Kwanini Mungu aliwaagiza wana wa Israeli wasikisaze chakula?

Kwanini Mungu aliwaagiza wana wa Israeli wasikisaze chakula?

SWALI: Kwanini Mungu aliwaagiza wana wa Israeli siku ile ya kuondoka wasikisaze chakula hata asubuhi?


JIBU: Kusaza chakula maana yake ni kukibakisha ili ukimalizie kukila baadaye au kesho yake…Na hiyo inaweza kutokana na mtu kushiba sana wakati huo, hivyo badala ya kukimwaga anakuwa anakihifadhi hicho chakula ili akimalizie kukila tena wakati mwingine.

Kama tunavyojua siku ile wana wa Israeli walipokuwa wanatoka Misri, Mungu aliwapa maagizo kuwa usiku ule kabla ya kuondoka wamchinje mwanakondoo, na damu yake waipake kwenye miimo ya milango, na kisha wamle yule mwanakondoo waliomchinja, (na maagizo hayo yaliihusu kila familia), hivyo kila familia ilichinja mwanakondoo na damu yake kuipaka milangoni, na kumla yule mwanakondoo..Na yalikuwepo pia maagizo ya namna ya kumpika, utaona waliambiwa wasimtokose majini, yaani wasichemshe(wasile mchemsho), bali wamuoke motoni..vilevile  wamle pamoja na mboga chungu, na kwa haraka sana maana yake wasijivutevute wakajikuta kumepambazuka na bado hawajamaliza kula ikawa dhambi.

Sasa pamoja na maagizo yote hayo walipewa agizo lingine tena la msingi, kwamba Huyo mwanakondoo watakayemla, kila familia ihakikishe haisazi nyama yake mpaka asubuhi, maana yake ni kwamba aidha wamle wote amalizike, au wamle mpaka pale watakapoona wameshiba na kama  bado nyama ipo, basi waitwae ile nyama na waiteketeze kwa moto, kisisalie chochote kabla hakujapambazuka..Maana yake ni kwamba kama kuna familia haitafanya hivyo, itakuwa imetenda dhambi kwa Bwana Mungu. Unaweza kuyasoma maagizo hayo vizuri katika kitabu cha (Kutoka 12:1-13).

Sasa ni kwanini Mungu alitoa hayo maagizo?

Sababu ni  kwamba Bwana alikuwa ameanza kuwafundisha wana wa Israeli wamtegemee yeye kwa asilimia mia moja. Kwamba wasiwe na hofu ya kesho, watakula nini, watavaa nini.. bali akili zao zote zianze kumfikiria yeye. Kwasababu asingefanya hivyo, watu usiku ule ule wangekula kidogo na kusema tuache kingine kwaajili ya kesho asubuhi kunywea chai, hivyo wangeanza kufikiri matumbo zaidi ya kumfikiria Mungu.

Na pia utazidi kuona Mungu hata ile MANA ambayo walikuwa wanalishwa iliyotoka mbinguni, Bwana Mungu aliwakataza wasiweke akiba, wala wasiisaze, aliwaambia wakusanye chakula cha siku moja, wakile wakimalize chote wasikisaze wakile tena kesho, kwasababu hiyo kesho Mungu atawapa kingine..hivyo wasiwe na hofu ya kesho kwamba watakula nini?..Lakini baadhi yao hawakuitii sauti ya Mungu, wakawa wanakisaza matokeo yake vikatoa uvundo..

Kutoka 16:19 “Musa akawaambia, Mtu awaye yote asikisaze hata asubuhi.

20 Lakini hawakumsikiza Musa; wengine miongoni mwao wakakisaza hata asubuhi, nacho kikaingia mabuu na kutoa uvundo; Musa akawakasirikia sana.

21 Basi wakaokota asubuhi baada ya asubuhi, kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa; na hapo jua lilipokuwa ni kali, kikayeyuka”

Jambo hilo hilo ni somo kwetu, kwamba Tusiwe na hofu sana kuhusu maisha yetu, baada ya kuokoka.. Hatupaswi kuwa na hofu ya kupitiliza kuhusu kesho zetu, kwamba tutakula nini, au tutavaa nini, hata kama leo tunaona hakuna dalili ya kuiona hiyo kesho.Bado tunapaswa kufahamu kuwa ya kesho itajisumbukia, na Mungu atafungua mlango tu. Kama Bwana Yesu alivyosema mahali fulani..

Mathayo 6:31  “Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini?

32  Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote.

33  Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.

34  Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake”.

Baba yetu anajua tuna haja na hayo yote, hawezi kutuokoa na kutuacha yatima kabisa..yupo pamoja na sisi kuhakikisha anatuhudumia kwa mahitaji yetu ya kila siku.

Sasa kama umeona ni wakati wa kuweka akiba sasa iweke, hufanyi dhambi, lakini jiangalie jinsi unavyojiwekea hiyo akiba, kwasababu kama utajiwekea akiba na huku moyoni mwako Mungu umemwacha, na huku tumaini lako lote lipo katika hiyo akiba yako uliyojiwekea, utapotea kama yule Tajiri wa kwenye Luka 16:19.

Lakini kama utajiwekea akiba kulingana na mapenzi ya Mungu, basi utafanikiwa…

Sasa swali utajiwekeaje akiba sawasawa na mapenzi ya Mungu ?

Turudi kwenye huo mfano wa Mana. Ukiendelea kusoma mbele kidogo utaona akiba iliyompendeza Mungu ilikuwa ni ipi..Tusome.

Kutoka 16: 21 “Basi wakaokota asubuhi baada ya asubuhi, kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa; na hapo jua lilipokuwa ni kali, kikayeyuka.

22 Basi ikawa siku ya sita wakaokota kile chakula sehemu maradufu, kila mtu pishi mbili; na wazee wote wa mkutano wakaenda na kumwambia Musa.

23 Akawaambia, Ndilo neno alilonena Bwana KESHO NI STAREHE TAKATIFU, SABATO TAKATIFU KWA BWANA; OKENI MTAKACHOOKA, NA KUTOKOSA MTAKACHOTOKOSA; NA HİCHO KITAKACHOWASALIA JİWEKEENI KILINDWE HATA ASUBUHI.

24 Basi wakakiweka hata asubuhi, kama Musa alivyowaagiza; NACHO HAKİKUTOA UVUNDO WALA KUINGIA MABUU.

25 Musa akasema, Haya, kuleni hiki leo; kwa kuwa leo ni Sabato ya Bwana; leo hamtakiona nje barani”.

Umeona hapo?.. Walipojiwekea akiba ili kwamba kesho yake (ambayo ni siku ya sabato), wasiwe bize kutafuta hicho chakula,ILA WAWE BIZE KUMTAFUTA MUNGU..Hapo ndipo akiba yako haikuoza, Na ndiyo akiba iliyompendeza Mungu, ndio maana hicho walichokiweka akiba hakikutoa uvundo kesho yake. Lakini pale walipojiwekea akiba kwa lengo la kujikusanyia hazina ya kesho, ili wastarehe tu ndani, kesho yake wasitoke kwenda kutafuta, wakafanye anasa, walale, wacheze, waruke, wafurahi, wacheze cheze kidogo, hapo ndipo akiba yao ilipoingia mabuu..

Hivyo na sisi akiba zinazompendeza Mungu, ni zile tutakazosema…Leo nitafanya kazi sana, au wiki hii yote nitatumia muda mwingi kufanya kazi sana, na kukusanya akiba ya wiki mbili…kwasababu wiki inayokuja yote nitakuwa bize kuomba, au nitakuwa bize kuhubiri, sitapata muda wa kushughulika…Ukiweka akiba kwa malengo hayo, hapo ndipo akiba hiyo inakuwa haiozi, na zaidi ya yote Mungu anafungua milango ya baraka mara mbili zaidi sasa.. Lakini akiba ya kujiwekea mali nyingi, na huku huna malengo yoyote na Mungu, akiba hiyo inaoza, unaweka akiba ili wiki ijayo upate muda wa kulala, upate nafasi ya kwenda disko, ili utakapokuwa mzee upumzike, utakapokuwa, uwe tajiri sana wa kuheshimika, hata mpaka jumapili huendi kanisani, … Kesho utaamka haipo, imepukutika yote, hiyo miaka itafika utaikuta hiyo akiba imeingia mabuu na inatoa uvundo.

Luka 12: 16  “Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana;

17  akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu.

18  Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu.

19  Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi.

20  Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?

21  NDIVYO ALIVYO MTU AJIWEKEAYE NAFSI YAKE AKIBA, ASIJITAJIRISHE KWA MUNGU”.

Bwana atusaidie na kutubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312 Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments