JINA LA MUNGU NI LIPI?

JINA LA MUNGU NI LIPI?

Shalom mtu wa Mungu. Wengi wanajiuliza swali hili, jina la Mungu hasaa ni lipi kwasababu kwenye biblia tunaona yanatajwa majina mengi tunashindwa kuelewa ni jina lipi la kusimamia. Ni kweli hili ni swali zuri, ambalo mtu aliyemaanisha kweli kumtafuta Mungu atatamani kufahamu jina halisi la Mungu ni lipi?.

Hili si swali gheni kwetu sisi, ni swali ambalo lilianza kuulizwa na wana wa Israeli tangu zamani kabla hata hawajatolewa katika nchi ya Misri, walikuwa wanajiuliza huyu Mungu wa Ibrahimu, wa Isaka na Yakobo tunayemtumainia siku zote jina lake ni Nani?..Na ndio maana utaona jambo la kwanza ambalo Musa alimuuliza Mungu kabla ya kwenda kuwaokoa wana wa Israeli, ni kuwa “watu hawa wakiniuliza jina lako ni nani niwajibuje”?. Unaona alijua kabisa ndio swali atakalokumbana nalo la kwanza kabla ya mambo mengine kwa wayahudi waliokuwa wanateseka kule Misri. Hivyo leo tutajifunza Jina hasaa la Mungu ni lipi kwa mujibu wa majibu aliyopewa Musa na Mungu katika maandiko… tusome:

Kutoka 3:13 “Musa akamwambia Mungu, Tazama, nitakapofika kwa wana wa Israeli, na kuwaambia, Mungu wa baba zenu amenituma kwenu; nao wakaniuliza, Jina lake n’nani? Niwaambie nini?

14 Mungu akamwambia Musa, MIMI NIKO AMBAYE NIKO;akasema,Ndivyo utakavyowaambia wana wa Israeli;MIMI NIKO amenituma kwenu.

15 Tena Mungu akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli maneno haya, Bwana, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenituma kwenu; hili ndilo jina langu hata milele, nalo ni kumbukumbu langu hata vizazi vyote.”

Hilo ndilo lilokuwa jibu la Mungu, jina lake wakimuuliza ni MIMI NIKO AMBAYE NIKO, au NITAKUWA KAMA NITAKAVYOKUWA…Lakini leo nataka tujiulize swali moja je hili jina “NITAKUWA KAMA NITAKAVYOKUWA”, Ni jina kweli?. Ukweli ni kwamba hili sio “jina”. Lakini kulikuwa na sababu kubwa Mungu kujitambulisha kwa Musa kwa namna hiyo mwanzoni kabisa, nataka nikuambie na hapo ndipo siri ya jina lake ilipolala.

Aliposema NITAKUWA KAMA NITAKAVYOKUWA…kwa Lugha nyepesi ni sawa na kusema, siku hiyo ikifika Nitajifunua au nitajulikana kama nitakavyokuwa.. hiyo siku ndio litajulikana, kwahiyo hiyo ni kuonyesha kuwa Mungu jina lake la si la mara moja tu kama ya kwetu sisi wanadamu yalivyo, bali linajifunua katika maumbile tofauti kulingana na wakati na majira… Ukimwelewa kwa hapo Mungu basi hutapata shida huko mbeleni.

Na ndio maana kipindi kifupi tu mbeleni mara baada ya Musa kwenda kumwonyesha Farao zile Ishara alizopewa na Mungu, na kukataa kuwaachia wana wa Israeli waende zao, kinyume chake akawazidishia utumwa, mpaka wana wa Israeli wakamnung’unikia Musa, na Musa akarudisha malalamiko yake kwa Mungu, ndipo tunaanza kuona sasa hatua ya kwanza ya “NITAKUWA KAMA NITAKAVYOKUWA” ilipoanza kutenda kazi. Tunaona Mungu alimwambia tena Musa mimi ni YEHOVA.

Kutoka 6:1 “Bwana akamwambia Musa, Sasa utaona nitakavyomtenda Farao; maana kwa mkono hodari atawapa ruhusa kwenda zao, na kwa mkono hodari atawafukuza katika nchi yake.

2 Kisha Mungu akasema na Musa, akamwambia, Mimi ni YEHOVA;

3 nami nilimtokea Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kama Mungu Mwenyezi, bali kwa jina langu YEHOVA sikujulikana kwao.

4 Tena nimelithibitisha agano langu nao, la kuwapa nchi ya Kanaani; nchi ya kukaa kwao hali ya ugeni.

5 Na zaidi ya hayo, nimesikia kuugua kwao wana wa Israeli, ambao Wamisri wanawatumikisha, nami nimelikumbuka agano langu.

6 Basi waambie wana wa Israeli, Mimi ni YEHOVA, nami nitawatoa ninyi mtoke chini ya mizigo ya Wamisri, nami nitawaokoa na utumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyoshwa, na kwa hukumu kubwa;

7 nami nitawatwaeni kuwa watu wangu, nitakuwa Mungu kwenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ni YEHOVA, Mungu wenu, niwatoaye mtoke chini ya mizigo ya Wamisri.”

Unaona hapo alimtokea Ibrahimu, na Isaka na Yakobo kama Mungu mwenyezi, (EL shadai) ukisoma mwanzo 17:1 utaona..Sasa Kwa utambulisho huu wa kumjua yeye kama mwenye enzi yote, mwenye Nguvu zote na uweza wote, ndio uliowafanya Ibrahimu na Isaka na Yakobo, wamwamini Mungu kwa kiwango kile cha juu namna ile, Unadhani mpaka mtu akuamini hivi hivi tu kuwa utakuja kumfanya kuwa taifa kubwa na mataifa yote duniani yatajibarikia kwako, na huku umeshazeeka, hapo inahitaji Mungu ajifunue kwako kama Mungu-mwenyezi vinginevyo hutaweza kuamini mpaka mwisho..

Lakini sasa Jina hili YEHOVA lilizuka mara baada tu ya Farao kuonyesha kiburi,..Na kama tunavyosoma habari Hiyo hatuna muda wa kuuleza moja moja hapa lakini kwa mapigo yale yaliyomfuata mpaka dakika ya mwisho, tunafahamu sio tu Farao na wayahudi walikiri kuwa Yule ni YEHOVA, bali pia mataifa yote duniani yalimtambua na kumwogopa Mungu kwa jina hilo.

Hata baada ya kuingia nchi ya kaanani Jina hili liliendelea kutumika kwa wana wa Israeli, lilichukua maumbile tofuatitofauti kulingana na wakati waliokuwa wanaupitia:

⧫Mfano utaona Mungu alijifunua kwao kama YEHOVA-RAFA: Maana yake Mungu-Nikuponyaye. (Kutoka 15:26.) Mungu aliwaahidia yale magonjwa yaliyokuwa Misri hayatawapa tena ikiwa watazishika amri zake..

⧫Alijifunua tena kama YEHOVA-NISI: Ikiwa na maana kuwa Mungu ni Bendera yetu (Berani ya vita) (Kutoka 15:26).

⧫Alijifunua tena kama YEHOVA-SHALOMU: Mungu ni Amani (Waamuzi 6:24). Gideoni alijenga madhabahu na kuiita jina hili baada ya kudhani kuwa Mungu angemuua pale alipokutana na malaika.

⧫YEHOVA-MEKADISHKEMU: Bwana atutakasaye (Kutoka 31:13)

⧫YEHOVA-ROHI: Bwana ndiye mchungaji wangu (Zab 23)

⧫YEHOVA-YIRE: Mungu atupaye (Mwanzo 22:14)..

Na mengine mengi hatuaweza kuyataja yote hapa.. Mungu alikuwa akijifunua kwa wana wa Israeli, akionyesha uweza wake na ukuu wake kwao, katika mazingira mbali mbali waliyokuwa wanapitia.

Hivyo hiyo ikaendelea mpaka wakati wa waamuzi,na wafalme na manabii..miaka mingi sana ilipita…

Na ulipofika wakati sasa wa Mungu kuikomboa dunia yote, sio kwa Taifa moja tena kama hapo mwanzo, bali dunia nzima ilimpasa ajichagulie jina la wakati huo.. Haleluya!! Na jina hilo ni lazima libebe sifa zote za majina yaliyotangulia, ili kusudi kwamba kusiwe na kitu chochote cha kando kilichosalia, Jina la dunia nzima…Jina ambalo manabii wa zamani mpaka Musa mwenyewe alitamani lifunuliwe wakati wao lakini ilishindakana…na jina hilo si lingine zaidi ya YESU KRISTO

Tafsiri ya YESU ni “YEHOVA-MWOKOZI” hiyo ndiyo tafsiri yake..Hivyo jina hili limebeba ukombozi mkamilifu wa viumbe vyote, sio wanadamu tu bali mpaka wa wanyama..tabia ya majina yote ya kwanza yamo ndani yake, jina hilo linaponya, linachunga, linatoa Baraka, linahuisha, linaokoa, linashindania vita, linaumba, linafunga, linafungua, linafanya kila kitu..Lile la kwanza lililishia kwa maadui wa mwilini lakini hili limechimba kwenye mizizi kabisa kwenye kiti cha enzi cha shetani huko kuzimu na kumshinda, na kumnyang’anya mamlaka yote na kumpa mwanadamu. Hivyo mwanadamu yoyote akipata ufunuo wa jina hili hakuna jambo lolote litakaloweza kumshinda hapa duniani.

Na ndio maana sasa biblia inasema..Matendo 4:12 “Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”

Jina hilo ni jina la YESU KRISTO. Utauliza ni wapi tena kwenye maandiko panaposema jina la Yesu ni jina la Mungu…Bwana Yesu alisema maneno haya..

Yohana 5:42 “Walakini nimewajua ninyi ya kuwa hamna upendo wa Mungu ndani yenu.

43 Mimi nimekuja kwa jina la Baba yangu, wala ninyi hamnipokei; mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea huyo”.

Hivyo ndugu jina la Mungu Yule ambaye anasema NITAKUWA KAMA NITAKAVYOKUWA sasa ndio hili YESU KRISTO. Uponyaji wako utaupata kwa kupitia hili, kushukuria utashukuria kwa jina hili, kutolea mapepo utatolea kwa jina hili hakuna jina lingine hapo..Vile vile kubatizwa utabatizwa kwa jina hili..Wapo watu wanaobatiza kwa jina la Baba na mwana na Roho Mtakatifu, (Mathayo 28:19). Wanakosa ufunuo Yesu alimaanisha nini pale kusema vile..Hawajui kuwa jina la (Baba na mwana na Roho Mtakatifu) ni jina moja hilo nalo ni jina la YESU. Na ndio maana mitume wote baada ya kulitambua hilo utaona mahali pote walikuwa wanabatiza kwa jina hilo la YESU KRISTO, soma (Mdo 2:38, 8:16, 10:48, 19:5) sehemu zote hizo mitume hawakubatiza kwa vyeo vya Baba na Mwana na Roho Mtakatifu. Bali kwa jina la YESU KRISTO…

Kwa akili ya kawaida tu kwanini pepo ukikemea hulikemei kwa jina la baba na mwana na roho mtakatifu? Badala yake unatumia jina la Yesu, ukiumwa unatumia jina la YESU likuponye iweje leo unapoenda kubatizwa unatua vyeo badala ya JINA?. Ni vizuri tuifahamu kweli na tuifuate, Dini zisitukwamishe.

Natumaini utakuwa umemfahamu MIMI NIKO AMBAYE NIKO kwa sasa jina lake ni lipi?.

Lakini Pia, fahamu kuwa Hili jina la YESU nalo halitadumu milele, kuna wakati unafika Mungu atabalika na kuja na jina jipya, na hilo litatumika katika ule utawala wa miaka 1000, pale Kristo atakapokuwa kama Bwana wa Mabwana na Mfalme wa Wafalme. Jina hilo litakuwa sio la ukombozi tena kama sasa, kwasababu ukombozi utakuwa umekwisha wakati huo…bali litakuwa na tabia nyingine ambazo tutazijua vizuri tukifika huko. Hivyo ni vizuri usiichezee neema tuliyonayo sasa ya ukombozi kupitia jina la Yesu, upo wakati utatamani kuokoka utashindwa kwasababu neema itakuwa imeshaondoka.

Ufunuo19:11 “Kisha nikaziona mbingu zimefunuka, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda, aitwaye Mwaminifu na Wa-kweli, naye kwa haki ahukumu na kufanya vita.

12 Na macho yake yalikuwa kama mwali wa moto, na juu ya kichwa chake vilemba vingi; NAYE ANA JINA LILILOANDIKWA, ASILOLIJUA MTU ILA YEYE MWENYEWE.

13 Naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa, Neno la Mungu.

14 Na majeshi yaliyo mbinguni wakamfuata, wamepanda farasi weupe na kuvikwa kitani nzuri, nyeupe, safi.”

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Zinazoendana:

KWANINI YESU ALIMUITA BABA YAKE “ABA”?

JINA LAKO NI LA NANI?

JE! UMEBATIZWA UBATIZO SAHIHI?


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
5 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
David
David
1 year ago

Kanisa ya ukweli ni

Anonymous
Anonymous
1 year ago

N

steve hamisi
steve hamisi
1 year ago

bado nina swali mbona majina mengine alijifunua kwa musa lkn jina la yesu ni wapi ambapo mungu amejifunua??

Given
Given
2 months ago
Reply to  steve hamisi

Yohana 5:42 “Walakini nimewajua ninyi ya kuwa hamna upendo wa Mungu ndani yenu.

43 Mimi nimekuja kwa jina la Baba yangu, wala ninyi hamnipokei; mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea huyo