TUUTAFUTE UMOJA WA ROHO.

TUUTAFUTE UMOJA WA ROHO.

Umoja wa Roho Mtakatifu upo katika vifungo 7, ambavyo kama kanisa ni lazima tujifunge katika vifungo hivyo.

Lakini kabla ya kuvitazama hivi vifungo 7 vya Roho Mtakatifu, ni vizuri tuweke msingi kidogo kumhusu Roho Mtakatifu.

Biblia inatufundisha kuwa kuna Roho 7 za Mungu, ambazo ndizo zinazotajwa kama Macho 7 ya Mungu.

Ufunuo 5:6  “Nikaona katikati ya kile kiti cha enzi na wale wenye uhai wanne, na katikati ya wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama, alikuwa kana kwamba amechinjwa, mwenye pembe saba na macho saba, AMBAZO NI ROHO SABA ZA MUNGU zilizotumwa katika dunia yote”

Vile vile inazitaja Roho hizi 7 kama TAA SABA ZA MUNGU, ikiwa na Maana kuwa hizo ndizo mwanga mbele ya kiti cha Enzi.

Ufunuo 4:5 “Na katika kile kiti cha enzi kunatoka umeme na sauti na ngurumo. NA TAA SABA ZA MOTO ZILIKIWAKA MBELE YA KILE KITI CHA ENZI, NDIZO ROHO SABA ZA MUNGU”.

Hii yote ikimaanisha kuwa Roho Mtakatifu anatenda kazi katika Nafasi zake 7, au hatua zake 7 katika kuwakamilisha watu wake, lakini haina maana kuwa Roho Mtakatifu wapo 7.

Kwa msingi huo basi twende tukazitazame jinsi anavyolikamilisha kanisa katika kifungo cha UMOJA katika hatua zake saba.

Tusome,

Waefeso 4:3 “ na kujitahidi kuuhifadhi UMOJA WA ROHO katika kifungo cha amani.

MWILI MMOJA, na ROHO MMOJA, kama na mlivyoitwa katika TUMAINI MOJA la wito wenu.

BWANA MMOJA, IMANI MOJA, UBATIZO MMOJA.

MUNGU MMOJA, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote”.

Tutazame moja baada ya nyingine:

1.MWILI MMOJA.

Mwili unaozungumziwa hapa ni Mwili wa Yesu, (Soma Waefeso 4:12 na Wakolosai 3:15), na Mwili huu unajengwa kupitia Vipawa na Karama ambazo Roho Mtakatifu ameziweka ndani yetu, ambapo kila mmoja ni kiungo ndani ya mwili huo.. Hivyo ili tuufikie umoja wa Roho kama kanisa ni lazima tuenende katika msingi huu kwamba kanisa linaongozwa katika karama za Roho Mtakatifu, na si itikadi, mapokeo au siasa.

1Wakorintho 12:13  “Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.

14  Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi”.

2. ROHO MMOJA.

Anaposema Roho mmoja, zipo roho nyingi, hata shetani naye ni roho.. ikiwa na maana kuwa ndani ya kanisa ni lazima tuwe na Roho mmoja anayezaa matunda yanayofanana kwa wote. Na matunda ya Roho ni yale yanayotajwa katika Wagalatia 5:22, kupitia hayo, tutakuwa tumekamilka katika kifungo cha pili cha Roho. Ndio maana biblia inatufundisha kuzichunguza roho, kwamaana zipo roho nyingi..

2Wakorintho 11:4 “Maana yeye ajaye akihubiri Yesu mwingine ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea ROHO NYINGINE MSIYOIPOKEA, au injili nyingine msiyoikubali, mnatenda vema kuvumiliana naye”

3. TUMAINI MOJA

Tumaini linalozungumziwa hapa ni “Tumaini la Utukufu ujao”.. Kwamba kila aliyeokoka analo tumaini la kuingia katika utukufu wa Mungu ujao,(Mbingu mpya na nchi mpya). Hili ni tumaini ambalo Kanisa lazima liufikie, na si kila mmoja anaamini analoliamini, kwasababu wapo wengine wanaosema hakuna ufufuo, mtu akifa amekufa!, jambo ambalo ni kinyume kabisa na maandiko. Ufufuo upo, na watakatifu watafufuliwa na kuingia katika utukufu wa milele.

Wakolosai 1:26  “siri ile iliyofichwa tangu zamani zote na tangu vizazi vyote, bali sasa imefunuliwa kwa watakatifu wake;

27  ambao Mungu alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo utajiri wa utukufu wa siri hii katika Mataifa, NAO NI KRISTO NDANI YENU, TUMAINI LA UTUKUFU”

4. BWANA MMOJA

Yupo Bwana mwingine (yesu mwingine), anayehubiriwa tofauti na yule wa kwenye maandiko matakatifu.

2Wakorintho 11:4 “Maana yeye AJAYE AKIHUBIRI YESU MWINGINE ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea roho nyingine msiyoipokea, au injili nyingine msiyoikubali, mnatenda vema kuvumiliana naye”.

Yesu mwingine ni yule anayesema Mungu haangalii mwili anaangalia Roho, ni yule anayesema mchukie adui yako, n.k. Lakini yule halisi anasema Mwombee adui yako, waombeeni wale wanaowaudhi, na wasameheni wale wanaowaudhi (Mathayo 5:43).

5. IMANI MOJA

Imani moja ni sahihi ni ile inayosema mpatanishi kati ya Mungu na mwanadamu ni mmoja (naye ni YESU KRISTO), Lakini Imani nyingine inasema “watakatifu waliokufa pia wanaweza kuwa wapatanishi” hivyo wanaweza kutuombea…

1Timotheo 2:5  “Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu”.

Vile vile inasema, mwombezi wetu kwa Baba ni yeye mmoja Yesu Kristo ( 1Yohana 2:1) na wala hakuna mwingine, lakini Imani nyingine inasema waombezi wanaweza kuwa wengi mbinguni. Hivyo kanisa ni lazima lifikie umoja wa Imani ya kweli ya kwenye biblia, kwamba mpatanishi ni mmoja na mwombezi ni mmoja, ambaye ni Yesu Kristo, na wala hakuna mwingine wa kumsaidia.

6. UBATIZO MMOJA.

Ubatizo mmoja wa kimaandiko ni ule wa Maji mengi (Yohana 3:23) na kwa jina la Bwana Yesu Kristo (Matendo 2:38, Matendo 10:48, Matendo 19:5). Ni lazima kanisa lifikie huu umoja, na si kila mmoja kuamini ubatizo wake.

7. MUNGU MMOJA.

Mungu mmoja wa kweli  ni yule aliyeumba mbingu na nchi, ambaye ni Baba wa yote, aliyeko juu mbinguni na si sanamu, wala miti, wala wanadamu. Hivyo ni lazima ndani ya mwili wa Kristo wote tufikie umoja huu wa kumwamini na kumwabudu Mungu mmoja, na kuchanganya ibada na miungu mingine au sanamu.

Adui anafanya kazi kwa nguvu, kuuvunja UMOJA HUU WA ROHO, kwasababu anajua ndio NGUVU YA KANISA, anataka kuweka umoja wake mwingine wa kidunia ndani ya kanisa, na kuutafsiri kama ndio umoja wa roho. Hivyo hatuna budi kuwa makini na kuyaishi maandiko.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mada Nyinginezo:

JE UNAMHUBIRI KRISTO KATIKA KWELI YOTE?.

Roho Mtakatifu ni nani?.

NI KWASABABU YA YESU KRISTO.

TUMAINI NI NINI?

Dinari ni nini na Rupia ni nini (Mathayo 20:2,Ufunuo 6:6)

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments