MAFUNUO YA ROHO.

MAFUNUO YA ROHO.

Neno Ufunuo maana yake “NI KITU KILICHOFUNULIWA”..Ikiwa na maana kuwa, hapo kwanza kilikuwa kimefungwa na sasa kimefunuliwa. Hapo kwanza kilikuwa hakionekani sasa kinaonekana, hapo kwanza kilikuwa hakieleweki sasa kinaeleweka.

Zipo funuo za aina nyingi. Mwana sayansi alipochunguza vitu vya asili ndipo akapata ufunuo wa kutengeneza ndege, alipochunguza kwanini Tai anapaa ndipo alipogundua kitu kinachoitwa ndege, Baada ya uchunguzi wa tabia za mawimbi ya sauti na mwangwi akapata ufunuo wa kutengeneza kifaa kinachoitwa simu..ambapo hapo kwanza mambo hayo yalikuwa hayajulikani. Hivyo hivyo mpaka Akapata ufunuo wa kutengeneza magari na mambo mengine mengi.

Hivyo Roho ya mwanadamu Mungu aliyoiweka ndani yake ndiyo inayovumbua mambo ambayo kwa akili za kawaida yanaonekana kama hayawezekani. Lakini roho ya mwanadamu haiwezi kuvumbua chochote endapo mtu hatakaa katika hali ya utulivu na katika hali ya uchunguzi wa hali ya juu. Ndio maana wanasayansi na wagunduzi wengi, wanapoteza masaa mengi ya utafiti kwa kutulia na kutafakari na kujifunza pasipo kujichanganya na mambo mengi..lengo lao sio wajiumize hapana! Lengo ni ili waweze kuipa akili nafasi ya kutafakari mambo kwa undani kwa utulivu na utaratibu pasipo kuingiliwa na mambo mengine. Na hivyo wanapata matokeo makubwa wanapata Ufunuo/ uvumbuzi wa jambo Fulani..Yale mafumbo magumu waliyokuwa hawawezi kuyapatia ufumbuzi Roho zao zinawapatia ufumbuzi.

Kadhalika na Roho Mtakatifu naye..yeye ndiye ayachunguzaye mafumbo ya Mungu, na kuyapatia ufumbuzi..Na ndio maana ukisoma kitabu cha Ayubu 28, Utaona Bwana akiitafuta tafuta hekima kwa kuichunguza, hata kuipata na kumwambia mwanadamu..Hivyo utaona Roho ya Mungu, inapeleleza na kutafuta tafuta duniani kote mambo yamuhusuyo Mungu na Mwanadamu.

Zekaria 4: 7 “..naam, hizi saba ndizo macho ya Bwana; yapiga mbio huko na huko duniani mwote”.

Kwahiyo ili mtu awe na ufahamu juu ya mambo ya Mungu, ni lazima awe na Roho Mtakatifu kwasababu yeye pekee ndiye ayajuaye na kuyachunguza na kuyavumbua mambo ya Mungu..Kama vile  mwanadamu yeyote ili avumbue jambo Fulani ni lazima awe mwanadamu vivyo hivyo na kwa Mungu, ili kuyafahamu mambo yake ni lazima tuwe na Roho yake ndani yetu.

1Wakorintho 2: 10 “LAKINI MUNGU AMETUFUNULIA SISI KWA ROHO. MAANA ROHO HUCHUNGUZA YOTE, HATA MAFUMBO YA MUNGU.

11 Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu.

12 Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu”

SASA NI KWA NAMNA GANI TUNAWEZA KUPOKEA MAFUNUO KUTOKA KWA ROHO MTAKATIFU ALIYE NDANI YETU?

Ni kwa njia moja tu tunayoweza kupokea Mafunuo ya Roho Mtakatifu..Na hiyo si nyingine zaidi ya kama ile ile wana-sayansi wanayoitumia…Wao wanajifungia ndani na kutafakari, na kusoma vitabu vingi, na kujizuia na mambo mengi…ILI Roho zao ziinuke zipate umakini wa hali ya juu ili kupata ufunuo.

Kadhalika na Ufunuo wa Roho, hauji tu kwa kuusubiria, hapana, bali unakuja KWA KUJIZUIA NA MAMBO MENGI YA ULIMWENGU HUU, NA KUFUNGA, na KUSOMA VITABU VINGI, VYA HISTORIA NA VYA WAHUBIRI MBALI MBALI AMBAO BWANA KAWATIA MAFUTA KWELI, na KWA KUCHUNGUZA VITU VYA ASILI KWA UNDANI sana. Kwa kujiweka katika hayo mazingira unampa ROHO MTAKATIFU NAFASI KUBWA SANA YA YEYE KUKUFUNULIA JAMBO AMBALO HAPO KWANZA ULIKUWA HULIJUI. Kwa kukufunulia Siri iliyopo ndani ya Yesu Kristo kwa undani.

Tunaweza tukaona mifano kadha wa kadha kwenye Biblia..Danieli baada ya kuchunguza chunguza kwa wahubiri waliomtangulia kabla yake mambo waliyokuwa wanayahubiri…alikutana na nyaraka za nabii Yeremia ambazo zilikuwa zimeandikwa miaka kamili ya wana wa Israeli kukaa utumwani..Na baada ya kupata ufunuo huo, akaendelea kumwomba Mungu aelewe vizuri maana ya hayo mambo..Na ndipo akaamua kufunga na Bwana akamfunulia zaidi ya pale, Malaika Gabrieli alikuja na akamfunulia MAJUMA SABINI YATAKAYOANZA BAADA YA WAO KUTOKA UTUMWANI.

Danieli 9: 1 “Katika mwaka wa kwanza wa Dario, mwana wa Ahasuero, wa uzao wa Wamedi, aliyetawazwa kuwa mfalme juu ya milki ya Wakaldayo;

2 katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danielii, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la Bwana lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini.

3 Nikamwelekezea Bwana Mungu uso wangu, ili kutaka kwa maombi, na dua, pamoja na kufunga, na kuvaa nguo za magunia na majivu”.

Mfano mwingine tonamwona Yule Mkushi aliyekuwa ametoka Yerusalemu kuhiji enzi za Mitume wa Kristo aliyekuwa anatafuta kuchunguza kwa bidii maandiko, Na katika kusoma kwake alikutana na maandiko magumu sana hakuyaelewa yaliyoandikwa na nabii Isaya…lakini kwasababu alikuwa na kiu ya kutaka kujua Bwana alimtimizia haja ya moyo wake na kumtumia ufunuo kupitia Mtumishi wake Filipo..Jambo hilo tunaweza kulisoma katika kitabu cha…

Matendo 8: 26 “Malaika wa Bwana akasema na Filipo, akamwambia, Ondoka ukaende upande wa kusini hata njia ile itelemkayo kutoka Yerusalemu kwenda Gaza; nayo ni jangwa.

27 Naye akaondoka, akaenda; mara akamwona mtu wa Kushi, towashi, mwenye mamlaka chini ya Kandake malkia wa Kushi, aliyewekwa juu ya hazina yake yote; naye alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu,

28 akawa akirejea, ameketi garini mwake akisoma chuo cha nabii Isaya.

29 Roho akamwambia Filipo, Sogea karibu na gari hili, ukashikamane nalo.

30 Basi Filipo akaenda mbio, akamsikia anasoma chuo cha nabii Isaya; akanena, Je! Yamekuelea haya unayosoma?

31 Akasema, Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza? Akamsihi Filipo apande na kuketi pamoja naye.

32 Na fungu la Maandiko alilokuwa akilisoma ni hili, Aliongozwa kwenda machinjoni kama kondoo, Na kama vile mwana-kondoo alivyo kimya mbele yake amkataye manyoya, Vivyo hivyo yeye naye hafunui kinywa chake.

33 Katika kujidhili kwake hukumu yake iliondolewa. Ni nani atakayeeleza kizazi chake? Kwa maana uzima wake umeondolewa katika nchi.

34 Yule towashi akamjibu Filipo, akasema, Nakuomba, nabii huyu; asema maneno haya kwa habari ya nani; ni habari zake mwenyewe au za mtu mwingine?

35 Filipo akafunua kinywa chake, naye, akianza kwa andiko lilo hilo, akamhubiri habari njema za Yesu.

36 Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe?

37 Filipo akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu.]

38 Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza.

39 Kisha, walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, yule towashi asimwone tena; basi alikwenda zake akifurahi.

40 Lakini Filipo akaonekana katika Azoto, na alipokuwa akipita akahubiri Injili katika miji yote, hata akafika Kaisaria”.

Unaona! Ukichunguza wote hawa, Roho Mtakatifu aliwafunulia kwasababu walikuwa na kiu, na walikuwa wanajitahidi kusoma maandiko na kuchunguza. Roho Mtakatifu hawezi kukufunulia jambo lolote kama hutaki kujizuia na mambo Fulani, na kuchukua gharama Fulani, Kama hutaki kutaka kujua mambo yanayokuja ya kwenda mbinguni basi hutajua chochote mpaka kanisa litakaponyakuliwa na hivyo kubaki katika dhiki kuu ya Mpinga-Kristo, na kutupwa katika lile ziwa la moto baadaye. Utaendelea kufikiri tu bado mamilioni ya Miaka mpaka Kristo arudi.

Mfalme Nebukadneza wa Babeli ambaye hakuwa hata mkristo, wakati Fulani usiku alipokuwa amejiegeza kitandani mwake akitafakari ni mambo gani yatakayotokea siku za Mwisho…pasipo kujua chochote usingizi ukampitia akiwa bado katika hayo mawazo na alipokuwa katika usingizi ule akaota ndoto sanamu kubwa ipo mbele yake ina kichwa cha dhahabu, na kifua cha shaba na mikono ya fedha na miguu ya chuma..Aliposhtuka aliisahau ile ndoto, lakini alijua kabisa ni ndoto yenye mahusiano na siku za mwisho, kwasababu ndio mawazo aliyokuwa anayawaza kabla hajalala..(Danieli 2:27-29)..na kwa kupitia Nabii Danieli Roho aliweza kumfunulia Nebukadneza mambo yatakayokuja kutokea siku za Mwisho.

Unaona hapo? Roho anawafunulia hata watu wasiokuwa wake, mambo yatakayokuja kutokea siku za mwisho, Na wewe je! Alishawahi kukufunulia kwamba tunaishi katika nyakati gani?, na ni mambo gani yatakayokuja kutokea siku za mwisho? Ulishawahi kukaa chini na kutafakari mambo yatakayokuja kutokea nyakati za Mwisho? Ulishawahi kukaa chini ukatafakari yale maneno Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi wake katika Mathayo 24??…aliposema mmoja atatwaliwa mmoja ataachwa ulishawahi kuketi chini na kutafakari mambo hayo?.

Muhubiri mmoja, Mjumbe wa Mungu anayeitwa WILLIAM BRANHAM, siku moja asubuhi wakati ametoka kulala tu! Akiwa amejiegemeza kichwa chake juu ya mto, akitafakari itakuwaje siku ile atakayoenda kumwona Bwana mawinguni, akiwa anatafakari akidhani kuwa mwendo ndio amekaribia kuumaliza, ghafla alisikia sauti ndogo ikimwambia “akaze mwendo ndio kwanza safari inaanza” wakati anaitafakari hiyo sauti alijikuta ametokea mahali palipo pazuri sana pa utulivu, penye nyasi nzuri ambazo anasema hajawahi kuziona hapo kabla, akawaona wadada na wakaka wengi wa makamu ya miaka kama 20-30 hapo, wamevaa vizuri sana, wanamjia wakiwa na nyuso za furaha, wote wakawa wanamkumbatia kila mmoja akimwambia “oo ndugu yetu wa thamani…oo ndugu yetu wa thamani” wote walionyesha nyuso za furaha na raha isiyokuwa ya kawaida..William akasikia ile sauti ikimwambia “hawa wote unaowaona ni wale watu uliowaleta kwa Kristo kupitia injili yako, waliotangulia kulala, sasa wako hapa wanakushukuru” Akashangaa sana kuona jinsi walivyo wengi..

Wakamwuliza akisema..lakini mbona wengine niliwaleta kwa Kristo wakiwa wazee, inakuwaje hapa nawaona wote ni vijana, akaambiwa huku hakuna wazee wote ni vijana..Akasikia ile sauti ikimwambia “siku ile ya mwisho” akaze mwendo ndio kwanza tu anaanza safari. Lile ono likampotea na alivyorudi katika hali yake ya kawaida, hiyo ilimtia nguvu kukaza mwendo zaidi ili siku ile afike sehemu ile ya Raha.

Unaona! Huyu ndugu BRANHAM ni moja ya watu, waliokuwa wakitafakari tu vitandani mwao, kama Mfalme Nebukadneza alivyofanya na ROHO MTAKATIFU akawafunulia baadhi ya mambo yajayo.

Ni maombi yangu kuwa BWANA ATAKUKIRIMIA NA WEWE KUYAFAHAMU MAFUMBO YAKE. Ni maombi yangu kuwa Bwana atakupa ukurasa mpya kuanzia leo, kutaka Kupata ufunuo kutoka kwake, Ni maombi yangu kuanzia leo Bwana atakujalia kutafuta kujifunza kwa bidii kama Danieli, mpaka Kupata kufunuliwa mambo yajayo. Ni maombi yangu kuwa Bwana atakupa kutafakari na kudadisi mambo yajayo mpaka atakapokupa ufunuo kama aliompa Nebukadneza, au aliompa mhubiri William Branham, Ni maombi yangu kuwa Bwana atakupa kuyadadisi maandiko sana, mpaka Roho atakapomtuma Mtumishi wake atakayekuelewesha vema mafumbo yake..kama alivyofanya kwa Yule Mkushi alipotumiwa Filipo.

Bwana Yesu akubariki.

Usiache “kus-share” ujumbe huu kwa wengine.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

TUSIPOUTHAMINI WOKOVU TUTAPATAJE KUPONA?

DHAMBI ILIYOMKOSESHA SHETANI:

JINSI MWISHO ULIVYOKARIBIA.

MANA ILIYOSHUSHWA KUTOKA MBINGUNI


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments