WAPE WATU WANGU RUHUSA ILI WAPATE KUNITUMIKIA.

WAPE WATU WANGU RUHUSA ILI WAPATE KUNITUMIKIA.

Safari ya wana wa Israeli kutoka Misri, kuelekea Kaanani, ni ufunuo kamili wa safari yetu ya Kristo kutuokoa katika dhambi na kutuingiza katika Neema ya wokovu. Musa anafananishwa na Kristo.. Kama vile Musa alivyowaongoza wana wa Israeli kutoka Misri, kwa ishara na miujiza Mingi aliyokirimiwa na Mungu, ndivyo Kristo alivyodhihirishwa kwetu kutuokoa kutoka dhambini, kwa ishara na miujiza mikubwa kuliko ile ya Musa. Sasa ni kwa namna gani safari ile ya wana wa Israeli imefananishwa na safari yetu ya wokovu, unaweza kusoma binafsi kitabu cha 1Wakorintho 10:1-12.

Lakini kuna kipengele kimoja ningependa tukiangalie katika Wito huo wa kutolewa Misri kupelekwa Kaanani..na hicho tunakisoma katika mstari ufuatao..

Kutoka 8:1 “Bwana akamwambia Musa, Ingia kwa Farao, ukamwambie, Bwana asema hivi, Wape watu wangu ruhusa, ili WAPATE KUNITUMIKIA”

Tusome tena;

Kutoka 9:13 “Bwana akamwambia Musa, Ondoka asubuhi na mapema, ukasimame mbele ya Farao, umwambie, Bwana, Mungu wa Waebrania, asema, Wape watu wangu ruhusa WAENDE ILI WANITUMIKIE”.

Kupitia mistari hiyo nataka tuona sababu Nyingine ya Mungu kuwatoa wana wa Israeli kwenye utumwa wa Farao ni ipi.

Hapo tunasoma kwamba Bwana aliwatoa ili WAKAMTUMIKIE. Maana yake ni kwamba Wamefunguliwa kwenye utumwa mmoja na kupelekwa kwenye utumwa mwingine. Hawajafunguliwa na kisha kuwekwa huru tu, kutembea tembea huko la!. Bali walifunguliwa kutoka kumtumikia Farao na kupelekwa katika utumwa wa kumtumikia Mungu.

Pia tunasoma maneno hayo hayo katika…

Kutoka 10:3 “Basi Musa na Haruni wakaingia kwa Farao, na kumwambia, Bwana, Mungu wa Waebrania, asema hivi, Je! Utakataa hata lini kujinyenyekeza mbele zangu? Wape watu wangu ruhusa waende zao, ILI WANITUMIKIE”.

Ndugu, ni muhimu kulifahamu hili kwasababu pia lengo la Kristo kututoa dhambini ni hilo hilo la sisi kwenda kumtumikia yeye. Anatufungua ile nira ya Adui ambayo ni ngumu, na kutuvisha nira yake iliyo laini..

Ndio Bwana Yesu alisema katika Mathayo 11:28  kwamba “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29  Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu”

SASA TUNAMTUMIKIA KWA NAMNA GANI?

  1. Namna ya kwanza ya utumishi wa Mungu: Ni kwa kulitii Neno lake na kuzishika Amri zake…(Huu ndio utumishi wa Kwanza kabisa na wa muhimu kuliko wote). Tunapolitii Neno lake tunafanyika kuwa watumwa wake, tunapolitii Neno lake linalosema usizini, usiibe, usiabudu sanamu n.k hapo tunafanyika kuwa watumwa wake na hivyo tunamtumikia yeye. Ndivyo biblia inavyosema..

Warumi 6:16  “Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii, kwamba ni utumishi wa dhambi uletao mauti, au kwamba ni utumishi wa utii uletao haki.

17  Lakini Mungu na ashukuriwe, kwa maana mlikuwa watumwa wa dhambi, lakini mliitii kwa mioyo yenu ile namna ya elimu ambayo mliwekwa chini yake;

18  na mlipokwisha kuwekwa huru mbali na dhambi, mkawa watumwa wa haki”

  1. Na utumishi wa Pili ni Utumishi wa kuwafundisha wengine kuzishika na kuzitii hizo amri.

Unapowahubiria wengine Neno la Mungu, hapo tayari umefanyika kuwa mtumishi wa Mungu..Unakuwa unamtumikia Mungu, na Mungu atakuheshimu..Na kumtumikia Mungu sio tu kuwa mchungaji, au Mhubiri mkubwa, au Nabii au Mtume. Hapana…popote pale ambapo unaweza kufaa katika kulitangaza Neno..Katika nafasi hiyo, tayari unamtumikia Mungu. Hakunaga karama ya Mhubiri Mkubwa, au Nabii Mkuu, au Mchungaji mkuu, au Mwalimu mkuu…kama ni mhubiri ni mhubiri mbele za Kristo wote ni sawa, kama ni mwalimu ni mwalimu mbele za Kristo wote wanaheshimika sawa n.k. Aliye nabii mkuu ni Yesu mwenyewe, aliye Mwalimu Mkuu ni Yesu pekee, aliye Mtume Mkuu ni Yesu pekee..wengine wote haijalishi wingi wa wafuasi walionao…wote mbele ya Kristo wanafanana.

Hivyo kwa hitimisho ni muhimu kufahamu tumetolewa dhambini ili tukamtumikie Mungu na si tukajitumike wenyewe au tukautumikie ulimwengu. Ndio maana wana wa Israeli hatua ya kwanza baada ya kutolewa Misri, walipelekwa nyikani kupewa sheria na amri za Mungu..Na walipoingia kaanani Bwana aliwapa jukumu la kuwafundisha wana wao na vizazi vyao vilivyokuja juu ya sheria, amri na hukumu za Mungu. Na sisi wa sasa tunalo jukumu hilo hilo baada ya kuokoka.

Umeokoka, nenda kamtumikie Mungu..kwa kuwafundisha wengine uliyojifunza.

Mathayo 28:19  “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu;

20  na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari”

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

Kutoka 10:1 “BWANA anasema atampa Farao moyo Mgumu, asimtii, je! hapo Bwana Atamhukumu Farao kama mkosaji siku ile?”

Konde la Soani ni nini? (Zaburi 78:12,43)

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 1

SIFONGO NA SIKI NI NINI?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments