UTUKUFU WA MUNGU, UPO KATIKA UMOJA

UTUKUFU WA MUNGU, UPO KATIKA UMOJA

Umoja katika Ukristo ni jambo linalokimbiwa na wengi lakini ndilo jambo pekee lililobeba UTUKUFU WA MUNGU wa moja kwa moja. Na maana ya Utukufu wa Mungu ni “MUNGU KUTUKUZWA”.. Maana yake Mungu anatukuzwa katika Umoja.

Labda utauliza ni kwa namna gani?.. Tusome maandiko yafuatayo..

Yohana 17:22 “Nami UTUKUFU ULE ULIONIPA nimewapa wao; ILI WAWE NA UMOJA kama sisi tulivyo umoja.

23  Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi”

Kumbe Utukufu Kristo aliotuachia lengo lake la kwanza ni ili tuwe na UMOJA.. Na si kutenda miujiza, na maajabu.. Maana yake Mungu anatukuzwa Zaidi katika UMOJA kuliko katika MIUJIZA na ISHARA. Na ndicho kitu pekee kilicho na nguvu ya kuwafanya watu wamwamini Mungu kuliko ishara na miujiza.

Watu watakapoona umoja wetu katika Mungu, ndipo watavutwa kumwamini Mungu kuliko hata kuona ishara na miujiza halafu hamna Umoja… Na ndicho kitu pekee kinachotufanya sisi tumwamini BWANA YESU, ni kwasababu alikuwa na Umoja na Baba.

Laiti Bwana YESU asingelikuwa na umoja na Baba, ingelikuwa ngumu kumwamini kwa ishara na miujiza pekee, lakini ule Umoja wa Roho kati yake na Baba, umetutengenezea sisi Upendo wa ajabu, na Imani kuu kwa BWANA YESU KRISTO, Kwamba yeye ni kweli na hamna uongo ndani yake.

Na vile vile sisi tukiwa na Umoja na Mungu, na tukiwa na umoja sisi kwa sisi ndipo USHUHUDA WETU UTAKAPOTHIBITIKA ZAIDI kuliko kukaa katika matengano.

Yohana 17:21 “WOTE WAWE NA UMOJA; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ILI ULIMWENGU UPATE KUSADIKI YA KWAMBA WEWE NDIWE ULIYENITUMA.

22  Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja.

23  Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi”.

Hapo mstari wa 21 anasema.. “WOTE WAWE NA UMOJA ….ILI ULIMWENGU UPATE KUSADIKI YA KWAMBA WEWE NDIWE ULIYENITUMA”.

Kumbe UMOJA WETU ndio utakaowaaminisha watu kuwa KRISTO ni BWANA! Na si mahubiri yetu kuwa mengi, au miujiza yetu kuwa mingi…ni UMOJA TU!.

Tukilikataa Neno hili, na kufuata njia zetu za matengano, tutakuwa tunajipunguzia wenyewe utukufu wa Mungu, kwasababu KRISTO hakujitenga na Baba, wala hakujitenga na wanafunzi wake.

> Unapochagua kuomba peke yako kila mara na huku ipo nafasi ya kuomba na mwingine mmoja au wawili ni roho ya matengano inayoondoa utukufu wa Mungu. (Bwana wetu YESU KRISTO mara nyingi alipanda mlimani kuomba na wanafunzi wake, na hata katika sehemu za faragha soma Mathayo 17:1, na Marko 14:33-34).

> Unapochagua kila mara kwenda kuhubiri peke yako na wakati kuna nafasi ya kwenda na mwingine mmoja au wawili, ni roho ya matengano ambayo inapunguza utukufu wa Mungu juu yako (Bwana YESU aliwatuma wawili wawili kuhubiri katika miji na vijiji soma Luka 10:1 na Matendo 13:2).

> Unapochagua kila mara kutosema na ndugu yako, kumfariji, au kumtia moyo au kukaa karibu naye, ili hali ni mtu wa Imani moja nawe, mnamwamini Bwana mmoja, mmepokea roho mmoja, na hata ubatizo mmoja hiyo ni roho ya matengano inayoharibu utukufu wa Mungu juu yetu.

Hivyo ni lazima tuuhifadhi Umoja wa Roho kama Neno la Mungu linavyotufundisha ili tusipungukiwe na utukufu wa Mungu.

Waefeso 4:3 “na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani.

4  Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.

5  Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja.

6  Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote”

Bwana atusaidie na kutuwezesha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

TUUTAFUTE UMOJA WA ROHO.

JE UNAMHUBIRI KRISTO KATIKA KWELI YOTE?.

TAFUTA UZIMA WA MILELE NA SI UZIMA TU!.

MARINDA KATIKA BIBLIA NI KITU GANI?

BWANA ni mtu wa vita,  BWANA ndilo jina lake.(Kutoka 15:3)

Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments