MIUJIZA YA KRISTO, HAITEGEMEI KANUNI ZA KIBINADAMU.

MIUJIZA YA KRISTO, HAITEGEMEI KANUNI ZA KIBINADAMU.

Shalom, karibu tujifunze Neno la Mungu, lakini kabla hatujaendelea, ningependa kwanza uzitafakari hizi habari mbili, kwasababu ndio kiini cha somo letu kilipo, zingatia sana sana  hiyo mistari iliyowekwa katika herufi kubwa.

Luka 5:4 “Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, TWEKA MPAKA KILINDINI, mkashushe nyavu zenu mvue samaki.

5 Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu.

6 Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika;

7 wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama”.

Pia, soma..

Yohana 21:3 “Simoni Petro aliwaambia, Naenda kuvua samaki. Nao wakamwambia, Sisi nasi tutakwenda nawe. Basi wakaondoka, wakapanda chomboni; ila usiku ule hawakupata kitu.

4 Hata asubuhi kulipokucha, Yesu alisimama ufuoni; walakini wanafunzi hawakujua ya kuwa ni Yesu.

5 Basi Yesu akawaambia, Wanangu, mna kitoweo? Wakamjibu, La.

6 Akawaambia, LITUPENI JARIFE UPANDE WA KUUME WA CHOMBO, nanyi mtapata. Basi wakatupa; wala sasa hawakuweza kulivuta tena kwa sababu ya wingi wa samaki”.

Nataka ufananishe hizo habari mbili, utaona mara ya kwanza Kristo anakutana na akina Petro baada ya kuwahubiria aliwapa maagizo ya kwenda kuvua samaki, akamwambia atweke mpaka vilindini, akiwa na maana waanze safari ya kutoka pale walipo, waende mbali sana kwenye bahari  kuu (Ndipo vilindini) ili wakavue samaki zao. Hatujui walisafiri umbali wa kilometa ngapi, lakini mpaka mtu ufike vilindini, ni sharti uende mbali sana na fukwe..Na walipofika wakazishusha nyavu zao kwa Neno la Bwana, kisha wakapata samaki wengi sana, mpaka nyavu zikawa zinakaribia kukatika kama tunavyosoma hiyo habari.

Lakini tunaona pia katika tukio lingine ambalo ni baada ya Kristo kufufuka, aliwaona tena wakihangaika usiku kuchwa kama pale mwanzo wakitafuta samaki wasipate.. Pengine safari hii Petro alitazamia ataambiwa “atweke mpaka vilindini” kama alivyoambiwa hapo kwanza, wakavue, lakini maagizo yalikuwa ni tofauti kabisa, bali palepale UFUKWENI walipokuwepo wametegesha vyombo vyao, Kristo aliwapa maagizo, wazitupe nyavu zao upande wa pili tu wa chombo. Ndipo walipofanya vile walipata samaki wengi sana tena wakubwa, kiasi cha kuwafanya hata wao washindwe kulivuta lile jarife  pale pwani walipokuwepo.

 Ni nini Kristo alitaka wanafunzi wake na sisi  sote tujue?

Kuna majira Kristo atakupa maagizo ya kukihangaikia kidogo kile unachokihitaji, na mwisho wa siku atakufanyia muujiza mkubwa sana katika jambo hilo.. Lakini pia kuna wakati hatokuagiza ukihangaikie hata kidogo, bali hapo hapo ulipo, atakupatia, kuhangaika kwako wewe kutakuwa ni kukusanya tu.

Mambo haya mawili ni vizuri ukayafahamu, wewe uliyeokoka, kwasababu wapo watu wanadhani, Mungu wa “Mana” amekufa, hawezi kutenda kazi tena leo hii, wanadhani njia pekee aliyobakiwa nayo ya Mungu kukubariki, au kukutendea miujiza ni lazima ukajitaabishe huko vilindini! Basi. Nataka nikuambie hilo kweli linawezekana, na likaja kama agizo la Mungu, lakini pia lile lingine nalo linawezekana, tena sana.

Bwana Yesu alisema maneno haya..

Mathayo 6:25 “Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi?

26 Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao?

27 Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja?

28 Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti

29 nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo.

30 Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba?

31 Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini?

32 Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote.

33 Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.

34 Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake”.

Hivyo usilipindue Neno la Kristo, kwa kuegemea upande mmoja tu, Yote yawezekana kwa Mungu (Mathayo 19:26), na vilevile Bwana Yesu alisema yote yawezekana kwake yeye aaminiye, sio Mungu tu peke yake, hata kwa mtu yeyote atakayemwamini Mungu, yatawezekana kwake (Marko 9:23). Hivyo ukimwamini Mungu katika njia ile atajifunua kwako katika hiyo, halikadhali ukimwamini katika njia ile nyingine atajifunua kwako katika hiyo. Hakuna formula kwa Mungu. Yeye sio mwanadamu. Ni Mungu wa milimani, pia ni Mungu wa mabondeni,.Njia zake hazitafutikani,

Warumi 11:33 “Jinsi zilivyo kuu utajiri na hekima na maarifa ya Mungu! Hukumu zake hazichunguziki, wala njia zake hazitafutikani!”

Hivyo huna haja, ya kuogopa  lolote, unachopaswa kufanya ni kuhakikisha unatembea naye katika njia zako zote, popote pale ulipo, uwe ni katika vilindi au katika fukwe, matokeo yatakuwa ni yale yale. Mwamini tu, huku ukimtumikia kwa moyo wako wote.

Mtafute Mungu ndugu yangu, hizi ni siku za mwisho, Usitoe kisingizio cha kusema nipo busy, siwezi kuomba, siwezi kwenda ibadani, siwezi kusoma Neno, nina majukumu ya kifamilia, hicho kisingizio hakitakuwa na mashiko siku ile ya mwisho utakaposimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu. Kwasababu wataletwa wenzako kama wewe ambao walikuwa buzy kuliko wewe mmojawapo ni Danieli, lakini watakuambia hatukuacha kumtafuta muumba wetu.

Je! Na wewe unatembeaje na Mungu wako, ukiwa hapa duniani?. Je umemkabidhi Maisha yako? Kama sivyo ni heri ukampokea leo kwasababu hakuna anayejua kesho kutatokea nini. Ondoa hofu ya Maisha, anza kumwamini Mungu, na atakuonekania katika mambo yako yote.

Zaburi 27:1 “Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani”?

Zaburi 23:1 “Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu.

2 Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza.

3 Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.

4 Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji”.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

TUNALINDWA NA NGUVU ZA MUNGU.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

SI MAPEPO YOTE NI YA KULIPUKA.

Chamchela ni nini kwenye biblia?(Zaburi 58:9, Amosi 1:14)

NITAUPATAJE UPENDO WA KI-MUNGU NDANI YANGU?

Tofauti kati ya mtume na mwanafunzi ni ipi kibiblia?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments