JE NI LAZIMA KUBADILISHA JINA BAADA YA KUOKOKA?

JE NI LAZIMA KUBADILISHA JINA BAADA YA KUOKOKA?

Jina la Bwana wetu Yesu, libarikiwe. Karibu tujifunze biblia.

Katika biblia Mungu hakuwabadilisha watu majina kutokana na tafsiri za hayo majina. Ni muhimu kufahamu sana hili, vinginevyo shetani anaweza kukutesa na tafsiri ya jina lako. Kwasababu usipomwelewa Mungu jinsi anavyotenda kazi, utachukuliwa na kila aina ya upepo wa elimu, na mafundisho ya mashetani, ambayo kazi ya hizo elimu ni kuwafunga watu wala sio kuwafungua, Kuwatwisha watu mizigo mizito na wala si kuwatua.

Yohana 8:36 “Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli”

Sasa hebu tuangalie watu wachache waliobadilishwa majina katika biblia, na tafsiri za majina yao kabla na baada ya kubadilishwa, ndipo tutajua tabia ya Mungu.

  1. Ibrahimu

Huyu mara ya kwanza alikuwa anaitwa “Abramu”. Tafsiri ya jina Abramu ni “Baba aliyeinuliwa” na Ibrahimu tafsiri yake ni “Baba wa mataifa mengi”.

Sasa kulingana na tafsiri hizo, sio kwamba Mungu aliona tafsiri ya jina lake la kwanza ilikuwa ni mbaya, na hivyo akataka kumpa jina jipya lenye tafsiri zuri, hapana!..ilikuwa ni nzuri tu… kuitwa “Baba aliyeinuliwa” sio jina baya, lakini ilipofika wakati wa Mungu kumpa agano kwamba atakuwa Baba wa mataifa mengi, ndipo jina lake likabadilishwa na kuwa Ibrahimu. (Hivyo lilibadilishwa kwasababu ya huduma iliyopo mbele yake).

  1. Sara

Huyu alikuwa ni mke wa Ibrahimu, ambaye hapo kwanza alikuwa anaitwa “Sarai” maana yake ni “binti wa mfalme” lakini jina lake lilibadilishwa na kuwa “Sara” ambalo maana yake ni “mama wa wana wa wafalme”. Hivyo halikubadilishwa kwasababu lilikuwa na maana mbaya, bali kwasababu ya Ahadi ya Mungu, ya mumewe Ibrahimu kuwa Baba wa mataifa mengi, hivyo hana budi na yeye kuwa mama wa mataifa na wafalme wengi,  Ni sawa wewe ubadilike sasa kutoka kuitwa mtoto, na kuitwa Baba wa watoto wengi…au kutoka kuitwa binti mpaka kuitwa mama wa mabinti wengi..(Ni kutokana na kubadilika majukumu, umetoka kwenye utoto sasa umeingia kuwa mama/baba)

  1. Yakobo

Mtu wa tatu ni Yakobo, mwana wa Isaka, jina lake lilibadilishwa kutoka kuitwa Yakobo hadi kuitwa Israeli.. Tafisiri ya jina “Yakobo” ni “mshika kisigino”..Jina hilo aliitwa kutokana na jinsi alivyozaliwa, kwani alipozaliwa alizaliwa huku kamshika ndugu yake kisigino.(Mwanzo 25:26)..na Tafsiri ya jina Israeli ni “Kushindana na Mungu”. Sasa Yakobo jina hilo halikubadilishwa kutokana na tafsiri yake ni mbaya..Hapana bali ni kutoka na ahadi mpya Mungu aliyokwenda kumpa baada ya kushindana na yule malaika na kumshinda..Kwasababu kama tafisiri ya Jina Yakobo lingekuwa ndio sababu ya Mungu kumbadilisha jina, basi Mtume wa Yesu aliyeitwa Yakobo, angepaswa naye pia abadilishwe jina. Na aliyeandika kitabu cha Yakobo, naye pia angepaswa abadilishwe.. Lakini tunaona hawajabadilishwa, lakini bado waliendelea kuwa Mitume wa Yesu, waaminifu mpaka mwisho.

  1. Petro

Petro hapo kwanza alikuwa anaitwa Simoni.. Yohana 1:42  “Akampeleka kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama, akasema, Wewe u Simoni, mwana wa Yohana; nawe utaitwa Kefa (tafsiri yake Petro, au Jiwe)”.  Sasa tafsiri ya jina Simoni ni “Amesikia”.. Na tafisiri ya Kefa/Pertro ni “jiwe dogo la kurusha” na sio “mwamba”. Hivyo kwa hali ya kawaida, Simoni ndio lenye tafsiri bora kuliko Petro..

Sasa utaona Bwana Yesu hakumbadilisha jina Simoni kwasababu lina maana mbaya, hapana bali ni kwasababu ya huduma yake inayokwenda kuanza, kwamba Bwana atamtumia kama jiwe lake, kwa kazi yake. Sasa jina “Simoni” lingekuwa na tafsiri mbaya inayomchukiza Mungu au yenye madhara kiroho kwa Petro, basi angembadilisha pia mtume wake mwingine miongoni mwa wale 12, ambaye naye pia alikuwa anaitwa Simoni mkananayo (Mathayo 10:4). Kwasababu Bwana asingeweza kumbadilisha mtume mmoja na kumwacha mwingine mwenye jina kama hilo hilo. (Kwahiyo Petro naye alibadilishwa kutokana na huduma iliyopo mbele yake)

  1. Sauli

Na wa mwisho tunayeweza kumwona ni Mtume Paulo ambaye hapo kwanza alikuwa anaitwa “Sauli” ambapo tafsiri ya jina hilo ni “Ombea” (mf. Kuombea kitu fulani kwa Mungu), hiyo ndiyo tafisiri ya jina Sauli, lakini jina hilo lilikuja kubadilishwa na kuwa “Paulo” ambalo maana yake ni “Mdogo”.

Hivyo unaona hapo, jina lake halikubadilishwa kwasababu lilikuwa na tafsiri mbaya, hata wewe katika hali ya kawaida ungeambiwa uchague uitwe jina lenye tafsiri ya “mdogo” au uitwe jina lenye tafsiri ya “Ombea”..Bila shaka ungechagua lenye tafsiri ya “ombea”. Lakini Mungu alimbadilisha Sauli na kumpa hilo lenye tafisiri ya mdogo.

Na kwanini Mungu alimpa jina hilo Paulo?. Ni kwasababu ya huduma yake, ambayo anakwenda kuifanya hapo mbeleni (ambayo itampasa awe mdogo sana na mnyenyekevu).

Waefeso 3:7  “Injili hiyo ambayo nalifanywa mhudumu wake, kwa kadiri ya kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa kadiri ya utendaji wa uweza wake.

8  MIMI, NILIYE MDOGO KULIKO YEYE ALIYE MDOGO WA WATAKATİFU WOTE, nalipewa neema hii ya kuwahubiri Mataifa utajiri wake Kristo usiopimika;

9  na kuwaangaza watu wote wajue habari za madaraka ya siri hiyo, ambayo tangu zamani zote ilisitirika katika Mungu aliyeviumba vitu vyote”.

 Kwahiyo jambo kubwa la kujifunza ni kwamba… tafsiri za majina yetu, hazina maana sana mbele za Mungu wetu. Ndio ni vizuri kuwa na jina lenye tafsiri nzuri, lakini hilo halikusogezi mbele za Mungu. Kwasababu majina yaliyoandikwa kwenye kitabu cha uzima, hayajaandikwa kulingana na maana za majina hayo, bali kulingana na matendo ya mtu.

Watakuwepo wengi mbinguni ambao majina yao hayana tafsiri nzuri, na vile vile watakuwepo wengi kuzimu wenye majina mazuri, watakuwepo wakina Ibrahimu wengi kuzimu, watakuwepo wakina Paulo wengi kuzimu, watakuwepo wakina Petro wengi kuzimu, na watakuwepo wakina Yohana wengi kuzimu. Vile vile watakuwepo wakina Sauli wengi mbinguni, watakuwepo wakina Yakobo wengi mbinguni, watakuwepo wakina matatizo wengi mbinguni, watakuwepo wakina Majuto wengi mbinguni, watakuwepo wakina masumbuko wengi n.k

Kwahiyo baada ya kuokoka, Tafsiri ya jina lako isikusumbue sana. Kama umependa kulibadilisha kwa mapenzi yako mwenyewe (kwamba hupendwi kuitwa hilo jina katikati ya jamii yako)ni sawa hutendi dhambi, na Kama Bwana amekuongoza kubadilisha jina lako pia ni sawa fanya hivyo!!, lakini kama Bwana hajakuongoza wala usiwe na hofu,  wala usitishwe na elimu zilizozagaa kwamba utapata mikosi kwa jina hilo, au jina hilo ni kikwazo kwako na mafanikio yako.

Kuwa tu kama Simoni Mkananayo mwanafunzi wa Yesu, ambaye jina lake lilibakia kuwa lile lile, lakini bado aliendelea kuwa mwanafunzi wa Yesu..ijapokuwa mwenzake alibadilishwa na kuwa Petro, yeye aliendelea kuwa vile vile Simoni. Kwasababu Mungu hatembei na wewe kwasababu ya tafsiri bora ya jina lako, bali kwasababu ya uaminifu wako kwake katika kuyafanya mapenzi yake. Kama vile asivyobagua rangi, vivyo hivyo habagui watu kutokana na tafsiri za majina yao.

Katika Biblia kuna mtu anaitwa Tabitha au Dorkasi, tafisiri ya jina hilo ni “Paa” kasome Matendo 9:36, sasa “paa” kwa lugha inayoeleweka ni “mnyama Swala”..Lakini pamoja na jina lake hilo lenye tafisiri isiyo na maana, tunasoma Tabitha alimpendeza Mungu sana..

Matendo 9:36 “ Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa”.

Kadhalika katika biblia kuna mtu aliyeitwa Yabesi (1Nyakati 4:9-10), huyu alipewa jina lenye tafsiri mbaya ya HUZUNI, lakini alimpendeza Mungu sana.(Kwa habari zake ndefu unaweza kututumia ujumbe inbox). Na ipo mifano mingine mingi kwenye biblia ambayo hatuwezi kuitaja hapa yote. Lakini kwa hiyo michache itoshe tu kusema kwamba, Kama ulikuwa na hofu na tafsiri ya jina lako, badilisha mtazamo sasa..Anza kuwa na hofu na mwenendo wa maisha yako katika hatima ya maisha yako, zaidi ya tafisir ya jina lako.

Ufunuo 20:12  “Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, SAWASAWA NA MATENDO YAO”.

Hivyo utazame mwenendo wako, je umesimama katika Imani sawasawa?..Je matendo yako yanampendeza Mungu?..kama bado basi rekebisha leo kabla hujafikia mwisho wa siku zako za kuishi hapa duniani.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

JINA LAKE KWA KIEBRANIA NI ABADONI, NA KWA KIYUNANI NI APOLIONI.

HAPO NDIPO WATU WALIPOANZA KULIITIA JINA LA BWANA.

CHAKULA CHA ROHONI.

CHAKULA CHA ROHONI.

TUMEPEWA MAMLAKA YA KUKANYAGA NG’E NA NYOKA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Hezron mwalongo
Hezron mwalongo
3 years ago

Bwana Yesu asifiwe mtumishi waBwana, natamani sana kuendelea kuyapata mafundisho ya neno la Mungu toka kwako kama itawezekana naomba uendelee kunitumia masomo mengine.