HAPO NDIPO WATU WALIPOANZA KULIITIA JINA LA BWANA.

HAPO NDIPO WATU WALIPOANZA KULIITIA JINA LA BWANA.

Shalom, Ni siku nyingine tena Bwana ametukirimia kuiona kwa neema zake nyingi, Hivyo nakukaribisha tuyatafakari kwa pamoja maneno makuu ya Mungu wetu maadamu siku ile inakaribia.

Leo tutakitazama tena kitabu cha mwanzo, hususani juu ya uchaguzi waliouingia watu wawili, ambao tutaona hatma zao mbeleni zilikuja kuwa nini katika kizazi cha saba..

Mtu wa kwanza tutakayemwangalia atakuwa ni Kaini na pili Ni Sethi.

Kama tunavyojua Kaini alikuwa ni mtu wa kwanza kuikaribisha laana ya Mungu katika Maisha yake, aliambiwa atakuwa mtoro na mtu asiyekuwa na kikao duniani.. Sasa wengi wetu leo hii tunapomfikiria Kaini kwa laana alizopewa na Mungu tunamwona kama ni mtu aliyekuja kufanana na kichaa tu kama wale waokota makopo na maskini..Lakini ninao uhakika kama wengi tungekuwepo wakati ule anaishi duniani basi wengi wangejipendekeza sana kwa Kaini, hususani wale wanaoangalia mafanikio ya mtu kama ndio kipimo cha kubarikiwa na Mungu, Kwasababu biblia inatuonyesha, sio tu Kaini alikuwa ni mtu mwenye maendeleo makubwa bali uzao wake wote pia baada yake, (yaani Watoto wake),walikuwa ni watu wenye akili nyingi, wenye elimu, na ujuzi wa kuvumbua mambo mbali mbali, (Soma 4:16-24).

Hivyo kama kubarikiwa kimwili na kiakili, basi Kaini alibarikiwa mara nyingi sana Zaidi hata ya Sethi,

Lakini tukirudi kwa Sethi sasa, ambaye alizaliwa kulijaza pengo la Habili, mambo yalikuwa tofuati kidogo, yeye muda mfupi tu baada ya kumzaa, mwanaye Enoshi,Akatafakari akaona mbona hali sio kama inavyopaswa iwe? Mbona bado kama haya Maisha yanaonekana ni bure bila Mungu hata kama tunajihangaisha vipi, Mbona kama mwenye hii dunia amekaa kimya na hatusemeshi, kwanini na sisi tuendelee kubakia tu hivyo hivyo tunajiamulia tu mambo yetu wenyewe bila yeye..Hapana hii sio sawa, ni lazima kuanza kumtafuta Mungu.

Sethi na Watoto wake wakaanza kuweka mipango Madhubuti na namna ya kumtafuta Mungu, pengine wakaanza kujifunza kusali, wakaanza kujifunza kufunga, wakaanza kujifunza kuishi Maisha ya haki, ili tu walau wampate Mungu waliyempoteza, walianza kujifunza kumtolea Mungu sadaka mbalimbali, Wakaliita jina la Bwana kwa nguvu zote na kwa bidii..

Biblia inatuambia..

Mwanzo 4:26 “Sethi naye akazaa mwana; akamwita jina lake Enoshi. HAPO NDIPO WATU WALIPOANZA KULIITIA JINA LA BWANA.”

Tofauti na Kaini Pamoja na uzao wake, wao uvumbuzi ulikuwa ni bora kuliko kitu kingine, uchumi, ulikuwa ni wa maana Zaidi katika Maisha kuliko kitu kingine chochote, elimu na ustaarabu ndio vilikuwa ni kiini cha ustaarabu wao..na Mungu hakuwa kitu kwao.

Lakini nataka uone matokeo ya kila mmoja alipofika katika kizazi kile cha saba..

Ukitazama pale, utaona Ule uzao wa Sethi, waliendelea hivyo hivyo kumwita Bwana bila kuchoka, ndipo akazaliwa mtu mmoja aliyeitwa Henoko, mtu huyu alikuwa mzao wa saba alitembea na Mungu hadi kufikia hatua ya kumpendeza na kunyakuliwa..akaenda moja kwa moja kifuani mwa Mungu..

Unaweza kuona hiyo ilikuwa ni bidii ya wao kuliita jina la Mungu, hadi mtu wao wa saba kunyakuliwa.

Lakini upande wa pili wa Kaini, mambo yalikuwa tofauti, mtu wa saba aliitwa Lameki, yeye ndio aliyekuwa mbaya mara kumi Zaidi hata ya Kaini baba yake..Licha ya kwamba yeye ndiye alikuwa mwanzilishi wa ndoa za mitara duniani, lakini alikuwa ni muuaji wa watu wasiokuwa na hatia wengi.. Lakini cha ajabu ni kuwa uzao wake uliendelea kuwa na mafanikio makubwa duniani, tusome..

Mwanzo 4:19 “Lameki akajitwalia wake wawili, jina la wa kwanza ni Ada, na jina la wa pili ni Sila.

20 Ada akamzaa Yabali; huyo ndiye baba yao wakaao katika hema na kufuga wanyama.

21 Na jina la nduguye aliitwa Yubali; huyo ndiye baba yao wapigao kinubi na filimbi.

22 Sila naye akamzaa Tubal-kaini, mfua kila chombo cha kukatia, cha shaba na cha chuma; na umbu lake Tubal-kaini alikuwa Naama.

23 Lameki akawaambia wake zake, Sikieni sauti yangu, Ada na Sila; Enyi wake za Lameki, sikilizeni usemi wangu; Maana nimemwua mtu kwa kunitia jeraha; Kijana kwa kunichubua;

24 Kama Kaini akilipiwa kisasi mara saba, Hakika Lameki atalipiwa mara sabini na saba”.

Ndugu, hata leo zao hizi mbili zipo duniani..Na zao hizi kwa agano jipya hazijaanza leo wala jana, bali tangu wakati wa Kristo Yesu kuwepo duniani..Uzao wa kwanza ndio ule wa kanisa la kwanza la mitume lililojulikana kama Efeso…Tangu ile siku ya pentekoste watu walianza kuliita jina la Bwana, na Kristo akawahidia kuwa atawanyakua..Lakini Unyakuo Mungu alikwisha upanga kwa mtu wa saba, ambalo ndio kanisa la Saba na la mwisho, ndio hili tunaloishi mimi na wewe, lijulikanalo kama Laodikia (Ufunuo 3)..

Hivyo moja ya hizi siku watakatifu wa kanisa hili watondolewa duniani ghafla kwa tukio maarufu lijulikanalo kama Unyakuo. Watakatifu wataondolewa! Kuipisha dhiki kuu duniani.

Lakini sasa ule upande wa pili uzao wa Ibilisi, huo tangu zamani hauna Habari na Mungu, wenyewe unatazama tu mambo ya duniani, elimu, pesa, uchumi, mafanikio, ukiueleza Habari za Mungu unakucheka, unakudhihaki, unakuona,, ukiuambia hizi ni siku za mwisho utakuambia wacha hadithi za kizee..

Ndugu tunaishi ukingoni mwa wakati, kama wewe ni mkristo, basi usiache kuliiita jina la Bwana kwa bidii maadamu una muda, kwasababu wakati si mrefu aidha uwe hai au uwe umekufa, parapanda italia na utaenda kwenye unyakuo mfano wa Henoko. Na hapo ndipo utakuwa mwisho wa mateso yako.

Lakini wewe kama Habari hizi za wokovu ni kelele tu kwako, nakushauri ubadilike sasa. Mgeukie Kristo na yeye atakupokea kigeuza nia yako.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Tofauti ya kazi ya Damu ya Yesu na Jina la Yesu ni ipi?

Mtu astahiliye hofu ni yupi?

Je! ni vema kwa mkristo kwenda hospitali au kutumia miti shamba anapougua?

RAFIKI WA KWELI NI YUPI?

Tamaa yako itakuwa kwa mumeo.Ni tamaa ipi ya Hawa?

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Dina Mgoloka
Dina Mgoloka
1 year ago

Bwana Asifiwe naomba kutumiwa masomo haya kwa njia ya email pia

Rogath
Rogath
4 years ago

Amina