EPUKA KUPELELEZA KILA KITU MUNGU ANACHOKUAHIDIA.

EPUKA KUPELELEZA KILA KITU MUNGU ANACHOKUAHIDIA.

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, nakukaribisha katika kuyatafakari maneno ya uzima ya Mungu wetu, Karibu sana.

Jambo ambalo tunapaswa tuwe makini nalo, ni kuchunguza chunguza au kupeleleza peleleza ahadi ambazo Mungu anatuahidia katika maisha yetu. Sio kwamba kupeleleza ni kubaya, hapana, lakini matokeo ya kufanya hivyo ni kuwa tutakayokutana nayo  yatakuja kinyume na matazamio yetu, na mwisho wa siku tukavunjika mioyo, na kupelekea hata kumuudhi Mungu, hadi kughahiri kutupa alichotuahidia.

Ili kulielewa hilo, tusome mfano mmoja wa wana wa Israeli, ambao tunajua wao walipotoka Misri, Mungu aliwaongoza jangwani kwa muda mfupi sana, sasa wakati wanakaribia kuingia katika ile nchi ya ahadi ambayo Mungu aliwaahidia kuwa ni nchi yenye kububujika maziwa na asali, wao hawakutulia kwenda na Mungu mpaka dakika ya mwisho, badala yake, wakataka kuharakisha mambo.

Hivyo walichokifanya ni kumwendea Musa, na kumwambia, awapelekee watu wakaipeleleze ile nchi, waone kama ni kweli Mungu alichowaahidia ndicho kilichopo au la. Kumbuka agizo hilo Mungu hakuwapa, bali ni wao wenyewe waliliwaza, na kumwambia Musa, baadaye Mungu ndio akawapa ruhusu kwa kumwagiza Musa awafanyie hivyo, lakini Mungu hakuliagizo hilo jambo,.

Sasa kama wengi tunavyojua habari, ni kweli waliona uzuri wa ile nchi, wakakiri kabisa ni nchi nzuri yenye kuvutia, lakini hakukuwa na uzuri tu peke yake, bali kulikuwa  pia na vitisho vingine vingi sana nyuma yake, hadi ule uzuri wote ukafunikwa na hayo mabaya..Mambo yakawa kinyume chake, wana wa Israeli badala ya kufurahia kwa wema waliouona wakaomboleza kwa mabaya, na misiba, na vifo walivyoviona mule, jinsi wale watu walivyowakubwa sana, wenye nguvu, wenye teknolojia ya hali ya juu, wenye silaha kubwa za kivita. Lakini jambo hilo likamuudhi sana Mungu, hadi akawaapia kuwa wote waliotoka Misri watakufa, hawataiona hiyo nchi,  isipokuwa Yoshua na Kalebu tu.

Wakamsababishia hadi na Musa naye kukasirikiwa na Mungu, na yeye pia akaambiwa atakufa.

Kumbukumbu 1:22 “Nanyi mkanikaribia kila mmoja wenu, mkasema, Na tupeleke watu mbele yetu, ili watupelelezee nchi na kutuletea habari za njia itupasayo kuipandia, na za miji tutakayoifikia.

23 Neno hili likanipendeza sana; nikatwaa watu kumi na wawili, mtu mmoja wa kila kabila.

24 Nao wakageuka, wakapanda mlimani wakafika bonde la Eshkoli, wakalipeleleza.

25 Wakatwaa baadhi ya matunda ya nchi ile mikononi mwao, wakatuletea huku chini, wakatuletea habari tena, wakasema, Nchi hii anayotupa Bwana, Mungu wetu, ni nchi njema.

26 Lakini hamkukubali kukwea huko, mlihalifu neno la Bwana, Mungu wenu;

27 mkanung’unika hemani mwenu, mkasema, Ni kwa sababu Bwana ametuchukia, ndipo akatutoa katika nchi ya Misri, apate kututia katika mikono ya Waamori, ili kutuangamiza.”;…………..

34 Bwana akaisikia sauti ya maneno yenu, akaghadhibika, akaapa, akasema,

35 Hakika yangu hapana mmoja miongoni mwa watu hawa wa kizazi hiki kibaya atakayeiona nchi hiyo nzuri, niliyowaapia baba zenu kuwapa,

36 isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, huyo ataiona; nami nitampa yeye na watoto wake nchi hiyo aliyoikanyaga; kwa kuwa amemfuata Bwana kwa kila neno.

37 NA BWANA ALINIKASIRIKIA MIMI KWA AJILI YENU, akasema, Wala wewe hutaingia humo;

Sasa hiyo yote ni kutufundisha kuwa,  Sio kwamba Mungu anachukizwa na sisi, kupeleleza ahadi alizotuahidia, lakini hatari yake ni kuwa, zipo katikati ya uharibifu. Mungu huwa anaficha Baraka zake, katika mazingira ya kushangaza sana,wakati mwingine katika vifungo, na dhiki, na magonjwa, na taabu, na mateso. Na ndio maana anataka watu wake sikuzote waishi kuwa imani ya kumtegemea yeye tu.

Embu mwangalie Yusufu, alionyeshwa kuwa ndugu zake watakuja kumwinamia, sasa kama angeishi kwa kudhani jambo hilo litatokea katika raha sikuzote ghafla bin vuu.. Hakuna  kuuzwa na ndugu zake, hakuna kufungwa kwenye magereza ya mfalme miaka ya kutosha, hakuna kuwa mtumwa  wa mtu mwingine kwa muda mrefu, angeshamwacha Mungu siku nyingi sana.

Vivyo hivyo na wewe, uliyeokoka, Ahadi zote na Baraka zote ambazo Mungu aliahidi kwa wateule wake wote waliomwamini, zitakuja tu kwa wakati wake, Pengine Mungu alikuonyesha atakutumia katika viwango vingine vya kiutumishi, au atakupatia vya mwilini kama vile, fedha, nyumba, mali, n.k. Usichunguze chunguze ni lini, usifikiri fikiri mema tu muda wote, kuwa  hapo katikati (Neutral), mtegemee Mungu katika kila hali, kwasababu unaweza kumbana leo na mikosi, ukadhani Mungu hayupo na wewe, kumbe ndio njia ya kuelekea maono yako.

Bwana atusaidie tujue kutembea katika kanuni zake za kiroho.

Mungu akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Kwanini Mungu aliwaagiza wana wa Israeli wasikisaze chakula?

WAISRAELI WENGI SANA WANARUDI KWAO SASA.

Kwanini Paulo aungane na wale watu wanne wenye nadhiri?

UFUNUO: Mlango wa 17

MBINGU MPYA NA NCHI MPYA. (Sehemu ya 1)

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Devis Julius administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments