KIWANGO CHA TATU CHA IMANI.

KIWANGO CHA TATU CHA IMANI.

Kuna aina tatu za Imani zilizoonekana katikati ya kundi lililokuwa likumfuata Yesu waponywe.

Kundi la Kwanza: Ni lile lililohakikisha kuwa linamwona Yesu uso kwa uso, na kuzungumza naye, na kumwomba Bwana Yesu awaponye au kama mgonjwa wao hayupo hapo basi litahakikisha Bwana Yesu anaambata nao hadi makwao ili waombewe, Kundi hili linatabia ya kumwachia Yesu afanye shughuli zote.

Kundi hili ndio lililokuwa kubwa kushinda yote, na hata leo lipo na ni kubwa pia, hawa ndio wale watu ambao ni ili waponywe au wafanyiwe haja zao ni lazima wawatafute watumishi wa Mungu mahali popote walipo kwa gharama zozote zile, wapo radhi kwenda mpaka Nigeria, china bila kujali gharama za fedha wanazoingia ilimradi tu waonane na watumishi wa Mungu wawaombee.

Kundi la Pili:

Ni lile ambalo, lilipata ufunuo wa Zaidi wa kutambua uweza wa Yesu, Hivyo halikuhitaji mpaka Yesu afike nyumbani kwao ndipo waponywe. Mfano wa hili ni yule Akida aliyemfuata Yesu..

Tusome..

Mathayo 8:5 “Hata alipoingia Kapernaumu, akida mmoja alimjia,

6 akamsihi, akisema, Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza, anaumwa sana.

7 Yesu akamwambia, Nitakuja, nimponye.

8 Yule akida akamjibu, akasema, Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu; lakini sema neno tu, na mtumishi wangu atapona.

9 Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya.

10 Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa namna hii, kwa ye yote katika Israeli”.

Unaona mtu huyu alitafakari kwa ukaribu sana akaangalia na kazi yake anayoifanya kila siku ya Uakida akasema moyoni mwake kama mimi nikitoa tu amri kwamba kitu fulani kifanyike , huwa kinatendeka haraka sana hata kama mimi sipo huko..Sasa si Zaidi huyu ambaye ni Masihi mwenyewe, mkuu wa ufalme wa mbinguni, anao uwezo pia wa kunitamkia tu uponyaji mahali nilipo na malaika zake wakalishughulika na hilo mara moja na mambo yote yakawa sawa..

Hivyo kwa ufunuo huo huo akamwambia Bwana huna haja ya wewe kuja nyumbani kwangu, ya nini kujichosha, wakati unalo jeshi la malaika chini yako?..SEMA NENO TU! Na mtumishi wangu atakuwa mzima..

Haleluya

Bwana alistaajabia sana, kwasababu kundi la watu wenye hiyo haikuiona kabisa, anasema hata katika Israeli nzima, ikiashiria kuwa watu wenye Imani ya namna hiyo iliyojaa ufunuo wa kumchukulia Yesu kama ni Zaidi ya wanavyomfikiria walikuwa nao wachache.

Watu wa namna hii pia leo wapo isipokuwa ni wachache sana, watu wenye Imani na YESU aliye ndani ya mioyo yao, watu ambao hawategemei watumishi wa Mungu kuwaombea, watu ambao hawahangaiki huku na kule kutafuta maombezi, Ni kwasababu wamepata ufunuo wa uweza wa nguvu za YESU, Mungu anapendezwa nao sana, hawa wakiwa na haja wanapiga magoti wenyewe wanamwomba YESU aliye ndani yao..Na mwisho wa siku wanapokea miujiza yao..Na kundi hili huwa ni rahisi Zaidi kupokea kuliko lile la kwanza.

Kundi la tatu:

Ni kundi ambalo halikuhitaji ruhusu yoyote ya YESU ili kupokea kitu kutoka kwake ..Halikuhitaji kumwita Yesu aje manyumbani kwao, wala halikuhitaji YESU awatamkie Neno lolote wala halikumuhitaji Yesu afahamu jambo lolote,..Lilifanya kimya kimya lakini matokeo yake yalikuwa ni makubwa na ya papo kwa papo..Mfano wa kundi hili tunaona ni yule mwanamke aliyetokwa na damu miaka 12, tusome:

Luka 8:43 “Na mwanamke mmoja, ambaye ametokwa na damu muda wa miaka kumi na miwili, [aliyekuwa amegharimiwa mali zake zote kwa kuwapa waganga] asipate kuponywa na mtu ye yote,

44 alikwenda nyuma yake, akaugusa upindo wa vazi lake; na mara hiyo kutoka damu kwake kulikoma.

45 Yesu akasema, Ni nani aliyenigusa? Basi, watu wote walipokana, Petro alimwambia, Bwana mkubwa, makutano haya wanakuzunguka na kukusonga.

46 Yesu akasema, Mtu alinigusa, maana naona ya kuwa nguvu zimenitoka.

47 Yule mwanamke, alipoona ya kwamba hawezi kusitirika akaja akitetemeka, akaanguka mbele yake, akamweleza mbele ya watu wote sababu yake ya kumgusa, na jinsi alivyoponywa mara.

48 Akamwambia Binti, imani yako imekuponya; enenda zako na amani”.

Hapa ndipo Bwana Yesu anapotaka kila mmoja wetu afikie, mahali ambapo Yesu anakutafuta wewe, na sio wewe unamtafuta Yesu..kwamba tuwe na mamlaka kamili ya kuweza kutumia nguvu zake bila kipimo chochote. Na hatua hii ikikomaa vizuri ndani ya mtu ndio ile inakuja kuitwa IMANI TIMILIFU, (Wakorintho 13:2) ambayo mtu akiwa nayo anakuwa na uwezo wa kikiambia kitu hichi kwa jina la YESU ondoka nenda kule, nacho kikatii, Anao uwezo wa kuamrisha milima na kufanya jambo lolote kwa jinsi atakavyo yeye, hapo si kwamba anaomba kwa Mungu hapana, bali anafanya kwa amri yake mwenyewe kwa jina la Yesu nacho kinatokea..

Tumwombe Mungu sana tufikie huko.

Na njia pekee ya kufikia huko ni kuwa na maarifa ya kutosha, ya YESU KRISTO, tunahitaji kumjua sana Yesu KRISTO kwa mapana na marefu, kiasi kwamba ile Imani ya kufanya chochote kwa jina lake ijengeke yenyewe ndani yetu.

Bwana atujalie tufike huko, katika tumtafakari sana Bwana YESU, Mfalme wa Wafalme, kama ipasavyo ambaye biblia inatuambia “ndani yake yeye hazina zote za hekima na maarifa zimesitirika”(Wakolosai 2:3).

Bwana akubariki sana, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments