UTAKASO NI SEHEMU YA MAISHA YA MKRISTO YA KILA SIKU.

UTAKASO NI SEHEMU YA MAISHA YA MKRISTO YA KILA SIKU.

Jina kuu la Bwana wetu Yesu libarikiwe.

Ni siku nyingine tena Bwana ametupa pumzi yake kuiona, leo tutajifunza somo linalohusiana na utakaso kwa mtakatifu. Lakini kabla hatujafika kwenye utakaso, ni vizuri tufahamu kwanza mtakatifu ni mtu wa namna gani kibiblia..

Wengi tunafahamu  labda mtu mpaka aitwe mtakatifu ni lazima awe ameshakaa kwenye wokovu miaka mingi,, lakini kibiblia sio hivyo. Bali pale mtu anapoamua kuokoka, pale anapoamua kuacha maisha yake ya dhambi, na kumgeukia Bwana Yesu, na kusafishwa na damu yake, na kubatizwa, wakati huo huo anakuwa tayari kashafanyika kuwa mtakatifu, haijalishi mambo mengine yatakuwa hayajaondoka vizuri ndani yake,..Kile kitendo tu cha kumpokea Yesu maishani mwake, mtu huyo mbinguni ni mtakatifu kwasababu hana deni la dhambi,  anakuwa sawasawa tu na mkristo mwingine aliyekaa  katika wokovu kwa miaka 50.

Lakini tatizo linakuja ni pale ambapo mtu huyo anadhani akishampokea Yesu, ndio basi inatosha, Nataka nikuambie hilo halipo katika safari ya ukristo. Utarudi nyuma tu siku sio nyingi, na takatifu wako utakufa na utakuwa  kama vile mtu ambaye hajaokolewa.

Fahamu baada ya kuwa mtakatifu, hatua inayofuata kwako ni lazima iwe Kujitakasa.. Ndio maana Bwana Yesu alisema maneno haya..

Ufunuo 22:11 “Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na MTAKATIFU NA AZIDI KUTAKASWA”.

Unaona inasema mtakatifu azidi kutakaswa, ikiwa na maana ukiwa mtakatifu hupaswi kubakia pale pale sikuzote, ni jukumu lako kujitakasa siku baada ya siku. MTAKATIFU ni kama BETRI ya simu. Pale inaponunuliwa ndani yake huwa imeshaumbiwa nguvu ya kutosha ya kuifanya simu iwake kwa muda wa miaka mingi sana hata 10 na zaidi. Lakini Betri hiyo haitegemei tu ile nguvu iliyowekwa ndani yake kuipa uhai simu siku zote, hapana, bali inatarajia pia iwe inachajiwa mara kwa mara, hata kila siku, ili kuzisisimua nguvu zilizoko ndani yake iendelee kuifanya simu iwake  kwa muda wote huo.

Lakini kama isipochajiwa, ni wazi kuwa haitaweza kuwasha simu, na matokeo yake ni kuwa itakuwa kama jiwe tu lisilokuwa na maana yoyote, haijalishi kuwa ndani yake kuna nguvu nyingi kiasi gani.Vivyo hivyo na utakatifu nao.. utakatifu bila utakaso Umekufa.

Unapookoka leo hii, unapoamua kumpa Yesu maisha yako, hiyo peke yake haitoshi zipo hatua za kuanza kupiga, ili kuufanya ule utakatifu kuwa hai ndani yako siku baada ya siku. Yapo maisha unapaswa uanze kujizosha kuishi ili Mungu aweze kukutakasa (kukutia nguvu ) ya kuendelea kuishi maisha ya utakatifu siku baada ya siku .

Warumi 6:22 “Lakini sasa mkiisha kuwekwa huru, na kuwa mbali na dhambi, na kufanywa watumwa wa Mungu, MNAYO FAIDA YENU, NDIYO KUTAKASWA, na mwisho wake ni uzima wa milele”.

SASA MTU ANAJITAKASAJE?

Kwanza ni kwa kukujifunza Neno la Mungu kwa bidii: Unapookoka, ni jukumu lako kusoma Neno na kusikiliza Neno, hususani mafundisho yanayolenga utakatifu. hiyo itakusaidia kujua biblia inasema nini katika kila jambo unalotaka kulifanya. Hivyo kuwa rahisi kujiepusha na mambo ambayo hayampendezi Mungu.

1Petro 1:22 “Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii kweli, hata kuufikilia upendano wa ndugu usio na unafiki, basi jitahidini kupendana kwa moyo”.

Pili ni kwa kuwa mwombaji na kufunga: Maombi ni nguzo nyingine inayomtia mtu nguvu ya kuendelea kudumu katika utakatifu Mungu anaouhitaji ndani ya mtu. Usipokuwa mwombaji huwezi kudumu katika wokovu, huwezi kuyashinda majaribu kwa namna yoyote ile. Vilevile na katika kufunga, kunakusaidia kufikiria zaidi mambo ya rohoni kuliko ya mwilini na matokeo yake kuzishinda tama zake.

Tatu ni kwa kujizoeza kuishi maisha yampendezayo Mungu: Kujizoesha ni jambo lingine la msingi sana, kwamfano mtu aliyejizoesha kuamka alfajiri sana, huwa  inafikia wakati kuamka kwake asubuhi kunakuwa ni kwepesi sana tofauti na Yule ambaye hajajizoesha kuamka mapema.. Vivyo hivyo  na katika Utakatifu, tukijizoesha kuishi maisha ya haki, baadaye yanakuja kuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku yenyewe bila hata kutumia bidii nyingi.

1Timotheo 4:8 “Kwa maana kujizoeza kupata nguvu za mwili kwafaa kidogo, lakini utauwa hufaa kwa mambo yote; yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa, na ya ule utakaokuwapo baadaye”.

Nne, Ni kwa kuifanya kazi ya Mungu: Kuitenda kazi ya Mungu ikiwemo kuwahubiria wengine ni chaji nzuri sana ya utakatifu. Kwasababu inakufanya ukae katika uwepo wa  ki-Mungu muda mrefu, kwasababu unamlazimisha Roho Mtakatifu aje kufanya kazi na wewe, na sikuzote alipo Roho Mtakatifu, lazima uwepo utakatifu.

Hivyo kwa kuhitimisha, ni jukumu la kila mmoja wetu KUJITAKASA kila siku, ili aendelee kudumu, hakunaga Utakatifu wa kusema mimi nimeokoka, halafu huonyeshi bidii yoyote, hapo utakuwa unajidanganya mwenyewe, utasema tu kwa mdomo lakini kwa matendo utakuwa mbali nao.  Ni lazima tujichaji (tujitakase) ili tuweze kudumu kwenye huo utakatifu. Siku hizi za mwisho Bwana Yesu alitusisitiza sana kufanya hivyo, kwasababu maovu yameongezeka, na yeye yupo mlangoni kurudi.

2Petro 1:8 “Maana mambo hayo yakiwa kwenu na kujaa tele, yawafanya ninyi kuwa si wavivu wala si watu wasio na matunda, kwa kumjua Bwana wetu Yesu Kristo.

9 Maana yeye asiyekuwa na hayo ni kipofu, hawezi kuona vitu vilivyo mbali, AMESAHAU KULE KUTAKASWA DHAMBI ZAKE ZA ZAMANI.

Mimi na wewe tusisahau utakaso wa kila siku.

Maran atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Nini maana ya ‘Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu’ ?

Nini maana ya “yasiyokuwapo hayahesabiki”(Mh 1:15)

TUSIWE WATU WA KUPUNGUKIWA AKILI.

MWANZO WA INJILI YA YESU KRISTO.

Nini maana ya ‘kuhuluku’ kama tunavyosoma katika biblia?

Kwanini Mungu aliwaagiza wana wa Israeli wasikisaze chakula?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
2 years ago

Mbarikiwe kwa kazi nzuri

Anthony Juma
Anthony Juma
2 years ago

Mmebarikiwe kwa kazi nzuri