HUTATAMBUA LOLOTE, SIKU YA UNYAKUO IKIFIKA.

HUTATAMBUA LOLOTE, SIKU YA UNYAKUO IKIFIKA.

Bwana Yesu alitupa dalili za kurudi kwake, akatuambia mkiona dalili Fulani Fulani kama vile matetemeko, mlipuko wa magonjwa, manabii wa uongo, vita n.k. Basi tujue yupo mlangoni kurudi. Lakini kamwe hakutupa dalili ya SIKU yenyewe atakayorudi itakuwaje.. Na hiyo ndio hatari Zaidi kwasababu watu wengi leo hii japokuwa wanajua Yesu atarudi siku yoyote kutokana na kuwa dalili hizo zimeshatimia zote, Lakini bado wanachunguza chunguza siku yenyewe, wakidhani  labda watashtukia lolote.

Bwana Yesu alisema siku ya kuja kwake, inafanana na siku zile za Nuhu, Siku zile mpaka Nuhu anaingia kwenye Safina hakuna mtu yeyote alitambua kuwa tayari Mungu ameshaihukumu dunia.. mpaka zikapita siku saba, nyingine ndipo mvua ya gharika ikashuka kwenye dunia.

Mathayo 24:38 “Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina,

39 WASITAMBUE, HATA GHARIKA IKAJA, IKAWACHUKUA WOTE, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.

40 Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa;

41 wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.

42 Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu”.

Unaona? Leo hii, kama wewe sio “bibi-arusi” wa kweli wa Kristo, nikimaanisha, kama sio mkisto aliyesimama katika wokovu kweli kweli, usitazamie utatambua lolote siku  Kristo anarudi kuwanyakua watakatifu wake. Kwasababu hata Bibi-arusi wake mwenyewe hatojua siku hiyo itakavyokuwa sembuse wewe?..

Na ndio maana aliwaambia mpaka na wateule wake, kwamba wajiweke tayari, waifanye kazi yake, watimize wajibu wao walioitwa hapa duniani wa kuitangaza injili yake, kwasababu saa wasiodhani ndio atakayokuja..

Mathayo 24:43 “Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa.

44 Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika SAA MSIYODHANI MWANA WA ADAMU YUAJA.

45 Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake?

46 Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo.

47 Amin, nawaambieni, atamweka juu ya vitu vyake vyote.”

Hakuna mtu atakayeitambua siku hiyo, itakuja ghafla tu bila hodi, hakuna dalili yoyote itakayotutambulisha, itakuwa kama tu ilivyo leo, au jana,  wakati ambapo watu wanapanga mipango yao ya kimaisha, wanalijenga taifa lao, wanauza pombe, na kufanya biashara hapo hapo, Unyakuo unapita , mmoja anatwaliwa mmoja anaachwa..

Watu wengi sana wataingiwa na butwaa, wakisema mbona Bwana hakutupa taarifa au kiashirio fulani, mbona, angani hakukuonekana chochote, mbona tulitazamia jambo Fulani kwanza tulione, ndio unyakuo upite, imekuwaje, amesharudi, wakati watu wengine hawajahubiriwa bado injili. Lakini ndio hivyo tayari watakatifu wameshaondolewa.

Wakati huo upo karibu sana ndugu yangu, ridhika na dalili tunazoziona, kwasababu hakutakuwa na nyingine Zaidi ya hizo zilizoandikwa kwenye biblia.  Usidhani malaika atatokea hapo mawinguni kutuhubiria injili kwamba kesho Yesu ndio anarudi.

Kama utakosa unyakuo, basi ujue, utakuwa katika majuto na vilio na kusaga meno kusikokuwa kwa kawaida. Majuto hayo, unaweza ukayaona sio kitu leo kwasababu bado hayajakukuta, lakini  subiri siku hiyo ikufikie, hutatamani uishi. Hicho kiburi cha uzima ulichonacho leo, siku hiyo kitayeyuka chote, utamtafuta Mungu hutamwona. Utalia hakuna atakayekusikia, makanisa yatakuwa hayana faida yoyote kwako. Hakuna chochote kitakuwa na maana kwao, kwasababu hata pesa hazitafanya kazi wakati huo.

Ndugu, ndani ya hichi kipindi kifupi tulichobakiwa nacho bado unayo nafasi ndogo sana ya kutubu, Tubu leo kwa kumaanisha kabisa kuacha dhambi zako, na Kristo atakupokea.

Shalom.

Kumbuka katika saa usiyodhani Kristo anakuja!

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Je ni wanyang’anyi wawili waliomtukana Bwana Yesu au mmoja?

Ni kweli Waliolala Katika Kristo Wamepotea?(1Wakor 15:18)

Je! ile habari ya watu wawili wenye pepo inajichanganya?

NAMNA YA KUMTAMBUA BIBI ARUSI WA KWELI WA KRISTO.

MATESO YA KUZIMU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
11 months ago

Amina