SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?

SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?

Siku ya unyakuo itakukutaje?


Shalom.Jina la Bwana wetu Yesu Krito libarikiwe.

Karibu tujifunze Biblia..Je unajua kuwa kuna siku Kristo atakuja kuwachukua wateule wake? Na kwenda nao mbinguni?..Je unajua watakaokwenda mbinguni ni wachache sana?…Biblia inasema njia ile imesonga na mlango ni mwembamba?..

Mathayo 7:14 “ Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache”.

Je unajua…baada ya unyakuo kupita…watu watakaoachwa watajuta sana?..Wengi watatamani muda urudishwe dakika 5 tu nyuma angalau watubu…lakini watakuwa wameshachelewa…Je unajua karibia kila mtu duniani tayari kashaonyeshwa aidha kwa ndoto au kwa maono siku ya unyakuo? awe mwenye dhambi au asiye mwenye dhambi…tayari kashaota ndoto angalau moja inayohusiana na kurudi kwa Kristo mara ya pili?. Na wengi wao wanaoonyeshwa hayo wanakuwa wameachwa?..Na wanapata hisia kali sana baada ya kuamka na wanashukuru Mungu imekuwa ni ndoto na wala si kitu cha kweli?.

Binafsi nilishawahi kuota ndoto kama hizo mara kadhaa zamani sana…na zote nilikuwa najiona nimeachwa ni chache sana nilijiona nimekwenda na Bwana lakini nyingi nimeachwa.…na nikiwa ndani ya ndoto nilikuwa nalia na kuomboleza na kumwomba Mungu anirudishe muda angalau dakika 5 nyuma kabla ya unyakuo nirekebishe mambo yangu!…na nikishtuka kutoka usingizini nashukuru Mungu kwamba ni ndoto na si kitu halisi..Hivyo nakwenda kutubu na kumuahidi Mungu kuzidi kujitakasa ili nisije nikaachwa kwenye unyakuo halisi utakapofika…

Lakini yote hayo ni tisa..kumi ni siku tutakayokutana na tukio lenyewe la kuachwa kwenye unyakuo!!…

Siku moja, muda mrefu kidogo umepita, tulikuwa ndani ya nyumba nyakati za jioni kama saa moja na nusu hivi usiku…Umeme ulikatika mtaa mzima..Kukawa na giza lile tororo kabisa..tukaamua kutoka ndani kukaa nje…Na Mahali tulipokuwa tunaishi sio mahali penye watu wengi wanaojichanganya na wengine ni mahali ambapo ikifika jioni tu ni kimyaa na kila mtu kajifungia kwake..Sasa wakati tumekaa nje kidogo tulikuwa wawili mimi na ndugu yangu…tukasema hebu tutazame juu kidogo tuangalie nyota utukufu wa Mungu mbinguni…

Siku hiyo haikuwa na mawingu hivyo nyota zilikuwa zinaonekana vizuri hata zile zinazotembea….….Sasa wakati tunatazama juu ulitokea mwanga fulani wa ajabu wenye rangi unaokaribiana na blue hivi unaong’aa sana, kama mita 5 hivi juu yetu..ukimulika kutokea upande wa magharibi kuelekea upande wa mashariki..na ulikuwa kama unasogea hivi…. Haukuwa na sauti hata kidogo lakini ulikuwa na mwangaza mkali na ulidumu kwa muda kama wa sekunde 3 hivi au Zaidi kidogo..halafu ukatoweka!..ulimulika pale tulipokuwepo kote kukawa kama mchana hivi…

Haukuwa mwanga wa radi kwasababu kipindi hicho kilikuwa ni kipindi cha kiangazi, na wala haikuwa ile mianga inayotokea inamulika bila sauti yoyote wakati wa vipindi vya mvua. Siku hiyo juu hakukuwa na wingu hata moja ni nyota tuu zilikuwa zimetanda anga zima..tokea kaskazini, kusini mashariki mpaka magharibi..hakukuwa na dalili ya wingu…Na mwanga huo hakuja na sauti yoyote…Nakumbuka siku chache tu nyuma tulikuwa tunazungumzia masuala ya unyakuo..Na tulikuwa tunaufahamu ule mstari unaosema…

Luka 17:24 “kwa kuwa, kama vile umeme umulikavyo toka upande huu chini ya mbingu hata upande huu chini ya mbingu, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu katika siku yake.”

Kwahiyo baada ya tukio hilo..Mstari huo ukaja kichwani haraka sana!…tukajua kwamba kuna uwezekanano tayari unyakuo umeshapita na tumeachwa…Baada ya hapo ilikuja hisia moja ambayo siwezi kuilezea, ambayo tangu huo wakati ndio ikanifanya nisichukulie tena kiwepesi suala la kubaki kwenye unyakuo…

Nilihisi kuvunjika moyo na kujuta majuto ambayo sijawahi kuyajuta…Nilianza siku zote nilikuwa nafanya nini mpaka siku hii imenikuta kama mjinga…Nikaanza kuwaza siku chache tu mbeleni nakwenda kumshuhudia mpinga-Kristo kwa macho yangu..siku chache mbeleni nakwenda kupokea chapa…siku chache mbeleni nakwenda kukutana na dhiki kuu, kama sitakufa basi nitashuhudia mapigo yote yale yaliyoandikwa kwenye kitabu cha Ufunuo sura ya 16, maji kuwa damu, jua kutiwa giza, mvua ya mawe n.k..Nikawaza siku chache tu mbeleni hakutakuwa tena na ndugu, wala mama, wala marafiki…wala hakutakuwa tena na kitu kinachoitwa nyumbani…wala hakutakuwa tena na kufanya kazi..Mwisho wa mambo yote umeshafika!.

Nikawaza tena wakati huu sasa hivi watakatifu, waliojitakasa na kuyachukia Maisha yao kwaajili ya Kristo wanafarijiwa mbinguni..sasa hivi Paulo, anafutwa machozi na tabu zake zote zinageuzwa kuwa furaha…Nikarudi kuwaza tena..Nikifa katika dhiki kuu ninakwenda kusimama mbele ya kiti cha hukumu..kuonana uso kwa uso na Yesu Kristo… na mwishowe kuhukumiwa nakwenda kutupwa kwenye ziwa la moto.. Nikakumbuka tena hakuna kutubu katika hii hali tuliyopo sasa..Wakati tunatafakari hayo wote wawili tulijua unyakuo umepita na tumeachwa….Tukawaza tutajibu nini mbele ya kiti cha hukumu.

Usiku ulizidi kuingia nikitamani hata mvua inyeshe ili tujifariji kwamba angalau ulikuwa ni mwanga wa radi ya mvua lakini wapi hakuna chochote…Nikatazama tena ujirudie juu ili pengine tuseme ni kawaida mianga mianga kupiga wakati wa mvua lakini wapi…..hakuna kilichotokea!…palikuwa pakame na juu kulikuwa kweupe vile vile, nyota zimetanda kote na hakuna hata dalili ya wingu …Zile hisia kali za kutazamia mambo yatakayoikumba dunia zilikuwa tayari zimeshafunika hisia za wakati tuliopo…nilitamani siku hiyo iwe ndoto..nizinduke usingizini nitubu kwa kumaanisha kubadilika kabisa..lakini wapi! Ilikuwa ni hali halisi kabisa..

Ndipo asubuhi Bwana akaanza kutufundisha…kwamba haukuwa unyakuo, bali Bwana alikuwa anataka kutufundisha hali itakayotukuta endapo tukiukosa unyakuo..(Na pia kuhusu jambo lingine ambalo halihusiani na hii mada ya leo alituambia kuhusu tukio hilo). Lakini kikubwa ni kuhusu siku ile itakavyokuwa. Na hisia zitakazowapata watu siki hiyo.

Hisia hizo ndizo zitakazowakuta wengi watakaoukosa unyakuo..na siku hiyo watakaoumia sana ni wale ambao tayari kwa namna moja au nyingine walishawahi kuisikia injili huko nyuma lakini hawakutubu au walipuuzia…ambao jana tu walitoka kuhubiriwa lakini wakaikataa injili au wakaipuuzia, ambao juzi tu wametoka kusikia au kusoma habari za kuja kwa Yesu mara ya pili lakini walipuuzia…Hao ndio watakaoomboleza sana na kulia..wengine wote wataona kawaida.

Hiyo kwetu ilikuwa ni ishara kubwa sana ambayo Mungu alizungumza na sisi..Kwa kweli ilitubadilisha Maisha yetu tangu huo wakati…Mpaka leo hii siwezi kuisahau hiyo hisia…nasema nikose chochote lakini sio UNYAKUO..Na namshukuru Mungu kwa kuzungumza na mimi kwa ishara ya nje kabisa kwani angesema nami kwa ndoto tu kama siku zote pengine nisingechukulia kwa uzito kwa kiwango hicho na mpaka leo ningebaki kuchukulia kuachwa ni jambo la kawaida.

Ndugu Kuna uchungu wa ajabu na hisia mbaya sana kwa watu watakaoukosa unyakuo…Hebu jiweke kwenye mazingira leo hii ndio unyakuo umepita na umeachwa?..utajisikiaje! labda unaweza usielewe sasa mpaka siku hali hiyo itakapokukuta…Lakini usitamani uwepo..Siku hiyo utasikia unyakuo umepita masaa machache tu umepishana na mahubiri ya kukuonya utubu.

Je! Umejiweka tayari?..Biblia inasema katika Waebrani 10:37 “Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia”.

Leo hii unasema unyakuo bado sana..siku hiyo ikifika utatamani urudishwe dakika 5 nyuma urekebishe mambo yako lakini utakuwa umeshachelewa.

Kama hujaokoka leo mlango wa Neema upo wazi..Hivyo pale ulipo jinyenyekeze kwa Mungu..Mwombe akusamehe dhambi zako zote ulizokuwa unazifanya za makusudi na ambazo sio za makusudi..Kisha baada ya kutubu fanya kama ulivyotubu..acha kufanya dhambi ulizokuwa unazifanya…kama ulikuwa mwasherati..acha uasherati, ulikuwa mwizi vivyo hivyo unaacha, ulikuwa unavaa nusu uchi..unaacha..ulikuwa mtazamaji wa picha chafu mitandaoni unazifuta na kuanza maisha mapya..

Ukishafanya hivyo Kristo atakupa amani ya ajabu moyoni mwako.Amani hiyo utakayoipata ndio itakuwa uthibitisho wa msamaha wako..Baada ya kufanya hivyo nenda kabatizwe kama hujabatizwa, ubatizo sahihi ni ule wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo. Na Roho Mtakatifu ndani yako atakuongoza katika mambo mengine yaliyosalia ikiwemo kukupa uwezo wa kushinda dhambi na ufahamu wa kuyaelewa maandiko. Ukiishi katika hali hiyo biblia imetupa uhakika wa kunyakuliwa Kristo atakaporudi..Hakuna namna yoyote ambayo unaweza usinyakuliwe.

Bwana azidi kutupa Neema yake tushinde ulimwengu huu kama yeye alivyoshinda. Ili siku ile tuifarahie karamu aliyotuandalia mbinguni milele.

Maran atha!

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

UNYAKUO.

Ule mfano wa wanawali 10 (Mathayo 25), wale watano hawakuwa na mafuta ya ziada katika chupa zao je yale mafuta ya ziada yanawakilisha nini?

SIKU YA TAABU YA YAKOBO.

MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.

DHAMBI ILIYOMKOSESHA SHETANI:

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments