KWASABABU MUDA TULIOBAKIWA NAO SI MWINGI.

KWASABABU MUDA TULIOBAKIWA NAO SI MWINGI.

Mtume alituasa wakati huu wa mwisho ni wakati wa kutojishikamanisha sana na mambo ya mwilini, au ya ulimwenguni. Embu tutafakari kwa pamoja hivi vifungu hapa chini. Anasema.

1Wakorintho 7:29 “Lakini, ndugu, nasema hivi, muda ubakio si mwingi; basi tokea sasa wale walio na wake na wawe kama hawana;
30 na wale waliao kama hawalii; na wale wafurahio kama hawafurahi; na wale wanunuao, kama hawana kitu.
31 Na wale wautumiao ulimwengu huu, kama hawautumii sana; kwa maana mambo ya ulimwengu huu yanapita.
32 Lakini nataka msiwe na masumbufu. Yeye asiyeoa hujishughulisha na mambo ya Bwana, ampendezeje Bwana;
33 bali yeye aliyeoa hujishughulisha na mambo ya dunia hii, jinsi atakavyompendeza mkewe.
34 Tena iko tofauti hii kati ya mke na mwanamwali. Yeye asiyeolewa hujishughulisha na mambo ya Bwana, apate kuwa mtakatifu mwili na roho. Lakini yeye aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia hii, jinsi atakavyompendeza mumewe.
35 Nasema hayo niwafaidie, si kwamba niwategee tanzi, bali kwa ajili ya vile vipendezavyo, tena mpate kumhudumia Bwana pasipo kuvutwa na mambo mengine”.

Unaweza kupata picha alikuwa analenga nini hapo? Ni kwamba hatutakiwi tuvutwe kwenye mambo ya ulimwengu sana, mpaka tukasahau kuwa tunahitaji kumtumikia pia Mungu, angali tukiwa hapa dunia ndani ya hichi kipindi kifupi tulichobakiwa nacho.

Hii inatokea pengine mkristo mmoja ameingia katika ndoa, anasahau kabisa mambo ya Mungu, anaanza kujitaabisha na masuala ya mumewe au mkewe ampendezeje, maombi ameacha, kujifunza neno hafanyi tena.. Sasa katika mazingira kama haya Paulo alisema ukiingia kwenye ndoa, na uwe kama hujaoa, au uwe kama hujaolewa, usilikuze sana jambo hilo, mpaka likakufanya ukawa mlegevu kwa Mungu, kwasababu muda tuliobakiwa nao ni mchache.

Kwani  mambo ya kuoa au kuolewa ni ya hapa tu duniani, tukifika huko ng’ambo hayatakuwepo, hivyo si mambo ya kuyatilia mkazo sana, na kusahau mambo ya uzima wa milele  mbinguni.

Mwingine amezama katika masomo, kiasi kwamba hata muda wa kuongea na Mungu wake anakosa kabisa..

Mwingine utakuta ameingia katika biashara, na kwa bahati nzuri Mungu amemfanikisha sana, matokeo yake ni kuwa anasahau kabisa mambo ya rohoni anajikita muda wote katika biashara zake, hatengi tena muda wa kusali, au kwenda ibadani, au wa kumfanyia Mungu kitu.

Biblia inatuambia,

31 “Na wale wautumiao ulimwengu huu, kama hawautumii sana; kwa maana mambo ya ulimwengu huu yanapita”.

Ni kweli tupo katika huu ulimwengu, hatuna budi kuutumia kwa sehemu, lakini tumeaswa, tuwe kama vile hatuutumii, tuwe kama tumejiegesha tu, tusizame huko moja kwa moja, kiasi cha kutufanya tusahau kama sisi ni wapitaji, wenyeje wetu upo mbinguni.

Bali sisi tuishi kama wale mashujaa 300 wa Gideoni, ambao wenyewe, walipopelekwa mtoni kunywa maji, hawakunywa kama Ng’ombe kwa kupeleka midomo yao moja kwa moja kwenye maji, bali walikunywa kwa kuchota kwa mikono yao na kuyalamba kama mbwa midomoni,. Ikiwa na maana kuwa hata maadui zao wangeweza kuja wakati wanakunywa maji yao wasingeweza kuwaua kwa haraka kwasababu wangewaona tokea mbali , tofauti na wale wengine ambao midomo yao ilielekea kwenye maji moja kwa moja, hawaelewi kitu kingine.(Waamuzi 7:4-7)

Vivyo hivyo na sisi, tunaishi hapa duniani, lakini tunapaswa tuishi kwa kuchukulia kawaida kila kitu, ili tusimpe shetani nafasi ya kutuvuta katika mambo mengine, tusizame moja kwa moja kwenye ulimwengu, tunapaswa  tupate na nafasi kwa Mungu, kama ni shule, kama ni biashara, kama ni kazi, kama ni ndoa, kama ni sherehe, kama ni jambo lolote lile, sio la kuliumizia kichwa chako sana, au kulisumbukia, au kuliwazia kupitiliza, au kulifurahia sana.

Tukifanya Hivyo biblia inatuambia tutapata muda pia kwa Bwana. Na matokeo yake, hata siku ile ikifika haitatujilia kwa ghafla kama vile mwizi usiku. Maana biblia inasema ndivyo itakavyoujilia ulimwengu mzima. Na hiyo yote ni kwasababu watakuwa buzy katika mambo ya mwilini wakati huo.

Luka 31: 34 “Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo;
35 kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima”.

Kwahiyo kila siku  tulifahamu hili, kuwa sikumoja inapopita, ndivyo tunavyoikaribia ile siku Kuu ya Unyakuo. Hivyo ni wajibu wetu na sisi kuhakikisha ni kwa namna gani tunampendeza Mungu wetu katika hichi kipindi kifupi tulichobakiwa nacho.

Wafilipi 4: 6 “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu”.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho mengine

Mada Nyinginezo:

JIFUNZE KUELEWA MAANA YA KUOA/KUOLEWA KABLA YA KUINGIA HUKO.

UFUNUO: Mlango wa 14

Nini maana ya “yasiyokuwapo hayahesabiki”(Mh 1:15)

Kutabana ni nini? (Mika 5:12)

FAHAMU UWIANO MUNGU ANAOHITAJI KUUONA KWETU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Devis Julius administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments