NJIA YA KUPATA WOKOVU.

NJIA YA KUPATA WOKOVU.

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, Ni neema tumeiona tena siku ya leo, hivyo nakukaribisha katika kuyatafakari Maneno ya uzima wa roho zetu.

Leo tutajifunza jinsi wokovu unavyopatikana.. Tunapozungumzia wokovu maana yake ni tunazungumzia Uponyaji wa Roho zetu. Upo uponyaji wa mwili na uponyaji wa roho. Sasa njia ya uponyaji wa mwili ni tofauti na ile ya roho.

Sasa kama utakumbuka katika hatua za mwanzo kabisa za wana wa Israeli kutolewa Misri, utaona Farao alikuwa akipigwa kwa mapigo kadha wa kadha…Utaona alikuwa analetewa makundi ya nzige, mara nzi, mara Vyura na chawa n.k.  Na kila walipomlilia Bwana awaondolee hayo mapigo Mungu alikuwa anayaondoa katikati yao..

Kutoka 8: 8 “Ndipo Farao akawaita Musa na Haruni na kuwaambia, Mwombeni Bwana, ili awaondoe vyura hawa kwangu mimi na kwa watu wangu; nami nitawapa watu ruhusa waende zao, ili wamtolee Bwana dhabihu.

 9 Musa akamwambia Farao, Haya, ujitukuze juu yangu katika jambo hili; sema ni lini unapotaka nikuombee wewe, na watumishi wako, na watu wako, ili hao vyura waangamizwe watoke kwako wewe na nyumba zako, wakae ndani ya mto tu.

10 Akamwambia, Kesho, Akasema, Na yawe kama neno lako; ili upate kujua ya kwamba hapana mwingine mfano wa Bwana, Mungu wetu.

11 Hao vyura wataondoka kutoka kwako wewe na nyumba zako, na watumishi wako, na watu wako; watasalia mtoni tu.

 12 Basi Musa na Haruni wakatoka kwa Farao; Musa akamlilia Bwana katika jambo la hao vyura aliokuwa amewaleta juu ya Farao.

13 Bwana akafanya sawasawa na neno la Musa; na hao vyura wakafa kutoka katika zile nyumba, na katika viwanja, na katika mashamba”

Na Mainzi ni hivyo hivyo na mapigo mengine yote… Wamisri walipomwomba Mungu awaondolee, Mungu aliwasikia na kuliondoa lile tatizo…soma Kutoka 8:29-30.

Lakini tunakuja kuona mbele kidogo tu, wakati wana wa Israeli tayari wameshavuka bahari ya Shamu, walipomuudhi Mungu, na Mungu alipowaletea zile nyoka za moto…Walimlilia Mungu aziondoe lakini hakuziondoa…badala yake aliwatafutia dawa ili kila aliyeumwa, wanapoitazama ile nyoka ya shaba wapate kupona.

Hesabu 21: 5 “Watu wakamnung’unikia Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu.

 6 Bwana akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa.

7 Watu wakamwendea Musa, wakasema, Tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung’unikia Mungu, na wewe; utuombee kwa Bwana, atuondolee nyoka hawa. Basi Musa akawaombea watu.

 8 Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo ataishi.

  9 Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi”.

Hapo Bwana hakuwaondoa hao nyoka, kama alivyoondoa wale vyura, au nzige, au chawa wakati wa Farao. Badala yake aliwaacha nyoka waendelee kuwepo (maana yake waendelee kuuma watu)..Na mtu mwenyewe achague aidha UZIMA au MAUTI. Kama atachagua uzima basi atajinyenyekeza na kwenda kuitazama ile nyoka wa shaba, lakini kama hatataka na kuamua kutafuta njia zake yeye mwenyewe anazozijua za kujitibu, basi atakufa.

Sasa Jambo hilo ufunuo wake ni upi?

Bwana Yesu mwenyewe alitufumbua macho na kutupa ufunuo wa tukio hilo katika kitabu cha Yohana. Anasema;

Yohana 3:14  “Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa;

15  ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye”

Umeona?.. Yule nyoka wa shaba ni mfano wa Yesu Kristo pale msalabani, na wale nyoka ni dhambi iletayo mauti. Hivyo kila mtu anayetumikishwa na dhambi ambayo mshahara wake ni mauti, Akitaka tiba ya hiyo dhambi ni kumtazama Kristo tu.

Kristo kazi yake hakuja kuiondoa dhambi katikati ya jamii yetu, hapana, dhambi ipo ndio maana unaona mpaka leo watu wanaitenda. Alichokuja kukileta ni dawa ya hiyo dhambi. Na sio lazima mtu kupokea uponyaji, ni uchaguzi wa mtu, kuchagua uzima au kifo. Kwa namna ile ile, jinsi wale nyoka walivyoendelea kuachwa katikati ya wana wa Israeli, hawakuondolewa..ili kila mtu ajue kifo kipo na hivyo achague uzima au kifo.

Ndugu usomaye ujumbe huu. Kama hujayakabidhi maisha yako kwa Yesu,  biblia inasema..

Kumbukumbu 30:15 “Angalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya”

Wokovu sio wa kuchaguliwa na mtu, au kuletewa na mtu, ni jukumu la wewe binafsi kuchagua.. Mungu hawezi kulazimisha wokovu uingie ndani yako kama wewe hutaki. Hivyo ni jukumu lako aidha kuchagua kuishi katika dhambi siku zote ambapo mshahara wake ni mauti ya mwilini na rohoni, au umtazame Kristo pale msalabani upate uzima wa milele. Uchaguzi ni wako.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

KWANINI YESU KRISTO NI WA MUHIMU KWETU SASA?

WAPE WATU WANGU RUHUSA ILI WAPATE KUNITUMIKIA.

UMUHIMU WA KUZALIWA MARA YA PILI.

Bwana Yesu alikuwa anamaanisha nini kusema Marko 2:19″walioalikwa harusini wawezaje kufunga maadamu bwana-arusi yupo pamoja nao?”

JE UPENDO WAKO UMEPOA?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Ezra ndambuki
Ezra ndambuki
10 months ago

Hapo ni kweli wokovu sio rahisi ni Jambo la kuamua
MUNGU awatie nguvu zaidi kwa kuenenza injili be yake Amina