MAMBO SITA, AMBAYO MUNGU HUTUMIA KUONDOA UOVU NDANI YA MTU.

MAMBO SITA, AMBAYO MUNGU HUTUMIA KUONDOA UOVU NDANI YA MTU.

Nakusalimu katika jina kuu la mwokozi wetu Yesu Kristo, karibu katika kujifunza Neno la Mungu. Leo tutaona mambo Makuu sita (6), ambayo Mungu anatumia kuondoa uovu ndani ya mtu, na kumfanya awe mtakatifu kabisa kama yeye alivyo. Ikiwa wewe umemfuata Kristo basi tarajia mambo haya matano atayatumia katika maisha yako, kukukamilisha.

  1. Damu
  2. Maji
  3. Moto
  4. Fimbo
  5. Pepeto
  6. Dawa

Tukianza na

DAMU:

Kumbuka sisi sote tulizaliwa na deni la dhambi. Hivyo tulistahili hukumu ya mauti, (Warumi 6:23), Lakini deni hilo lilikuja kulipwa na Bwana wetu Yesu kwa kifo chake pale msalabani (Warumi 5:8). Kumwagika kwa damu yake, sote tumepokea “msamaha wa dhambi” bure kwa neema. Hakuna mwanadamu yoyote anayeweza kukubaliwa na Mungu, kwa uweza wake mwenyewe. Kwahiyo damu ya Yesu imekuwa hatua ya kwanza ya sisi kukubaliwa na Mungu.

Sasa tunaweza kupokea msamaha kweli, tukasemehewa, lakini dhambi bado ikawepo ndani yetu. Na hilo sio kusudu la Mungu atusemehe tu, halafu atuache tuendelee kuwa watumwa wa dhambi ndani kwa ndani. Si lengo la Mungu, hata mtu mwenye upendo wa dhati wa Yule aliyekosewa naye, anapoona amemsamehe, huwa hamwachi tena kesho arudie kosa lile lile ili, amsamehe, hapana, bali humwonyesha njia ya kuepuka makosa ili yeye mwenyewe aweze kusimama kwa ujasiri mbele zake. Na ndivyo ilivyo kwa Mungu mara baada ya kupokea msamaha wa dhambi, huyo mtu anaanza hatua ya utakaso wa Mungu ambao sasa hufanywa na Roho Mtakatifu aliyeingia ndani yake, Ndio hapo inakuja hatua ya pili,

NENO:

Biblia inasema Neno ni kama maji, ambayo yanasafisha.

Waefeso 5:26  ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; 27  apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa.

Umeona, Kristo hulisafisha kanisa lake, kwa Neno, ndio maana wewe kama mtu uliyempokea Yesu, Ni lazima uwe na juhudu nyingi sana za kusoma Neno la Mungu kila siku, usikie maonyo, fundisho, agizo,  njia, (2Timotheo 3:16), Na kwa jinsi unavyojifunza sana, ndivyo unavyosafishwa moyo wako na roho yako, hatimaye unaanza kujiona mtu ambaye huna hatia ndani yako. Na hapo ndipo unapojikuta unaacha baadhi ya mambo uliyokuwa unafanya huko nyuma. Kumbuka biblia uliyonayo sio kitambulisho cha mkristo au pambo la mkoba, bali ni maji hayo ya kukusafisha, hivyo oga kila siku, uwe msafi. Kwasababu usipofanya hivyo utakuwa mchafu tu sikuzote.

MOTO:

Kwa kawaida sio kila uchafu hutoka kwa maji, mwingine huitaji moto ili kuundoa. Kwamfano ukiupata mwamba wenye dhahabu ndani yake ukipitisha maji huwezi toa uchafu uliogandamana nao,hivyo wale wafuaji, wanaupitisha kwenye moto, kisha unayeyuka na baada ya hapo uchafu na dhahabu hujitenga kisha wanaikusanya dhahabu. Ndivyo ilivyo na Mungu kwa watoto wake. Upo moto ambao wewe kama mwana wa Mungu ni lazima tu utapitishwa hata iweje, kuondoa mambo sugu yaliyogandamana na wewe yasiyoweza kutoka kwa Neno tu bali kwa hatua ya kimaisha, ndio huo unaoitwa “ubatizo wa moto”. Mfano wa huu ndio ule uliompata mfalme Nebukadreza (Danieli 4), kukaa miaka saba maporini kula majani ili tu aondolewe kiburi ndani yake. Ni aina Fulani ya maisha ambayo kwako yatakuwa kama moto, lakini mwisho wake hukuletea faida ya roho yako.

1Petro 1:6  Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali;7  ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo.

FIMBO:

Zipo tabia nyingine ambazo Mungu anaona mwanawe anakuwa nazo kwa ujinga tu, hivyo, ili kuundoa ujinga huo, haihitaji maji wala moto, bali kiboko. Anapoona unafanya jambo Fulani kwa makusudi na alishakukataza hapo awali fahamu pia kiboko kitapita juu yako.

Waebrania 12:6  Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, Naye humpiga kila mwana amkubaliye.

7  Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye?

8  Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali. 9  Na pamoja na hayo tulikuwa na baba zetu wa mwili walioturudi, nasi tukawastahi; basi si afadhali sana kujitia chini ya Baba wa roho zetu na kuishi?

10  Maana ni hakika, hao kwa siku chache waliturudi kama walivyoona vema wenyewe; bali yeye kwa faida yetu, ili tuushiriki utakatifu wake.

Biblia inasema pia..

Mithali 22:15 Ujinga umefungwa ndani ya moyo wa mtoto; Lakini fimbo ya adhabu itaufukuzia mbali.

PEPETO:

Yohana mbatizaji kwa uvuvio wa Roho aliandika maneno haya kuhusu  Bwana Yesu..

Mathayo 3:11  Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.

12  Ambaye pepeto lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake; na kuikusanya ngano yake ghalani, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.

Yesu akija kwako, fahamu kuwa mkononi ameshika pepeto pia, na wewe utawekwa juu yake, Anajua kabisa ulipo wewe makapi pia yapo, uliyotoka nayo huko shambani (ulimwenguni), hivyo ili kukutenga nayo, ataanza kukupepeta, kama vile ngano, utarushwa juu, utashushwa chini, utarushwa juu utashushwa chini, huwezi kuachwa utulie, lengo ni kuhakikisha makapi yote yanapeperushwa na upepo, iwe ni watu, vitu, utaona tu unapelekwa mbele, unarudishwa nyuma..baadaye akishaona ni ngano tu imebakia chini, hapo ndipo anapokuacha, unaanza kuona ushwari. Hii ilimkuta Ibrahimu, Bwana anamtoa Uru, anampeleka kaanani, mara anakimbilia Misri, mara anarudisha, lakini baadaye Mungu alimpa pumziko, baada ya kuona wote waliokuwa wameshikamana naye hawapo naye.

Usishangae kutokuwa na utulivu katika nyakati fulani za maisha yako wokovu, wakati Fulani unafanikiwa, halafu unarudi chini, wakati Fulani unapata amani kotekote, gafla inaondoka, unapata, ghafla tena unapoteza, tulia tu, kuwa na amani ndani ya Kristo, utakuwa tu, imara, wala hiyo misukosuko haitakuwepo tena, ni kwanini iwe hivyo? Ni kwasababu makapi yanapeperushwa na upepo.

DAWA:

Kaa ukifahamu Yesu anajulikana pia kama tabibu,(Marko 2:17) na anajua maovu mengine unayoyafanya yanatokana na magonjwa na majeraha ya rohoni, anajua hali yako ilivyo hivyo anachokifanya ni kukutibu yeye mwenyewe, ndio hapo unashangaa tu mwingine anatokwa na mapepo yaliyokuwa yanamsumbua na kumpelekea kutenda dhambi mwingine anapona udhaifu fulani, uliokuwa unamfanya amkosee Mungu, mwingine anapokea faraja, amani, utulivu usio wa kawaida, anashangaa kuona tofauti kubwa  ya sasa na hapo kabla. Hili nalo mtu aliyempokea Kristo ataliona kwenye maisha yake. Na atimaye anakuwa mwema yeye tu mwenyewe, asukumwi tena na presha ya dhambi fulani. Kwasababu tabibu mkuu ameshamponya, ambaye akikuweka huru, unakuwa huru kwelikweli.

Ufunuo 3:18

Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na DAWA ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.

Hivyo, wewe kama mwana wa Mungu, tambua yote hayo yatapita katika sehemu Fulani ya maisha yako. Usidhani kusafishwa tu na damu ya Yesu ndio basi, utatakaswa na hiyo ni katika maisha yako yote. Haiwezekani mtu aliyeokoka ambaye amepokea Roho maisha yake yote awe Yule Yule wa zamani, hizo sio kanuni za wokovu, wala sio kusudi la Mungu. Ukubali utakaso, au usiwe mkristo kabisa. Kwasababu hivi viwili huenda sambamba wala haviwezi kutenganishwa. Huo ndio upendo wa Mungu.

Utukufu na heshima ni vyake  milele na milele.

Bwana akubariki.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> hhttps://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

MADHARA YA KUKOSA MAJI YA UZIMA BAADA YA KIFO.

(Opens in a new browser tab)UTAKASO NI SEHEMU YA MAISHA YA MKRISTO YA KILA SIKU.

Ipi tofuati kati ya UTAKATIFU na UKAMILIFU?

Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments