Ni kitu cha kushangaza jinsi injili ya Kristo, Bwana wetu inavyogeuzwa leo hii kutoka katika kitu cha kutolewa bure hadi kuwa kitu cha kutolewa kwa masharti,.Tunaweza tukadhania ni ustaarabu mzuri kufanya hivyo lakini kibiblia huo haukuwa mpango wa Kristo tangu zamani alipowaita mitume wake..kwasababu ni jambo linalozuia injili ya Kristo kusonga mbele. Na leo tutaona ni kwa namna gani.
Embu tafakari kwa utulivu jambo hili walilolifanya mitume, na majibu Bwana YESU aliyowapa,
Marko 9:38 “Yohana akamjibu, akamwambia, Mwalimu, tulimwona mtu akitoa pepo kwa jina lako, ambaye hafuatani nasi; tukamkataza, kwa sababu hafuatani nasi. 39 Yesu akasema, Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya mwujiza kwa jina langu akaweza mara kuninenea mabaya; 40 kwa sababu asiye kinyume chetu, yu upande wetu”.
Marko 9:38 “Yohana akamjibu, akamwambia, Mwalimu, tulimwona mtu akitoa pepo kwa jina lako, ambaye hafuatani nasi; tukamkataza, kwa sababu hafuatani nasi.
39 Yesu akasema, Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya mwujiza kwa jina langu akaweza mara kuninenea mabaya;
40 kwa sababu asiye kinyume chetu, yu upande wetu”.
Mitume walipomwona mtu huyu anatenda kazi zile zile wanazozifanya wao, wanatumia jina lile lile wanalolitumia wao, tunaweza kusema pia anawabatiza watu vilevile kama wanavyowabatiza wao, anafufua wafu vilevile kama wanavyofufua wao, badala ya wao kumfurahia na kumchukua wafanye naye kazi pamoja, kinyume chake wanamkemea na kumkataza kwamwe asikae kufanya kitu kama hicho tena, pengine walimtisha na kuahidi kumshitaki endapo atarudia kutumia jina hilo bila idhini yao…Na hiyo yote ni kwasababu moja tu, kwamba HAFUATANI NAO basi! Hakuna kingine, wala hakuna ubaya wowote waliuona ndani yake…ni kwasababu tu HAFUATANI NAO! Embu jaribu kufikiria mtu yule alipotoka pale alivunjika moyo kiasi gani..ule moto uliokuwa ndani yake ulizimishwa ghafla kwa kiasi gani, alikuwa anahubiri injili kwa kujifichaficha akiogopa labda pengine wale watu watamwona tena na kumkamata na kumpeleka kwa kadhi.
Na Zaidi ya yote alitegemea pengine hao Mitume ndio wangekuwa wakwanza kumsapoti lakini kinyume chake wakawa wakwanza kumpinga.
Hata leo hii, Hicho ndio kikwazo cha watumishi wengi wa Mungu, wapo watu wengi wanaotamani kumhubiri Kristo kwa mafundisho yao, au vitabu vyao, au nyimbo zao, lakini wanatishwa na vikwazo vya namna hiyo, wanaogopa wakifanya tu, watakamatwa na kuambiwa ni nani kakupa ruhusu ya kusambaza hiki au kile.
Wameiwekea injili hati miliki kwamba mtu huwezi kufundisha wanachokifundisha wao, mpaka upewe kibali fulani kutoka kwao, huwezi kuziimba nyimbo zao mahali fulani mpaka upewe kibali fulani kutoka kwao, ili ulipie kwanza kiwango fulani cha fedha..Injili ya Kristo nayo imegeuzwa na kuwa kama staili ya kibiashara hivi, kwamba mtu fulani amegundua aina yake ya mafundisho basi hataki mwingine aibe aifundishe sehemu nyingine, ameimba nyimbo fulani, hataki mwingine aiimbe mahali pengine kwa utukufu wa Mungu..lengo tu ni ili nyimbo yake isichuje haraka au aitwe yeye aimbe ili apate faida kidogo..Ndivyo ilivyo sasa hivi.
Kipindi fulani nyuma, kuna ndugu nilimuhubiria akakata shauri la kuokoka, hivyo akawa anahitaji abatizwe pia, kwa kuwa mkoa aliokuwepo ni mbali kidogo na mimi nilipo ikanibidi nimtafutie kanisa la kiroho liliokaribu naye abatizwe na adumu katika fundisho la pale, lakini nilipopiga simu na mhudumu mmojawapo wa kanisa alipokea, ili nimkabidhishe huyo mtu kwake, kuzungumza naye tu maneno machache na kugundua mimi sio mshirika wa makanisa yao, akasema mimi ni ndugu wa uongo, ni nani aliyenipa ruhusu hiyo, hawakutaka kusikia habari yangu, hata na huyo kondoo ambaye alikuwa anatafuta malisho..Nilihuzunika na kushangaa sana,..kwani hawakuangalia faida ya Kristo bali waliangalia je kama hichi kitu kinatoka katika jumuiya yao ya kidini kama mitume walichokuwa wanajaribu kukifanya.
Vitabu au Makala za Kikristo tunazozichapishwa, tunachopaswa kuzuia tu kwa wale wanaofanya na kuuza kwa biashara, lakini kama ni mtu ameona upo ujumbe mzuri ndani yake ambao unaweza kuwabadilisha wengine, hivyo akaamua kwenda kuchapisha Makala hizo nyingi na kwenda kuzitoa bure kwa watu wengine bila hata ya kukueleza, au kupata idhini yako, wewe unakwazika nini katika hilo? wewe hofu yako ni nini? Kwani kazi hiyo ni yako au ya Kristo?. Kwanini kila kitu unawaza kukiwekea mipaka na vizuizi, hujui kuwa kazi ya Kristo inasimama kwa ajili yako. Mwingine akisikia kuna mtu kahubiri mahali pengine kitu alichokihubiri yeye na hajatajwa jina anapata wivu?.
Kwanini upate wivu? Kuna umuhimu gani wa kukutaja wewe kama kweli una Nia ya Kristo ndani yako? Unapaswa ufurahi kwasababu ulichokizaa wewe kimekwenda kuzaa vingine vingi, sasa hiyo si ni faida? Wengine mpaka wanawapa masharti wanaowahubiria kwamba watakapohubiri mafundisho yao mahali pengine wawataje!.
Yule mtu aliyekuwa anatenda miujiza kwa jina la YESU alitambua kabisa kuwa Kristo mwenyewe yupo duniani, na kwamba angetaka kwenda kumwomba ruhusa angekwenda, lakini yeye hakuona hata ulazima wa kumwomba Ruhusa mwenye jina lenyewe badala yake aliliondoka kimya kimya na kwenda kuuendeleza ufalme,..Na Kristo hakumkemea kwa hilo wala kumwita kutaka kumjua, aliona ni sawa tu..aendelee..
Iweje sisi ambao hata hatumwoni Kristo tuwazuie wengine wasimtangaze Kristo kwa kazi zetu?. Jitafakari vizuri wewe unayejiita kiongozi wa dini, wewe unayejiita mchungaji, wewe unayejiita mwalimu, wewe unayejiita mwandishi, wewe unayejiita MWIMBAJI WA NYIMBO ZA INJILI wewe unayejiita mwinjilisti, wewe unayejiita mshirika…
Usiwe kikwazo cha injili ya Kristo kuhubiriwa.
Shalom.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
HATARI YA KUHUBIRI INJILI TOFAUTI NA ILIYOANDIKWA KWENYE BIBLIA.
KIWANGO CHA TATU CHA IMANI.
SADAKA YA MALIMBUKO.
Yeshuruni ni nani katika biblia?
Rudi Nyumbani:
Print this post