KUTOKUIHUBIRI INJILI,KUNA MADHARA GANI?

KUTOKUIHUBIRI INJILI,KUNA MADHARA GANI?

Kutokuihubiri injili, madhara yake ni yapi?


Shalom, Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe..Karibu tujifunze Biblia mtu wa Mungu…Leo tutajifunza mambo machache muhimu yahusuyo majukumu yetu ya kuihubiri Injili.

Injili maana yake ni “Habari njema”..Habari yoyote au ujumbe wowote unaoupeleka kwa mtu au watu ulio mwema huo tayari ni injili…Zipo Injili za aina nyingi duniani lakini ipo injili moja tu ya wokovu..Au kwa lugha nyingine inaitwa “Injili ya Msalaba”…Injili ya Msalaba inamhusu Yesu Kristo mwana wa Mungu aliyetumwa kuichukua dhambi ya ulimwengu..Hiyo inahusu wokovu wa mwanadamu ambaye alipotea dhambi. Na Kumbuka wanadamu wote walipotea dhambini hivyo injili hii inamuhusu kila mmoja wetu.

Sasa Baada ya Bwana Yesu kuondoka ilikuwa ni sharti injili ihubiriwe ulimwenguni kote kwa kila kiumbe, na kwamba kila mwanadamu lazima aisikie injili hiyo ya wokovu…Na kwa hiari yake mwenyewe achague UZIMA au MAUTI. Kwasababu hiyo basi akawaagiza mitume wake akawaambia..

Marko 13.9-10

Marko 13.9 “Nanyi jihadharini nafsi zenu; maana watawapeleka ninyi mabarazani; na katika masinagogi mtapigwa; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao.

10 NA SHARTI INJILI IHUBIRIWE KWANZA KATIKA MATAIFA YOTE”.

Hapo anasema ni SHARTI!..Maana yake ni lazima injili ifike kila mahali..Kwa uzima na kifo, hata ikigharimu uhai ni lazima injili iwafikie watu..Hivyo hilo ni jukumu tulilopewa watu wote tuliompokea Kristo..Ni lazima tuihubiri Injili…Na siku zote Mungu anatumia watu kuhubiri Injili, kawachagua watu kusimama madhabahuni kumwakilisha…kamwe hatumii wanyama, wala malaika, wala kiumbe kingine chochote kamchagua mwanadamu tu!!..

Sasa kuna hatari kubwa sana ya kutokuihubiri injili…Kuna hatari kubwa sana ya kutokuitumia karama Mungu aliyokupa katika kuwahubiria wengine..Bwana amekuokoa wewe, ili na wewe ukawe msaada kwa wengine…hajatuokoa ili tu tufurahi sisi wenyewe..Kama tunavyojua wengi wetu hatujampokea Yesu kwa kutokewa na yeye…wengi wetu tumesikia injili ikihubiriwa mahali fulani na mtu Fulani wa Mungu ndipo kwa kupitia hayo mahubiri tukaokoka… Kutokuihubiri injili ni kosa kwa mtu anayeitwa mkristo.

Injili ni kuambukiza:

Kadhalika huo ndio utaratibu wa Mungu, Ni lazima tuisikie kutoka kwa mtu fulani wa Mungu…na hivyo na sisi pia lazima tuwahubirie wengine ambao nao watasikia kutoka kwetu, ni kama mnyororo huyu anamzaa huyu katika imani, huyo anamzaa Yule na kuendelea..

Sasa kama umeokolewa na hutaki kuzaa wengine…kuna hatari kubwa sana…Tukirudi kwenye biblia tunamsoma Nabii mmoja aliyeitwa EZEKIELI..Huyu alikuwa ni nabii wa Mungu wa kweli kabisa., ambaye alikuwa miongoni mwa watu wachache waliochukuliwa kwenda Babeli…wakati yupo huko Mungu mwenyewe alimtokea akamwonyesha maono akiwa ameketi katika kiti chake cha Enzi huku maserafi na makerubi wakiwa wamemzunguka pande zote..akasikia sauti ya Mungu mwenyewe..Na Mungu akamtuma aende kuwaambia wana wa Israeli maovu yao na maasi yao na mambo yatakayokuja kuwatokea huko mbeleni wasipotubu.

Lakini yeye alipotoka pale baada ya kuona maono hayo…akaenda kukaa kimya, hakuwaambia watu chochote… sio kwamba alikuwa na dharau hapana! Hakumdharau Mungu…lakini alikuwa anaogopa kuwaambia(Alikuwa na hofu)….alikuwa na uchungu kweli na hasira moyoni, kwa maovu yaliyokuwa yanafanyika katikati ya watu wake lakini alikuwa anajifikiria fikiria namna ya kuwaambia..…akakaa siku saba hawaambii hao watu maono aliyoonyeshwa na Mungu…Baada ya siku saba maono yakamjia tena na kumwonya kwa anachokifanya cha kutowaambia watu maneno ya Mungu..Mungu akamwonya vikali kwa tabia hiyo..

Tusome..

Ezekieli 3:15 “Ndipo nikawafikia watu waliohamishwa, huko Tel-abibu, waliokuwa wakikaa karibu na mto Kebari, nikafika huko walikokuwa wakikaa; nikaketi huko miongoni mwao muda wa siku saba, katika hali ya ushangao mwingi.

16 Hata ikawa, mwisho wa siku saba, neno la Bwana likanijia, kusema,

17 Mwanadamu, nimekuweka kuwa mlinzi wa nyumba ya Israeli; basi, sikia neno hili litokalo katika kinywa changu, ukawape maonyo haya yatokayo kwangu.

18 Nimwambiapo mtu mbaya, Hakika utakufa; wewe usimpe maonyo, wala husemi na huyo mtu mbaya ili kumwonya, kusudi aache njia yake mbaya na kujiokoa roho yake; mtu yule mbaya atakufa katika uovu wake; lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako.

19 Lakini ukimwonya mtu mbaya, wala yeye hauachi ubaya wake, wala njia yake mbaya, atakufa katika uovu wake; bali wewe umejiokoa roho yako”.

Umeona?..Ezekieli baada ya kusikia maneno hayo kutoka kwa Bwana kwamba “damu ya mtu itakuwa juu yake endapo hatamwambia maneno aliyoambiwa amwambie”..Ndipo akaelewa hakuna suala la mizaha tena kwenye kupeleka ujumbe wa Mungu kwa watu…Tangu wakati huo chochote alichoonyeshwa aliwafikishia wahusika kama kilivyo…Kwasababu alijua atadaiwa damu!. Hakuishi maisha ya kutokuihubiri injili tena.

Ndugu..Kama Bwana anakuonyesha maono ya kuwaonya watu juu ya dhambi zao na wewe huwaambii jifunze kwa Ezekieli hapo juu, kama unafahamu Neno na uwaambii wengine kuna hatari…Ni afadhali uwaambie wakatae kwa mapenzi yao wenyewe wewe utakuwa umenawa mikono..kuliko kutowaambia kabisa…mtu huyo akitoka na kwa bahati mbaya akagongwa na gari na kufa, unadhani wewe utakuwa katika hali gani?.

Kama umefahamu kuwa wazinzi na waasherati watakwenda kuzimu wasipotubu, na wewe mwenyewe sio mwasherati kwanini usiwaambie?…Mwambie ili aokoke, suala la kumbadilisha sio juu yako…wewe kazi yako ni kuhubiri tu injili…Lakini pia kama na wewe binafsi unafanya mambo hayo hayo wanayowafanya hao basi hapo usiwahubirie kwasababu wewe mwenyewe unahitaji wokovu..Na kipofu hawezi kumwongoza kipofu mwenzake..biblia inasema hivyo.

Anza kuchukua hatua:

Hivyo kama ulikuwa uhubiri..anza leo!..Kama ulikuwa unaogopa kuwaambia watu juu ya habari ya siku za mwisho anza kuwaambia..Ezekieli aliogopa kuliko wewe lakini aliposikia suala la damu ya hao watu itatakwa juu yake, aligueka mara moja na wewe hivyo hivyo geuka leo..Na Bwana atakusaidia. Ipo hatari kubwa sana ya kutokuihubiri injili

Na kama hujaokoka kabisa..Tubu leo, mlango wa Neema bado upo wazi.. ila hautakuwa hivi siku zote..Umesoma hapo juu kitu gani kitamtokea mtu Yule atakayekufa katika dhambi zake huku ameonywa na amekataa…

Tusome tena…

Eze.3:19 “Lakini ukimwonya mtu mbaya, wala yeye , wala njia yake mbaya, atakufa katika uovu wake; bali wewe umejiokoa roho yako”.

Na wewe leo umesikia injili usipotaka kutubu utakufa katika dhambi zako na madhara ya kufa na dhambi ni ziwa la moto.

kwahiyo pale ulipo mwombe Bwana msamaha, tubia uasherati wako kama ni mwasherati, ulevi wako,uongo wako, rushwa zako, usengenyaji wako,wizi wako, matusi yako… kisha katafute Ubatizo sahihi kama hujabatizwa na Roho Mtakatifu atakutakasa na kukufanya kuwa mkamilifu kama yeye alivyo mkamilifu…

Marko 1:15 “akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili”.

Bwana akubariki.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Shalom.

Mada Nyinginezo:

KILEMBA CHA NEEMA, JE! UMEMVIKA MWANAO?

JE VIBWENGO NI KWELI VIPO?

 

KISIMA CHA MAJI YA UZIMA NI KILE KILE CHA ZAMANI.

UPAKO NI NINI?

Ulinzi wa daima (eternal security) Je! ni neno la kimaandiko?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Rogaht
Rogaht
4 years ago

Samahani ndugu. Ikiwa mimi nina kasoro za kusikia je naweza kuhubiri injili kwa njia ya simu?