NITAFUNGUAJE MILANGO ILIYOFUNGWA MBELE YANGU?

NITAFUNGUAJE MILANGO ILIYOFUNGWA MBELE YANGU?

Nifanye nini ili niifungue milango iliyofungwa mbele yangu?

Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe. Moja ya mada inayozungumzwa na wakristo wengi hususani wa kanisa hili la Mwisho ni juu ya namna ya kufungua milango iliyofungwa mbele yetu.

Na kwa haraka haraka wengi wetu tunatafuta njia za haraka haraka ilimradi tu, Milango iliyopo mbele yetu ifunguke. Ndio hapo utaona baadhi wanaenda kwa watumishi wawaombee, wengine watatafuta mahali panapouzwa Mafuta fulani, au maji fulani ya baraka au upako. Wengine watakwenda kutafuta kwa kuombewa nyota zao na kutabiriwa. Na mambo mengine mengi yanafanyika katikati ya wakristo. Na Bahati mbaya wengi baada ya kufanya hivyo hali inabakia kuwa vile vile. Ni kwanini?. Ni kwasababu hiyo sio njia au Namna Mungu aliyoiweka ya kufungua milango iliyofungwa mbele yetu.

Biblia inasema katika..

Ayubu 22:21 “Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia.”

Kumjua Mungu maana yake ni kutafuta maarifa ya kujua ni nini Mungu anataka, Yakikosekana maarifa ya kumjua Mungu ni rahisi sana kuangamia.

Sasa leo kwa ufupi sana tutatumia biblia kujua namna yakufungua milango iliyopo mbele zetu. Na pia kumbuka kabla ya yote kuwa sio kila mlango uliofungwa mbele yako. Ni shetani kahusika! Hapana mingine ni Mungu mwenyewe kaifunga kwaajili ya makusudi yake. Na tunajua makusudi ya Mungu siku zote ni Mema. Hivyo tutazungumzia kwa ujumla namna ya kufungua milango yote (Iliyofungwa na Mungu au shetani)

Tusome.

Ufunuo 3:7 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye, naye afunga wala hapana afunguaye.

8 Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, KWA KUWA UNAZO NGUVU KIDOGO, NAWE UMELITUNZA NENO LANGU, WALA HUKULIKANA JINA LANGU”.

Kwanza tunaona hapo kumbe Kristo anaweza kufunga kitu na hakuna awezaye kukifungua..Na pia anauwezo wa kufungua na hakuna awezaye kuufunga. (Hiyo ni point ya kwanza ya kuweka akilini). Ili tufahamu kuwa sio kila mlango uliofungwa mbele yetu ni shetani kahusika. Hapana bali mengine ni Kristo mwenyewe ndiye aliyehusika.

Lakini tukiendelea na mstari wa 8 ndio tutapata majibu ya swali letu. “Tutafunguaje milango iliyofungwa mbele yetu?”.

Bwana Yesu mwenye ufunguo wa mambo yote anaanza kwa kusema…Nayajua matendo yako!. Ikifunua kuwa mlango kufunguliwa au kufungwa unahusiana na “Matendo ya Mtu”..Anaendelea na kusema “nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, KWA KUWA UNAZO NGUVU KIDOGO, NAWE UMELITUNZA NENO LANGU, WALA HUKULIKANA JINA LANGU”

Umeona sababu za huyu mtu kufunguliwa mlango?. Sababu zipo tatu.

Ya kwanza Kwa kuwa anazo nguvu kidogo. Ya pili Kwa kuwa amelitunza Neno lake. Na ya tatu Hakulikana jina lake.

Kristo hajabadilika sababu zile zile alizozitumia kale ndizo anazozitumia leo kufungua milango iliyofungwa mbele yetu.

 

Ni lazima kwanza tuwe na nguvu za rohoni. Biblia inasema.

1 Yohana 2: 14 “….Nimewaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mna nguvu, na Neno la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi mmemshinda yule mwovu”. Kuliweka Neno la Mungu ndani yetu ndio NGUVU ZA ROHONI. Mtu asiye na Neno la Mungu ndani yake, nguvu zake za rohoni zipo chini sana. Na kumbuka kuliweka Neno moyoni sio kujua vifungu vingi vya Biblia, kwa kuikariri. Hapana bali kuliweka Neno la Mungu moyoni ni kuliishi Neno moja lililoandikwa katika biblia. Ni kuona matokeo ya lile Neno katika maisha yako.

Kwamfano biblia inaposema “wapendeni Adui zenu, waombeeni wanaowaudhi..Mathayo 5:44”. Kama mtu kaushika huo mstari kwa kuukariri na hautendei kazi hicho kilichoandikwa hapo. Mtu huyo hajalishika Neno la Mungu moyoni mwake, lakini kama anakitendea kazi kwa kuwaombea wengine huyo kaliweka moyoni Neno la Mungu.

2) Sababu ya Pili ya Kufunguliwa mlango. Ni kwa kulitunza NENO LA MUNGU.

Kulitunza ni tofauti kidogo na kuliishi. Kulitunza maana yake unalitenda lile Neno kila siku katika maisha. Sio leo unalitenda kesho unaliacha.

3) Na sababu ya tatu na ya mwisho ni Kutolikana JINA lake.

Maana yake ni kutoikana Imani. Kulikana jina la Mungu na kuikana Imani ni kitu kimoja. Kuikana Imani kunajumuisha kurudi nyuma kiimani. Petro alimkana Bwana Yesu maana yake alirudi nyuma kiimani. Kadhalika mtu anayerudi nyuma kiimani ni sababu tosha ya kujifungia milango ya Baraka mbele yake.

Ndugu hatupaswi kukimbilia maji ya Upako kupata kibali mbele yetu. Au kupata fursa Fulani mbele yetu. Njia pekee ya kupata fursa ya kitu Fulani ni kurekebisha MATENDO YETU na KULITUNZA NENO LA MUNGU maishani mwetu. Na ndipo hayo yote yaliyosalia uliyokuwa unamwomba Mungu yanafunguka.

Kama ulikuwa hujampa Kristo maisha yako, unageuka sasa kwa kudhamiria kuacha dhambi kabisa. Na humfuati kwasababu tu unataka fursa Fulani. Hapana bali kwasababu umejigundua wewe ni mwenye dhambi na unahitaji kubadilishwa. Na Kristo mwenyewe anapenda watu wanaotubu dhambi zao na kukiri kuwa ni wakosaji. Yeye anawapa msamaha bure wote wanaokimbilia kwake haijalishi wameasi kiasi gani. Na baada ya kupata msamaha huo ambao utaambatana na AMANI Fulani moyoni isiyokuwa ya kawaida. Moja kwa moja usikawie nenda kakamilishe wokovu wako kwa kubatizwa katika maji tele(Yohana 3:23) na kwa jina la Yesu kulingana na (Matendo 2:38). Na Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu ambaye atakuongoza katika kuijua kweli yote ya maandiko na kukusaidia kushinda dhambi ambazo ulikuwa huwezi kuzishinda kwa nguvu zako.

Hapo utakuwa umeokoka kwa kuzaliwa mara ya pili. Na utakuwa na tumaini la uzima wa milele. Na kwasababu umeupata kwanza ufalme wa Mungu na Haki yake. Na hizo fursa na milango iliyofungwa ambayo umekuwa ukiitabikia kwa muda mrefu itafunguka yenyewe pasipo stika wala chumvi.

Bwana akubariki.

Mada Nyinginezo:

DANIELI: Mlango wa 2

MIHURI SABA

USIPOLITENDEA KAZI NENO LA MUNGU.

Inaruhusiwa Kula nyama ya Nguruwe kwa Mkristo wa Kweli?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Leave a Reply