NAMNA YA KUMTAMBUA BIBI ARUSI WA KWELI WA KRISTO.

NAMNA YA KUMTAMBUA BIBI ARUSI WA KWELI WA KRISTO.

Nitamtambuaje bibi arusi wa kweli?

Shalom.

Ni vizuri tukafahamu kuwa katika ukristo yapo makundi matatu ya waaminio. Tukilielewa hilo itatusaidia sisi kujipima tupo katika kundi lipi. Na hatua zipi tuchukue ili tusimame katika upande salama.

kundi la kwanza:

Ni kundi la watu wanaojiita wakristo, hawa wanaweza wakawa wamezaliwa katika familia za kikristo au walioupokea ukristo kama dini yao mpya tu,. Au kama kitambulisho chao tu, Na kuwatambua hawa ni rahisi, huwa hawana habari na Mungu hata kidogo, kinachowatofautisha tu wao na ulimwengu ni hicho kitambulisho cha kikisto walichozaliwa nacho au walichokipokea basi.

Lakini mambo mengine yote yaliyosalia hayana tofuati na watu wengine wote wasiomjua Mungu, ukimuuliza Je! unajua kama unyakuo upo karibu atakwambia sifahamu unazungumzia nini. Ukimuuliza Je umeokoka atakwambia hiyo dini siijui..hana habari na ibada wala, wala kitu chochote cha ki-Mungu yupo tu, kama wapagani, lakini anajivunia ukristo wake. Na hawa wapo wengi sana.

Kundi la Pili:

Ni kundi la wakisto ambao wanaamini kila kitu, wanafahamu kila habari katika maandiko. Wanahudhuria ibadan, lakini ni vuguvugu, nusu kwa Mungu, nusu kwa shetani, Biblia inawafananisha hawa na wale wanawali wapumbavu tunaowasoma katika Mathayo 25..Na kwa jina lingine wanajulikana kama Masuria, hawana muunganiko rasmi na Kristo.

Hawa ndio siku ile watakapojigundua wameachwa katika unyakuo ndio watakaolia n kuomboleza, kwasababu nao pia walikuwa wanamtazamia Kristo lakini kwasababu ya kuwa vuguvugu, wataachwa..Na hawa pia wapo wengi katika kanisa.

Kundi la Tatu:

Ni Wakristo ambao wamedhamiria kweli kuifuata njia ya Kristo. Ukristo sio dini yao, bali ni Imani yao. Hawa ndio wale wanawali werevu waliotwaa taa zao pamoja na mafuta ya ziada katika vyombo vyao vya pembeni..Na hawa ndio bibi arusi wa Kristo, ambao Kristo anawaandaa katika kila kipindi cha Kanisa..Na hawa ni wachache sana katika Kanisa.

Jambo la muhimu la kufahamu ni kuwa kati ya haya makundi matatu ya wanaojiita wakristo, ni kundi moja tu ndilo litakalonyakuliwa kwenda mbinguni..Nalo ndio hilo kundi la tatu. Bwana YESU leo hii hatafuti Masuria, wala watu walio baridi, bali anamwandaa bibi arusi wake haijalishi atakuwa ni mmoja au mia au elfu hilo halijalishi idadi yake ikishatimia haangalii ulimwengu mzima unafikiri vipi. Watanyakuliwa na kwenda mbinguni kwenye karamu ya mwana kondoo

Sasa kwa ufupi embu tuangalie ni kwa namna gani tunaweza kumtambua bibi arusi wa kweli wa Kristo.

Kama wengi wetu tunavyofahamu Ile habari ya Ibrahimu kwenda kumtafutia mwanawe Isaka mke katika nyumba ya baba yake. Ni habari inayofunua siri ya Kristo na bibi arusi wake jinsi atakavyompata katika siku za mwisho. Sasa tukisoma ile habari tunaona ulifika wakati Ibrahimu aliona mwanawe Isaka ameshakuwa mtu mzima. Na mama yake ameshafariki,hana mtu wa kumfariji, akaona ni vema akamtafutie mwanawe binti wa kuoa,..Ndipo akamtuma mtumwa wake alimwamini sana katika mali zake zote aliyeitwa Eliezeri afunge safari pamoja na Ngamia 10 watoke katika nchi ya Kaanani waende mpaka Mesopotamia nchi ya Baba yake,..asafiri umbali mrefu kusudi tu ampatie mwanawe mke aliye bora…

Na Ndivyo Mungu alivyofanya kwa mwanawe mpendwa YESU KRISTO, Hakumtafutia bibi Arusi wake safi kutoka katika kanisa la Israeli badala yake alikuja mbali kwa watu wa mataifa yaani mimi na wewe ili kututwaa tuwe pamoja naye katika kiti chake cha enzi..

Safari ya kwenda kumtafuta Bibi arusi.

Sasa Eliezeri akafunga safari mamia kwa mamia ya kilometa akiwa na ngamia zake 10 pengine alitumia wiki kadhaa au miezi kusafiri. Ndipo akafika karibu na nchi ile, nje kidogo na mji ambapo pana kisima cha maji ambapo mabinti wengi wa mji wanakitumia wakati wa jioni kuja kutweka maji. Kwa ajili ya shughuli za nyumbani.

Kama tunavyosoma habari ile, Eliezeri alimwomba Mungu ishara, akasema binti Yule nitakayemwomba maji ya kunywa katika mtungi wake, na kusema sitakupa tu wewe bali nitanyesha mpaka na ngamia zako basi huyo na awe mke wa mwana wa bwana wangu..Biblia inatuambia wakati wazo hilo bado lipo katika kichwa chake muda huo huo akatokea binti pale kisimani, kuchota maji tusome..

Mathayo 24:12-20.

Mwanzo 24: 12 “Naye akasema, Ee Bwana, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, nakuomba mambo yangu uyajalie yawe heri leo, ukamfadhili bwana wangu Ibrahimu.

13 Tazama! Nimesimama karibu na kisima cha maji, na binti za watu wa mjini wanatoka kuteka maji,

14 basi na iwe hivi; yule msichana nitakayemwambia, Tua mtungi wako, nakuomba, ninywe; naye akasema, Unywe, nami nitawanywesha na ngamia zako pia; basi huyu na awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka; na kwa hayo nitajua ya kuwa umemfadhili bwana wangu.

15 Ikawa, kabla hajaisha kunena, tazama, Rebeka anatokea, binti wa Bethueli mwana wa Milka, mkewe Nahori, ndugu wa Ibrahimu, naye ana mtungi begani pake.

16 Naye yule msichana alikuwa mzuri sana uso wake, bikira, wala mwanamume hajamjua bado; akashuka kisimani, akajaza mtungi wake, akapanda.

17 Ndipo yule mtumishi akapiga mbio kwenda kumlaki, akasema, Tafadhali unipe maji kidogo katika mtungi wako ninywe.

18 Naye akasema, Unywe, bwana wangu, akafanya haraka, akatua mtungi wake mkononi mwake, akamnywesha.

19 Hata alipokwisha kumnywesha akasema, Na ngamia zako nitawatekea, hata watakapokwisha kunywa.

20 Akafanya haraka, akamwaga maji ya mtungi wake katika birika, akapiga mbio kisimani ateke, akawatekea ngamia zake wote”.

Zoezi la kunywesha Ngamia 10.

Ukiendelea kusoma utaona Yule mtu ndipo alipopata uhakika kuwa huyu binti ndiye Mungu aliyemkusudia kuwa bibi arusi wa Isaka. Ni rahisi kuona kama alimwomba Mungu ampe ishara nyepesi, lakini ile haikuwa ishara ndogo kama ukichunguza vizuri, kwa mazingira yale yaliyokuwepo.

Embu jaribu kufikiria Yule alikuwa ni mtoto wa kike, pili alikuwa na mtungi mmoja tu mdogo labda tuseme wa lita 10 ambayo ni sawa na ndoo moja ya maji. Na unaambiwa ngamia ni mnyama anayekunywa maji haraka sana zaidi ya wanyama wengi, ndani ya dakika tatu tu tayari kashamaliza lita 200 za maji..Hivyo ilihitajika mitungi/ndoo 20 za maji kukata kiu ya ngamia mmoja..Ukizingatia ngamia walikuwa 10 pale, hivyo kama ni kuwanyeshwa ngamia basi inakugharimu si chini ya ndoo 200, kushuka kisima na kupanda kuwashibisha ngamia wote..Hilo sio zoezi ndogo..

Kwa wakati ule ilikuwa ni rahisi sana kusaidiwa kunyeshwa kondoo zako 100 za maji na mbuzi zako lakini si ngamia. Tena ilikuwa inafanywa na wanaume si wanawake..Hivyo Eliezeri kumwomba Mungu ishara kama ile, alitambua kabisa kwa namna ya kawaida ni kama haiwezekani…Lakini msichana Rebeka hakujali hilo, kwa jinsi roho ya kujali ilivyokuwa imejaa ndani yake.

Alikwenda hivyo hivyo alishuka kisimani, akapanda mpaka mitungi yote mia mbili akaimaliza. Na Eliezeri hakufanya chochote, wala hakumsaidia bali alikuwa anamwangalia tu, labda kama atakata tamaa katikati ya safari, aseme sio huyo, asubirie mwingine kuja kuchota maji lakini Rebeka alichota maji ndoo zote labda 200 mpaka akamaliza..

Je! jiulize wewe binti wa kike unaweza ukafanya ukarimu kama huo kwa mtu usiyemjua ikiwa tu kumpisha mzee kwenye daladala ni shida itakuwaje kwa kazi kama hiyo?. Hata kwa kulipwa tu unaweza usifanya..Na kumbuka Rebeka alikuwa ni mzuri wa uso sana, kuwazidi wengi. Lakini hakujali hilo.Hapo ndipo Eliezeri akapata uthibitisho sasa kuwa huyu Rebeka ndio bibi arusi mwenyewe..Ukiendelea kusoma habari utaona hadi alipochuliwa na kuletwa Kaanani kwa mume wake Isaka.

Lakini habari hiyo inafunua nini kwa kanisa la leo?.

Kumbuka Eliezeri anasimama kama kundi la watumishi wote wa Mungu ambao wametumwa ulimwenguni kote kuhubiri Injili. Kumtafutia Kristo bibi arusi safi wa kwenda naye mbinguni kwenye karamu ya mwana-kondoo.Kama Mtume Paulo anavyosema katika..

2Wakorintho 11: 2 “Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi”.

Na watumishi wa Mungu pia wamepewa ishara ya kuwatambua bibi Arusi hao, na Ishara yenyewe ni kama ile ya Rebeka..Ndugu Tukijiona tunahubiriwa injili lakini tunaishia tu kwenye kile tunachoambiwa, labda tuseme tutubu au tubatizwe , halafu baada ya hapo basi, hatuonyeshi bidii zetu binafsi za kuthibitisha wito wetu kwa Mungu..Basi tujue kuwa sisi bado sio bibi arusi wa Kristo.

Kama Sisi wenyewe binafsi hatutaki kumtafuta Mungu wetu atufundishe zaidi. Hatutaki kuomba wenyewe bila ya kushurutishwa, tunangojea tu tufundishwe biblia jumapili kwa jumapili sisi hatuna muda na mambo hayo tunaendelea na shughuli zetu. Basi tujue sisi tutakuwa ni Masuria tu, wale wanawali wapumbavu, Unyakuo utakapopita tutabaki hapo..

Bibi arusi kama Rebeka haridhiki na hali ile ile aliyopo kwa muda mrefu, anafanya zaidi ya yale anayoelekezwa na kuambiwa. Soma habari ile ya wanawali 10 utaona wale werevu walijiongeza, kutafuta mafuta ya ziada kwa ajili ya TAA zao. Kwasababu walijua yale pekee hayawatoshi. Usitegemee kuhubiriwa tu peke yake.

Ndugu hizi ni siku za hatari, watakaonyakuliwa ni wachache sana, tuombe Mungu na vilevile tuongezee bidii zetu binafsi ili tustahili kuwa miongoni mwa bibi arusi wa Kweli wa Kristo.

Bwana akubariki sana.

Mada Nyinginezo:

UNYAKUO.

KARAMU YA MWANA-KONDOO.

Biblia inamaanisha nini kusema Yeye aliye na sikio, na asikie?

UNATAKA KUBARIKIWA? BASI USIKWEPE GHARAMA ZAKE.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Mwakanyamale Clement Manning
Mwakanyamale Clement Manning
5 months ago

Your teachings have tought me deeply about Our Lord Jesus,Iam blessed and farmore my faith has been abundantly nourished. Through teachings I strongly feel deep in my Soul to extend what i have got from you with my church members through Sundy school,Preaching,Evagelism and my family at large. Much Obliged