NITAUVUTAJE UWEPO WA ROHO MTAKATIFU KARIBU NAMI?

NITAUVUTAJE UWEPO WA ROHO MTAKATIFU KARIBU NAMI?

Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe,

Leo tutajifunza jinsi ya kuuvuta uwepo wa Roho Mtakatifu karibu nasi. Yapo mambo makuu matatu yanayovuta uwepo wa Mungu karibu nasi.

  1. MAOMBI

Hili ni jambo la kwanza linalohifadhi uwepo wa Roho Mtakatifu ndani yetu. Tunapoingia kwenye maombi Roho Mtakatifu anazidi kusogea karibu nasi,  anasogea kuomba pamoja na sisi (Warumi 8:26) na vile vile anasogea kuzungumza na sisi.

Kama wewe ni msomaji wa biblia utakumbuka kipindi, Bwana Yesu anabatizwa katika mto Yordani na Yohana, utaona Roho Mtakatifu alishuka juu ya Bwana kwa mithili ya HUA (Yaani Njiwa).

Lakini katika tukio hilo kuna siri moja imejificha pale, ambayo ukisoma kwa haraka haraka unaweza usiigundue. Na siri yenyewe ni MAOMBI!. Utaona baada ya Bwana kutoka majini, na kusogea pembeni utaona alianza KUOMBA!, na wakati akiwa katika maombi, ndipo Mbingu zilipofunguka na Roho Mtakatifu kushuka juu yake.

Luka 3:21 “Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, NAYE ANAOMBA, mbingu zilifunuka;

22 Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili, kama hua; sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe”.

Umeona? Ni wakati alipokuwa anaomba ndipo Roho Mtakatifu alishuka juu yake, na sio wakati anabatizwa tu peke yake.

Vile vile utaona kipindi cha Pentekoste, Mitume na wanafunzi wengine wapolikuwa wamekusanyika mahali Pamoja katika ghorofa wakidumu katika kusali, na kule kule ndipo Roho Mtakatifu akashuka juu yao na kuwajaza nguvu (Soma Matendo 1:13-14, Matendo 2:1-2).

Na sehemu nyingine nyingi, utona kuwa Roho Mtakatifu alishuka wakati watu wakiwa kwenye maombi..

Matendo 4:31 “Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri”.

Vile vile na sisi tukitaka kuuvuta uwepo wa Roho Mtakatifu hata tumuhisi ndani yetu, au katikati yetu basi hatupaswi kuyakwepa MAOMBI, kadhalika tukitaka tumsikie anataka nini kwetu au anasema nini, njia pekee ni Maombi!

Sasa inawezekana hujui namna ya kuomba, ni rahisi sana.. Kama utatamani kupata mwongozo wa namna ya kuomba basi tutumie ujumbe inbox, ili tuweze kukutumia somo linalohusu “Njia bora ya kuomba”

  1. KUSOMA NENO.

Hii ni njia nyingine ya Muhimu ya kuuvuta uwepo wa Roho Mtakatifu karibu nasi. Kazi mojawapo ya Roho Mtakatifu ni kutuongoza na kututia katika Kweli yote (Yohana 6:13-14), na Kweli ni Neno la Mungu (Yohana 17:17). Hivyo tunapotenga muda wa kuishika biblia na kuisoma kwa lengo la kujifunza, basi Roho Mtakatifu anasogea karibu nasi sana. Ni lazima atusogelee kwasababu ndio kazi yake yeye kutufundisha na kutufunulia maandiko.

Tunaweza kujifunza kwa yule Mkushi aliyekuwa anarudi nchini kwao, ambapo njiani alijikuta anafungua kitabu cha Isaya 53, kilichokuwa kinazungumzia Habari za Masihi, Yesu lakini hakuwa na ufunuo wowote juu ya hilo, Ndipo Roho Mtakatifu akaingia kazini kujisogeza karibu naye ili amtie katika kweli yote!!..

Roho Mtakatifu akaanzaa kuzungumza kwanza na Filipo siku kadhaa kabla hata ya Mkushi huyo kufikiria kusoma hilo andiko, Roho Mtakatifu akaanza kutengeneza njia ya kumkaribia Mkushi huyo, akamwambie Filipo ashuke njia ya jangwa, na alipokutana na yule Mkushi yupo matatani haelewi maandiko, ndipo Roho Mtakatifu akaanza kuzungumza kupitia kinywa cha Filipo. Na hatimaye kumfunua macho yake na kumtia katika kweli yote.

Matendo 8:29 “Roho akamwambia Filipo, Sogea karibu na gari hili, ukashikamane nalo.

30 Basi Filipo akaenda mbio, akamsikia anasoma chuo cha nabii Isaya; akanena, Je! Yamekuelea haya unayosoma?

31 Akasema, Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza? Akamsihi Filipo apande na kuketi pamoja naye.

32 Na fungu la Maandiko alilokuwa akilisoma ni hili, Aliongozwa kwenda machinjoni kama kondoo, Na kama vile mwana-kondoo alivyo kimya mbele yake amkataye manyoya, Vivyo hivyo yeye naye hafunui kinywa chake.

33 Katika kujidhili kwake hukumu yake iliondolewa. Ni nani atakayeeleza kizazi chake? Kwa maana uzima wake umeondolewa katika nchi.

34 Yule towashi akamjibu Filipo, akasema, Nakuomba, nabii huyu; asema maneno haya kwa habari ya nani; ni habari zake mwenyewe au za mtu mwingine?

35 Filipo akafunua kinywa chake, naye, akianza kwa andiko lilo hilo, akamhubiri habari njema za Yesu.

36 Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe?

37 Filipo akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu.]

38 Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza.

39 Kisha, walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, yule towashi asimwone tena; basi alikwenda zake akifurahi”.

Roho wa Yesu ni yule yule na tabia zake ni zile zile, tukitaka atukaribie, tumsikie, au tumwone basi ni lazima pia tuwe wasomaji wa Neno.

  1. KUHUBIRI/KUSHUHUDIA.

Agizo kuu ambalo Bwana alilotupatia ni kupeleka injili ulimwenguni kote.

Marko 16:15 “Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.

16 Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa”.

Kwanini kuhubiri/kumshuhudia Yesu kunamsogeza Roho Mtakatifu karibu nasi?. Kwasababu kila tunapofika mahali na kushuhudia tunafanyika vyombo vya Roho Mtakatifu, Hivyo Roho Mtakatifu hana budi kila wakati kuwa nasi kwasababu wakati wote tunatumika kama vyombo vyake, hakuna wakati uwepo wake utakaa mbali na sisi!..

Mathayo 10:18 “nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa.

19 Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema.

20 KWA KUWA SI NINYI MSEMAO, BALI NI ROHO WA BABA YENU ASEMAYE NDANI YENU”.

Kwahiyo kama wakati wote tutakuwa katika hayo mazingira ya kumshuhudia Kristo, maana yake wakati wote, kinywa kitakachokuwa kinasema ndani yetu ni kinywa cha Roho Mtakatifu, hivyo uwepo wake utakuwa nasi muda wote!, lakini kama hatutakuwa katika mazingira yoyote ya kumshuhudia Kristo ni ngumu Roho Mtakatifu kuwa na sisi, kuzungumza kupitia vinywa vyetu, au kusema nasi!.

Je! Na wewe leo Umempokea Yesu?

Na kama ndio je! Wewe ni MWOMBAJI?..wewe ni MSOMAJI WA NENO?…wewe ni MSHUHUDIAJI?. Kama hufanyi hayo basi, uwepo wa Roho Mtakatifu utawezaje kuusikia?, vile vile sauti yake utaweza kuisikia?!.

Leo shetani kawafanya wakristo wengi wasiwe Waombaji?..utakuta mkristo mara ya mwisho kutenga angalau lisaa limoja kuomba yeye binafsi hata hakumbuki!, (yeye atakuwa anapenda kusikiliza na kusoma mahubiri tu!, na kuombewa lakini kuomba mwenyewe hataki/hawezi), Utakuta mkristo mara ya mwisho kusoma Neno binafsi ni muda mrefu sana, leo hata ukimuuliza mkristo biblia ina vitabu vingapi hajui, ukimpa biblia afungue kitabu cha Yeremia atapepesuka nusu saa hajui kilipo mpaka akaangalie kwenye index, hiyo ni kuonesha ni jinsi gani biblia ni kitabu-baki tu kwake!, na si kila kitu kwake!.

Leo hii ukimwuliza mkristo mara ya mwisho kuzungumza na mtu mwingine Habari za wokovu, au kumshuhudia Kristo, hana hiyo kumbukumbu!, lakini shuhuda za mipira, na za Maisha ya watu wengine zimejaa katika kinywa chake!..

Kumbuka Bwana anatamani yeye kuwa karibu na sisi kuliko sisi tunavyotamani yeye awe karibu nasi, hivyo ni wajibu wetu kuongeza bidii katika kuomba, kusoma Neno, kushuhudia Pamoja na kuishi Maisha matakatifu.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

KUSUDI LA MIMI KUWEPO DUNIANI NI LIPI?

Shekina ni nini? Na Je! Utukufu wa shekina unamaana gani?

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

MLANGO MWINGINE WA ADUI KUTULETEA MAJARIBU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
6 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Jackson
Jackson
11 months ago

May God bless the teacher who taught us the secrets of God and may he be blessed with these teaching

NEEMA ALICE
NEEMA ALICE
1 year ago

Nimebarikiwa sana na neno hili MUNGU awabariki sana Kwa kazi nzuri mnaoifanya ningependa kujua namna ya kuomba pia

Selina Masegese
Selina Masegese
1 year ago

Naomba kujua namna ya kuomba

Mary
Mary
2 years ago

Asante nimependa mafundisho yenu Mungu awa bariki sana