MWANZO WA INJILI YA YESU KRISTO.

MWANZO WA INJILI YA YESU KRISTO.

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Karibu katika kujifunza maneno yale yale ya uzima ambayo yalikuwepo tangu zamani, ukweli pekee uliodumu na utakaodumu duniani kwa wakati wote.

Leo tutajifunza jambo moja katika kitabu cha Marko.. Tukisoma pale mwanzoni Inasema..

Marko 1:1 “Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.

2 Kama ilivyoandikwa katika nabii Isaya, Tazama, namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako”.

Kama tunavyoona hapo kitabu hichi cha Marko, kimeanza na utambulisho wake, ambao ni “mwanzo wa injili ya Yesu Kristo”, tofauti na kitabu kama cha Yohana, ambacho chenyewe kinaanza kwa utambulisho wa “Hapo mwanzo kulikuwa na Neno, naye Neno alikuwa kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.”.. Sasa ni vizuri tukazingatia sana tambulisho hizi za mwanzoni mwa Vitabu, kwani hiyo itatusaidia kujua maudhui ya injili nzima inaegemea wapi.

Na ndio maana ukisoma kitabu cha Yohana chote, utaona, hakijajikita katika kueleza mizunguko ya Yesu na kazi alizozifanya sana..Bali kilikuwa kimejikita kwa sehemu kubwa kumshuhudia Yesu kama Nuru ya ulimwengu. Ni kitabu kinachomzungumzia Bwana Yesu kama Neno la kweli, la Mungu kwa namna ya kipekee sana, kiasi kwamba ukikisoma katika utulivu chini ya uongozo wa Roho Mtakatifu, utajikuta unampenda Bwana zaidi na imani yako kuimarika sana.

Sasa tukirudi kwenye kitabu cha Marko nacho kinaanza kwa namna yake, kinasema “Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.”..Hii ikiwa na maana kuwa  kitabu hiki kimeegemea sana katika kuizungumzia injili yake. Sasa ni lazima tujue injili hiyo ilikuwa ni ya namna gani, na alihubiri nini..Ili na sisi tujifunze misingi ya injili ya kweli inavyopaswa iwe.

Hivyo ukiendelea mbele kidogo kwenye mstari wa 14 tutaona ni nini Yesu alianza kukihubiri katika huduma yake, Tusome;

Marko 1:14 “Hata baada ya Yohana kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya Mungu,

15 akisema, WAKATI UMETIMIA, na UFALME WA MUNGU UMEKARIBIA; TUBUNI, na KUIAMINI INJILI”.

Umeona, injili yake iliegemea katika  vipengele hivyo vinne.

  1. WAKATI UMETIMIA; Hii ikiwa na maana wakati wa mataifa kuokolewa umetima. Wakati uliokuwa unasubiriwa ndio umefika. Wakati wa wokovu kupatikana bure kwa kila kiumbe duniani haijalishi atakuwa ni muafrika, mzungu, mpagani, muabudu miungu. Na sisi pia tunapaswa kuhubiri kwetu tuhubiri kutimia kwa wakati huu. Ni wakati ambao mlango umefunguliwa kwa watu wote. Hivyo kila mmoja ni wajibu wake kuhakikisha neema hiyo haimpiti.
  2. UFALME WA MUNGU UMEKARIBIA: Kwamba mwisho wa kila kitu umekaribia; Dunia haitakuwa na wakati mrefu kabla ya mambo yote kuisha, Na utawala mpya wa Mungu kuanza..dalili zote zinaonyesha. Hivyo watu waelekeze macho yako sana mbinguni, kuliko kwenye mambo ya ulimwengu huu.
  3. TUBUNI: Sasa kwa kuwa wakati umetia, na ufalme wa mbinguni umekaribia sana, kilichobakia kwa mtu ni kutubu dhambi zake. Kukubali kuoshwa dhambi zake, kukubali kumgeukia muumba wake, katika wakati mchache aliobakiwa nao.
  4. NA KUIAMINI INJILI: Maana yake ni kuamini maneno yote ya uzima na kuyaishi. Kuyasikiliza mafundisho yote ya Yesu Kristo. Katika hali ya utakatifu.

Hivyo ni vipengele mama, vya injili. ili injili ikamilike ni lazima vipengele hivyo viwepo. Huko ndiko kulikuwa kuhubiri kwa Bwana wetu Yesu, na kwa namna hiyo Mungu alimthibitisha kuwa ndiye mwana wake wa pekee.

Hivyo na sisi tuende katika nyayo hizo hizo. Vilevile tujue kuwa hizi ni nyakati za mwisho Jiulize! Wewe kama wewe Je! upo ndani ya wokovu kisawasawa?. Embu chunguza maisha yako, uangalie umesimama wapi. Saa ya wokovu ni sasa na sio kesho…

Ukiwa unaichezea hii neema, ujue haitadumu siku zote juu ya maisha yako. Kuna wakati itaondoka, na ndio maana ikaitwa neema, maana yake ni kama offer tu, ambayo hukustahili wala hatukustahili, na siku zote offer huwa haidumu wakati wote, kuna kipindi itaondolewa, vivyo hivyo na neema itaondoka tu wakati Fulani ukitimia juu yako, kama hutaiamini injili, unyakuo utapita na wale wote ambao hawajampokea Yesu watabaki hapa duniani. Kama Mungu aliiondoa kwa Israeli wateule wake Israeli na kutupa sisi. Hatashindiwa kutuondolea na sisi na kuwapa wengine.

Warumi 11:17 “Lakini iwapo matawi mengine yamekatwa, na wewe mzeituni mwitu ulipandikizwa kati yao, ukawa mshirika wa shina la mzeituni na unono wake,

18 usijisifu juu ya matawi yale; au ikiwa wajisifu, si wewe ulichukuaye shina, bali ni shina likuchukualo wewe.

19 Basi utasema, Matawi yale yalikatwa kusudi ili nipandikizwe mimi.

20 Vema. Yalikatwa kwa kutokuamini kwao, na wewe wasimama kwa imani yako. Usijivune, bali uogope.

21 Kwa maana ikiwa Mungu hakuyaachia matawi ya asili, wala hatakuachia wewe”.

Hivyo tubu, ukabatizwe kama bado hujabatizwa katika ubatizo sahihi. Na Mungu atakupa Roho wake Mtakatifu.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

JE UDHAIFU WANGU UNAWEZA KUZUIA INJILI?

IVUMBUE INJILI YA KRISTO KUTOKA KATIKA KILA JAMBO.

HATARI YA KUHUBIRI INJILI TOFAUTI NA ILIYOANDIKWA KWENYE BIBLIA.

KUTOKUIHUBIRI INJILI,KUNA MADHARA GANI?

Naomba kujua nini maana ya kuteguka uvungu wa paja?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments