KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 1

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 1

Karibu katika kujifunza NENO la Mungu, leo tukikiangalia kitabu cha Yuda, kilichojaa maonyo makubwa kwa kanisa la leo. Yuda aliyeandika kitabu hichi sio Yule Yuda mwanafunzi wake YESU au yule aliyemsaliti hapana, bali ni Yuda yule aliyekuwa ndugu yake Bwana Yesu kwa kuzaliwa(Marko 6:3). Hivyo kwa uongozo wa Roho Mtakatifu aliuandika waraka huu mfupi kwa WATU WALIOITWA TU!! (yaani wakristo) na sio watu wote wa ulimwengu ambao sio wakristo, Leo tutasoma mstari wa 1-6″, Bwana akitupa neema tutaendelea na mistari inayofuata katika sehemu ya pili na ya tatu.

Biblia inasema…

Mlango 1:1-6″ Yuda, mtumwa wa Yesu Kristo, ndugu yake Yakobo, KWA HAO WALIOITWA, WALIOPENDWA, katika Mungu Baba, na kuhifadhiwa kwa ajili ya Yesu Kristo.

2 Mwongezewe rehema na amani na upendano.

3 Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ILI NIWAONYE KWAMBA MWISHINDANIE IMANI WALIYOKABIDHIWA WATAKATIFU MARA MOJA TU.

4 Kwa maana kuna watu waliojiingiza kwa siri, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, makafiri, wabadilio neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi, nao humkana yeye aliye peke yake Mola, na Bwana wetu Yesu Kristo.

5 Tena napenda kuwakumbusha, ijapokuwa mmekwisha kujua haya yote, ya kwamba Bwana, akiisha kuwaokoa watu katika nchi ya Misri, ALIWAANGAMIZA BAADAYE WALE WASIOAMINI.

6 Na malaika wasioilinda enzi yao wenyewe, lakini wakayaacha makao yao yaliyowahusu, AMEWAWEKA KATIKA VIFUNGO VYA MILELE CHINI YA GIZA KWA HUKUMU YA SIKU ILE KUU”.

Kama tulivyotangulia kusema waraka huu uliandikwa kwa watu walioitwa peke yao, yaani watu waliokwisha kumwamini Bwana Yesu Kristo, Ikiwa na maana wakristo wote (mimi na wewe). Hivyo tunaposoma maandiko haya tufahamu kuwa maonyo haya yanatuhusu sisi tunaojiona kuwa tupo katika IMANI na kwa namna moja au nyingine haziwahusu watu ambao wapo nje ya ukristo. Kwahiyo unaposoma usilichukulie kiwepesi wepesi na ndio maana Yuda alianza na kusema “Napenda kuwakumbusha ijapokuwa mmeyajua haya yote.” Kwahiyo inawezekana umeyajua, lakini unakumbushwa tena.

Sasa Tukisoma ule mstari wa 3 anasema 

“Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ILI NIWAONYE KWAMBA MWISHINDANIE IMANI WALIYOKABIDHIWA WATAKATIFU MARA MOJA TU. “

Umeona hapo anazungumza juu ya IMANI waliyopewa watakatifu, ambayo wamepewa mara moja tu! na kama ni mara moja inapaswa ishindaniwe kwa bidii na kushikiliwa kwa maana ikidondoka tu! hakutakuwa na nafasi ya pili ya kuipata tena. Huo ndio msisitizo mkubwa hapo.

Na kushindania Imani ni nini?. Ni kudumu katika kile ambacho umekiamini na kujiangalia usianguke, Na ndio maana ukiendelea kusoma Yuda aliuchukua mfano wa Wana wa Israeli akifananisha na safari ya wakristo (yaani walioitwa), alisema, ” Bwana, akiisha kuwaokoa watu katika nchi ya Misri, ALIWAANGAMIZA BAADAYE WALE WASIOAMINI. “

 

Sasa tukichunguza habari ya wana wa Israeli, tunaona wote waliokolewa kweli, wote walibatizwa, wote walikuwa wanashiriki baraka zote za rohoni, wote walikuwa chini ya Neema, wote walikula chakula cha Bwana n.k. lakini “WENGI” wa hao Mungu hakupendezwa nao na kuangamizwa jangwani, kumbuka sio wachache bali ni “WENGI”. Kama tunavyosoma katika biblia.

1Wakoritho 10:1 Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari;

2 wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari;

3 wote wakala chakula kile kile cha roho;

4 wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo.

5 LAKINI WENGI SANA KATIKA WAO, Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani.

6 Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani.

7 Wala msiwe waabudu sanamu, kama wengine wao walivyokuwa; kama ilivyoandikwa, Watu waliketi kula na kunywa, kisha wakasimama wacheze.

8 Wala msifanye uasherati, kama wengine wao walivyofanya, wakaanguka siku moja watu ishirini na tatu elfu.

9 Wala tusimjaribu Bwana, kama wengine wao walivyomjaribu, wakaharibiwa na nyoka.

10 Wala msinung’unike, kama wengine wao walivyonung’unika, wakaharibiwa na mharabu.

11 Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani.

12 Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke”.

Umeona hapo biblia inasema mambo hayo yameandikwa ili kutuonya sisi, Wana wa Israeli ni mfano wa wakristo wote ulimwenguni, ambao kwa pamoja tulipoamini tulitoka Misri na siku tulipobatizwa tulivuka bahari ya Shamu. Lakini huo ndio ulikuwa mwanzo wa safari yetu sio kwamba ndio tumefika, la! bali kuanzia hapo ndio IMANI INAANZA KUSHINDANIWA.

Kama tunavyosoma katika maandiko waliofika Kaanani, ni wawili tu kati ya mamilioni ya watu waliotoka Misri, Kadhalika na kanisa la siku za mwisho, japo kuna mamilioni ya watu wanaojiita wakristo na wameokoka, na wamebatizwa kweli katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa, wanaoupako, wanaona kabisa wakibarikiwa na Mungu katika mambo yao yote (huko ndiko kula mana kwenyewe kutoka mbinguni), wananena kwa lugha, wanatenda miujiza, wanayajua maandiko, n.k. lakini biblia imetabiri katika siku za mwisho watakaofika ng’ambo ya pili ni wachache sana kwasababu walioitwa ni wengi, lakini wateule ni wachache. Lakini ni sababu ipi itakayowafanya watu wengi washindwe kuilinda imani, ni kwasababu kama hizo hizo tu za wana wa Israeli.

Tuzitazame:

> Ibada za sanamu: Wana wa Israeli walitengeneza sanamu za dhahabu wakiwa katikati ya safari yao ya Imani na kuanza kuziabudu, Hivyo Mungu akakasirishwa nao kuliko hata watu wa mataifa, ikapelekea kufanya dhambi isiyosameheka, mfano halisi wa leo mkristo upo safarini, Unafahamu kuwa ibada za sanamu, kuabudu picha au sanamu za watakatifu fulani waliokufa zamani angali unajua kufanya hivyo ni dhambi. Kuna hatari kubwa mno ya kuangamizwa na Mungu mwenyewe.

Sababu nyingine ni Uasherati: Wana wa Israeli walifika mahali wakasahau maagizo ya Mungu na kuanza kuzini na wanawake wa kimataifa: Kadhalika na watu wanaojiita wakristo kuzini au kufanya uasherati nje ya ndoa takatifu, pamoja na kuvaa mavazi ya kikahaba yanayowasababishia wengine kutenda dhambi za uzinzi nafsini mwao vile vile ni kujiangamiza mwenyewe, ipo hatari kubwa ya kuondolewa kabisa katika neema.

> Manung’uniko: Hili nalo liliwafanya wana wa Israeli wakataliwe na Mungu, japo ni kweli waliitwa na Mungu mwenyewe na kubatizwa lakini manung’uniko yalifamfanya Mungu achukizwe nao. Ni mfano halisi wa sasa wakristo wengi wanapopitia na mitikisiko kidogo tu, wanasahau fadhili zote Mungu alizowatendea nyuma. Pengine anapitia misiba, anaanza kutoa maneno ya makufuru, anapitia, kuugua kidogo anaanza kulaumu Mungu kamuacha, mtu kapungukiwa kidogo tu! anaanza kunung’unika moyoni mwake anasahau kuwa miaka mingine nyuma Mungu alikuwa anamfanikisha n.k.. Sasa mambo kama hayo ndio yanayosababisha safari kuwa fupi…Biblia inasema atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokoka..Safari ya ukristo inahitaji uvumilivu wa hali ya juu.

Pia tabia ya kutamani mabaya na kumjaribu Mungu. Ni kikwazo kingine kilichowafanya wengi wa wana wa Israeli wasimalize safari yao. Kwa mfano Mungu aliwakusudia wale mana tu! mpaka wakati watakapoingia nchi ya ahadi, wao wakawa wanataka nyama tena kwa njia ya kumjaribu, wakijua kabisa Bwana anaweza kufanya hivyo. Vivyo hivyo watu wa leo Hawataki kuridhika katika njia Mungu aliowakusudia wapitie, wanataka wakiwa wakristo bado wafanane na watu wa kidunia, wanaenda kanisani leo kesho wanaenda disko, wanaongea vizuri leo kesho wanatukana n.k. Hizi zote ni sababu kubwa zinazokwamisha safari. Ni heri mtu kama huyo asingeanza safari kabisa, kuliko kuingia na kufanya machukizo, maana nafasi ya pili haipo kwasababu IMANI INAKABIDHIWA MARA MOJA TU.

Na ndio maana tukiendelea kusoma tunaona Yuda aliwafananisha watu hawa na watu WALIOJIINGIZA KWA SIRI katikati ya kundi la Mungu, ni magugu katikati ya ngano, Alisema;

” 4 Kwa maana kuna watu waliojiingiza kwa siri, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, makafiri, wabadilio neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi, nao humkana yeye aliye peke yake Mola, na Bwana wetu Yesu Kristo.

5 Tena napenda kuwakumbusha, ijapokuwa mmekwisha kujua haya yote, ya kwamba Bwana, akiisha kuwaokoa watu katika nchi ya Misri, aliwaangamiza baadaye wale wasioamini.

6 Na malaika wasioilinda enzi yao wenyewe, lakini wakayaacha makao yao yaliyowahusu, amewaweka katika vifungo vya milele chini ya giza kwa hukumu ya siku ile kuu “

Hivyo mtu yeyote anayefanya hayo na bado anajiita mkristo ni sawa na mtu aliyejiingiza kwa siri katikati ya kundi la Mungu mfano wa akina Kora, na dathani katikati ya wana wa Israeli ambao walishaandikiwa hukumu yao tangu zamani. Na biblia imewafanisha hawa na wale malaika walioasi (Shetani na malaika zake), ambao hawakuilinda enzi yao. sasa hivi wamefungwa katika vifungo vya giza wakisubiria ile hukumu ya siku ile watakapotupwa wote kwa pamoja katika lile ziwa la moto. Katika kanisa la kwanza walikuwepo watu waliojiingiza kwa siri, na hata sasa wapo wengi.

Hivyo ndugu kwanini unaendelea kuichezea au kuichukulia Imani yako juu juu, kumbuka upo safarini na imani umekabidhiwa mara moja tu, na wanaomuudhi na wanaompendeza Mungu siku zote huwa ni wale walio safarini na sio wasiomjua Mungu, hao Mungu atawahukumu mwenyewe siku ya mwisho. Na ndio maana anasema ni heri uwe moto au baridi kuliko kuwa vuguvugu. Hatari kubwa ipo kwako wewe uliye mkristo vuguvugu, usipoilinda ENZI YAKO, na KUISHINDANIA IMANI utafananishwa na wale malaika walioasi ambao wameandaliwa ziwa la moto.

Huu ni wakati wa KUTUBU na kufanya IMARA WITO WAKO, NA UTEULE WAKO. Tunaishi katika siku za mwisho na Bwana yupo karibu kuja, Je! utaenda nae?.

Mungu akubariki.

Tafadhali share kwa wengine ujumbe huu.

Kwa maombezi/ Ushauri/ Ratiba za Ibada/Maswali/ Whatsapp/ Piga namba hizi: +255693036618/ +255789001312

Kwa mwendelezo >>> KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 2

Mada Nyinginezo:

VIFUNGO VYA GIZA VYA MILELE.

KUNDI LA MALAIKA WALETAO MABAYA.

NGUVU YA UPOTEVU.

MTI UANGUKAPO, PAPO HAPO UTALALA.

EPUKA MUHURI WA SHETANI.

JE! KUCHORA TATTOO NI DHAMBI?


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
5 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Tunda lusanga severin pastor
Tunda lusanga severin pastor
1 year ago

Ubarikiwe mtumishi

nengo
nengo
2 years ago

Mungu akubariki, umenisaidia na kunikumbusha. ujumbe huu ni muhimu kuliko wa POKEAAAAAAAA…. RECEIVEEeeeeeeee

MBONIMPA COSMAS
MBONIMPA COSMAS
2 years ago

Shaloom.
Baraka za Kristo Bwana wetu zizidi sana kwenu kwa kadri ya uaminifu na kujitoa kuyahubiri mafundisho na njia ya wokovu.