KUJIFUNUA KWA YESU KWA PILI.

KUJIFUNUA KWA YESU KWA PILI.

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe daima. Ni wasaa mwingine tena ambao Mungu ametujalia kuufikia hivyo  nakukaribisha tuyatafakari  kwa pamoja maneno ya uzima ndugu yangu.

Biblia inatuambia kuwa Bwana Yesu alipofufuka kutoka kwa wafu, aliwatokea baadhi ya watu, ambao idadi yao ilikuwa kama  watu 500,(1Wakorintho 15:6) , Lakini ulishawahi kujiuliza ni kwanini iwe hivyo? Je hao watu 500 walikuwa na kitu gani cha ziada kuwashinda wengine wote mpaka watokewe wao tu?

Ni vizuri tukafahamu kuwa hii ni kawaida ya Kristo, kwamba kuna wakati  ataonekana na watu wote, lakini pia upo wakati hataonekana  na watu wote bali wachache tu aliowachagua, Na ndicho kilichotokea hapa, miaka yote 33 aliyoishi duniani, kila mtu angeweza kumtembelea kama angetaka, kila mtu angeweza kwenda kumtazama kama angetaka, lakini mara baada ya kufufuka kwake, hakuna mtu yeyote angeweza kumwona, isipokuwa Yule tu aliyejidhihirisha kwake.

Na ndio maana aliwaambia wayahudi maneno haya Yohana 7:34 “Mtanitafuta wala hamtaniona; nami nilipo ninyi hamwezi kuja”.

Sasa hawa watu 500 ambao walipata neema ya kumwona Yesu baada ya kufufuka kwake, hawakuwa ni watu tu ambao bahati imewaangukia, hawana habari na Yesu, au hawajawahi kumfuatilia au kumsikia,.. Hapana, biblia inatuambia walikuwa ni watu ambao waliambatana naye, tangu akiwa Galiliya mpaka Yerusalemu, yaani tangu ncha moja ya taifa la Israeli mpaka ncha nyingine ya Israeli.

Matendo 13:29 “Hata walipokwisha kumaliza yote aliyoandikiwa, wakamtelemsha katika ule mti, wakamweka kaburini.

30 Lakini Mungu akamfufua katika wafu;

31 akaonekana siku nyingi na wale WALIOPANDA NAYE KUTOKA GALILAYA HATA YERUSALEMU, ambao sasa ndio walio mashahidi wake mbele ya watu”.

Hawa ndio waliotokewa na Yesu mara ya pili, Ni watu ambao walitembea na Yesu, tangu zamani sana, ni watu ambao waliokuwa wanazungumzia habari zake, Mfano wake utaona ni wale watu wawili waliokuwa wanaelekea kile kijiji cha Emau baada ya kufufuka kwake(Luka 24:13)..

Hao ndio watu ambao Yesu aliona kuna umuhimu wote wa kuwatokea  katika utukufu mwingine baadaye. Siku zote wale wanaomuheshimu Mungu, Mungu nao anawaheshimu, wanaomkaribia Mungu, Mungu naye anawakaribia wao.(Yakobo 4:8). Na mmojawapo kati ya hawa ndiye aliyefanywa mtume kuchukua nafasi ya Yuda.

Sasa kutokea kwake mara ya pili kwao, haikuwa maonyesho tu. Bali Kristo aliwapa karama nyingine ambayo iliwafanya kuwa tofauti kabisa na watu wengine. Na karama yenyewe ni kuwa MASHAHIDI WA YESU.  Hao ndio waliochaguliwa na Mungu kuisambaza injili ya Kristo ulimwenguni kote, kwa nguvu za Roho wa Mungu zilizoachiliwa juu yao,

Matendo 10:40 “Huyo Mungu alimfufua siku ya tatu, akamjalia kudhihirika,

41 SI KWA WATU WOTE, BALI KWA MASHAHIDI WALIOKUWA WAMEKWISHA KUCHAGULIWA NA MUNGU, NDIO SISI, TULIOKULA NA KUNYWA PAMOJA NAYE BAADA YA KUFUFUKA KWAKE KUTOKA KWA WAFU.

42 Akatuagiza tuwahubiri watu na kushuhudia ya kuwa huyu ndiye aliyeamriwa na Mungu awe Mhukumu wa walio hai na wafu”.

Soma pia Matendo 2:31-32

Unaona Ikiwa leo hii, hatutaki kujibidiisha kumtafuta Yesu, hatutaki kujifunza Neno lake, hatutaki kusikia habari zake,tunaona kama zinatuchosha, na bado tunasema tumeokoka, tufahamu kuwa, zipo hatua ambazo kamwe hatutakaa tumfikie Yesu.

Tunakosa shabaha pale tunapodhani kumjua Yesu ni kuokoka tu, na kutoa pepo halafu basi. Hatujui kuwa YESU NDIO SIRI YA MUNGU mwenyewe.. ambao utimilifu wote wa Mungu unakaa kwa namna ya kimwili (Wakolosai 2:9). Kiasi kwamba tukifikia utimilifu wote wa kumjua yeye, basi hakuna kitu chochote hapa duniani tutakachoshindwa kufanya, au kukijua.  Na shetani hapa ndipo anapopapiga vita, kwasababu anajua siku mtu akimfahamu Yesu ipasavyo basi habari yake ndio imeishia hapo.

Waefeso 4:13 “hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;

14 ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu”.

Kwahiyo na sisi tuonyeshe bidii ya kutafuta kumjua yeye, nasi tufikie hatua ya kutufanywa na mashahidi wake kweli kweli , kama alivyofanya kwa mitume wake na wale wengine mwanzoni.

Lakini tukiridhika na Yesu wa kuokokea tu, vivyo hivyo na yeye atajifunua kwetu kama huyo, lakini tukionyesha bidii ya kumtafuta, na kutaka kujua njia zake, na yeye atajifunua kwetu katika nguvu za kufufuka kwake, tutamjua kwa mapana na marefu yake, kama alivyofanya kwa wale watu wachache sana (500). Tutakuwa watu wengine kabisa.

Tuanze kulipigia hatua na hili.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

KUNA MAJIRA MUNGU ATAIVURUGA MIPANGO YETU.

Nini maana ya “mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili”?

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

Mafundisho

Mataifa ni nini katika Biblia?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments