TUNA WAJIBU WA KUOMBEA MAHALI TULIPO.

TUNA WAJIBU WA KUOMBEA MAHALI TULIPO.

Tuna wajibu wa kuombea mahali tulipo. hata kama ni pabaya kiasi gani.

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze Biblia, leo tutajifunza kwa ufupi umuhimu wa kuombea nchi tuliyopo, sehemu za kazi tulizopo, nyumba tunazoishi, mitaa tunayoishi hata kama ndani yake inatupa shida na mateso kiasi gani. Maadamu tunaishi ndani yake hatuna budi kuiombea.

Tunajifunza kwa wana wa Israeli kipindi kile walichomwudhi sana Mungu kwa dhambi zao. Mpaka kufikia hatua ya Mungu kuwaadhibu kwa kuwatoa katika nchi yao na kuwapeleka utumwani Babeli. Na tunaona tarehe za kwanza kwanza kabisa za wao kufika Babeli wakiwa na minyororo mikononi na miguuni, Mungu alimwambia Nabii Yeremia ambaye alibaki Israeli, kwamba awaandikie waraka waisraeli wote waliofungwa huko Babeli kwamba, hiyo nchi waliyoifikia waitakie mema.

Yeremia 29: 4 “Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, awaambia hivi watu wote waliochukuliwa mateka, niliowafanya wachukuliwe toka Yerusalemu mpaka Babeli;

5 Jengeni nyumba, mkakae ndani yake, kapandeni bustani, mkale matunda yake;

6 oeni wake, mkazae wana na binti; kawaozeni wake wana wenu, mkawaoze waume binti zenu, wazae wana na binti; mkaongezeke huko wala msipungue.

7 Kautakieni amani mji ule, ambao nimewafanya mchukuliwe mateka, MKAUOMBEE KWA BWANA; KWA MAANA KATIKA AMANI YAKE MJI HUO NINYI MTAPATA AMANI”.

Unaona hapo?. Ni mji wa shida ni mji wa mateso na mji wa Ugenini, Ni mji wa wapagani, waabudu mizimu, ni mji ambao uliuteketeza mji wao na kuuwa ndugu zao. Lakini Bwana anawaambia wauombee amani mji huo, wasiulaani.

Kwanini?

Ni kwasababu Mji huo ukiwa na Amani na wao watapata amani, na kinyume chake mji huo ukichafuka na wao watapata tabu. Hilo ni funzo tosha la hali tunazopitia sasa, kuna umuhimu mkubwa sana kuombea mahali tulipo, Nchi unayoishi, hata kama sio nchi yako lakini maadamu unaishi ndani ya hiyo nchi ni lazima uiombee. Kwasababu madhara yakija hata kama unamcha Mungu kiasi gani na wewe pia yatakuathiri tu.

Hebu fikiria vita vitokee ghafla katika nchi uliyopo, mabomu yakapigwa huku na kule. Barabara zikaharibika, miundombinu ya maji na umeme ikaharibika kiasi kwamba maji yakakosekana na umeme vilevile. Unadhani wewe unayemcha Mungu jambo hilo halitakuathiri?..Litakuathiri tu kwa namna moja au nyingine. Kwasababu unahitaji barabara kupitisha gari lako,..unahitaji umeme kuendesha shughuli zako..Unahitaji maji kwa matumizi yako binafsi na mifugo yako..Watoto wako wanahitaji kwenda shule, na sasa hawawezi kwenda tena kwasababu mji umechafuka n.k

Kwahiyo ni muhimu kuombea sehemu tulipo. Kadhalika unaishi kwenye nyumba ambayo si yako, wewe ni mgeni au mpangaji, au si mwanafamilia . Lakini umekaribishwa tu katika hiyo nyumba, Ni wajibu wako kuiombea hata kama hupati hisani wanazozipata wanafamilia. Ni wajibu wako kuiombea kwasababu Nyumba hiyo ikipata Amani nawe pia utanufaika kwahiyo amani…lakini usipoiombea ikipata shida na wewe hutasalimika utateseka mara mbili.

Sehemu zote ulizopo..

Vivyo hivyo katika sehemu ya kazi uliyopo. Una wajibu wa kuiombea hata kama wewe ndiye mfanyakazi unayelipwa mshahara kidogo kuliko wote..Kwasababu ukipaombea pakistawi na wewe pia utastawi..Lakini pakididimia na wewe utaathirika tu. Ndio maana Mungu akawaambia wana wa Israeli hapo juu “MKAUOMBEE KWA BWANA; KWA MAANA KATIKA AMANI YAKE MJI HUO NINYI MTAPATA AMANI”.

Ukiwa shuleni ni hivyo hivyo. Unaiombea shule uliyopo, au chuo. Kwasababu shule ikistawi na wewe utastawi ndani yake. Lakini usipoiombea na kuacha tu bila kujali, waalimu wakiwa wabaya itakuathiri na wewe… Miundo mbinu ikiwa mibovu itakuathiri na wewe… Wanafunzi wenzako wanaokuzunguka wakiwa wabaya utapata usumbufu usio wa lazima..Haijalishi wewe utakuwa mkamilifu kiasi gani, hizo tabu hutazikwepa. Na mambo mengine yote ni hivyo hivyo..Ni lazima kuyaombea. Ni lazima kuombea mahali tulipo Mpaka hapo Naamini utakuwa umeongeza kitu juu ya vile unavyovijua.

Bwana akubariki sana.

Kama hujampa Yesu Kristo Maisha yako. Mlango upo wazi ila hautakuwa hivyo siku zote. Wakati dunia inafurahia anasa…Ujio wa Kristo unazidi kukaribia kila sekunde inayosogea, ujio wake upo karibu kunashinda tunavyofikiri. Watu wa ulimwengu wataomboleza siku ile watakapokuja kugundua kwamba walikuwa wanapoteza muda kujifurahisha na anasa za ulimwengu. Bwana atusaidie tusiwe mimi na wewe. Hivyo Tubu kama hujatubu, na pia tafuta ubatizo kama hujabatizwa, na Upokee Roho Mtakatifu. Kwa hatua hizo tatu utakuwa umekamilisha wokovu wako.

Maran atha!jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

Maandiko yanasema Eliya aliomba kwa bidii hadi akasimamisha mvua kunyesha kwa MUDA wa miaka 3 na nusu.(Yakobo5:17) Je! kuomba kwa bidii ni kuomba kwa namna gani?

UWE MWAMINIFU HATA KUFA.

SIKU ILE NA SAA ILE.

UMEPATANISHWA NA MAADUI ZAKO?

JIEPUSHE NA MANENO YA MANABII WA UONGO.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments