JE! JICHO LAKO LINAONA NINI KATIKATI YA MAJARIBU?

JE! JICHO LAKO LINAONA NINI KATIKATI YA MAJARIBU?

Shalom.

Karibu tujifunze maneno ya uzima,

Biblia inatuambia, Bwana wetu Yesu alijaribiwa sawa sawa na sisi, katika mambo yote, lakini hakutenda dhambi wala kutetereka katika imani, Sio kwamba alikuwa mgumu sana kuliko sisi, hapana, yeye mwenyewe alisema..

Yohana 16:33 “Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu”.

Bwana anajua kabisa siku unapokuwa mkristo, si wakati wote mambo yatakuwa mteremko kama wengi wanavyodhani, utakutana na majira mengi tofauti tofauti, ya kucheka, mengine ya kulia, ya kuwa mpweke, mengine ya kuchangamka, ya kupata, ya kupoteza, ya kupungukiwa, ya kujaliwa, ya kuugua, ya kuwa na afya n.k. yote hayo ni majira, lakini sote tunajua hali inakuwa mbaya zaidi pale tunapopitia katika hali za majaribu. Au kujaribiwa. Hivyo ni vizuri kujua kuwa tunapopitia majira kama hayo tunapaswa tufanye nini.

Embu leo tuangalie, ni nini kilikuwa kinaendelea katika mazingira ya kujaribiwa kwa Bwana Yesu alipokuwa hapa duniani.

Marko 1:12 “Mara Roho akamtoa aende nyikani.

13 Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na Shetani; naye alikuwa pamoja na wanyama wa mwitu, na malaika walikuwa wakimhudumia”.

Kama tunavyosoma hapo, katika kujaribiwa na shetani, vipo vitu viwili viliambatana naye. Cha kwanza ni wanyama wa mwituni. Akiwa jangwani alikutana na wanyama ambao hajazoea kukutana nao  katika maisha ya kawaida, sehemu moja aliposogea alikutana na mbweha, mbele  kidogo pengine alikutana na simba wenye njaa, siku tatu tena mbeleni tena alikutana na dubu, kila siku usiku anawaona  chui wanakatiza, kwasababu yupo nyikani, wanyama wa nyikani kukutana nao, litakuwa ni jambo la kawaida.

Inafunua nini, wakati wa majaribu usishangae kukutana na mbwa mwitu wakali mbele yako, ambao pengine hapo nyuma hukuwahi kuwaona.., unapitia ugonjwa fulani mbaya, pengine unatarajia kuona faraja katika huo, kinyume chake ndio unaona watu wakikukimbia, wengine wanakusema vibaya, Umekuwa mkristo, ukitazamia familia yako ndio ikufurahie, kinyume chake ndio inakutenga na kukurushia maneno, wengine hawakudhara., Unakataa rushwa kazini, maboss wako ndio wana kuundia visa ufukuzwe kazi n.k.. Mambo kama hayo utakutana nayo kwa namna moja au nyingine.

Lakini pia tunaona Bwana Yesu katikati ya majaribu yale, lilikuwepo kundi lingine lisiloonekana ambalo lilikiwa likimuhudumia, na hao sio wengine zaidi ya malaika watakatifu.. Hapo ndipo kiini chetu cha somo kilipo..Ni faraja iliyoje. Wakati ambapo macho yake yanaona maadui waliomzunguka, lakini roho yake ilikuwa inawaona malaika wa Mungu wamemzunguka wakimuhudumia..kuhakikisha hadhuriki na maadui wake, kuhakikisha hafu, kuhakikisha analivuka lile jaribu haijalishi kuwa yupo katika wakati mgumu kiasi gani, kuhakikisha anapata faraja ya kweli kutoka kwa Mungu.

Hapa ndipo wengi wetu tunaposhindwa kupaona, na matokeo yake majaribu yanatuzidi nguvu mpaka kuiacha imani, au kurudi nyuma. Hilo ndio lililokuwa linataka kumtokea Yule mtumishi wa Elisha, siku ile walipozungukwa na majeshi ya maadui zao, jambo ambalo lilimpelekea  aogope sana na kupaniki, na kulia.. Alipoanza kufikiria jinsi atakavyokwenda kukatwa vipande pande, au jinsi atakavyoondolewa kichwa chake, hilo lilimfanya atamani hata ardhi ipasuke saa ile ile , azame.

Lakini jicho la Elisha lilikuwa linaona mbali zaidi, lilikuwa linaona upande wa pili yupo nani, lilikuwa linaona jeshi la mbinguni lililokuwa pamoja naye, pindi anapopitia majira ya majaribu kama hayo, Ndipo baadaye akamwomba Mungu, amfungue macho yule kijana, akafunguliwa na kuona idadi isiyohesabika ya malaika wa Mungu wakiwa karibu yao wamewazunguka, kwa lengo la kuwahudumia.

2Wafalme 6:15 “Hata asubuhi na mapema mtumishi wake yule mtu wa Mungu alipoondoka, na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi la watu, na farasi na magari, wameuzingira mji ule. Mtumishi wake akamwambia, Ole wetu! Bwana wangu, tufanyeje?

16 Akamjibu, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.

17 Elisha akaomba, akasema, Ee Bwana, nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona. Bwana akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote”.

Hizo ndio siri zilizowafanya manabii wote wa kale, kuyashinda majaribu mazito, kwasababu waliacha kuwaangalia maadui zao, wakaliangalia jeshi la Mungu mwenyezi lililo pamoja nao. Vile vile utaona wakati ule walipomkamata Danieli na kwenda kumtupa katika lile tundu la Simba, Danieli hakupeleka mawazo yake  sana kwa wale simba, bali alimuawaza Mungu wa majeshi, akijua kuwa jeshi alilonalo la malaika watakatifu la kumuhudumia yeye ni kubwa sana. Na ndipo alipotupwa tu mule tunduni, wale simba hawakumdhuru, Na baadaye  mfalme alipomuuliza ni nini?, Danieli akamwambia maneno haya

Danieli 6:22 “Mungu wangu AMEMTUMA MALAIKA WAKE, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno”.

Hivyo na wewe pia fahamu kuwa, katikati ya majaribu, wapo malaika wa Mungu kukuhudumia usipatwe na dhara lolote, katikati ya shida zako, mateso yako na magonjwa upo muujiza wa Mungu mkononi mwa malaika zake. Hivyo usiwe na hofu, wala wasiwasi wala uoga.

Subiri tu, utaona mambo ya ajabu. Ni vile tu, Mungu huwa si kila jambo atatufumbua macho yetu  tuone, lakini kama angetaka iwe hivyo uone kila kitu, usingekaa uogope jaribu lolote lililo mbele yako. Hivyo tulia,utahudumiwa kwa namna ya kimbinguni, ondoa tu woga,mtazame Mungu. Acha kufikiria juu ya mateso na dhiki, mfikirie Mungu hilo tu. Utaona kazi za malaika wa Mungu wazi wazi mbele ya macho yako.

Shalom

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

MAJARIBU MATATU YA YESU KRISTO

KUMTUMIKIA MUNGU, KUNAWEZA KUWE KINYUME NA MATARIJIO YAKO.

NAWE UTAGEUZWA KUWA MTU MWINGINE.

KUNA MAJIRA MUNGU ATAIVURUGA MIPANGO YETU.

Ngome ni nini?  Kwanini Mungu anafananishwa na ngome?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
lucas mhula
lucas mhula
2 years ago

Amen 🙏🙏