Nini maana ya..“wakiwazuia watu wasioe” (1Timotheo 4:1)

Nini maana ya..“wakiwazuia watu wasioe” (1Timotheo 4:1)

Swali: Mtume Paulo anasema katika 1Timotheo 4:3, kwamba “wakiwazuia watu wasioe”. Alikuwa ana maana gani hasa?.

Jibu: Tusome

1Timotheo 4:1  “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani;

2  kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe;

wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli”.

Ni kweli nyakati za Mwisho biblia imetabiri watu watajitenga na imani na “kusikiliza roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani”.. Na pia “watawazuia watu wasioe”

 Ukisoma hapo kwa makini utaona ni anasema “watawazuia watu wasioe” na sio “watawakataza”.. Kuwakataza ni tofauti na kuwazuia. Sasa Bwana Yesu alisema maneno haya..

Luka 11:52 “Ole wenu, enyi wana-sheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia.”

Maana yake ni kwamba mtu anayegeuza maarifa ya Ufalme wa mbinguni, au anayeyapotosha, na kwenda kuwapotosha wengine, ni sawa na amewazuia watu hao kuingia katika ufalme wa mbinguni, kwasababu ameuondoa mlango wa maarifa.

Kwamfano mtu anayepotosha maarifa ya jinsi ya kuoa kibiblia na kumfanya yule mtu asioe kabisa au aoe kimakosa, hapo amemzuia mtu huyo kuoa.

Sasa Utauliza hilo jambo lipo leo?.. Mbona leo tunaona makanisani watu wanahubiriwa waje wapokee wachumba?..hatusikii watu wakizuiliwa kuoa?

Ndio jambo hilo lipo kwa sana, na limeenea duniani kote. Watu wengi sana wamezuiliwa kuoa/kuolewa pasipo wao wenyewe kujijua ingawa wapo katika mahusiano, au kile kinachoitwa ndoa. Kwasababu roho hii inatenda kazi kwa siri sana.

Kwamfano makanisa yanayofungisha ndoa za jinsia moja, na kuzibariki, na kusema ni ndoa takatifu. Watu wa namna hiyo, wanawazuia watu kuoa, kwasababu hiyo ndoa ya jinsia moja waliyoifungisha sio ndoa, bali ni kitu kingine. Hivyo mtu ataendelea kubaki katika hiyo ndoa ya kishetani akijua tayari kaoa, au kaolewa, kwasababu tu mchungaji wake kaidhinisha.. kumbe yupo katika laana, kwa kuzuiliwa kuoa/kuolewa inavyopaswa..

Pia leo hii kuna kundi kubwa la wanaume ambao hawajaoa (maana yake hawajafunga ndoa ya kikristo) lakini wanaishi na wanawake na kuzaa nao watoto na bado wanajiita wakristo, na wanahudhuria kanisani, wala hawaambiwi chochote katika kusanyiko walilopo, zaidi wanawekewa mikono na kubarikiwa ndoa yao hiyo batili, hawaambiwi chochote pengine kwasababu ni wachangiaji wakubwa hapo katika hilo kusanyiko. Hawa nao wamezuiliwa kuoa (yaani wamefungiwa mlango wa maarifa na viongozi wao wa dini). Kwasababu viongozi wao hao wanajua kabisa waasherati hawataurithi uzima wa milele lakini bado hawawafundishi au kuwakumbusha watu wanaowaongoza. Ambapo wangepaswa wawaambie na kuwakemea watubu, na wakafunge ndoa watoke katika hayo maisha ya uasherati wanayoishi.

Katika kanisa la kwanza, watu wa namna hiyo (wanaoishi pamoja huku hawajaoana) walikuwa wanatengwa kabisa, mpaka watakapotubu (na hiyo ni kwa faida ya roho zao)..lakini leo hii wanabarikiwa, jambo ambalo linahuzunisha sana.

Kadhalika yapo makanisa yanayofungisha ndoa za watu walioachana..Utakuta mwanamke kaachana na mumewe bila sababu yeyote, na kaenda kutafuta mwingine na anampeleka kanisani, kufungisha ndoa nyingine ya pili, na viongozi wengi pasipo kumhoji wala kufuatilia historia ya yule mtu kabla ya kuifungisha hiyo ndoa, wanafungisha hivyo hivyo tu, (ili pengine wasije wakamkwaza yule mshirika kipofu, kwasababu pengine ndiye mchangiaji mkubwa pale) bila kujua wamemzuia kuoa inavyopaswa kimaandiko yule mtu anayeoa, (wamemfungia mlango wa maarifa), na kumfanya aishi maisha ya uzinzi maisha yake yote.

Kwasababu huyo anayekwenda kumuuoa tayari ni mke wa mtu, hivyo anakwenda kufanya uzinzi..lakini kwasababu anaona hata mchungaji kakubaliana na hilo, na yeye dhamira yake inampa kibali kuoa kitu kilichoachwa, kwasababu mchungaji wake kakubali.. (Huyu naye kazuiliwa kuoa pasipo yeye kujijua)..Bwana Yesu alisema maneno yafuatayo.

Luka 16:18  “Kila amwachaye mkewe na kumwoa mke mwingine azini; naye amwoaye yeye aliyeachwa na mumewe azini”.

Pia yapo makusanyiko yanayofundisha na kufungisha ndoa za mitara (yaani za wake wengi). Utakuta kijana amefikia umri wa kuoa, na kwa dhamira njema anatafuta mtu wa kuoa, lakini anambiwa na kiongozi kwamba ni ruksa kuoa hata wake wawili, hivyo anakwenda kuoa wanawake wawili, na bila kujua kuwa alichofungishwa sio ndoa bali ni kitu kingine, na bila kujua kuwa tayari kashazuiliwa kuoa, kama maandiko yanavyosema.

Na pia watu wote wanaoishi na magirlfriend au maboyfriend na wanafanya uasherati, na wanahudhuria kusanyiko au kanisa ambalo viongozi wao hawawaambii ukweli, au basi wamezuiliwa kuoa, na pia kama wanaujua ukweli lakini hawataki kuoana lakini wanaendelea kudumu katika uasherati wao, hawa wamejizuia wenyewe kuoa/kuolewa, hivyo wasipotubu watahukumiwa, (Biblia inasema hivyo)

Waebrania 13:4  “Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu”.

Hivyo hii roho inafanya kazi kwa nguvu sana nyakati hizi za Mwisho, na inawachukua wengi. Ni kwanamna gani mtu anaweza kujihadhari nayo?..Ni kwa kufanya mambo yafuatayo.

 1. Kwanza kwa kumpenda Mungu kwa moyo wako wote, nguvu zako zote na akili zako zote.

Ukimpenda Mungu kwa viwango hivyo, itakufanya umtafute Mungu kwa bidii sana, itakufanya usiku na mchana utafute kulijua Neno lake kwa kulisoma na kulitafakari hiyo itakusaidia kujaa maarifa ya kutosha kumhusu Mungu, na hivyo kukufanya usiwe rahisi kuchukuliwa na kila upepo wa mafundisho ya uongo, mfano wa hayo ya ndoa za mitara, au za jinsia moja au za kuachana. Kwasababu utakuwa unalijua neno vizuri, hivyo hata mtu akija kukuambia Sulemani alioa wake wengi hivyo na wewe unaweza kuoa wake wengi, uwe unajua andiko la kuweza kuiangusha hiyo roho. Lakini kama Neno la Mungu halipo kwa wingi ndani yako, utahubiriwa mafundisho ya uongo nawe utaamini na kupotea. Na kujikuta upo kwenye mahusiano kumbe mbele za Mungu unazini na umeshazuiliwa kuoa kitambo sana.

2. Kwa kusali na kuomba kwa bidii.

Hizo ni silaha mbili kuu ambazo katika hizo ni ngumu kuchukuliwa na adui kwa vyovyote vile.

Bwana atubariki sote na kutusaidia.

Kama hujampokea Yesu, kumbuka siku zinaenda, na ile siku inazidi kukaribia, jiulize akirudi leo utakuwa wapi?

Marana atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

Uchaji ni nini kama tunavyosoma katika 1Timotheo 2:10?

JE NI LAZIMA KUBADILISHA JINA BAADA YA KUOKOKA?

KUNA MAJIRA MUNGU ATAIVURUGA MIPANGO YETU.

MAWE YALIYOKWISHA KUCHONGWA MACHIMBONI.

TABIA YA WAZI INAYOWATOFAUTISHA MANABII WA UONGO NA WALE WA UKWELI.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments