NENO NI LILE LILE, LAKINI UJUMBE NI TOFAUTI.

NENO NI LILE LILE, LAKINI UJUMBE NI TOFAUTI.

Neno ni lile lile, lakini ujumbe ni tofauti.


Shalom.

Wakati wana wa Israeli wanatoka Misri kuelekea Nchi yao ya ahadi walipokuwa wanapitia jangwani, walifikia mahali panapoitwa Kadesh-Barnea, eneo hilo lilikuwa ni kame sana, na ni eneo lililokuwa limezungukwa na milima mikubwa na mabonde mengi. Katika jangwa hilo ndilo eneo lililokuwa gumu kuliko yote kulivuka..Wana wa Israeli walipoona nyuma walipotoka ni mbali na mbele wanapoelekea ni mbali, Waakanza kumnung’unikia Mungu na Musa..

Ndipo Mungu akamwambia Musa autazame mwamba uliokuwa mbele yao, kiisha aende akaupige kwa ile fimbo aliyokuwa nayo na utatoa maji (Kutoka 17:6)..Musa akafanya kama alivyoagizwa, akaupiga mwamba ule, na maji yakatoka wana wa Israeli wakanywa wakashiba..Safari ikaendelea..

Lakini kikapita tena kipindi kirefu cha miaka mingi, Wakiwa wanazunguka tu huko huko jangwani kwa miaka 40, Mungu akawaleta tena wana wa Israeli eneo lile lile..Kama ilivyo kawaida eneo lile ni baya kushinda maeneo yote yaliyokuwa jangwani wakati ule, hali inazidi kuwa mbaya wakiutazama ule mwamba uliokuwa unachuruzika maji zamani sasa hautoi maji tena. Wakiangalia watoto wao na mifugo yao inaangamia kwa kiu..Kilichobakia kwao ni nini kama si kurudia yale yale waliyoyafanya mwanzoni, ya kumng’unikia Mungu na Musa..

Ndipo Musa akaenda kwa Bwana kumuuliza afanye nini, Ndipo Mungu akamwambia nenda ukasimame mbele ya mwamba ule, UUTAMKIE maji yatoke, nayo yatatoka..Lakini Musa hakuzingatia maagizo Mungu aliyompa..Akaenda kwa desturi na mazoea, akidhani Mungu naye yupo hivyo hivyo kama yeye.. Aliona kwasababu eneo ni lile lile la Kadesh-Barnea, mazingira ni yale yale, mwamba ni ule ule na wala si mwingine..Basi akahitimisha kuwa hata maagizo ni yale yale, ya kwenda kuupiga mwamba..

Hivyo akaenda kuupiga mwamba badala ya kuzungumza nao..Kilichotokea ni kweli maji yalitoka katika mwamba ule, watu wakanywa wakashiba, akadhani tayari kashatimiza kusudi la Mungu..Lakini Mungu alimwambia…

Hesabu 20:12 “Bwana akamwambia Musa na Haruni, Kwa kuwa hamkuniamini mimi, ili kunistahi mbele ya macho ya wana wa Israeli, basi kwa sababu hiyo, hamtawaingiza kusanyiko hili katika ile nchi niliyowapa”.

Ni kawaida ya Mungu kurudia mazingira yale yale kuzungumza na wewe, Lakini hiyo hauufanyi ujumbe kuwa ni ule ule..Kwamfano hii biblia tunayoisoma, ni ndogo tu yenye vitabu 66. Ukisoma unaweza ukaimaliza yote ndani ya wiki moja tu. Na wapo watu wameshaisoma na kurudi hata zaidi ya mara 500 siku zote za maisha yao. Lakini kama utaisoma tu kwa lengo kupata habari nyingine mpya, hutaambulia chochote, kwasababu kwako itakuwa ni kurudia rudia, na mwisho wa siku itakuboa.

Lakini kama utaisoma kwa lengo la kuisikia sauti ya Mungu, kila siku mstari mmoja utauona ni mpya kwako, kana kwamba hukuwahi kuusoma huko nyuma kabisa. Ni kwasababu gani, ni kwasababu uliweka ufahamu wako wote, kuisikia sauti ya Mungu, zaidi ya kuangalia uzoefu wako katika ulichokisoma au kukisikia.

Mfano mwingine katika maandiko ni huu, Kama ukisoma Kitabu cha Ufunuo, sura ile ya pili na ya tatu, utaona Bwana Yesu akimpa Yohana zile barua azipeleke katika yale makanisa 7 ya Asia ndogo..

Na ni kweli Yohana alipotoka katika kisiwa cha Patmo, alizitawanya zile barua kwa watakatifu wote waliokuwa katika miji yote saba ya Asia ndogo, na kila kanisa lilikuwa na ujumbe wake maalumu uliokuwa unalihusu kanisa hilo husika..Lakini kumbe ujumbe ule haukuwa tu kwa kipindi kile..Lakini Sisi tunaoishi katika wakati huu wa mwisho ndio tunaoelewa vizuri kuwa makanisa 7 pia yanamaanisha makanisa ya nyakati… Tangu kipindi cha mitume hadi sasa zimepita Nyakati saba za kanisa, na sisi ndio tunaoishi katika lile kanisa la mwisho na la saba linalojulikana kama Kanisa la Laodikia ambalo lilianza mwanzoni mwa karne ya 20 yaani miaka ya 1900, na litaisha na unyakuo.

Hivyo tunapaswa tuwe makini sana, katika kuisikia sauti ya Mungu, na kutokulizoelea Neno lake kwa kigezo cha mazingira yale yale yanayojirudia…kwa kigezo cha mistari ni ile ile tuliyowahi kuisoma… Laiti kama Musa angeisikia sauti ya Mungu ni nani ajuaye kuwa Mungu alikuwa amepanga mwamba ule utitirishe maji yake daima, utoe mto ndani yake ambao utafuatana nao mpaka watakapoingia katika nchi ya ahadi, tofauti na ile mara ya kwanza umbapo ulitoa tu maji kwa muda na ukakata?.

Kwasababu biblia inasema mwamba ule ulikuwa unamfunua Kristo, na Kristo huwa hatoi maji ya muda tu, bali chemichemi za maji ya uzima zinazotiririka daima. (1Wakorintho 10:4)

Hivyo, Mungu anafundisha tusilizoelee Neno lake, yapo mengi anataka kutufundisha kila siku, zipo hatua nyingi anataka kutupigisha kila siku, lakini kama tukishasema, Aah! Hichi tayari nilishahubiriwa, au hichi tayari nilishakisikia.. tujue kuwa bado tu wachanga katika kuielewa sauti ya Mungu.

Biblia inasema katika 1 Wakorintho 8:2

“Mtu akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno lo lote bado, kama impasavyo kujua”.

Ni matumaini yangu na maombi yangu, sisi sote kwa ujumla, tutaanza kuitafuta sauti ya Mungu, bila kujali ni tumeshahubiriwa Neno lile lile mara ngapi, tumeshalisoma Neno lile lile mara ngapi..

Zaburi 12: 6 “Maneno ya Bwana ni maneno safi, Ni fedha iliyojaribiwa kalibuni juu ya nchi; Iliyosafishwa mara saba”.

Ubarikiwe sana. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

IELEWE SAUTI YA MUNGU.

PENGINE MUNGU ALISHASEMA NAWE KWA NJIA HII.

KAMA MUNGU ANABORESHA KAZI ZAKE, KWANINI WEWE USIBORESHE ZA KWAKO?.

 

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 1

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 1

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
lucas mhula
lucas mhula
2 years ago

Amen