UWE MWAMINIFU HATA KUFA.

UWE MWAMINIFU HATA KUFA.

Uwe mwaminifu hata kufa…

Ufunuo 2:2 “Nayajua matendo yako, na taabu yako, na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena umewajaribu wale wajiitao mitume, nao sio, ukawaona kuwa waongo;

3 tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka”.

Wengi wanasema Kristo hatujali.. Lakini kiuhalisia ni kwamba anatujali kuliko sisi tunavyodhani. Kila kitu tunachokifanya anakiona, na anakihesabu. Hakuna kinachoenda bure mbele zake. Alisema katika Neno lake “lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote.( Mathayo 10:30)”. Sasa mtu anayejua idadi ya nywele zetu zote na hakuna hata moja inayopotea bila yeye kujua ataachaje kufahamu kila tendo jema tunalolifanya?

Ukiona mtu anasema naijua tabu yako. Ni wazi kuwa ni mtu anayejali….tena anakuambia najua Taabu yako na shida zako unazozipitia, anajua uvumilivu wako, na subira yako…Na anajua jitihada zako na jinsi gani huchoki kufanya mema. Ni wazi kuwa ni mtu anayekujali sana na anap moyo wa upendo na wewe.

Ndio maana tunasoma katika kitabu cha Ufunuo, Bwana Yesu alipotoa ujumbe kwa kila kanisa alianza na Neno hili “Nayajua matendo yako,”. Ikifunua kuwa Bwana anatujua sana, kila dakika anatuangalia..Kama ni mabaya tunayafanya anayaona, vile vile kama mema tunayafanya anayaona..Leo ulimhurumia mtu Fulani mnyonge anaona!. Na anarekodi, leo ulimsamehe mtu aliyekuudhi ingawa alikuumiza sana kiasi kwamba ilikuwa hata ni ngumu kumsamehe lakini ulimsamehe tu hivyo hivyo, anakuona. Na atalitaja tukio hilo siku ile mbele ya malaika wake watakatifu.

Ulimhurumia mtu Fulani na kumsaidia katika hali aliyokuwepo. Analiona tendo hilo.

Ulimwombea mwingine katika maombi yako, ingawa yeye hakuna lolote analokufanyia. Bwana anaona na analiandika katika kumbukumbu isiyoweza kusahaulika. Ulitukanwa ukavumilia na wala hukurudisha tusi anaandika. Ulimtolea sadaka yako ingawa ndio hiyo tu uliyokuwa nayo huna nyingine. Ameliweka moyoni mwake zitapita siku kadhaa wewe utasahau lakini yeye lipo moyoni mwake. Kila siku kila dakika linamrudia rudia katika mawazo yake milele na milele.

Wakati mwingine ingawa unaomba lakini majibu yanachelewa, lakini bado unamvumilia. Jambo hilo analiona na uvumilivu wako kwake, upo akilini mwake kila dakika. Mateso na dhiki unazopitia ambazo bado hujaona tumaini na bado hujaiachilia Imani. Nataka nikuambia anaona! Na inamwingia moyoni kuliko hata wewe inavyokusumbua.

Sehemu nyingine anasema “Nayajua matendo yako na upendo na imani na huduma na subira yako; tena kwamba matendo yako ya mwisho yamezidi yale ya kwanza. (Ufunuo 2:19)”

Ufunuo 2:8 “Haya ndiyo aneneyo yeye aliye wa kwanza na wa mwisho, aliyekuwa amekufa, kisha akawa hai.

9 Naijua dhiki yako na umaskini wako, (lakini u tajiri) najua na matukano ya hao wasemao ya kuwa ni Wayahudi, nao sio, bali ni sinagogi la Shetani.

10 Usiogope mambo yatakayokupata; tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.”

Wakati mwingine huyu huyu Yesu wetu mwema anaruhusu tujaribiwe kwa dhiki na vifungo. Na wakati mwingine anakaa mbali kama vile hayupo. Tambua ya kwamba yupo pembeni yako hata wakati wa tabu. Na anaiona shida yako, Anasema Uwe mwaminifu tu hata kufa. Naye atakupa Taji ya Uzima,Usianze kunung’unika nung’unika kama walivyofanya wana wa Israeli kule jangwani. Ukifanya hivyo utapoteza Taji yako.

Bwana Yesu naye alipitia majaribu mazito kuliko hata sisi. Yeye alitiwa mikononi mwa shetani ili ajaribiwe, akatundikwa msalabani. Na wakati akiwa msalabani japo kuwa alikuwa ni mwana wa Mungu lakini alisikia hali Fulani ya ukame wa kiroho isiyokuwa ya kawaida mpaka akasema Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?. Lakini alikuwa mwaminifu mpaka kufa hakuikana imani wala kunung’unika akiwa pale msalabani. Na Mungu akampa Taji ya Uzima ambayo leo hii tunamtukuza kama MFALME MKUU ASIYESHINDWA. Haleluya!.

Kwahiyo na sisi wakati mwingine Mungu ataruhusu tujaribiwe. Ila tunapaswa na sisi tuwe waaminifu mpaka kufa. Tukifahamu kuwa Mwangalizi wetu yupo mbinguni akirekodi kila tukio na kila tendo jema tunalolipitia, akirekodi kila chozi, na kila tendo tunalolivumilia. Akirekodi kila jeraha tunaloumizwa na tunaposamehe. Tukilitambua hilo itatufanya tuishi maisha ya kujipa moyo kila siku Kuwa mateso ya Ulimwengu huu ni ya kitambo tu. Ipo taji tumewekewa mbinguni. Na upo wakati wa kufutwa machozi.

Malaki 3:13 “Maneno yenu yamekuwa magumu juu yangu, asema Bwana. Lakini ninyi mwasema, Tumesema maneno juu yako kwa namna gani?

14 Mmesema, Kumtumikia Mungu hakuna faida; na, Tumepata faida gani kwa kuyashika maagizo yake, na kwa kwenda kwa huzuni mbele za Bwana wa majeshi?

15 Na sasa twasema ya kwamba wenye kiburi ndio walio heri; naam, watendao uovu ndio wajengwao; naam, wamjaribuo Mungu ndio waponywao.

16 Ndipo wale waliomcha Bwana waliposemezana wao kwa wao. Naye Bwana akasikiliza, akasikia; na kitabu cha ukumbusho kikaandikwa mbele zake, kwa ajili ya hao waliomcha Bwana, na kulitafakari jina lake.

17 Nao watakuwa wangu, asema Bwana wa majeshi, katika siku ile niifanyayo; naam, watakuwa hazina yangu hasa; nami nitawaachilia, kama vile mtu amwachiliavyo mwanawe mwenyewe amtumikiaye”.

Bwana akubariki.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

KITABU CHA UKUMBUSHO

UNATAKA KUBARIKIWA? BASI USIKWEPE GHARAMA ZAKE.

PENGINE MUNGU ALISHASEMA NAWE KWA NJIA HII.

INJILI YA KRISTO HAITANGAZWI KWA HATI MILIKI.

SIKU ILE NA SAA ILE.

WOKOVU NI SASA

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Ibrahim Njela
Ibrahim Njela
2 years ago

Hallelujah, jina LA BWANA lihimidiwe. Nafurahia mafundisho haya Mungu awabariki sana. Msichoke katika kufundisha, kutangaza habari njema za injili ya Yesu Kristo kuhusu toba iletayo ondoleo La dhambi na kuurithi ufalme wa Mungu. Amebarikiwa mtu wa kujitoa kwa ajili ya injiri maana aiponya nafsi yake. Ongera sana.