INJILI YA MANENO LAINI ITAKUGHARIMU.

INJILI YA MANENO LAINI ITAKUGHARIMU.

Ukiona unahubiriwa juu ya hukumu ya Mungu, au juu ya habari ya siku za mwisho halafu unachukia au unakwazika, lakini wakati huo huo ukiambiwa habari za mafanikio na mema ndio unafurahia, basi fahamu kuwa upo karibu sana kupotea.

Kwasababu kitengo hicho ndicho kitengo-mama cha shetani kuwadanganyia watu, Embu fikiria pale Edeni Mungu hakuwaficha chochote bali aliwaeleza Adamu na hawa madhara ya dhambi, akawaambia mkila matunda la ujuzi wa mema na mabaya hakika MTAKUFA..

Lakini shetani akaibuka na mahubiri yake laini, kinyume na yale Mungu aliyowaangiza, na kuwaambia hakika HAMTAKUFA,…Unaona? Hawa aliposikia habari za mema zimekuja, habari za mafanikio, habari za uzima wakati wote, habari za kuwa juu tu, haijalishi kuwa utamkasirisha Mungu kiasi gani, haijalishi kuwa utazini kiasi gani, atatoa mimba nyingi namna gani,  maadamu ni ya kutakiwa mema, basi akayachukua tu na kuyadharau yale ya Mungu, akayashilia yale ya shetani akayaamini kwelikweli kuwa hatakufa, bali ataishi naye atayasimulia matendo ya Bwana.

Ndugu yangu hizi ni siku za mwisho, ambazo biblia ilizitabiri kuwa kutatokea wimbi kubwa la manabii wa uongo, ambao kimsingi kazi yao kubwa itakuwa ni hiyo..kuwahubiria watu maneno laini, haijalishi watakuwa hawajaokoka, au la, hilo haliwahusu, kazi yao ni kuwatabiria mafanikio tu na uzima, na mema, lakini madhara ya dhambi hawataambiwa.. Kama alivyofanya shetani kwa Hawa pale Edeni.

Isaya 30:9 “Kwa maana watu hawa ni watu waasi, watoto wasemao uongo, watoto wasiotaka kuisikia sheria ya Bwana;

10 wawaambiao waonaji, Msione; na manabii, Msitoe unabii wa mambo ya haki, TUAMBIENI MANENO LAINI, HUBIRINI MANENO YADANGANYAYO;

Kwa  hawa manabii, na waalimu wa uongo kamwe hutasikia Neno ‘ukizini hakika utakufa’, na kwenda jehanamu, huwezi kusikia maneno kama hayo, kwasababu shetani anataka wewe uendelee kubakia hivyo hivyo katika ujinga, ili ufe ghafla ujikute kuzimu uanze kujuta kwanini sikufahamu haya yote.

Angalia shida tunazozipitia duniani leo hii, ni kwasababu ya wazazi wetu kusikiliza injili laini za shetani,  Inasikitisha kuona pale mtu unapoambiwa kuhusu dhambi zako, unaona kama vile unahukumiwa. Mama yetu  Hawa aliona kama Mungu anamtamkia mabaya, akafanya makosa yale..Na sisi vivyo hivyo tukipuuzia injili ya kuambiwa ukweli, injili za kukemewa dhambi, injili za ziwa la moto. Tujue kuwa tunajiandaa kwa majuto ya milele.

Mara nyingi wana wa Israeli waliingia katika makosa kama haya mpaka wakapelekwa utumwani Babeli kwasababu ya kuwasikiliza manabii wa uongo waliokuwa wanawatabiria amani tu muda wote, bila kushughulika na dhambi zao, ambazo ndio kiini cha matatizo yao.

Soma vifungu hivi;

Ezekieli 13:16 “yaani, manabii wa Israeli, watabirio habari za Yerusalemu, na kuona maono ya amani katika habari zake; wala hapana amani, asema Bwana MUNGU”.

Yeremia 6:14 “Wameiponya jeraha ya watu wangu kwa juu juu tu, wakisema, Amani, Amani, wala hapana amani”.

Unaona yaliyokuwa yanaendelea kale ndiyo yanayoendelea sasa.

Leo swali linakuja kwako, Je unaufungaje mwaka wako?, mwaka huu wa 2020 ndio unapita, unakuja mwingine mpya wa 2021, kumbuka kwa jinsi miaka inavyosogea ndivyo tunavyoyakaribia mambo mawili makuu mbele yetu, la kwanza Ni Unyakuo. Na la pili ni Kifo chako. Maelfu ya watu kila sekunde wanakufa duniani, vilevile na wewe hujui siku yako itakuwa ni lini, pengine ni kesho, au mwanzoni mwa mwaka ujao, Jiulize ukifa leo ghafla huko utakapokwenda utakuwa ni upande gani?

Vilevile jiulize ikiwa unyakuo utapita leo usiku halafu ukaachwa, utakuwa kwenye hali ya namna gani..Kumbuka ni siku kama hizi  ndizo Bwana atakazorudi, watu watakuwa wakila na kunywa, wakipanda na kujenga, wakisherehekea, ndipo huo mwisho utakapokuja..Jiulize utakuwa wapi wakati huo ukikujia kwa ghafla.

Ukijifunza kuyatafakari hayo, hutaishi maisha ya ilimradi tu hapa duniani, bali utajiangalia sana mwenendo wako, ili siku ile isije ikakunasa kama mtego.

Hivyo, tubu dhambi zako mgeukie Muumba wako, usikubali uanze mwaka mpya na viporo vya dhambi vya mwaka huu, mgeukie Yesu Kristo leo hii, akusafishe dhambi zako.

Ikiwa upo tayari kutubu sasa, basi uamuzi huo utakuwa ni wa busara sana kwako. Mahali popote ulipo, tafuta sehemu ya utulivu, piga magoti, kisha kwa kumaanisha kabisa kutoka katika moyo wako sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU  MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE, NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Basi kwa sala hiyo fupi, Mungu ameshakusamehe, kilichobakia kwako ni kubatizwa, ikiwa hukubatizwa, na kudumu katika neema na utakatifu siku zote za maisha yako.

Ikiwa utahitaji msaada zaidi ya kiroho, basi tutafute kwa namba hizi +255693036618

Mungu akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

UNYAKUO.

JE! JICHO LAKO LINAONA NINI KATIKATI YA MAJARIBU?

KUMTUMIKIA MUNGU, KUNAWEZA KUWE KINYUME NA MATARIJIO YAKO.

BIBLIA INAITAJA NJIA KUU YA MFALME, NJIA HII NI IPI?

NJIA YA KUPATA WOKOVU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments