Yezebeli alikuwa ni mwanamke mwenye asili ya nchi ya Lebanoni, mahali pajulikanapo kama Sidoni (1Wafalme 16:31), karibu sana na mji wa Tarshishi, ule ambao Nabii Yona alienda kuhubiri, na alikuwa ni binti wa kifalme, hivyo alitokea katika familia tajiri.
Mwanamke huyu hakuwa Mwisraeli, ila aliolewa na Mfalme wa Israeli aliyeitwa AHABU, ikambidi ahame kutoka katika Taifa lake hilo na kuhamia Israeli, katika mji wa Samaria pamoja na miungu yake, na tamaduni zake.
Mfalme wa Israeli akamfanya kuwa Malkia, jambo ambalo BWANA Mungu alishalikataza kwa kinywa cha mtumishi wake Musa kuwa wana wa Israeli wasioe wanawake wa kimataifa, kwasababu watawageuza mioyo waabudu miungu mingin, Lakini Mfalme Ahabu alifumba macho yake asione hilo, na badala yake akamwoa YEZEBELI.
Na Yezebeli kwakuwa si Mwisraeli, bali alitoka Taifa lingine lenye miungu mingine, basi aliingia Israeli na miungu yake hiyo, na makuhani wake.. Hapo ndipo mambo yalipoanza kuharibika kwa wana wa Israeli!.. shida ikawa kubwa mpaka Bwana MUNGU kumnyanyua Eliya Nabii.
Sasa zifuatazo ni roho (3) alizokuwa nazo Malkia Yezebeli, zilizoliharibu Taifa la Israeli, na zinazofanya uharibifu leo katika kanisa na nje ya kanisa.
1. UKAHABA
Hii ni sifa ya kwanza ya Malkia Yezebeli,..Biblia inasema alikuwa ni “Mzinzi”, kwani ndiye mwanamke pekee aliyeonekana katika biblia kapaka UWANJA usoni na KUJIPAMBA KICHWA! Kwa lengo la kuvutia ukahaba..Hakuna mwanamke mwingine yoyote katika biblia yote anayetajwa kufanya mambo hayo..
2Wafalme 9:30 “Hata Yehu alipofika Yezreeli, Yezebeli akapata habari; AKATIA UWANJA MACHONI MWAKE, AKAPAMBA KICHWA CHAKE, akachungulia dirishani”
Yezebeli anamwona YEHU anakuja, kwa tabia yake ya uzinzi, anaanza kujipaka uwanja machoni, na kupamba kichwa ili amlaghai YEHU apate kulala naye!. Na wala hata hakuwa na uchungu kwa kifo cha mwanae, yeye anawaza uzinzi tu.
Roho hii inatenda kazi hata leo… huoni hata watu leo wanaenda misibani wamejipodoa… mahali pa kwenda kutafakari mwisho wa safari ya mtu ulimwenguni, wengine wanaenda wamejipodoa kwa lengo la kuvutia ukahaba kama alivyofanya Yezebeli, katika msiba wa mwanae..
Roho hii imeingia mpaka makanisani, utaona wanawake na mabinti sehemu za ibada wanaingia kwa mionekano kama ya YEZEBELI, bila aibu wala hofu!..viungo vyao vipo wazi, nguo walizovaa ni za nusu tupu, nyuso zimejaa rangi, na vichwa vimepambwa kama Yezebeli, na hawaambiwi chochote, na wala wenyewe hawasikii chochote ndani yao kikiwahukumu… pasipo kujua kuwa hiyo ni roho ya YEZEBELI, inaishi na kutenda kazi, kama ilivyokuwa enzi za mfalme Ahabu.
Dada, Mama acha kupamba uso!!!, ndani na nje ya kanisa, hiyo ni roho ya YEZEBELI, ya Ukahaba…usidanganywe na shetani kwa kukuambia kuwa ni urembo tu.. ni urembo tu!!.. hakuna urembo ndani ya sare ya kikahaba.. Utavaaje sare ya askari na ukasema ni urembo tu!!..
Na hii roho ya Yezebeli imeingia pia kwa wanaume,..kama mwanaume anasuka nywele zake, na kupaka uwanja usoni, na kuvaa nguo nusu tupu, na kujichora mwili wake… roho ya Yezebeli inatenda kazi ndani yake.
2. UCHAWI
Pamoja na kwamba Yezebeli alikuwa ni kahaba, biblia inasema pia alikuwa ni mchawi.
Na Uchawi wa Yezebeli ulianzia nchini kwake alikotoka, kutokana na aina ya miungu aliyokuwa anaiabudu. Kwani alikuwa anaabudu “mungu baali”, ambaye kwa asili makuhani wake wote walikuwa ni wachawi na Yezebeli ndiye aliyekuwa mkuu wao.
2Wafalme 9:22 “Ikawa, Yoramu alipomwona Yehu, akasema, Je! Ni amani, Yehu? Akajibu, Amani gani, maadamu uzinzi wa mama yako Yezebeli na UCHAWI WAKE NI MWINGI?”
Na uchawi wa Yezebeli mbali na kuloga, alikuwa pia ni mkaidi
3. NABII WA UONGO.
Ufunuo 2:20 “Lakini nina neno juu yako, ya kwamba wamridhia yule MWANAMKE YEZEBELI, yeye AJIITAYE NABII na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ILI WAZINI na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu”.
Roho ya Yezebeli inawafundisha watu “Kuzini”.. Inawafundishaje?.. si kwa njia nyingine isipokuwa kwa injili ya kwamba “Mungu haangalii mwili anaangalia roho”… Injili hii, inawafanya watu wavae watakavyo..ili lile neno Bwana YESU alilolisema kuwa “amtazamaye mwanamke kwa kumtamani amekwisha kuzini naye nafsini mwake” litimie juu yao kupitia yale mavazi ya kikahaba wavaayo.
Dada/mama fahamu kuwa uvaapo mavazi ya kikahaba kama Yezebeli halafu mwanaume akikutamani tayari umekwisha kuzini naye, hata kama hajakushika mkono. (wewe na yeye wote mmezini, na si yeye tu!.. bali hata na wewe, ambaye hujui kama umetamaniwa kwa mavazi yako). Sasa jiulize unapotembea mtaani umevaa nguo hizo za nusu uchi, umezini na wanaume wangapi!
Hii roho ya Yezebeli ipo makanisani leo!.. ipo kwa wengi wanaotambulika kama watumishi wa Mungu, hii ni roho ya Unabii wa Uongo, inayowafundisha watu UZINZI!, kwa kujua na kutokujua.
Hivyo jihadhari na injili hiyo ya adui, isemayo “Mungu anaangalia roho na haangalii mwili”.. Ulinde mwili wako usiwe chanzo cha kuipoteza roho yako moja kwa moja.
Na tabia ya hii roho ya YEZEBELI ni kushindana na Roho ya kweli ya Mungu.. Ndio maana utaona Malkia Yezebeli katika Uzinzi wake, na uchawi wake na unabii wake wa uongo, hakuwahi kamwe kupatana na Nabii Eliya, wala kujinyenyekeza kwake..zaidi sana utaona Yezebeli baada ya kusikia ishara Eliya aliyoifanya ya kushusha moto na kuwaua manaabii wake wa baali, aliapa kumlipa kisasi Eliya, na wala hakumwogopa hata Mungu. (Ni roho ya kiburi).
Roho hii ikishakita mizizi ndani ya mtu, inamfanya kuwa na kiburi, na mkatili hususani katika matumishi wa kweli wa Mungu, na inakuwa inamfanya mtu kuichukia njia ya kweli na watumishi wa Mungu wa kweli.
Jivue roho ya UYEZEBELI.. Mvae BWANA YESU (Warumi 13:14). Hizi ni siku za Mwisho na Bwana YESU anarudi.
Maran atha!
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
YEZEBELI ALIKUWA NANI
JINSI ROHO MTAKATIFU ANAVYOKUJA JUU YA MTU.
Roho Mtakatifu ni nani?.
KIMBIA! KIMBIA! KIMBIA!
ROHO YA MPINGA KRISTO IKITENDA KAZI SIKU HIZI ZA MWISHO
Rudi Nyumbani
Print this post