Je! ile habari ya watu wawili wenye pepo inajichanganya?

Je! ile habari ya watu wawili wenye pepo inajichanganya?

SWALI: Biblia inajichanganya yenyewe katika Marko 5:1-6 na Mathayo 8:28-31?..Kwa maana tunaona ni habari moja lakini kila moja imezungumzwa tofauti na nyingine.


JIBU: Tusome

Marko 5:1  “Wakafika ng’ambo ya bahari mpaka nchi ya Wagerasi.

2  Na alipokwisha kushuka chomboni, mara alikutana na mtu, ambaye ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu;

3  makao yake yalikuwa pale makaburini; wala hakuna mtu ye yote aliyeweza kumfunga tena, hata kwa minyororo;

4  kwa sababu alikuwa amefungwa mara nyingi kwa pingu na minyororo, akaikata ile minyororo, na kuzivunja-vunja zile pingu; wala hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda.

5  Na sikuzote, usiku na mchana, alikuwako makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikata-kata kwa mawe.

6  Na alipomwona Yesu kwa mbali, alipiga mbio, akamsujudia;

7  akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese”

Lakini habari hiyo hiyo tunaisoma pia katika Mathayo inasema..

Mathayo 8:28  “Naye alipofika ng’ambo, katika nchi ya Wagerasi, watu wawili wenye pepo walikutana naye, wanatoka makaburini, wakali mno, hata mtu asiweze kuipitia njia ile.

29  Na tazama, wakapiga kelele, wakisema, Tuna nini nawe, Mwana wa Mungu? Je! Umekuja kututesa kabla ya muhula wetu?

30  Basi, kulikuwako mbali nao kundi la nguruwe wengi wakilisha.

31  Wale pepo wakamsihi, wakisema, Ukitutoa, tuache twende, tukaingie katika lile kundi la nguruwe”.

Sasa swali la msingi la kujiuliza, ni kwanini habari zinatofautiana hapo?.

Ili kupata jibu la hili swali vizuri , hebu tutafakari mfano ufuatao.

Upo wewe na rafiki yako, mmeenda mahali labda kwenye interview ya kazi, mlipofika sehemu ya kazi, mkasimamishwa getini na mlinzi, ili mkaguliwe kabla ya kuingia ndani, na kwenye hiyo ofisi ndogo ya mlinzi ndani kulikuwa na mlinzi mwingine wa pili, alikuwa kasimama pembeni akitazama, ambaye ni kama msaidizi, hivyo baada ya kukaguliwa na huyu mlinzi wa kwanza hapo nje, mkaandikishwa majina yenu,  kisha mkaruhusiwa muingie ndani. Na mlipomaliza interview mlitoka getini mkasaini kisha mkaondoka.

Mlipofika majumbani kwenu mkaulizwa kila  mmoja mambo yaliendaje  huko?..Na ushuhuda wa kila mmoja ulikuwa kama ifuatavyo.

WEWE: Wewe ulianza kusimulia, kwamba baada ya kutoka nyumbani mlifikia salama hadi sehemu ya interview lakini mlipofika getini mlisimamaishwa mkakaguliwa na MLINZI, kisha mkaruhusiwa kuingia ndani, na kufanya interview salama na kutoka. (sasa zingatia hilo neno MLINZI {maana yake ni mmoja}).

RAFIKI YAKO: Ushuhuda wa rafiki yako, naye akasimulia akasema… “Tulipotoka hapa tulifika kweli eneo la kazi, lakini tulipofika pale hatukuingia moja kwa moja, kulikuwa na WALINZI, pale getini wakatukagua, kisha wakaturuhusu kuingia ndani, tukaenda kufanya interview salama na tukaondoka. (Zingatia hilo neno WALINZI, maana yake ni zaidi ya mmoja)”.

Sasa hao ni mashuhuda wawili wanaelezea tukio moja!..Je kwa shuhuda zao hizo walizotoa, ni kwamba wametoa ushuhuda wa uongo au wa kujichanganya?.. Maana wa kwanza kasema kakaguliwa na MLİNZİ MMOJA, wa pili kasema KAKAGULİWA NA WALİNZİ maana yake ni zaidi ya mmoja… Sasa yupi tumwamini hapo, na yupi tusimwamini?.

Umeona?..ukitafakari kwa makini utagundua kuwa sio kwamba wote ni waongo, isipokuwa kila mmoja kaelezea kile alichokiona chenye umuhimu zaidi kwake..Ndio maana huyu wa kwanza kaeleza kakaguliwa na mlinzi mmoja..jambo ambalo ni kweli kabisa!..Aliyemkagua ni mlinzi mmoja tu na sio wawili, yule wa pili alikuwa ndani pembeni akitazama.

Na rafiki yako naye alikuwa yupo sahihi kusema “tulikaguliwa na walinzi” kwasababu ni kweli pale kulikuwa na walinzi wawili, ambao kazi yao wote ni moja, na wote wanashirikiana. Hivyo naye pia hajatoa ushuhuda wa uongo, kazungumza ukweli.

Sasa kwa mfano huu, tutakuwa tumeanza kupata picha ni nini kilichokuwa kinaendelea hapo kwenye Mathayo na Marko.

Ni kwamba Ushuhuda wa Mathayo hauwezi kufanana na ushuhuda wa Marko wala hauwezi kufanana na ushuhuda wa Luka asilimia mia moja. Lazima kutakuwa na tofauti kidogo, vinginevyo kama utakuwa umefanana asilimia mia basi ni uthibitisho kuwa sio ushuhuda wa ukweli lazima kutakuwa na (ku-copy na ku-paste). Na pia kulikuwa hakuna haja ya kuwepo injili tofauti tofauti kwasababu zote zingekuwa zinaeleza kitu kimoja.

Hiyo ndio sababu utaona Marko anatoa ushuhuda wa mtu mmoja aliyetoka makaburini, na Luka anatoa ushuhuda wa watu wawili. Lakini kiuhalisia walikuwepo pale watu wawili waliotoka makaburini, isipokuwa ndiye aliyekuwa amepagawa zaidi na ndiye aliyekuja kumsujudia Yesu na kumsihi asimtese.

Na sio tukio hilo tu katika biblia, ambapo habari mbili zinaonekana zikishuhudiwa tofauti. Lipo tukio lingine wakati Petro anamsaliti Bwana, sehemu moja inasema “kabla jogoo hajawika mara mbili utanikana mara tatu” na katika kitabu kingine inasema tu “kabla jogoo hajawika utanikana mara tatu”. Sababu ni hizo hizo tulizozitaja hapo juu.

Bwana akubariki

Tunaomba usibadilishe chochote katika ujumbe huu na mwingine wowote, na pia jihadhari na watumishi wa shetani ambao wanatumia masomo haya, kwa kusema kuwa wao ni waalimu wa huduma hii, na mwisho  wanaomba hela!, wanaochangia huduma hii ni wale wanaoguswa wenyewe kwa moyo wao kuchangia lakini sio kwa kuombwa fedha. Wingu la Mashahidi haijawahi kumpigia mtu simu na kumwomba hela. Ukiona mtu yeyote kashare au kushiriki masomo haya na mwisho akaweka namba zake za simu tofauti na hizi zetu +255789001312. Tunaomba umwonye aache kufanya hivyo au utujulishe kwa namba yetu hii hii +255789001312

Maran atha

Na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

Je! Ni kweli ubatizo wa maji hatuuhitaji tena?

Wenye kubatizwa kwa ajili ya wafu ni wakina nani?

Jehanamu ni nini?

NINI KINATOKEA BAADA YA KIFO?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments