BUSTANI YA NEEMA.

BUSTANI YA NEEMA.

Jina la Bwana Yesu litukuzwe. Karibu tujifunze Biblia tena.

Tunasoma katika kitabu cha Mwanzo. Baada ya Adamu na Hawa kula matunda ya mti wa ujuzi wa Mema na Mabaya ambayo waliagizwa wasiyale. Macho yao wote wawili yalifumbuliwa na kujijua kuwa wapo uchi.

Mwanzo 3:6 “Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala.

7 Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo”.

Matokeo ya kufumbuliwa macho ni kujisitiri. Na yaliyofumbuliwa ni macho yao ya rohoni, na si ya mwilini.

Baada ya kula tunda walichomwa mioyo na kujigundua kuwa wamefanya makosa makubwa sana. Ulishawahi kufanya kitu ambacho baada ya kumaliza kukifanya Moyo wako ukakuchoma sana! Kwa ulichokifanya?.

Au Ulishawahi kumkosea Mtu Fulani Labda ni boss wako au mkubwa wako mahali Fulani?ambaye sikuzote alikuwa ni mwaminifu kwako, na anakuamini na anakujali na kukupenda sana kwa dhati, wala hajawahi kukufanyia jambo lolote baya?. Halafu baadaye akajua ubaya uliomfanyia na hata baada ya kujua hajakuongelesha chochote.

Unajua huwa Kuna hali Fulani inakuja ambayo unaona aibu hata kukutana naye kumwangalia usoni! Unakuwa unamkwepa kwepa tu muda wote. Unaanza kujihukumu kabla hata ya yeye kukuhukumu.Hata ukikutana naye uso kwa uso unatamani uongee naye kwa dakika chache sana tena ikiwezekana huku umevaa miwani, au huku unaangalia chini. Maana utasikia aibu sio aibu. Usaliti sio usaliti, yaani hali Fulani isiyoelezeka.

Ndicho kilichowatokea wazazi wetu wa Kwanza Adamu na Hawa.

Kwa walichokifanya mbele ya macho ya Mungu iliwafanya wajione wao sio kitu tena, hawana maana tena. Wafiche wapi nyuso zao?. Wafiche wapi viungo vyao mbele za Mungu?. Watawezaje tena kumwangalia Mungu usoni, ambaye hapo kwanza alikuwa anatembea nao kama rafiki? Na anawaamini?..Ni uchungu uliochanganyikana na Aibu.

Suluhisho lililobaki ni kujificha tu mbele ya uso wa Mungu, na kutafuta njia ya kumkwepa kwepa. Ndio unaona sasa wakaamua kutengeneza nguo kwa majani ya mtini. Kumbuka hawakushona nguo kwasababu wanaoneana aibu wao kwa wao. Hapana wao walikuwa hawaoneani aibu. Waliyekuwa wanamwonea aibu ni Mungu.

Na pia nguo hizo za nyasi walizojitengenezea hazikufunika tu sehemu zao za siri, bali zilifunika mwili mzima mpaka kichwa. Kwasababu ni Aibu!. Utawezaje kuonyesha kifua chako tena mbele za Mungu? Uso tu shida, si zaidi mgongo au kifua au mapaja?. Ndio maana waliendelea mpaka kujificha katikati ya vichaka!. Kujishonea nguo za nyasi peke yake waliona haitoshi.

Ndugu sasahivi katika nyakati hizi tupo katika Bustani ya Mungu inayoitwa Neema. Bustani hii ni Bustani ya Yesu Kristo, ambayo anatembea na sisi kama Rafiki. Kama Mungu alivyotembea na Adamu pale Edeni.

Yohana 15:14 “Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo.

15 Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu”.

Neema ni kitu cha ajabu sana, Maana unaweza kupata chochote utakacho, kwa jina la Yesu, Msamaha wa dhambi unapatikana ndani ya Neema, uponyaji, Baraka n.k. Ni kama Edeni tu! Kila kitu kilikuwa kinapatikana pale bila nguvu nyingi.

Lakini Neema hii tulionayo sisi haitadumu milele maandiko yanasema hivyo. Wakati huu ambapo Yesu kwetu ni Rafiki. Kuna wakati utafika huyu huyu Yesu tunayempenda sasa na kumwona ni rafiki, Na kuufurahia wema wake atageuka na kuwa Mhukumu.

Wakati huo wewe unayeidharau injili sasa macho yako yatafumbuliwa na utasema!.. Nifiche wapi uso wangu huu na aibu hii kwa kuidharau Neema niliyokuwa nimepewa?..Hutatamani hata kusimama mbele za Bwana Yesu, ambaye leo hii anatembea kwako kama rafiki. Ambaye unaweza ukajiamulia chochote tu na asikueleze.

Adamu na Hawa hawakutamani hata kuuona uso wa Mungu kadhalika Yuda baada ya kumsaliti Bwana Yesu, yeye naye yalifumbuliwa macho yake na kujiona yupo uchi katika roho, aliona ni heri akajinyonge kuliko hata kwenda kumtazama pale msalabani. Akasema

Mathayo 27:3 “Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, alipoona ya kuwa amekwisha kuhukumiwa, alijuta, akawarudishia wakuu wa makuhani na wazee vile vipande thelathini vya fedha, akasema, Nalikosa nilipoisaliti damu isiyo na hatia.

4 Wakasema, Basi, haya yatupasani sisi? Yaangalie haya wewe mwenyewe.

5 Akavitupa vile vipande vya fedha katika hekalu, akaondoka; akaenda, akajinyonga”.

Adamu na Hawa walijuta na hivyo kuishia Hukumu kubwa kama ile mpaka sisi vitukuu vya vitukuu tunashiriki laana yao.

Je! Itakuwaje siku ile macho yako yatakapofumbuliwa mbele ya kiti cha Hukumu? Ni majuto ya milele katika ziwa la moto, wala usifikiri siku ile utaona kama umeonewa! Utakiri kwamba ni kweli ulikosa na unastahili adhabu! Kama Yuda alivyokiri.

Wakati huu ambapo utukufu wa Neema ya Mungu upo. Wakati Kristo ni rafiki. Ushikilie wokovu, usisikilize uongo wa shetani, leo hii unaokuambia kunywa pombe sio shida, unaokuambia kuvaa vimini sio shida, kuvaa suruali kwa mwanamke sio shida! Kuishi na mtu ambaye hamjafunga naye ndoa sio shida!..Ukisikiliza huo uongo na kuutii ni kweli sasa hutaona kwamba ni shida sasa. Lakini siku ile utajuta sana macho yako yatakapofumbuliwa.

Waebrania 10:29 “Mwaonaje? Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, na kumfanyia jeuri Roho wa neema?

30 Maana twamjua yeye aliyesema, Kupatiliza kisasi ni juu yangu, mimi nitalipa. Na tena, Bwana atawahukumu watu wake.

31 Ni jambo la kutisha kuanguka katika mikono ya Mungu aliye hai”.

Ikiwa hujaokoka. Unapaswa uokoke sasa hivi. Na si kesho, kwasababu saa ya wokovu ni sasa. Hapo ulipo jitenge dakika chake peke yako, Omba toba ya dhati mbele ya Mungu Baba, mwambie akusamehe makosa yako yote uliyoyafanya huko nyuma na unayoyafanya sasa. Na kwamba hutaki kuyafanya tena. Na kisha baada ya toba hiyo, Amani Fulani ya kiMungu itakuja ndani yako. Ambayo utahisi kama kuna mzigo Fulani umeondoka. Amani hiyo ni uthibitisho kwamba umesamehewa.

Hivyo kuihifadhi hiyo amani shetani asiiibe, nenda katafute mahali wanapobatiza ubatizo sahihi wa maji tele na kwa jina la Yesu Kristo. Ubatizwe hapo kama hujabatizwa. Na kama ulishabatizwa hivyo kwa usahihi huna haja ya kubatizwa tena.

Utaanza kuona Roho Mtakatifu aliyeingia ndani yako akiyatengeneza maisha yako upya kwa namna ambayo hatuwezi tukaelezea hapa. Wewe mwenyewe utaona. Kikubwa hapo ni kumkubali tu Kristo tu katika Maisha yako na kufuta yote anayokulekeza, yaliyosalia yeye mwenyewe atayashughulikia.

Bwana akubariki.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo;

Nifanyaje ili nijue kuwa uamuzi ninaokwenda kuchagua kufanya ni mapenzi ya Mungu?

DHAMBI ILIYOMKOSESHA SHETANI:

KWANINI DAUDI ALIKUWA NI MTU ALIYEUPENDEZA MOYO WA MUNGU?

JISHUSHE ILI MUNGU AKUHUDUMIE.

Rudi Nyumbani;

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
2 years ago

AMEN Watumishi