Raheli aliwalilia vipi watoto wake?

Raheli aliwalilia vipi watoto wake?

Shalom ni Raheli yupi aliyekuwa anawalilia watoto wake?, na Watoto hao ni wakina nani? Na kiliwatokea nini?.. (Yeremia 31:15 na Mathayo 2:18).

Jibu: Tusome,

Yeremia 31:15 “Bwana asema hivi, Sauti imesikiwa Rama, kilio, na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake; asikubali kufarijiwa kwa watoto wake, kwa kuwa hawako”

Katika Unabii huo kuna vitu viwili vya kuzingatia navyo ni “Rama” na “Raheli”..Tukianza na Raheli, huyu kama inavyojulikana alikuwa ni Mke wa Yakobo..Na ndiye mke wa ahadi ambaye Yakobo alimpenda kuliko wengine wote.

Na “Rama” ni mtaa uliokuwa ndani ya mji wa Bethlehemu, ambao tutakuja kuona mbele kidogo ulitumika wapi kutimiza unabii huo wa Yeremia.

Sasa Raheli mke wa Yakobo, ni mwanamke aliyekufa mapema kabla kabla ya kuona hata Baraka za watoto wake (Yusufu na Benyamini), Na alikufa akiwa katika uchungu wa kuzaa Benyamini….. Na maandiko yanasema alipokufa alizikwa katika mji wa Bethlehemu…ambao ndio ule ule mji aliokuja kuzaliwa Bwana Yesu, miaka mingi baadaye.

Mwanzo 35: 19 “Akafa Raheli, akazikwa katika njia ya Efrathi, ndio Bethlehemu”.

Kwahiyo kwasababu Raheli, alikuwa ni mwanamke aliyemcha Mungu kuliko wake wengine wote wa Yakobo, na ndiye aliyekuwa mke wa ahadi, na alikufa pasipo kuziona Baraka za wanawe..hivyo kwasababu yake yeye, pale mahali alipokufa na kuzikwa, Bwana alipatukuza kwa heshima yake, na kupafanya kuwa mji atakaokuja kuzaliwa mwokozi wa ulimwengu, Yesu Kristo, miaka mingi baadaye..

Mika 5:2 “Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele”.

Na pia Mathayo 2:6 inazungumzia jambo hilo hilo..

Mathayo 2:4 “Akakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao, Kristo azaliwa wapi?

5 Nao wakamwambia, Katika Bethlehemu ya Uyahudi; kwa maana ndivyo ilivyoandikwa na nabii,

6 Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda; Kwa kuwa kwako atatoka mtawala Atakayewachunga watu wangu Israeli”.

Kwahiyo Bethlehemu ulipata hadhi hiyo na neema hiyo kufuatia huyu mke wa Yakobo (Raheli). Hivyo Raheli ndio akawa kama nembo ya mji wa Bethlehemu katika roho. Kama vile Daudi alivyokuwa nembo ya mji wa Yerusalemu.

Sasa tukirudi kwenye huo unabii wa Yeremia unaosema..

Yeremia 31:15 “Bwana asema hivi, Sauti imesikiwa Rama, kilio, na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake; asikubali kufarijiwa kwa watoto wake, kwa kuwa hawako”

Wakati Yeremia anatangaza maneno haya, tayari Raheli alikuwa ameshakufa miaka mingi sana na kuzikwa hapo Bethlehemu, lakini kuna tukio la kipekee lilitokea katika mji wake huo aliozikwa.. Kwani wakati Nebukadneza anaiteketeza Yerusalemu, kwa kuwaua watu kikatili, watoto kwa wazee, wanaume kwa wanawake..lilibakia kundi dogo ambalo halikuuawa, badala yake lilifungwa na kupelekwa Babeli utumwani.

Sasa kituo kilichotumika kuwakusanya hao mabaki machache ambayo hayajauawa, tayari kwa kupelekwa utumwani.. kilikuwa ni huo mtaa mdogo ulioutwa “RAMA”, hapo Bethlehemu katika mji huo wa Raheli. Na baada ya kukusanywa na kufungwa kwa siku kadhaa, ndipo wakaondolewa na kuanza safari ya kupelekwa utumwani Babeli..

Yeremia 40:1 “Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, baada ya wakati ule Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, ALIPOMWACHA AENDE ZAKE TOKA RAMA, baada ya kumchukua hali ya kufungwa minyororo, pamoja na wafungwa wote wa YERUSALEMU NA YUDA, WALIOCHUKULIWA HALI YA KUFUNGWA MPAKA BABELI”.

Wakati wanaondoka, ile ahadi ambayo Mungu aliiahidi pale Bethlehemu kwaajili ya Raheli, ikawa inamlilia Mungu katika roho, pale mabaki ya wana wa Israeli walipokuwa wanaondolewa…na ahadi ile, ndio kama “Sauti ya Raheli”…kama vile “sauti ya damu ya Habili ilivyokuwa inamlilia Bwana kutoka katika ardhi, baada ya Kaini ndugu yake kumuua (Soma Mwanzo 4:10) ”

Yeremia 31:15 “Bwana asema hivi, Sauti imesikiwa Rama, kilio, na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake; asikubali kufarijiwa kwa watoto wake, kwa kuwa hawako”

Lakini ukiendelea kusoma utaona Bwana anatoa faraja, kuwa watoto wake watarudi tena (maana yake Israeli watarudishwa tena katika nchi yao kama mwanzo, Yeremia 31:16-17).

Sasa hiyo ni sehemu ya kwanza ya unabii huo, kwani wakati ulipofika kweli Israeli walirudishwa katika nchi yao, baada ya ile miaka 70 waliokaa utumwani Babeli.

Lakini wakati wa Bwana Yesu kuzaliwa, kuna jambo lingine tena lilitokea kama hilo hilo..likafanya unabii huo kujirudia tena..

Bwana alivyozaliwa huko Bethlehemu Herode alitafuta kumuua, lakini alishindwa kwani Mariamu na Yusufu waliondoka pamoja na mtoto kwenda Misri..na kumfanya Herode akasirike na kwenda kufanya mauaji katika ule ule mji wa Raheli, (Bethlehemu), kwani alianza kuua watoto wote walio chini ya umri wa miaka miwili, na kufanya sauti ile ile ya Raheli irudi, kama ilivyosikika wakati wa kwanza Israeli wanachukuliwa utumwani..

Mathayo 2:16 “Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi.

17 NDIPO LILIPOTIMIA NENO LILILONENWA NA NABII YEREMIA, AKISEMA,

18 SAUTI ILISIKIWA RAMA, KILIO, NA MAOMBOLEZO MENGI, RAHELI AKIWALILIA WATOTO WAKE, ASIKUBALI KUFARIJIWA, KWA KUWA HAWAKO”.

Sasa endapo tukio hilo lingetokea mahali pengine, au kwenye mji mwingine kama Yerusalemu..pengine asingetajwa Raheli  tena, pengine ingekuwa  Daudi au mtu mwingine, lakini kwasababu ni Bethlehemu, hakuna budi awe Raheli aliyekuwa kama nembo ya mji ule.

Hiyo inatufundisha nini?

Unabii wa Mungu unaweza kutimia zaidi ya mara moja..Neno la Mungu halina tarehe ya kuisha matumizi (expire date). Hapo tunaona unabii mmoja umetimia vipindi viwili tofauti..Kadhalika na nabii nyingine zote, hazina mwisho wa muda wa matumizi..Kwa nafasi yako unaweza kusoma (Hosea 11:1 na Mathayo 2:15), utaona jinsi unabii mmoja unavyoweza kutimia vipindi viwili tofauti.

Biblia inaposema kutatokea mpinga-Kristo siku za mwisho..hatuna kufahamu kuwa hilo neno tayari linatimia sasa hata kabla ya kumfikia huyo mpinga kristo mmoja aliyetabiriwa, maana yake, wapinga-kristo wapo hata sasa…

1Yohana 2:18 “Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho”.

Vile vile unabii wa Yuda kumsaliti Bwana, uliotabiriwa katika Zaburi 41:9, haukutimia kwa Yuda tu, ukaishia pale, hapana!.. bali pia unaendelea kutimia mpaka sasa. Sio kwamba Yuda alikuwa na bahati mbaya sana kuliko sisi..wala unabii huo hakuandikiwa yeye peke yake. Na kwamba ulishatimia juu yake na hauwezi kujirudia tena..

 Nataka nikuambie katika siku zetu hizi za mwisho watakuwepo watu wenye hatia kubwa ya kumsaliti Bwana kuliko hata Yuda, na watakuwa wametimiza hilo andiko la Zaburi 41:9. Hivyo hatuna budi kuongeza umakini katika Ukristo wetu, ili tusiwe sehemu ya kutimiza maandiko mabaya bali yale mazuri.

Luka 13:1 “Na wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao.

2 Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo?

3 Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.

4 Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua, mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu?

5 Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo”.

Mwisho kama bado hujatubu na kumpokea Yesu, fahamu kuwa hizi ni siku za mwisho, na Kristo yupo mlangoni kurudi..jiulize akija leo, atakukuta katika hali gani?..je tumaini lako ni nini?..ni mali?, ni mke? ni watoto? Au ni nini?…Bwana mwenyewe alisema… “Itakufaidia nini upate kila kitu halafu upate hasara ya nafsi yako”?

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Nini maana ya Dirii, Chepeo na Utayari?

KUJIFUNUA KWA YESU KWA PILI.

KWANINI NI YESU KRISTO WA NAZARETI?

JE UMEJIANDAA KUTIMIZA UNABII UPI?

BASI, IWENI NA HURUMA, KAMA BABA YENU ALIVYO NA HURUMA

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Matilda
Matilda
1 year ago

Shalom. Kwa nini Raheli aliiba miungu ya baba yake ?