KWANINI MIMI?

KWANINI MIMI?

Kuna wakati unaweza kupitia mahali ukajikuta upo katika hali ambayo hujui sababu ni nini, haujui kosa lako ni lipi mpaka upokee mapigo mazito kama hayo.  Unabakia kujiuliza maswali kwanini mimi?

Ayubu alipitia mazingira kama hayo, katika maisha yake yote alijitahidi sana kuwa mkamilifu na mwelekevu mbele za Mungu, hakuruhusu dhambi imtawale katika maisha yake yote, alikuwa ni mwombaji, na mkaribishaji mzuri wa wageni, hivyo Mungu akambariki sana.

Lakini ukafika wakati, akashangaa ghafla mambo yamebadilika, mifugo yake yote imeibiwa, mali zake zote zimepotea, kama hilo halitoshi akasikia watoto wake wote 10 wamekufa kwa ajali mbaya sana ndani ya siku moja.. Wakati yupo katikati ya msiba, ghafla tena anaanza kuugua kwa magonjwa ya ajabu, kiasi kwamba inambidi akae kwenye majivu muda wote, alikondoa kiasi cha kuona mifupa tu.

Embu jiweke wewe katika hiyo nafasi, unadhani haitakuwa rahisi kumkufuru Mungu? Ni rahisi sana, na ndicho alichokifanya mke wa Ayubu. Lakini Ayubu hakumkufuru Mungu, yeye hakufikia hatua hiyo mbaya bali aliishia kusema KWANINI MIMI?

Kwanini mimi na si mtu mwingine,…Na hiyo kwanini mimi ilimpelekea mpaka kuanza kulaani, kila kitu kwenye maisha yake, akailaani mpaka siku ya kuzaliwa kwake, akaona kama vile yeye si mtu mwenye bahati, ni heri tu asingezaliwa duniani.

Ayubu 3:2 “Ayubu akajibu, na kusema;

3 Na ipotelee mbali ile siku niliyozaliwa mimi, Na ule usiku uliosema, Mtoto mume ametungishwa mimba.

4 Siku hiyo na iwe giza; Mungu asiiangalie toka juu, Wala mwanga usiiangazie.

5 Ishikwe na giza, giza tupu, kuwa yake; Wingu na likae juu yake; Chote kiifanyacho siku kuwa giza na kiitishe………

11 Mbona si kufa mimi tokea mimbani? Mbona nisitoe roho hapo nilipotoka tumboni?

12 Mbona hayo magoti kunipokea? Au hayo maziwa, hata nikanyonya?

13 Maana hapo ningelala na kutulia; Ningelala usingizi; na kupata kupumzika;”

Ayubu, kila kukicha alitamani afe.(Ayu 7:4)

Hiyo hali inawakumba watu wengi sasa hivi hususani pale wanapopitia matatizo fulani madogo au makubwa, aidha wanapofiwa na wazazi wao, au watoto wao, au wanapopoteza mali zao, au vitu vyao ya thamani, au wanapokumbana na magonjwa mazito yasiyotibika, kama vile kansa, kisukari, au ukimwi, wanajiuliza ni tatizo gani walilolifanya mpaka wayapate magonjwa hayo, mbona wanakula vizuri tu, mbona hawatendi dhambi, inakuwaje wakumbane na hizo shida kwenye miili yao.

Wengine, wanauliza kwanini mimi nizaliwe kipofu, nilimkosea nini Mungu, kwanini nizaliwe mfupi, kwanini niwe mlemavu, kwanini nina mapungufu haya n.k..

Sasa katika haya maswali , kwanini! kwanini! kwanini!.. Mungu naye alianza kumuuliza Ayubu maswali mengine ya ziada, ambayo alitaka na yeye ampe majibu yake. Ukisoma Ayubu 38 na kuendelea utaona maswali aliyoulizwa Ayubu ni yapi, ambayo tunajua yote alishindwa kuyatolea majibu yake..Kwamfano maswali haya aliulizwa;

Ayubu 38:28 “Je! Mvua ina baba? Au ni nani aliyeyazaa matone ya umande?

29 Barafu ilitoka katika tumbo la nani? Na sakitu ya mbinguni ni nani aliyeizaa?

30 Maji hugandamana kama jiwe, Na uso wa vilindi huganda kwa baridi.

31 Je! Waweza kuufunga mnyororo wa Kilimia, Au kuvilegeza vifungo vya Orioni?

32 Je! Waweza kuziongoza Sayari kwa wakati wake? Au waweza kuongoza Dubu na watoto wake?

33 Je! Unazijua amri zilizoamuriwa mbingu? Waweza kuyathibitisha mamlaka yake juu ya dunia?

34 Waweza kuiinua sauti yako mpaka mawinguni, ili wingi wa maji ukufunikize?

35 Waweza kuutuma umeme, nao ukaenda, Ukakuambia, Sisi tupo hapa?

36 Je! Ni nani aliyetia hekima moyoni? Au ni nani aliyetia ufahamu rohoni?”

Akagundua kuwa kumbe ni mambo mengi sana huku duniani, Mungu hajatupa majibu yake, , lakini tunaendelea tu kuishi nayo, wala hatuumizi vichwa vyetu kutaka kuyajua, na maisha yanaendelea kama kawaida. Sasa kwanini tutake kutolea majibu kila hali tunayopitia.

Ayubu baada ya kulijua hilo, alikaa kimya. Akamwambia Mungu hakika nilikosea kuzungumza kuzungumza maneno yasiyofaa. Na baada ya Mungu kugundua kuwa Ayubu kalijua hilo, akaugeuza uteka wake akampa mara dufu zaidi ya vile alivyovipoteza. Na sisi pia, tuliookoka, mambo yanapogeuka na kuwa ndivyo sivyo, sio wakati wa kuanza kulaumu, kwanini iwe mimi na sio Yule,..Kumbuka kila mtu anayo mapito yake, sio kila tatizo utalipatia jawabu lake sasa hivi,  pengine utakuja kujua mbeleni au usijue kabisa, kikubwa mshukuru Mungu, na usonge mbele.Wakati utafika jaribu hilo litaisha, usianza kuuliza maswali ambayo hujui majibu yake, utaishi kulaumu, Mtumaini Mungu.

Songa mbele kama mkristo uliyeokoka..Timiza wajibu wako wa kumwomba Mungu na kumshukuru, na kuishi maisha ya utakatifu, Upo wakati Mungu atakuondolea huo ugonjwa, au hilo tatizo, au hiyo shida.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

HUDUMA YA (ELIFAZI, SOFARI, NA BILDADI).

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 9 (Kitabu cha Ayubu).

Maswali na Majibu

JINSI SHETANI ANAVYOZUIA MAJIBU YA MAOMBI YETU.

KWANINI KRISTO AFE?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments