VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 9 (Kitabu cha Ayubu).

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 9 (Kitabu cha Ayubu).

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu katika uchambuzi wa vitabu vya biblia, tumekwisha jifunza vitabu kadhaa vya mwanzo, kama utakuwa hujavipitia na ungependa kufanya hivyo, basi unaweza kufungua hapa>> VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 1

Na leo tutazidi kusonga mbele, kwa kutazama kitabu kimoja Zaidi ambacho ni kitabu cha Ayubu.

KITABU CHA AYUBU.

Kitabu cha Ayubu ndio kitabu kikongwe kuliko vitabu vyote vya biblia, Kitabu hichi kiliandikwa kabla ya kuandikwa kitabu cha Mwanzo. Kitabu cha Mwanzo kiliandikwa na Nabii Musa, kadhalika na kitabu hichi cha Ayubu, ni nabii Musa huyo huyo ndiye aliyekiandika.

Nabii Musa alikiandika kwanza kitabu hichi kisha ndio vikafuata vitabu vingine vingine vya torati kama kitabu cha Mwanzo, kutoka n.k.. Sasa sio kwamba Musa alikuwepo wakati Ayubu anaishi duniani na akawa ananakili Maisha aliyokuwa anayapitia hapana!.. Ayubu aliishi miaka mingi sana kabla ya Nabii Musa kutokea, na mambo yote Ayubu aliyoyapitia yalinakiliwa na Ayubu mwenyewe Pamoja na watu waliomzunguka Ayubu (maana yake marafiki zake na ndugu zake). Hivyo hata baada ya kufa Ayubu, historia ya Maisha yake iliendelea kuwepo, lakini haikuwepo katika mpangilio bora,  Sasa Musa alipokuja kutokea miaka mingi baadaye, kwa uongozo wa kiMungu alikusanya Pamoja taarifa zote za Ayubu kwa usahihi na kuziweka kwenye mfumo wa kitabu, ndio kikatokea hicho kitabu cha Ayubu tunachokisoma leo katika biblia.

Kitabu cha Ayubu kinaanza na Historia ya Ayubu mwenyewe mahali alipozaliwa na uelekevu wake kwa Mungu. Ayubu alizaliwa katika nchi ya “Usi”. Nchi ya Usi kwasasa ni maeneo ya kusini mwa nchi ya YORDANI. (kufahamu nchi ya Yordani ilipo, unaweza kutazama ramani).

Ayubu aliishi kabla ya Ibrahimu, hivyo hakuwa Mwisraeli. Lakini alimjua Mungu wa kweli wa mbingu na nchi na alimcha yeye, kutoka kwa mababu zake (akina Nuhu)

Kitabu cha Ayubu kimegawanyika katika Sehemu kuu 4.

  • Sehemu ya kwanza (1) ni kuanzia Mlango wa kwanza hadi ule Mlango wa pili (Sehemu hii inaelezea wasifu wa Ayubu  na  majaribu aliyoyapitia)
  • Sehemu ya Pili(2) ni kuanzia mlango wa 3 hadi mlango wa 38, ni (Sehemu hii inaelezea majibizano ya Ayubu na Rafiki zake watatu)..
  • Sehemu ya tatu (3) ambayo ni ule mlango wa 39 hadi 41, Bwana anaingilia kati majibizano yao na kuyakatisha..
  • Na sehemu ya nne(4) na ya mwisho ambayo ni ule mlango wa 42 Mungu anapitisha hukumu kwa Ayubu na wale marafiki zake watatu kwa mazungumzo yao.

Tukianza na sehemu ya kwanza:

Sehemu hii ni ile milango miwili ya mwanzo, na ndio milango iliyo mirahisi kuieleweka kuliko milango mingine yote inayofuata. Hapa inaelezea Ayubu jinsi alivyokuwa Mkamilifu na mwelekevu mbele za Mungu, kwamba alikuwa ni mcha Mungu na ni mtu aliyejiepusha sana na uovu.

Lakini pia katika Sura hizi mbili za Mwanzo ndizo Sura pekee katika biblia nzima zilizotupa, taswira kamili ya kinachoendelea katika katika mamlaka yaliyopo juu yetu sisi wanadamu. Sura hizi ndizo zimetufumbua macho na kuelewa kuwa kumbe wakati sisi tunaendelea na Maisha yetu, kuna mmoja anatushitaki mbele za Mungu, na ndiye sababu ya majaribu yetu yote tunayoyapitia. Ni ukurasa mmoja tu katika biblia lakini umekuwa muhimu sana kwetu. Inaeleza jinsi sababu ya mwenye haki wakati mwingine kupitia majaribu. Sasa ili kujua kwa urefu ni kwa namna gani mashitaka hayo yanaendelea juu mbinguni dhidi yetu, unaweza kufungua hapa na kusoma upatapo nafasi >>> JINSI SHETANI ANAVYOZUIA MAJIBU YA MAOMBI YETU.  Kwasasa hatutaingia sana huko.

Sehemu ya Pili: 

Sehemu hii ni kuanzia ule mlango wa 3 hadi wa 38, Sehemu hii ni imeelezea majibizano kati ya Ayubu na Rafiki zake watatu, walioitwa ELIFAZI, BILDADI, na SOFARI.

Marafiki hawa walikuwa ni marafiki wa Ayubu wa kitambo kirefu, na walikuwa wamejaa hekima ya ki-Mungu ndani yao. Na waliposikia Rafiki yao kapatwa na majanga yale, na misiba ile walitoka huko walipokuwepo kuja kumliwaza na kumshauri.

Rafiki zake hawa walikuja na Mashauri yao, lakini hawakujua kuwa Mashauri yao hayakuwa yaliyonyooka mbele za Mungu. Wenyewe katika akili zao waliamini asilimia mia moja kwamba Ayubu kuna mahali atakuwa alimkosea Mungu ndio maana akapatwa na majanga yale, walitumia mitazamo yao tu, hawakujua kuhusu vita vilivyokuwa vinaendelea mbinguni. Hivyo walikuja kwa nia moja tu, KUMWAMBIA AYUBU ATUBU!!, Atubie dhambi zake zote alizozifanya kwa siri, zilizompelekea apate majanga yote yale. Kwasababu walimwambia hakuna mtu anayeweza kukutwa na majanga yale, kama hajamkosea Mungu.

 Na Ayubu alipowaambia kwamba hajafanya chochote kilicho kibaya cha siri, bado hawakumwamini Ayubu..waliendelea kumwambia kwamba amemkosea Mungu. Hivyo ikawa mlolongo mrefu wa mashauriano, kila mmoja akitumia hekima yake kutoa Mashauri yake dhidi ya Ayubu. Ayubu naye akitumia hekima zake kuwajibu kuwa hajafanya kosa lolote..mazungumzo yakawa marefu mno, mwishoni wakachoka kumshauri Ayubu, kwasababu alionekana anajihesabia haki machoni pake mwenyewe. Akatokea kijana mmoja aliyeitwa Elihu, naye pia akajaribu kutoa Mashauri yake kwa Ayubu na Rafiki zake watatu.

Na katika mazungumzo yao wote wanne (yaani Ayubu na Rafiki zake watatu, yalikuwa yamfikia Mungu juu pasipo wao kujua, na Mungu alikuwa anawasikiliza. Sasa kwa urefu pia kuhusu huduma za hawa Rafiki zake Ayubu, Na kufahamu jinsi, shetani anavyoweza kuwatumia watu wanaoitwa watumishi wa Mungu kuwamaliza watumishi wengine wakamilifu,  fungua hapa kwa ajili ya somo hilo kwa urefu >> HUDUMA YA ELIFAZI, BILDADI NA SOFARI, 

Sehemu ya Tatu:

Baada ya mazungumzo yao yote, Mungu anamjibu Ayubu kwa upepo wa kisulisuli, maana yake kwa Tufani, jambo ambalo Ayubu hakuwahi kuliona hapo kabla, na anaanza kwa kumuuliza.

Ayubu 38:1 “Ndipo Bwana akamjibu Ayubu katika upepo wa kisulisuli, na kusema,

2 Ni nani huyu atiaye mashauri giza Kwa maneno yasiyo na maarifa?”

Maana yake ni “Ni nani huyo anayehoji kazi zangu kwa maneno ya upumbavu”…Swali hilo Mungu alimwuliza Ayubu, akimlenga Ayubu na marafiki zake watatu.. Kutokana na maneno waliyokuwa wanazungumza, juu ya Mungu alichomfanyia Ayubu.

Na ukiendelea kusoma mpaka huo Mlango wa 41, utaona Bwana anaendelea kumuuliza maswali Ayubu, kuhusu utukufu wake, ambayo maswali hayo hayana majibu mpaka sasa..(Ili Ayubu ajue kuwa hakuna mtu yeyote anayeweza kuzihoji kazi zake wala kuzipatia majibu)…Mfano wa swali moja Mungu alilomuuliza Ayubu ni ili..

Ayubu 38:4 “Ulikuwa wapi nilipoiweka misingi ya nchi? Haya! Sema, kama ukiwa na ufahamu.

5 Ni nani aliyeamrisha vipimo vyake, kama ukijua? Au ni nani aliyenyosha kamba juu yake?”

Hili swali hakuna mtu anaweza kutoa jibu lake. Na maswali mengine mengi aliyoulizwa unaweza kuyasoma mpaka mlango ule wa 41.

Sehemu ya Nne:

Na baada ya Mungu kumuuliza Ayubu hayo maswali.  Ayubu alikosa majibu, na akajinyenyekeza akatubu, naye akajiona alikosea sana katika kunyanyua mdomo wake kuzihoji hoji kazi za Mungu, Pamoja na marafiki zake, ijapokuwa hakuzihoji kwa ubaya, lakini kitendo cha kushindana tu, tayari alitambua lilikuwa ni kosa. Hivyo akatubu mbele za Mungu kwa kuvaa nguo za magunia, na kufunga mdomo wake. Utasoma habari hiyo katika ule mlango wa 42.

Ayubu 42:1 “Ndipo Ayubu akamjibu Bwana, na kusema.

 2 Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika.

 3 Ni nani huyu afichaye mashauri bila maarifa? KWA MAANA, NIMESEMA MANENO NISIYOYAFAHAMU, MAMBO YA AJABU YA KUNISHINDA MIMI, NISIYOYAJUA.

4 Sikiliza, nakusihi, nami nitanena; Nitakuuliza neno, nawe niambie.

 5 Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio; Bali sasa jicho langu linakuona.

 6 Kwa sababu hiyo NAJICHUKIA NAFSI YANGU, NA KUTUBU KATIKA MAVUMBI NA MAJIVU”.

Na baada ya Ayubu kujinyenyekeza na kujua kosa lake, Bwana aliwageukia wale Rafiki zake watatu, Elifazi, Bildadi na Sofari, ambao ndio waliomfanya Ayubu, azungumze maneno mengi, na zaidi ya yote, maneno yao ndio yaliyozihoji vibaya kazi za Mungu kuliko hata Ayubu. Hivyo Mungu akawakasirikia na kutaka kuwaadhibu.

Ayubu 42:7 “Basi ikawa, baada ya Bwana kumwambia Ayubu maneno hayo, Bwana akamwambia huyo Elifazi Mtemani, Hasira zangu zinawaka juu yako, na juu ya hao rafiki zako wawili; kwa kuwa ninyi hamkunena yaliyo sawa katika habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu.

 8 Basi sasa, jitwalieni ng’ombe waume saba, na kondoo waume saba, mkamwendee mtumishi wangu Ayubu, mjisongezee sadaka ya kuteketezwa; na huyo mtumishi wangu Ayubu atawaombea ninyi; kwa kuwa nitamridhia yeye, nisiwatende sawasawa na upumbavu wenu; kwani ninyi hamkunena maneno yaliyonyoka katika habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu.

 9 Basi Elifazi, Mtemani, na Bildadi, Mshuhi, na Sofari, Mnaamathi, wakaenda, wakafanya kama vile Bwana alivyowaamuru; naye Bwana akamridhia Ayubu”.

Na mwisho, katika kitabu hichi tunaona, tunaona Mungu akimuhurumia Ayubu na kumbariki tena na kumpa mara dufu ya vile alivyokuwa navyo.

Kuonyesha jinsi mwisho wa Mungu ulivyo mwema.

Kwa hitimisho katika kitabu hichi tunajifunza mambo yafuatayo:

1 .  Kumcha Bwana na kuepukana na uovu kama Ayubu:

2. Uvumilivu wakati wa majaribu: (Yakobo 5: 11 Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma.)

3. Kuishi Maisha ya usafi: kwasababu mshitaki wetu ibilisi, anapeleka mashitaka kuhusu sisi kila siku. Kama alimshitaki Ayubu kwa uzuri wake, unadhani tukiwa wabaya atakuwa anapeleka nini mbele za Mungu kama si kutuchongea tuangamizwe.

4. Kutokuwa na mashindano ya dini (hata kama unajua kitu, sio busara kulumbana na mtu asiyetaka kuamini unachokiamini) Ayubu alijua yupo sahihi, na marafiki zake hawapo sahihi, lakini kitendo cha kujibizana vile, ikawa tayari ni jambo lisilompendeza Mungu. Hivyo na sisi hatupaswi kuwa hivyo (Tito 3:9, 2Timotheo 2:14).

5. Mwenye haki kupitia mateso, haimaanishi Mungu hayupo naye; Tofauti na mitazamo ya watu wengi leo hii, wakishaonekana tu mtu aliyeokoka, anapitia hali Fulani mbaya labda ni hali ngumu ya kifedha, au ni magonjwa, basi moja kwa moja wanahitimisha kuwa Mungu amemwacha, au Mungu hayupo pamoja naye.

6. Kuwaombea Rafiki zetu na maadui zetu. (Hapo tunaona japokuwa Ayubu aliudhiwa na kukoseshwa na marafiki zake hao, lakini mwishoni aliwaombea rehema kwa Mungu, na wala hakuwalaani, na kwa kufanya vile {yaani baada ya kuwaombea tu}ndio ikafungua mlango wa baraka zake za mwisho).

Ayubu 42:10 “Kisha Bwana akaugeuza uteka wa Ayubu, hapo alipowaombea rafiki zake; Bwana naye akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza”.

Hivyo na sisi tukitaka kufungua milango ya baraka hatuna budi kuwapenda adui zetu, na kuwaombea wale wanaotuudhi sawasawa na maneno ya Bwana wetu Yesu aliyotuasa katika..

Luka 6:27  “Lakini nawaambia ninyi mnaosikia, Wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi,

28  wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi”

Je umeokoka? Kama bado unasubiri nini ndugu?..Kristo anarudi, je akirudi leo kulichukua kanisa utakuwa wapi?..hayo Maisha ya uasherati, ulevi na anasa yanakusaidia nini sasa? Zaidi ya kukuharibu tu?.

Kama leo utaamua kuokoka utakuwa umefanya uamuzi bora ambao hautaujutia, ni vizuri ukafanya hivyo sasa, na wala usingoje kesho…kwamaana hujui yatakayozaliwa ndani ya siku moja.. Hivyo kama upo tayari kutubu leo na kumpokea Kristo fungua hapa kwa msaada Zaidi >>> SALA YA TOBA.

Usikose mwendelezo wa vitabu vinavyofuata.

Bwana akubariki.

Kwa maombezi/ Ushauri/ Ratiba za Ibada/Maswali/ Whatsapp/ Piga namba hizi: +255693036618/ +255789001312

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

KUJIPAMBA NI DHAMBI?

DANIELI: Mlango wa 1

UTAWALA WA MIAKA 1000.

SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?

KWANINI NI YESU KRISTO WA NAZARETI?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments