Nifanyaje ili nijue kuwa uamuzi ninaokwenda kuchagua kufanya ni mapenzi ya Mungu?

Nifanyaje ili nijue kuwa uamuzi ninaokwenda kuchagua kufanya ni mapenzi ya Mungu?

SWALI : Ninatamani kwenda kusomea udaktari , lakini nina mashaka labda sio mapenzi ya Mungu kwangu, inanifanya nisiwe na maamuzi ya kueleweka..Naomba ushauri nifanyeje ili nijue masomo Mungu aliyoyakusudia nisomee katika maisha yangu.?


JIBU: Swali hilo linafanana na lile la mtu anayemwomba Mungu mpenzi sahihi wa kuoa/kuolewa katika maisha yake.. Mara nyingi tunatarajia Mungu atufunulie aidha kwa ndoto au maono au unabii au kwa njia nyingine iliyo dhahiri juu ya mpenzi wa kuoa, na hiyo inatufanya tufikiri labda pengine Mungu asipotumia njia kama hizo kabisa basi tumeoa mke/mume asiyesahihi, au tumeingia mahali pasipotupasa.   Lakini kumbuka Mungu kujitambulisha kwetu kama MSHAURI WA AJABU,(Isaya 9:6) ni uthibitisho tosha kuonyesha kuwa Mungu sio dikteta wa mawazo ya mtu. Ikiwa na maana kuwa kama angekuwa hataki wewe uwe na uchaguzi wako binafsi, basi asingejitambulisha kwako kama mshauri badala yake angejiita “kamanda”..

Tatizo linakuja ni pale ambapo hatumfanyi Mungu kuwa mshauri wetu, na ndio hapo tunaingia katika maamuzi yasiyo sahihi..   Lakini mtu atajiuliza je! Tunamfanyaje Mungu kuwa mshauri wetu?..Jibu lipo wazi , na mashauri yake yapo wazi kabisa na karibu kila mtu anayafahamu na ameshayasikia, na hayo si mengine zaidi ya MAANDIKO MATAKATIFU.   Hivyo ikiwa tumefikiria kufanya jambo Fulani ambalo tumelipenda, pengine tunataka kuoa au kuolewa na mtu fulani, jambo la kufanya kwanza ni kutuliza akili, pata muda wa kutosha wa kuombea jambo hilo, kisha ukishamaliza hatua hiyo lichukue katika maandiko, uangalie je! Litapinga imani yako au la!..kwa mfano unaweza ukawa umetamani kweli kufanya biashara Fulani ya kuuza vinywaji,lakini ndani yake kuna pombe,..sasa hata kama uliiependa biashara hiyo lakini ushauri wa Mungu unakuambia hapana maandiko hayaruhusu pombe…  

Hivyo moja kwa moja unapaswa uache , utafuate kitu kingine. Inawezekana pia binti umempenda mwanaume mzuri, lakini ni wa imani tofauti, na yeye anataka mfunge ndoa muishi pamoja,..Lakini ushauri wa Mungu unakukataza katika maandiko, kwamba ndoa inapaswa ifungwe katika Bwana tu!, hivyo ikiwa mtu huyo hatataka kuigekia imani ya kweli ya Yesu Kristo, basi unachopaswa kufanya ni kukataa jambo hilo hata kama ulikuwa unampenda kiasi gani.. Hiyo ni kwa faida yako mwenyewe.  

Lakini ikitokea sasa umeshavipitisha vyote hivyo kwenye mizani ya ki-Mungu na kuona kuwa hakuna chochote kinachopingana na maandiko na ndani yako umekipenda kweli na unasikia amani kukifanya, kwamfano, unahitaji kwenda kusomea udaktari hapo hakuna ubaya wowote, maadamu tayari ulishatenga muda wa kumwomba Mungu akutangulie basi hiyo inatosha kukupa amani kuwa Mungu ameshakusikia..Hivyo usiogope kwenda kusomea..   Kwasababu biblia inasema.

Mithali 16:1 “Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu; Bali jawabu la ulimi hutoka kwa Bwana.”

Hivyo hata ikitokea hicho ulichomwomba Mungu kukifanya au kukitenda hakikuwa ni sawasawa na mapenzi yake, kwa kuwa ulishamshirikisha mawazo yako kabla ya kuingia basi yeye mwenyewe atahakikisha anakuepusha nacho, au atakuandalia mazingira mazuri ya kutimiza kusudi lake ndani yake. Kama hajakujibu kwa ndoto au maono vile vile atakuepushia nacho pasipo ndoto wala maono kama sio mpango wake..

Mungu wetu hatuweki kwenye mtego kwamba tumwombe akae kimya na aruhusu tufanye jambo fulani kimakosa ili kesho na kesho kutwa aje kutulaumu!..yeye hayupo hivyo wanadamu ndio wapo hivyo..   Kwahiyo Kikubwa tu hakikisha huchukui uamuzi wowote bila kuupeleka kwanza kwenye maombi kwa muda wa kutosha, (sio maombi ya chai, hapana walau tenga kipindi kirefu kidogo, kuonyesha umakini kwamba umekusudia kweli kumkabidhi Mungu njia zako, hata ikiwezekana funga siku kudhaa,) ,Na pili hakiki kama kinaathiri imani yako au kinapingana na maandiko..ikiwa vitu hivyo viwili umevizingatia ipasavyo na hakuna shida basi endelea mbele kufanya unachotaka kufanya kwasababu Mungu atakuwa pamoja na wewe kuyaonyoosha mapito yako. Usisubiri ndoto wala maono.

Mithali 16:3 Mkabidhi Bwana kazi zako, Na mawazo yako yatathibitika.

Lakini kama unasubiria maono au ndoto, au malaika akutokee ndipo achukue hatua…nakushauri acha kwasababu unaweza ukavunjika moyo pale ambapo majibu yatakuja usivyotarajia kwa kutokuona chochote, na mwisho wa siku ukajikuta upo njia panda hujui lipi la kufanya.  

Ubarikiwe sana.


Mada nyinginezo:

NJIA YA ‘UTAJIRI MKUU’ KWA KIJANA.

NJIA YA BWANA INATENGENEZWA WAPI?

NJIA SAHIHI YA KUFUNGA.

PENGINE MUNGU ALISHASEMA NAWE KWA NJIA HII.

NI NANI ALIYEIDHARAU SIKU YA MAMBO MADOGO?

IMANI “MAMA” NI IPI?


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments