KARAMA YA MUNGU NI UZIMA WA MILELE.

KARAMA YA MUNGU NI UZIMA WA MILELE.

 Kwanini karama ya Mungu ni uzima wa milele?

Ukikaa chini ukajaribu kutafakari kwa umakini hili Neno UZIMA WA MILELE, utashangaa sana, wakati mwingine utajiuliza hili jambo linawezekanaje kanaje, na ukilitafari sana utaona kama akili yako inafika sehemu inagota. Eti unaishi tu siku zote bila kuwa na kikomo, unaishi leo, miaka mia inapita bado unaendelea tu kuishi.

Miaka elfu inapita bado unaendelea kuishi, miaka milioni moja inapita bado unaendelea kuishi, miaka bilioni moja inapita bado unaendelea kuishi. Miaka trilioni moja inapita ndio bado hata maisha hayajaanza…unaendelea tu, miaka kuadrilioni moja (ambayo ni sawasawa na miaka trilioni elfu moja), inapita bado unaendelea kuishi, miaka kuintilioni moja inapita ndio bado hata hakuna dalili ya kufika mwisho, miaka seksitilioni moja, wewe bado unaendelea tu kuishi. Miaka oktilioni na nonilioni, na desilioni na anidesilioni inapita, hapo bado utaendelea tu,..miaka dodesilioni, na tradesilioni na kuatuordesilioni na kuindesilioni na seksidesilioni bado tu safari inaendelea ukiwa bado kama kijana mdogo tu, n.k. n.k. tukiziandika namba zote hapa tunaweza kujaza ukurasa mzima na bado zisitoshe….

Embu jaribu kufikiria hayo ni maisha marefu kiasi gani, leo hii tu ikipita miaka 20 au 30 unaona kama ilikuwa ni zamani sana, na tena unaiita enzi hizo, sasa hapo bado haijatapita miaka milioni moja sijui hiyo utaiitaje labda utaaita kama ile ya historia zama za mawe za kwanza, pengine hata kumbukumbu zake utakuwa umezipoteza..

Sasa Mungu asiyekuwa na mwisho ametuahidia zawadi hiyo kuu bure, Hata tusingepewa zawadi nyingine hiyo tu ya Uzima wa Milele ingetutosha. Ni zawadi kubwa sana isiyoelezeka.

Warumi 6:23 “Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni UZIMA WA MILELE katika Kristo Yesu Bwana wetu”.

Na kumbuka pia Mungu asiye na mipaka, miaka hiyo yote hatutakuwa tunaishi tu kama watu wasiokuwa na mwelekeo “idle”. Au unaishi tu bila maaana yoyote hapana! vinginevyo umilele utakuwa wa ku-boa.

Badala yake kila siku, kila wakati kutakuwa na matukio yake na mambo yake mazuri mapya, yaani tutayafurahia maisha kila iitawapo leo, kwasababu kila siku itakuwa na mambo yake, kutakuwa hakuna magonjwa, kutakuwa hakuna kuzeeka, kutakuwa hakuna shida, kutakuwa hakuna mahangaiko, wala kupigwa na jua hakutakuwepo, wala ulemavu hautakuwepo, wala uchungu, wala kuudhiwa, wala kuumizwa, wala kudaiwa. Siku zote tutaishi katika raha isiyo na kifani, tukiushangaa utukufu wa Mungu na kumwabudu yeye katika raha isiyoelezeka.

Mungu kashaipigia mahesabu kila siku moja ya umilele hivyo analijua tukio ambalo litatokea siku Fulani ya mwaka Fulani wa bilioni moja huko mbeleni kwamba wewe utakuwa unafanya kitu Fulani na Yule kitu fulani,..Huyo ndio YEHOVA..hatuishi kumshangaa kwa matendo yake ya ajabu.

Na ndio maana Mungu anasema katika..

Isaya 55:8 “Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana.

9 Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu”.

Kauli hiyo ya Mungu inatuthibitishia kuwa mipango ya Mungu aliyotuandalia sisi, hatuwezi kuidhania au kuifikiria ipasavyo hata kwa chembe ndogo sana. Kwasababu ipo mbali sana na upeo wetu wa kufikiri, na ndio maana ni jukumu letu kuhakikisha sisi sote hatuukosi huo uzima wa milele.. Kwasababu hapa ni kama tunaandaliwa tu kwa ajili ya kuishi maisha halisi, hapa duniani hatuna maisha, miaka 70 au 80 sio maisha. Bali tunaandaliwa tu kwa ajili ya kuishi kule ambako Mungu alitukusudia tuishi, tunatengenezwa tu ili tuweze kustahimili huo umilele unaokuja huko mbeleni..

Hivyo tukiwa tunayatafakari hayo kila siku tutapata nguvu ya kutokujali ni nini tunapoteza sasa tukiwa hapa duniani, kwa ajili ya maisha yetu ya umilele ya baadaye…hatutojali tunapoteza fursa ngapi za biashara kwa ajili ya kuhudhuria maombi, hatutojali tunapoteza hiki au kile kwa kwenda ibadani, kwa kujifunza Neno la Mungu…Hatutojali ni mambo mangapi ya kidunia yanatupita, sisi tunatazama maisha ya milele Mungu aliyotuandalia…

Hata mithali ya kidunia inasema, “usiache mbachao kwa msala upitao”. Ikiwa na maana tusiopoteze uzima wetu wa milele kwa vitu vya kidunia vinavyopita, ambavyo mwisho wake ni hapa tu..Itatufaidia nini tuupate ulimwengu mzima, kisha tupate hasara ya nafsi zetu.? Kwasababu mshahara wa dhambi ni mauti…lakini karama ya Mungu ni uzima wa milele.

Lakini uzima wa milele huu kuupata ni bure, nao unakuja kwa kumwamini tu YESU KRISTO, pale unapotubu kwa kudhamiria kwa dhati kutoka moyoni mwako kwamba kuanzia leo unaacha dhambi zako zote..Unafanya maamuzi ya kuacha pombe, kuacha uasherati, kucha uvaaji mbaya, kuacha rushwa, kuacha wizi n.k. Na vitu vyote ulivyokuwa unaviona vinakufaidisha sana vya kidunia unaviacha vyote unavihesabia kama ni mavi. Kama Mtume Paulo alivyovihesabia.

Wafilipi 3.7 “Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo.

8 Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama MAVI ili nipate Kristo”

Na baada ya kutubu na kuyahesabia mambo yote uliyokuwa unayafanya machafu kama MAVI. Hatu inayofuata ni kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamwisha katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO, kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako sawasawa na Matendo 2:38,.Kisha Bwana atakupa kipawa cha Roho Mtakatifu..Hivyo Hatua hizo zote zikikamilika juu yako basi na wewe utakuwa umefanyika kuwa mwana wa Mungu na yeye mwenyewe atakupa karama hii ya uzima wa milele bure..

Kumbuka …Warumi 6:23 “Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu”…Na sio katika Ulimwengu.

Ubarikiwe sana.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

UFUNUO: Mlango wa 1

INJILI KULINGANA NA TEKNOLOJIA

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA KITABU CHA RUTHU:

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 3

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments