JINSI ROHO MTAKATIFU ANAVYOKUJA JUU YA MTU.

JINSI ROHO MTAKATIFU ANAVYOKUJA JUU YA MTU.

Katika agano la kale, wayahudi walivyochanganyikiwa sana juu ujio wa masihi mpaka kupelekea kugawanyika makundi mengi, ndivyo ilivyo hata katika agano jipya watu wengi wanavyochanganyikiwa katika habari ya Roho Mtakatifu jinsi anavyokuja juu ya mtu, hadi sasa imepelekea kutokea makundi mengi tofauti tofauti ambalo kila moja linaamini katika uthibitisho wake.

Kama tunavyofahamu katika agano la kale biblia ilishatabiri kuwa Masihi (YESU KRISTO) atakuja, lakini kwa bahati nzuri au mbaya haikueleza katika mtitiriko unaoeleweka sana, bali sisi wa agano jipya kwa Kutazama maisha ya Kristo ndio tunaoelewa jinsi maandiko yalivyotimia ,..Lakini katika agano la kale ilikuwa ni ngumu sana kuelewa, na saa nyingine maandiko yaliyonekana kama yanajichanganya..Kwamfano unabii alioutoa Isaya kuhusu Kristo katika (Isaya 53), inaonyesha kuwa Masihi atakuja kuteswa na kuuliwa kwa ajili ya dhambi za watu wengi..Lakini sehemu nyingine katika kitabu hicho hicho cha Isaya inasema Masihi atakuwa mfalme, naye ataketi katika kiti cha enzi cha Daudi, naye atadumu milele.

Unaona sehemu moja inasema atakufa lakini sehemu nyingine inasema atadumu milele,..Lakini je! Wale walioshikilia tu unabii mmoja labda tuseme wale walioamini kuwa Masihi atasulibiwa, au wale walioamini tu Masihi ataishi milele, je! wote Hawapo sawa? Jibu ni La!..Sisi tunaoishi katika agano jipya ndio tunaojua kuwa Wote wapo sawa kabisa, lakini wote walioweza kuamini nabii zote mbili ndio wapo sawa zaidi kuliko wale wengine, kwani ni Kweli kuna wakati Kristo atasulibiwa atakufa lakini atafufuka na atarudi tena, na atakaporudi atakuja kama Mfalme wa Wafalme na Bwana wa Mabwana, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho kama nabii zote mbili zilivyotabiri.

Yohana 2:33 “Aliyanena hayo akionyesha ni mauti gani atakayokufa.

34 Basi mkutano wakamjibu, Sisi tumesikia katika torati ya kwamba Kristo adumu hata milele; nawe wasemaje ya kwamba imempasa Mwana wa Adamu kuinuliwa? Huyu Mwana wa Adamu ni nani?

35 Basi Yesu akawaambia, Nuru ingaliko pamoja nanyi muda kidogo. Enendeni maadamu mnayo nuru hiyo, giza lisije likawaweza; maana aendaye gizani hajui aendako”.

Sasa tukirudi katika habari za Roho Mtakatifu, kama tusipoweza kuyavunja maandiko na kufahamu utendaji kazi wake, tutaishia kuchanganyikiwa sana, na mwisho wa siku kila mmoja ataamini anachokiamini…

Leo hii kuna watu wanaomini kuwa uthibitisho pekee wa mtu kuwa na Roho Mtakatifu ni kudhihirisha karama Fulani ndani yake, kama vile kunena kwa lugha, kutoa unabii, kufundisha, kuhubiri n.k…na mtu yeyote asipodhihirisha mojawapo ya karama yoyote basi huyo bado hajapokea Roho Mtakatifu na maandiko wanayoyasimamia ni haya …

Matendo 2:17 “Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto.

18 Naam, na siku zile nitawamwagia watumishi wangu wanaume na wanawake Roho yangu, nao watatabiri”

Na ….

1Wakoritho 12:4 “Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule”:

Vile vile wapo wengine wanaoamini kuwa uthibitisho wa Roho Mtakatifu, ni kuwa atakuongoza na kukutia katika kweli yote sawasawa na Yohana 16:13 “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.” ….

na hivyo uthibitisho mwingine wowote mbali na huo ni uongo..

Halikadhalika wapo wanaoamini kuwa uthibitisho pekee wa Roho Mtakatifu ni pale anapokushuhudia ndani yako kuwa wewe ni mwana wa Mungu, …sawasawa na Warumi 8:16 “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu;”

Wapo wengine wanaoamini uthitisho wa Roho Mtakatifu peke yake ni kukufanya uwe mtakatifu kama vile jina lake lilivyo.…

Na makundi mengine mengi…

Lakini swali ni kama lile lile tu la watu wa agano la kale, je! Wote hawa ni waongo?…Jibu ni hapana wote wapo sawa kabisa!!, isipokuwa tu wanashindwa kutofuatisha utendaji kazi wa Roho Mtakatifu juu ya mtu kulingana na wakati na majira. Kama tu vile wale wa agano la kale walivyoshindwa kufahamu kuwa kuna kuja kwa kwanza kwa Kristo na kuja kwa pili.

Ifahamike kuwa Bwana Yesu aliposema hakuna mtu anaweza kuja kwake kama hakuvutwa na Baba yake aliyempeleka, alimaanisha kusema vile, Leo hii “huwezi hata kuchomwa moyo na maneno ya Mungu kama siyo matunda ya Roho Mtakatifu yanayofanya kazi ndani yako”, ukiona tu unaamini kuna Mungu, ukiona unatamani kumfahamu Mungu hata kama hujaokoka, ukiona unahukumiwa ndani yako kwa ajili ya dhambi zako, ukiona una hofu ya Mungu, basi ufahamu kuwa huyo ni Roho Mtakatifu anatenda kazi ya kukuvuta kwake,..Jambo ambalo si watu wote wanalo, usidhani kuwa injili unayoisikia na kukuchoma moyo inamchoma kila mtu duniani, dhambi uzifanyazo na kusikia kuhukumiwa zinamuhukumu kila mtu duniani, kama ingekuwa hivyo kusingekuwa na vitendo vya kinyama unavyoviona kila mahali..Si wote wapo hivyo, na ndio maana hupaswi kuichezea hiyo neema kwasababu kuna wakati utafika Roho Mtakatifu hatakuvuta tena kwa Mungu, ukishafika huo wakati ndugu, hata Bwana Yesu mwenyewe akutokee hapo, na malaika wote mbinguni, hutakaa ugeuke, kwasababu Roho wa kukuvuta hayupo.

Sasa, ikitokea mfano Yule mtu akautii ule wito na kuamua kutubu dhambi zake, na kufuata vigezo vyote alivyoambiwa na Bwana Yesu vya kwenda kubatizwa, katika maji mengi na kwa Jina la BWANA YESU, hapo ndipo Yule Roho aliyekuwa anamvuta anapata kibali cha kuingia ndani yake, na kufanya maskani humo, na akishaingia anakuwepo huko milele, mtu huyo ndio anakuwa amezaliwa mara ya pili..Sasa kwa kuwa Yule mtu bado ni mchanga kiroho, Roho Mtakatifu anaanza kazi kadha wa kadha ndani yake..mojawapo ni kumsafisha na kuua baadhi ya vitu ambavyo alikuwa hawezi kuviacha, Roho Mtakatifu anamfanya upya tena..

Tito 3:5 “si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu;’’

Anaanza kumfanya aupende utakatifu kuliko kitu kingine chochote, hapo ndipo hamu ya baadhi ya mambo ya kidunia inakufa kabisa…hizo ni dalili za awali kuwa Roho Mtakatifu yupo ndani yako..Kwa nje unaweza usione chochote, wala usisikie msisimko wowote lakini ndani kunawaka moto wa kutaka kuwa kama Mungu..

Pili anatenda kazi ya kumwongoza na kumtia katika kweli yote: Hapa Anaanza kumwongoza katika vyanzo sahihi vya Neno lake, anaanza kumpa kiu ya kujifunza Neno la Mungu, faraja yake mtu huyo inakuwa kwenye Neno la Mungu tu, na si mahali pengine, anaanza kuona Mungu kwake ndio kila kitu..Uthibitisho ni kuwa hapo kabla hayo mambo alikuwa hayaoni…Ile kiu inaongezeka siku baada ya siku.

Jambo lingine analolifanya Roho Mtakatifu ni kumshuhudia huyo mtu kuwa yeye ni mwana wa Mungu, kushuhudiwa huku sio kusikia sauti inakuambia wewe ni mwana wa Mungu, hapana, bali ni kuona maisha yako unayopitia yanafanana na wana wote wa Mungu waliopita huko nyuma,…..yaliyowapata watakatifu wa nyuma na wewe yanakupata yawe ni mema yawe ni mabaya..Biblia ndio itakuwa uthibitisho wako..Mungu kwako anajidhihirisha kama Baba.

1Petro 5:9 “….mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani.”

Jambo lingine ni anakuwa kwako kama mfariji, na mshauri(1Thesalonike 1:16, 2Wakoritho 13:14)): Utaona tu, jinsi atakavyokuwa anakutia nguvu wakati baada ya wakati, unapoishiwa nguvu, utashangaa anaachilia jambo Fulani kubwa ambalo linakupa nguvu ya kuendelea mbele kwa muda mrefu sana…Na ndio maana tunasema mtu yeyote aliye na Roho Mtakatifu kweli hawezi kuishia njiani katika safari yake ya wokovu..(Isaya 40:27-31)

Na ndio maana katika hicho kipindi chote Roho wa Mungu anachokutengeneza, hupaswi kumzimisha,..Wengi wanamzimisha kwa kuanza kuyarudia yale machafu waliyoyaacha huko nyuma, tayari Mungu alishawafanya kuwa huru, lakini bado wanaurudia utumwa..Hapo ndipo mtu hakui wala hasongi mbele kiroho, anabakia kuwa katika hali ile ile, miaka nenda miaka rudi..yeye ni mchanga tu.

Lakini ikiwa mtu huyu atatembea na Roho Mtakatifu kwa uaminifu wote, Roho anakuwa anajaa ndani yake kidogo kidogo, mpaka anafikia ujazo kamili wa Roho Mtakatifu, na ujazo huo ni uhitimu. Hapo ndipo Roho Mtakatifu anakuvika nguvu za kuweza kuwa shahidi wake, kama vile Bwana Yesu alivyoaambia mitume wake..

Matendo 1:8 “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi”.

Hichi ndio kile kilichomkuta Bwana Yesu wakati ule anakwenda kubatizwa, sio kana kwamba ile ndio ilikuwa mara yake ya kwanza kumpokea Roho hapana bali Roho alikuwa naye tangu kuzaliwa kwake, lakini kwasababu ya kazi ilimpasa Mungu amwongezee nguvu kwa Roho Yule aliyekuwa ndani yake ili kushuhudia habari za ufalme wa mbinguni. Na ndicho kilichokuwa juu ya Mitume sio kwamba kipindi walichokuwa wanatembea na Bwana walikuwa hawana Roho Mtakatifu, walikuwa naye, ndio yule aliyemfunulia Petro kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu n.k isipokuwa walikuwa naye si katika kile kiwango kile Mungu alichokikusudia kwa kazi yake waliyokuwa wanakwenda kuifanya hapo mbele.

Ndivyo ilivyo hata sasa, wengi tunatamani tupokee Roho Mtakatifu katika hatua ya mwisho, lakini sio kuanzia katika hatua ya kwanza.. siku hiyo hiyo tumempa Kristo maisha yake, bado siku hiyo hiyo wanataka Roho Mtakatifu atupe nguvu ya kuwa mashahidi wake kwa mfano wa mitume,..Ni kweli Roho anaweza kufanya yote kwa pamoja, lakini fahamu kuwa ndani yake, bado utakaa chini tu akufundishe,atembee na wewe, akuandae na akuthibitishe.

Hivyo kaka/dada, fahamu kuwa Roho Mtakatifu ni zaidi ya kunena kwa lugha, au kuona maono..Usifurahie kusema tu nilipokea Roho Mtakatifu siku ile nilipoamini,,jiulize je! Hadi sasa Roho Mtakatifu anatembea na wewe, au ulishamzimisha siku nyingi..Je! anakurudisha katika utakatifu?, Je! Anakushuhudia kuwa wewe ni mwana wa Mungu. Je! Anakuongoza katika kweli yote..Je! anakupasha bahari ya mambo yanayokuja?..Ikiwa hivi vitu vimekufa ndani yako, tubu upesi umgeukie Mungu, mwambie Bwana nataka nianze na wewe upya.

Na ikiwa bado Roho Mtakatifu yupo mbali na wewe nikimaanisha kuwa hujamkabidhi bado Bwana maisha yako, fahamu kuwa biblia ipo wazi inasema, Warumi 8:9… “Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake”.

Pasipo huyo, usidhani kuwa utaiona mbingu, au utamfahamu Mungu..Tubu leo kwa kumaanisha kumfuata Kristo itii injili, kisha nenda kabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi, na kwa jina la Bwana Yesu Kristo, Roho Mtakatifu aingie ndani yako na aanze kufanya kazi kwako.

Bwana akubariki sana. Tafadhali “Share” Ujumbe huu kwa wengine. Na Bwana atakubariki. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazondana:

Je! Umepokea kweli Roho Mtakatifu?

Hatua za Roho Mtakatifu katika kutuongoza.

Je! karama ni uthibitisho pekee wa kuwa na Mungu?

HOME

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
8 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Joseph
Joseph
1 year ago

Nashukuru sana mwalimu kwa fundisho zuri
Ubarikiwe

Isack
Isack
1 year ago

Nimepokea sana barikiwa mtumish wa mungu

Sephania
Sephania
1 year ago

Ase! Nimefalijika kweli kwa somo hili !Mungu wa !Mbingu na nchi na awabaliki

David Akleo
David Akleo
2 years ago

Ubarikiwe mtumishi wa Mungu, bwana akubariki na akutie nguvu uendelee kutoa mafundisho yaliyo mema juu ya ufalme wenye nguvu upitao falme zote.

Emmanuel Kitengule
Emmanuel Kitengule
2 years ago

Barikiwa sana mwalimu.

lucas mhula
lucas mhula
2 years ago

Yaani watumishi katika siku mmejibu maswali yangu yote kuhusu Roho Mtakatifu ni kupitia somo hili, yaani mbarikiwe kwa sana sana sana, hakika nimejifunza kitu leo KIKUBWA SANA.🙏🙏🙏