KUMTUMIKIA MUNGU, KUNAWEZA KUWE KINYUME NA MATARIJIO YAKO.

KUMTUMIKIA MUNGU, KUNAWEZA KUWE KINYUME NA MATARIJIO YAKO.

Shalom, karibu tujifunze Neno la Mungu, Biblia inatuambia Neno lake ni kama fedha iliyosafishwa motoni mara saba,(Zab 12:6) ikiwa na maana kuwa Neno lile lile moja linaweza kuwa na mafunuo saba. Hivyo hatuchoki wala hatuachi kujifunza Neno lake kila inapoitwa leo. Na ndio maana biblia ni kitabu pekee kilichobaki duniani ambacho hakijawahi kupitwa na wakati.

Kuna jambo la muhimu sana, naamini tunaweza kujifunza kwa wale watu watatu waliopewa talanta na Bwana wao kwenda kuzizalisha. Tukisoma pale tunaona yule wa kwanza alipewa talanta 5, na kuwa uaminifu akafanikiwa kuzalisha nyingine tano, na yule wa pili alipewa talanta 2 na kwa uaminifu naye pia akaweza kuzalisha talanta nyingine mbili, Lakini yule wa tatu, ambaye hakuzalisha chochote,  kuna maneno aliyazungumza, ambayo yalifichua siri ya Bwana wake, jinsi alivyokuwa na hiyo ndio ikawa sababu kubwa ya yeye kutokwenda kuzalisha chochote.

Embu tusoma habari yake, kwa ufupi, na mbeleni kuna jambo geni ambalo Mungu atatufundisha leo.

Mathayo 25:24 “Akaja na yule aliyepokea talanta moja, akasema, BWANA, NALITAMBUA YA KUWA WEWE U MTU MGUMU, WAVUNA USIPOPANDA, WAKUSANYA USIPOTAWANYA;

25 BASI NIKAOGOPA, NIKAENDA NIKAIFICHA TALANTA YAKO KATIKA ARDHI; TAZAMA, UNAYO ILIYO YAKO.

26 Bwana wake akajibu, akamwambia, Wewe mtumwa mbaya na mlegevu, ulijua ya kuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya;

27 basi, ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake.

28 Basi, mnyang’anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliye nazo talanta kumi.

29 Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa.

30 Na mtumwa yule asiyefaa, mtupeni mbali katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno”.

Sasa turudie tena huo mstari wa 24 anasema, nalitambua ya kuwa wewe ni mtu Mgumu.. Jiulize swali unadhani alikuwa anamsingizia Bwana wake kumwita mtu Mgumu? Hakuwa anamsingizia hata kidogo,alikuwa anazungumza kwa alichokiona kwa Bwana wake, ambaye alikuwa anamtumikia tangu siku nyingi…Tena akazidi kuendelea kumwambia, wewe huwa unavuna usipopanda, na unakusanya usipotawanya..Jiulize unadhani pia hapa alikuwa anamsingizia? Jibu ni la, nataka tusisimamie upande mmoja, embu tuangalie hoja za huyu mtumwa zilikuwa ni nini.

Kwa kauli zake ni kwamba alimwona huyu Bwana wake, ni mtu ambaye si mwepesi kuelewa,  hususani pale wanapokuwa kazini na mambo hayakuenda sawa siku hiyo, hata aelezejwe, ni mgumu sana kuelewa, akiambiwa kulikuwa na shida hii, ndio maana fedha haijapatikana ya kutosha, ni ngumu kuelewa, na ndio maana anasema Ninajua kuwa wewe ni mtu Mgumu.

Vilevile kulingana na maelezo yake, huyu Bwana wake ni mtu ambaye, anatarajia kupata vingi kutoka kwa wafanyakazi wake, licha ya kwamba, hawekezi vya kutosha, ni bwana ambaye hatimizi sana wajibu wake, kama tajiri, bali kazi yote anawaachia wafanyakazi wake,watumike na mwisho wa siku anataka mapato mengi kutoka kwao. Na ndio maaana akawa na ujasiri wa kumwambia Unavuna usipopanda..Yaani unatarajia upate mengi, mahali ambapo hujawekeza kwa vingi.

Sasa Kwa kauli zake hizi mbili, pengine ndio ikampelekea asikitendee kazi kile alichopewa na badala yake akakifukia chini

Lakini wakati yeye anafikiria hivyo, wakati yeye anaona Bwana wake hawajali wafanyakazi, huku nyuma wenzake wanaona hakuna haja ya kumfikiria Bwana wao vibaya, wakaenda kuvifanyia kazi vile walivyopewa. Hata kama kazi ilikuwa ni ngumu isiyo na vitendea kazi vingi lakini wao waliendelea kufanya hivyo hivyo tu.

Lakini huyu mmoja akasema mimi nitamuhifadhia fedha yake akirudi nimpe, nisipate lawama, kwasababu huyu boss wangu ninamjua , naweza kumzalishia kimoja tu, hapa, akaja kunikaripia ni kwanini sikumletea vingi, hivyo wacha nimwekee kilicho chake.akirudi akikute, niepukane na lawama.

Lakini kama tunavyosoma Bwana wake alipokuja na kumkuta hana faida yoyote alimwita mtumwa mbaya na mlegevu.. Kwanini asingeichukua na kuiweka kwa watoa riba, mahali ambapo hapana hatari ya kupata hasara, mpaka akaamua kwenda kuichimbia chini iozee huko.. ?

Mnyang’anyeni kile alichopewa wapewe wale wengine. Na akatupwe katika giza la nje. Ndiko kutakakokuwa na kilio na kusaga meno

Ndugu, mfano huu unatuhusu sisi, yaani mimi na wewe. Kazi ya Mungu leo hii tunaweza kuiona ni ngumu ya kuchosha, kinyume na matarajio yetu, mpaka inawapelekea  wengine kusema mpaka Mungu anipatie kwanza gari na nyumba ndio nitakwenda kumtumikia, mwingine anasema mpaka Mungu anipe fedha za kutosha ya kujenga kanisa ndio nitaanza kumtumikia kwasababu kazi ni yake na si yangu.

Ndugu yangu kama tunavisubiria tuvipate kwanza hivyo ndio tuanze ndo tumfanyie Mungu kitu tutasubiri sana, Kama tunangojea tuwezeshwe kwa vitu fulani vingi ndio tuseme leo tunajitoa kwa Mungu, hapo tusijidanganye, huo wakati hautafika. Kile ulichopewa na Mungu anzana nacho, na mbele ya safari Mungu atakufanikisha.

Wengine wanasema ngoja nipate pesa kidogo ya kuweza kumudu maisha yangu ndio nitaanza kumtolea Mungu, sadaka zangu. Kama mawazo yako yapo hivyo, ujue hicho kipindi kamwe hakitakaa kikufikie, utasubiri, utangoja, utamlilia Mungu akupe, kamwe hatakupa..Utoaji unaanzana na kile kimoja ulicho nacho, unakwenda kumtolea Mungu, Kama Mungu kakubariki kwa elfu mbili unamtolea elfu moja, hivyo hivyo, lakini ukisubiria upate vingi ndio upeleke kwa Mungu, sahau hilo jambo.

Ndivyo Kristo anavyofanya kazi hivyo, unaweza kumwona ni Bwana mgumu kweli, ambaye hawekezi vya kutosha kwanza kwa wafanya kazi wake, anawaacha wafanye kazi katika umaskini ..lakini hiyo ndio tabia yake. Unapaswa uielewe tu usonge mbele.

Leo hii utaona kama umetelekezwa lakini faida yake siku moja utaiona,  utatateseka, lakini thawabu yake ni kubwa kulinganisha na mateso yako ya leo. Embu tafakari wale aliowapa talanta tano aliwalipa nini baadaye, utaona aliwaambia wakatawale miji mitano, na wale wa mbili akawaambia wakatawale miji miwili. Unaona, faida kidogo tu inampelekea Bwana kukupa miji. Hivyo Mungu anayosababu kwanini atake umtumikie au umtolee katika hali hiyo uliyopo. Zipo thawabu nono zinatusubiria huko mbinguni

Hivyo na sisi tusianze kusema kazi ya Mungu ni ngumu, au kumtolea Mungu ni kugumu. Tufanye tu. Tusiwe watumwa walegevu na wabaya wenye sababu nyingi zisizojenga.

Bali tuwe kama wale wawili wa kwanza. Ili Kristo atakapouona uaminifu wetu, ndio atuongeze, na kutupa vingi zaidi kwa majira yake.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

THAWABU ZA SIRI, ZA WATAKATIFU MBINGUNI.

USIISHI BILA KUIFANYA KAZI YA MUNGU KABISA..

UTAWALA WA MIAKA 1000.

Nini maana ya..“wakiwazuia watu wasioe” (1Timotheo 4:1)

KIFO CHA MTAKATIFU POLIKAPI (Policarp).

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
lucas mhula
lucas mhula
2 years ago

Amen nimejifunza 🙏🙏🤝