUNGU USIKATE TAMAA.

MATUNDA YAPATANAYO NA TOBA!

JE! ADAMU ALIWASALIANA NA MUNGU KWA LUGHA IPI PALE BUSTANINI?

JE! KUCHORA TATTOO NI DHAMBI?


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
patrick
patrick
1 year ago

napenda kujifunza neno la mungu