Mataifa ni nini katika Biblia?

Mataifa ni nini katika Biblia?

Watu wa mataifa mengine yote ya ulimwengu tofauti na Taifa la Israeli, ndio wanaojulikana kama “watu wa Mataifa”.

 Mungu alipoanza mpango wake wa kurejesha uhusiano wake na mwanadamu ambao ulipotea tangu pale Edeni, alianza na Taifa moja tu lijulikanalo kama “Israeli”, Na Taifa hili lilianza na mtu mmoja ajulikanaye kama Ibrahimu, ambaye huyu Ibrahimu akamzaa Isaka,.Isaka akamzaa Yakobo, Yakobo akazaa Watoto 12, na kwa kupitia majina ya Watoto hao ndipo yakazaliwa majina ya makabila 12 ya Israeli. Na hao Watoto wakazaa wana, na hatimaye likawa jeshi kubwa la watu wengi wa jamii ya Israeli, na kuwa Taifa.

Sasa watu wengine wote tofauti na uzao huo wa Ibrahimu, ndio watu wa mataifa. Kwasababu duniani kulikuwa na watu wengine wengi wa jamii nyingi, walikuwepo waMisri (ambao ndio sasa nchi ya Misri), walikuwepo waashuri (Ambao kwasasa ni maeneo ya Syria), walikuwepo wakushi (ambao sasa ni maeneo ya huku Afrika)..walikuwepo Wakaldayo (ambao sasa ni maeneo ya Iraq), walikuwepo watu wa bara la Hindi (ambao sasa ndio India), walikuwepo watu wa Uajemi na Umedi ambao ndio kwasasa maeneo ya (Kuwait,Qatar, UEA{Dubai} na sehemu za magharibi ya Saudi Arabia), walikuwepo Warumi (ambao sasa ndio Italy), walikuwepo Wayunani (kwasasa ni Ugiriki) na mataifa mengine mengi (Yote hayo yalijulikana kama Mataifa).

Sasa Mungu amekuwa akitembea na Taifa la Israeli pekee Kwa miaka Zaidi ya 1,500, wakati huo wote Mungu hakushughulika na hayo mataifa mengi yote (haijalishi yalikuwa yameendelea kiasi gani au yalikuwa yana watu wazuri kiasi gani). Taifa lake teule na pekee lilikuwa ni moja tu ambalo ni Israeli, ndio maana utaona Amri 10, walipewa Israeli na si watu wa Mataifa mengine, na agano lote la kale inahusu Habari za wana wa Israeli mwenendo wao na Mungu wao.

Sasa sio kwamba Mungu alikuwa hana mpango kabisa na watu wa Mataifa!. La! Alikuwa ana mpango nao mkubwa sana. Lakini siku zote hakiwezi kuzaliwa cha pili, kabla ya kuzaliwa cha kwanza, hawezi kunyonya mtoto wa pili kabla hajanyonya wa kwanza, hawezi kukumbatiwa mtoto wa pili kabla ya wa kwanza. Hata mama anayejifungua Watoto, ni lazima azaliwe mtoto wa kwanza, ndipo afuate wa pili… Na yule wa kwanza atapendwa na kutunza kabla ya yule wa pili.

Kwahiyo Taifa la Israeli ni mzaliwa wa kwanza kwa Mungu, na watu wa mataifa ni mzaliwa wa pili..

Kutoka 4: 22 “Nawe umwambie Farao, Bwana asema hivi, Israeli ni mwanangu mimi, mzaliwa wa kwanza wangu;

23 nami nimekuambia, Mpe mwanangu ruhusa aende, ili apate kunitumikia, nawe umekataa kumpa ruhusa aende; angalia basi, mimi nitamwua mwanao, mzaliwa wa kwanza wako”.

Hivyo ulipofika muda wa “mzaliwa wa pili  kuzaliwa, (yaani wakati wa watu wa mataifa nao kukumbukwa na Mungu). Mungu alianza mpango wake huo kwa kumleta Mwanawe mpendwa Yesu Kristo, awe sababu ya wokovu kwa watu wote wa mataifa.

Kama kuku aliyeacha vifaranga vyake vya kwanza, kwa kuvidonoa na kuanza malezi mapya ya uzao wa pili, Ndicho alichokifanya Mungu kwa Israeli, Neema iliondoka kwao na kuhamia kwa watu wa mataifa (yaani mimi na wewe).

Warumi 11:25 “ Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili”.

Tangu wakati wa Bwana Yesu mpaka sasa, watu wa mataifa yote..tunaweza kumkaribia Mungu, na kuzirithi baraka zile zile za rohoni, kama walizokirimiwa Israeli.

Hiyo ndiyo SIRI YA MUNGU, ambayo ilifichwa kwa miaka mingi, ambayo hata wana wa Israeli wenyewe hawakujua kwamba ingefika siku moja, watu wa Mataifa nao watapata upendeleo kwa Mungu kama wao.

Paulo ambaye ni Muisraeli aliiandika siri hiyo kwa ufunuo wa Roho na kusema..

Waefeso 3:4  “Kwa hayo, myasomapo, mtaweza kuutambua ufahamu wangu katika siri yake Kristo.

5  Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho;

YA KWAMBA MATAIFA NI WARITHI PAMOJA NASI WA URITHI MMOJA, NA WA MWILI MMOJA, NA WASHIRIKI PAMOJA NASI WA AHADI YAKE ILIYO KATIKA KRISTO YESU KWA NJIA YA INJILI”.

Hivyo tangu Bwana Yesu aondoke duniani, imepita Zaidi ya miaka 2,000 kipindi kirefu Zaidi ya kile Mungu alichotembea na wana wa Israeli peke yao.. Maana yake ni kuwa kipindi cha Neema kwetu sisi watu wa mataifa nacho kinaenda kufikia ukomo. Na kitafikia ukomo kwa unyakuo.

Unyakuo ukishapita mlango wa Neema unakuwa umefungwa kwa watu wa Mataifa. Mungu atawarudia tena watu wake Israeli kwa kipindi kifupi sana cha juma moja ambalo ni sawa na Miaka 7, baada ya hapo, hukumu ya mataifa itaanza na Utawala wa amani wa Yesu Kristo wa miaka elfu.

Je umempokea Kristo?..Upo ndani ya neema?. Kama bado upo nje, basi jua umechelewa sana..hivyo usiendelee kupoteza muda, ingia ndani ya neema uisalimishe roho yako. Yesu anakupenda na alikufa kwa ajili yako.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

MPAKA UTIMILIFU WA MATAIFA UTAKAPOWASILI.

Masheki ni nini?(Zaburi 105:22, Ayubu 29:10)

ORODHA YA WAFALME WA ISRAELI.

WEWE U MWALIMU WA ISRAELI,NA MAMBO HAYA HUYAFAHAMU?

Nabii Elisha alikuwa ana maana gani kulia na kusema”Gari la Israeli na wapanda farasi wake”?

Nifanye nini ili niishi maisha ya ushindi siku zote?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments