WALA MSIUANGALIE MWILI, HATA KUWASHA TAMAA ZAKE.

WALA MSIUANGALIE MWILI, HATA KUWASHA TAMAA ZAKE.

Warumi 13:14 “Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo, wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake”.

Shalom, Jina la Bwana wetu Yesu Kristo, mweza wa yote libarikiwe daima. Nakukaribisha tena tuyatafakari kwa pamoja maneno ya uzima ya Bwana wetu.

Kama hayo maandiko hapo juu yanavyotuambia tusiuangalie mwili, kuangalia mwili maana yake ni kuujali mwili kupitiliza, na matokeo ya kufanya hivyo, mwisho wa siku huwa ni kuziwasha tamaa zake.

Na ikishafikia hatua hiyo ya kuwasha tamaa za mwili, ndio hapo unafanyika mtumwa au teja wa mwili, kiasi kwamba mwili ukitaka hivi, ni lazima upatiwe haja yake vinginevyo utakusumbua sana, kama sio kukuletea shida..

Leo kwa ufupi tutakwenda kuzitazama baadhi ya hizi tamaa za mwili na jinsi gani tutaweza  kuzidhibiti sisi kama wakristo. Zipo nyingi lakini tutazitazama hizi kuu tatu (3), kwa leo.

Lakini kabla ya kwenda kuziangalia jambo ambalo tunapaswa tujue ni kwamba tamaa za mwili ni Mungu mwenyewe katuumbia, wala si shetani. Lakini hakutuumbia zitushinde, bali tuzitawale ili zitumike pale zinapopasa au zinapostahili.

Sasa embu tuzitazame baadhi ya hizo;

  1. USINGIZI.

Mwili huwa unatamani kupumzika, na ndio maana  utashangaa muda mwingine usingizi wenyewe unaanza kuja bila hata wewe kuukaribisha, sasa hiyo ni tamaa ambayo Mungu kaiweka katika mwili. Lakini sote tunajua si kila wakati ni wa kulala.  Kwasababu unajua kabisa ukifanya hivyo utapata hasara ya mambo mengi.

Mithali 20:13 “Usipende usingizi usije ukawa maskini; Fumbua macho yako nawe utashiba chakula”.

Ukiundekeza usingizi hutakwenda kazini kwako, hutakwenda shuleni, hutafanya jambo lolote lenye faida, wakati mwingine utashindwa hata kuamka usiku usali, kama ikiwa wewe utakuwa ni wa kulala kila wakati.  Lakini kiuhalisia ni kwamba, tamaa hii watu wengi wameweza kuishinda, kwasababu moja au nyingine, wameshauzoeza mwili mpaka mwili wenyewe umeshazoea,

Kwamfano utakuta labda mtu amejipangia ratiba ya kuamka kila siku za 11 alfajiri awahi kazini, kwa kuwa ameshajijengea huo utaratibu kwenye kichwa chake, ukishafika huo muda tu usingizi wenyewe unakata. Hata kama angejijengea iwe ni saa  9 alfajiri bado mwili ungezoea vilevile, lakini wakati huo huo utaona mtu mwingine atashindwa!! Inakuwa kama ni mtihani mkubwa kwake, , lakini ukiangalia sio kwamba yule aliyeweza amepewa uwezo tofauti hapana, utagundua kwamba mmoja kauendekeza na ndio maana unamshinda, na mwingine kaudhibiti na ndio maana anaamka muda ule bila shida yoyote. Japo mwanzoni alianza kwa shida, Lakini aliweza kwasababu alijizoesha.

2) CHAKULA.

Tamaa nyingine ya mwili ni chakula. Kila mmoja ameumbiwa njaa na kiu. Hivyo utafika wakati, unajisikia tu mwenyewe hamu ya kuweka kitu tumboni, au kuburudisha koo lako, na kama tunavyojua katika kula na kunywa ipo burudani Fulani mtu anaipata.

Lakini pia kwenye chakula au kwenye vinywaji mtu asipokuwa na kiasi tunajua ni kitu gani kitampata, yaani kila wakati yeye ni kula tu, ataishia kuvimbiwa, au kupata uzito wa kupita kiasi na magonjwa,

Lakini ni heri angekuwa inaishia kwenye kuvimbiwa tu, lakini mtu kama mlevi ni kwasababu gani amekuwa mlevi? ni kwasababu ameitii KIU ya mwili wake. Ameona mwili wake unahitaji kuburudisho cha namna ile na yeye akautii, akaanza kunywa mpaka akawa mlevi, anasahau madhara yatakayotoka na unywaji ule. Halikadhalika wavutaji sigara, na watumiaji wa madawa ya kulevya, wote, hawa ni matokeo ya kutii kiu na miili yao, na ndio maana wanakuwa majeta wa mambo hayo..

Mithali 23:20 “Usiwe miongoni mwao wanywao mvinyo; Miongoni mwao walao nyama kwa pupa.

21 Kwa maana mlevi na mlafi huingia umaskini, Na utepetevu humvika mtu nguo mbovu”.

Aliyeacha pombe sio kwamba hakuwa na kiu kama uliyo nayo wewe, lakini alipata ufahamu ni jinsi gani ya kudhibiti matamanio ya kiu yake na hivyo, akajizuia. Akawa anakunywa tu soda. Na mwisho wa siku mwili wake ukazoe, mpaka ile kiu ya pombe ikakatika ndani yake. Asione tena ni shida kuiacha, hali kadhalika na sigara na madawa ya kulevya waliaocha, wengi wao walifanya vivyo hivyo.

3) ZINAA.

Hii ni moja ya tamaa ya mwili, ambayo nguvu yake hainatofauti sana na ile ya usingizi au chakula,  kuishinda, isipokuwa watu wengi wameiendekeza kwa kutaka kwao wenyewe. Kiuhalisia ni kwamba Mungu kaiweka tamaa hii ndani ya kila mwanadamu, Lakini itumike kwa wakati maalumu.. Na kwa kiasi pia. Na ni rahisi kuithibiti kabisa.

Mungu aliruhusu itumike kwa wana-ndoa tu, lakini pale mtu anapoanza kuichochea kabla ya wakati wake, hapo ndipo inapoleta madhara ambayo ni heri tu yangekuwa ya mwilini, lakini zaidi sana ni yanakwenda mpaka rohoni. Tutakuwa wanafki kama tutaweza kuudhibiti usingizi hata kama pale unapotulemea, mpaka inakuwa ni desturi yetu hatuoni shida tena, lakini tutashindwa kudhitibi zinaa.

Ukijizoesha utazishinda na wala hazitakuendesha, lakini ukiziendekeza kwa kuutazama mwili zitakushinda na utakuwa teja wa hizo. Utakuwa mzinzi kila siku, utakuwa mtazamaji wa video chafu mitandano, utakuwa mfanyaji wa punyeto kila siku, na hutashindwa kuziacha kwasababu umeuendekeza mwili kwa mambo kama hayo..

Wimbo 3:5 “Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe”.

Sasa utaacha kwa namna gani?

Ni kwa kuviweka mbali vichochezi vyote vya uzinzi vilivyo karibu na wewe, kama vile kuepuka mazungumzo ya kizinzi ukutanapo na rafiki zako.

Waefeso 5:3 “Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu;”

Vilevile kufuta muvi zote, na kuacha kuangalia tamthilia zenye maudhui za kimapenzi kwenye tv, pia kuacha kuperuzi peruzi na kusoma Makala na vitabu vyenye taswira kama hizo mitandaoni. Hilo litakusaidia sana kuzizima tamaa hizi za mwili. Kwasababu Biblia inasema..

Mithali 26: 20 “Moto hufa kwa kukosa kuni;…

Vilevile Kuacha kuchat-chat na watu wa jinsia tofauti na wewe, kwenye mambo yasiyokuwa na msingi..Hilo nalo ni lango ambalo shetani analitumia sana  kuwanasa watu wengi kwenye mitego hiyo.

Ukizingatia hayo tamaa hizo zitazimika ndani yako, na wewe mwenyewe utashangaa jinsi ilivyo rahisi kuvishinda, utaweza kukaa hata miaka 50, bila kufanya hayo mambo na usione ugumu wowote ule.

Na jambo hili, sio tu kwa wale ambao hawajaoa/ au kuolewa. Ni kwa watu wote, kwasababu kama pia usipokuwa na kiasi katika hili kwenye ndoa yako, shetani naye atakujaribu mpaka kwenye mambo mengine yasiyompendeza Mungu. Na ndio hapo utasikia wana-ndoa wanaingiliana kinyume na maumbile, au wengine wanatoka nje ya ndoa zao, hiyo yote ni kukosa kiasi.. Biblia inasema..

1Wakorintho 7:5 “Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu”.

Hivyo kwa kuhitimisha ni kwamba, kila mmoja wetu aanze kuishi maisha ya kutoutazama mwili, (yaani kutoruhusu tamaa za mwili wake kumwendesha). Na hiyo itatupelekea kuyashinda mambo mengi sana. Kwasababu adui wetu wa pili, baada ya shetani ni miili yetu. Na sisi hatupaswi kuwa watu wa mwilini kama wanyama. Bali watu wa rohoni, ambao tunaweza kudhibiti vyote kwa yeye atutiaye nguvu. Ambaye ni Bwana wetu Yesu Kristo.

Bwana akubarikijiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Soma na hapa; >> MOTO HUFA KWA KUKOSA KUNI.HATA UASHERATI NAO

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Choyo ni nini kibiblia? (Luka 12:15, Zaburi 10:3)

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 3

Nini maana ya “mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili”?

KUJIFUNUA KWA YESU KWA PILI.

UFUNUO: Mlango wa 15

NGAZI 7 AMBAZO MKRISTO NI LAZIMA AZIPANDE KUUFIKIA UKAMILIFU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
5 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Lucas mhula
Lucas mhula
2 years ago

Amen🙏🙏

Lucas mhula
Lucas mhula
11 months ago
Reply to  Admin

Amina mtumishi wa Bwana, ubarikiwe pia