TAFAKARI SANA KABLA YA KUAMUA HATIMA YAKO.

TAFAKARI SANA KABLA YA KUAMUA HATIMA YAKO.

Tafakari sana kabla hujafikia hitimisho Fulani ambalo ndio litakuwa la kudumu katika maisha yako.

Kuna watu wengi sana ambao shetani kawafumba macho, na kuwafanya wasifikiri vyema kabla ya kufikia hitimisho la maisha yao.

Kwamfano kuna watu wanatazama mwenendo wa watumishi wa uongo, au waliorudi nyuma, na kuhitimisha kwamba kamwe hawataokoka..kisa tu wameona hao watumishi wakifanya mambo ya ajabu yasiyopatana na wokovu kabisa.. Mtu wa namna hii tayari kafikia hitimisho la maisha yake bila kutenga muda wa kutafakari/ kufikiri sana.

Ndugu ni kweli umezunguka kila mahali hujaona mchungaji mkamilifu kama ulivyotaka wala ulivyotegemea…Lakini hiyo isikupe nafasi ya kusema hutamtafuta Mungu kamwe wala hutaokoka..Kwasababu ni kweli hujaona mchungaji mkamilifu lakini yupo aliye mkamilifu ambaye hakutenda dhambi kabisa hata moja, yaani YESU KRISTO, habari zake zimeelezwa kwa urefu katika maandiko, Umekataa kumsikiliza mchungaji wako kwasababu umeshuhudiwa kafumaniwa katika uzinzi, umekataa kumsikiliza muhubiri fulani maarufu kwasababu kakengeuka kawa kama watu wa kidunia n.k.. Lakini yupo mmoja aliye mkamilifu YESU KRISTO, mfuate huyo hao wengine waache.. Unafikiri utajitetea vipi siku ile ya hukumu?.

Utasema Bwana mimi nilikata tamaa ya kuendelea na wokovu kwasababu mchungaji wangu alinitaka kimapenzi, hakuwa mkamilifu,..ni kweli mchungaji wako anayo dhambi lakini alikuwepo YESU AMBAYE BADO NI MWAMINIFU, hana dhambi, mchungaji mkuu.. ungemfuata huyo Yesu, umwache mchungaji wako..Lakini wewe umewatapika wote…Utajitetea vipi siku ile???… kama vigezo vya utakatifu Bwana Yesu kavikidhi vyote, hana kosa wala hatia…Tafakari sana kabla ya kufanya maamuzi, usitafakari juu juu tu.

Bwana Yesu alisema maneno haya..

Yohana 8.46  “Ni nani miongoni mwenu anishuhudiaye ya kuwa nina dhambi? Nami nikisema kweli, mbona ninyi hamnisadiki?”

Mchungaji wako anayekuchunga anayo dhambi, pengine umemshuhudia akisema uongo, umemshuhudia akizini, lakini ni wapi Yesu umemshuhudia akisema uongo, ni wapi umemshuhudia akizini? …lakini wewe umemkataa Yesu aliye mkamilifu sawasawa na Mchungaji wako,..ni nani sasa utakayemkubali mwenye vigezo unavyovitaka wewe??…..Ndio maana anauliza swali hilo hapo juu “Ni nani miongoni mwenu anishuhudiaye ya kuwa nina dhambi?” … Yesu hana dhambi hata moja unamkataa…utamkubali nani kwamfano ukiulizwa hilo swali?….siku ile utajitetea vipi mbele ya Bwana?.

Utasema mimi ni kijana, siwezi kuishi maisha bila kufanya uasherati, kwasababu naishi mazingira ya vishawishi vingi…. Siku ile ataletwa kijana aliye mzuri kimwonekano kuliko wewe na aliyeishi katikati ya mazingira magumu kuliko wewe, lakini aliweza kuushinda uasherati kwa kishindo kikubwa…Hapo utazungumza nini cha kujitetea??.

Unajua ni kwanini biblia inasema watakatifu watauhukumu ulimwengu??

Ni kwa njia hiyo ya wanavyoishi…kama kuna dada ambaye mnaishi naye mtaani anavaa vizuri katikati ya dunia hii ya wanawake walioharibika akili, siku ya hukumu atawahukumu wanawake wote waliokuwa wanavaa vibaya…na atawahukumu si kwa maneno, bali maisha yake ndio yatawahukumu hao wengine…wakati hao wengine wanasema Bwana ilikuwa haiwezekani kila duka lilikuwa linauzwa nguo fupi, yeye atasimamishwa na kuulizwa alizipata wapi hizo ndefu..na hivyo maisha yake kuwa hukumu kwa wengine, (hiyo ndio maana ya watakatifu watauhukumu ulimwengu 1Wakorintho 6:2)

Kwahiyo usifikiri kwa vyovyote vile siku ile kuna kushinda hoja mbele ya kiti cha hukumu.. hakutakuwa na hoja yoyote ya kushinda, ndio maana leo hii..tunapata nafasi hii ya kukumbushwa kutafakari kwa makini kabla ya kufanya maamuzi.

Leo hii umeuacha wokovu kwasababu ya mchungaji wako, Rudi mgeukie Yesu Mchungaji mkuu asiye na dhambi, leo hii maneno ya muumini mwenzako yamekufanya usiupende wokovu au ukristo, ni wakati wa kumtazama Kristo na si mwanadamu.. Leo hii umevunjwa moyo na wakristo wenzako, au kiongozi wako katika imani, hata ikakufanya ukate tama kabisa ya kuendelea na wokovu…Ni wakati wa kuyaweka hayo mawazo pembeni kwasababu, shetani anataka ufikiri hivyo hivyo mpaka siku ya hukumu, ili ukose cha kujitetea siku ile.

Na kama hujampokea Yesu kwasababu nyingine yeyote, huu ni wakati wa kufanya hivyo, tunaishi siku za hatari sana, na adui yetu shetani ana wakati  mchache sana, amewekeza nguvu nyingi katika kuwafanya watu wasione mbele, badala yake wawe bize kutafuta mambo ya kidunia na kuwa na vijisababu vidogo vidogo vya kuhalalisha huo usingizi wa kiroho..Hiyo amka leo. Kristo anarudi, parapanda inakaribia kulia, na mwisho wa dunia kufika.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

Nini maana ya K.K, na B.K?  (B.C na A.D).

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

UWE MWAMINIFU HATA KUFA.

UTAKASO NI SEHEMU YA MAISHA YA MKRISTO YA KILA SIKU.

MZAZI, JALI MAISHA YA KIROHO YA MTOTO WAKO.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments